Saturday, October 2, 2010

Mbila: Nimefuata mageuzi ya kweli Chadema

Na Brandy Nelson

GEORGE Mbila ni Mgombea udiwani kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kabla ya hapo alikuwa ni diwani katika kata hiyo kuptia chama cha Wafanyakazi Tanzania (TLP). Je, nini kimemfanya akihame chama hicho na kukimbilia Chadema?

Mbila mwenyewe anaeleza sababu kuu ya kufanya maamuzi hayo kuwa ni kupoteza mwelekeo kwa TLP.

“Nilikuwa diwani wa kata ya ubaruku kwa tiketi yaTLP sasa nimehama sipo tena kwenye chama hicho na sasa nagombea kwa awamu ya pili lakini kwa kupitia chama changu kipya cha Chadema kwani chama cha TLP kwa sasa kimekosa mwelekeo na hivyo kusababisha wanachama wake kuyumba” anasema Mbila.


Anasema kuwa kabla ya kukihama chama hicho alifanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini chama ambacho kina sera zinazomlenga mwananchi ambaye ndiye mpiga kura.
Nimebaini kuwa Chadema ndiyo chama pekee ninachoweza kukitumikia katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kata ya Ubaruku.

Mbila anazitaja sera za Chadema katika uchaguzi huu wa mwaka 2010 zilizomvutia ni pamoja na Elimu kutolewa bure kuanzia madarasa ya awali hadi kidato cha sita ambapo anasema kuwa hilo linawezekana na katika sekta ya afya.

Anasema hata sera ya Chadema ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi inatekelezeka kwani kama diwani analipwa posho ya kikao kimoja sh 45,000, kwa wafanyakazi pia itawezekana.

Akielezea mambo aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita katika kata yake anasema kuwa katika kipindi hicho ameweza kufanikiwa katika sekta mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa na ushikiraikiano mzuri na wananchi na uongozi mzima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na hivyo kupata nguvu ya kuamua kugombea tena kwa awamu ya pili.

Anaeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano kwenye sekta ya elimu ameweza kuhamasisha na kufanikiwa kujengwa madara 12 na ofisi mbili za Walimu katika shule za kwa mpango wa MMEM.

Anazitaja shule hizo na idadi yake ya madarasa kuwa ni pamoja na shule ya msingi Mwanawala amefanikiwa katika ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja, Rujewa Mission madarasa manne, Ibohola madarasa manne,Urunda darasa moja na mpakani darasa moja na ofisi moja.

Mafanikio mengine katika sekta ya elimu ni pamoja na ujenzi wa nyumba 10 za Walimu kwa mpango wa MMEM ambapo katika shule ya Mwanawala nyumba mbili, Mahongole nyumba moja , Ibumila nyumba moja, Imlilo Songwe nyumba mbili, Mpakani nyumba moja, Utyego nyumba moja, Rujewa mission nyumba moja na Mkombe nyumba moja.

Katika shule za sekondari anasema kuwa, amefanikiwa kujenga madarasa 30 ambpo katika suhule ya sekondari Mbarali madarasa 21, Imalilo Songwe tisa na majengo ya utawala na hosteli moja ya wasichana katika shule ya sekondari Imalilo Usongwe na jumla ya madawati 590 yamechangwa katika kipidi hicho kwa shule za sekondari za Mbarali na Imalilo Usongwe.

Mbila anaeleza kuwa katika sekta ya maji ameweza kuhamasisha na kusimamia kupeleka miradi ya maji katika kijiji cha Utyego Mwakaganga kwa mpango wa DADS wenye thamani ya sh 62 miioni ambapo halmshauri ilitoa sh 52 milioni na wananchi walichangia sh10 milioni na nguvu kazi.

Anasema kuwa miradi mingine ni pamoja na ujenzi kisima cha maji katika kijiji cha Mwakaganga wenye thamani ya sh32 milioni na mradi wa maji ambao ulifadhiliwa na benki ya dunia katika kijiji cha Ubaruku uliogharimu sh 211 milioni ambapo maji hayo yanahudumia vijiji Viwili katika kata hiyo ya Ubaruku.


