Thursday, October 28, 2010

Tusikubali miaka mitano mingine ipotee

Evarist Chahali

MWAKA 2005 nilikuwa miongoni mwa waliokuwa na shaka juu ya uteuzi wa Jakaya Kikwete kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lakini baada ya ushindi wake wa kishindo, nilianza kuwa na imani naye, hasa kutokana na kauli zake za kuleta matumaini mapya.

Baada ya miaka 20 ya tawala za Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, nchi yetu ilihitaji mtu mwingine mwenye kuelewa kwa nini inazidi kuwa masikini wa kutupwa licha ya utajiri lukuki, mtu mwenye dhamira ya dhati ya kupambana na rushwa kwa vitendo, si maneno matupu (kwa mfano kutangaza kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kijirekebisha).

Awali, sikuamini kuwa Kikwete angeweza kuipatia Tanzania kiongozi wanayemuhitaji kwa vile hukuwa na rekodi hiyo. Licha ya kwamba urais si taaluma inayosomewa, lakini uongozi bora unaweza kubashiriwa kutokana na rekodi ya nyuma ya kiongozi mtarajiwa hasa kwa vile kabla ya kuwa rais wetu, Kikwete alikwisha kushika nyadhifa kadhaa lakini pasipo rekodi ya kujivunia.

Hofu yangu kuhusu Kikwete ilianza kuyeyuka baada ya kusikia kauli yake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ingekuwa kipaumbele chake kikuu pindi akichaguliwa, sambamba na kibwagizo cha Kasi Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya.

Hotuba yake wakati anazindua Bunge, Dodoma, ilileta msisimko mpya, matumaini na imani kwamba hatimaye sasa tumepata kiongozi wa kuifikisha Tanzania inakopaswa kuelekea. Na hata alipotangaza baraza kubwa la mawaziri (lililojumuisha sura zenye utata), nado niliendelea kuwa na matumaini naye na kukubaliana na utetezi wake kwamba ili afanikiwe kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania angehitaji timu kubwa.

Matumaini yangu yalianza kufifia pale ulipotoa hotuba na kutamka kwamba “nawafahamu wala rushwa kwa majina lakini nawapa muda wa kujirekebisha”. Nilivunjwa moyo na kauli hiyo kwa sababu sijawahi kusikia mahala ambako rushwa ilikoma baada ya kiongozi kutoa muda kwa wala rushwa kujirekebisha. Na labda hapa niulize, hivi ile deadline aliyotoa mwaka 2006 kwa wala rushwa (aliodai kuwafahamu kwa majina) kujirekebisha bado haijaisha? Au ilikuwa indefinite deadline (isiyo na ukomo)?

Baadaye alirejea kauli kama hiyo alipofanya ziara ya ghafla Bandari ya Dar es Salaam alikotamka bayana kwamba anawafahamu wala rushwa katika sehemu hiyo na kilichobaki ni kuwaumbua tu (nadhani alimaanisha kilichobaki ni kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria). Inasikitisha kuona hadi leo hakuna aliyewajibishwa huku mamlaka husika zikirejesha mpira huo kwake kwa maelezo ya “waulizeni Ikulu maana wao ndio walidai wana orodha ya wala rushwa hapa”.

Tuwe wakweli, hivi kama aliahidi kuwasilisha majina ya mafisadi wa bandarini lakini hajatimiza ahadi hiyo maana yake ni nini? Je, tunastahili kuendelea naye kama ahadi alizotoa ni zisizotekelezwa? Kama anashindwa kutekeleza ahadi anazotoa mwenyewe pasipo kulazamishwa ataweza vipi kutekeleza mambo muhimu ambayo japo hajaahidi ni lazima ayatekeleze?

Ni kweli kwamba kiongozi wa nchi lazima afanye safari za kujitambulisha nje, lakini hicho hakiwezi kuwa ndiyo kipaumbele kwa kiongozi mwenye dhamira ya dhati ya kurekebisha hali ya nchi masikini kama yetu. Hata Barack Obama na David Cameron, viongozi wa mataifa tajiri kabisa duniani, wametuthibitishia kwamba kwenda nje ya nchi kujitambulisha si kipaumbele kwa kiongozi mpya.

Lakini pengine eneo tata zaidi ni la mafisadi. Kusita kupambana na kundi hili kumezua tafsiri nyingi katika vichwa vya watu, nyingi za hizo, hazimsemi vizuri Rais Kikwete kwa vile imejikita imani kwamba kuwaacha mafisadi waendelee ndiko kulikokwamisha “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”.

Ni siri ya wazi kuwa aliingia madarakani kwa nguvu na jitihada za wanamtandao, wengi wao wakiwa watu wenye rekodi zisizopendeza. Kosa kubwa alilofanya ni kutotumia nafasi yake kama Rais kuwadhibiti, matokeo yake wameishia kuutumia urais wake kujinufaisha wao wenyewe.

Matukio mawili ambayo hayatafutika katika historia ya Urais wa Kikwete ni ujambazi wa fedha za EPA na utapeli wa kampuni ya Richmond na ‘binamu’ yake Dowans.

Kuhusu suala la EPA, wengi wetu tunaamini kwamba bado kuna maswali mengi kuliko majibu. Japo inapendeza kuwaona baadhi ya watuhumiwa wakifikishwa mahakamani, bado haieleweki kwa nini hadi muda huu wamiliki wa kampuni iliyokwiba fedha nyingi zaidi, Kagoda, wameendelea kuhifadhiwa.

Ni kweli safari hii pana ushindani wa kutosha kwenye kiti cha urais. Ni kweli pia kwamba kama akipita, Kikwete atakuwa, kwa mujibu wa Katiba, akitumikia kwa muhula wake wa mwisho. Ninachojiuliza ni kama amemudu kufumbia uoza wote huu katika kipindi muhula wake wa kwanza huku akijua fika kuwa baada ya miaka mitano angepaswa kuomba tena ridhaa ya kupigiwa kura, hali itakuwaje katika muhula wake wa mwisho ambao hatahitaji tena kura zetu?Barua-pepe:
epgc2@yahoo.co.uk

0 comments:

Post a Comment