Katika miundo mbinu ya barabara anaeleza kuwa katika kijiji cha Utyego kwa mpango wa Tasaf kijiji hicho kimejengewa barabara kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilometa tano (5km) na Mbarali hadi Mwanawala kilometa 13.

Anasema kuwa kupitia utaratibu waliojiwekea wa kutengeneza barabara kila mwaka wamefanikiwa kujenga barabara za Ubaruku mjini zenye urefu wa kilometa 12 ujenzi wa makaravati 10 katika sehemu korofi.

Anaeleza pia katika kipindi hicho miaka mitano katika sekta ya kilimo na mifugo kwa kushirikiana na wananchi ameweza kubuni mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji unaoitwa mwendo mtitu ambapo katika bajeti ya mwaka 2009/2010 halmshauri ya Wilaya ya Mbarali ilitoa milioni 20 kwa ajili ya upembuzi yakinifu katika mradi huo.

Anasema kuwa katika bajeti ya mwaka 2010/2011 ya halmashauri hiyo imetenga milioni 18 kwa ajili ya kutengeneza banio katika mradi huo na halmashauri inaendelea kutafuta mfadhili kwa ajili uchumbaji wa mifereji na kwamba vijiji vitakavyohusishwa ni pamoja na Mwakaganga, Hurunda, Imalilo Usongwe, Mwanawala, Igumilo na Nyelegete.

Mgombea huyo anaeleza kuwa katika kipindi hicho waliweza kuanzisha ujenzi wa machinjio ya ng`ombe wenye gharama ya milioni 15 ambapo ujenzi huo upo katika kijiji cha majengo.

Aidha anaeleza kuwa katika sekta ya Afya pia ameweza kupata mafanikio katika kipindi hicho cha maika mitano ambapo zahanati moja iliweza kujengwa katika kijiji cha Imalilo Usongwe wenye thamani ya sh 12 milioni, ujenzi wa nyumba mbili za waganga katika zahanati ya ubaruku na kituo cha afya Rujewa Mission zenye gharama ya sh16 milioni kwa kila nyumba.

“Pamoja na hayo yote niliweza kuomba ufadhili kituo cha malezi (UMATI) wa kutujengea kituo cha kutolea ushauri nasaha ambapo tayari tumeshafanyiwa lakini pia nimeweza kuishauri halmashauri kuipandisha zahanati ya Rujewa Mission kuwa kituo cha afya na ikawa hivyo” anasema

Anasema kuwa pia ameweza kuishauri Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuweza kuwalipia ada watoto yatima 190 katika shule ya sekondari Mbarali na Imalilo Usongwe.

Mimi mwenyewe nina watoto 10 ninaowalipia ada na wengine wanne tayari wameshamaliza kidato cha nne.

Mbila anaeleza mambo ambayo anatarajia kuyafanya endapo kama atachaguliwa kwa mara nyingine kuwa ni pamoja na kutekeleza sera za chama cha Chadema na kuhakikisha kata ya Ubaruku inakuwa mji mdogo ili kuweza kusogeza katibu huduma za kijamii kwa wananchi.

Anasema kuwa atahakikisha shule za sekondari zinakuwa na kidato cha tano na sita na kuhakikisha umeme katika shule ya sekondari mbarali unafika na kwamba ni mpango ambao tayari umeanza na mpaka sasa sh 1.4 milioni zimeshachangwa na maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kazi hiyo.


Mamabo mengine anayotarajia kufanya ni kujenga hosteli za wanafunzi wasichana na kuhamisha ujenzi wa barabara katika meneo korofi na kufikisha maji katika vijiji ambavyo bado havijapata maji na katika sekta ya afya ni kuhakikisha kila kijiji kina zahanati .

Kutokana na jitihada zake za maendeleo katika kata hiyo, Mbila anaamini kuwa atachaguliwa tena katika nafasi hiyo,
“Naamini wananchi watanichagua tena kutokana na kuwa wananipenda na kuniamini kwakuwa nimeshirikiana nao vizuri katika kipindi cha miaka mitano iliyopita”.

Mbila ana elimu yake ni ya kidato cha nne aliyoipata mwaka 1990 katika shule ya sekondari ya Meta iliyopo jijini Mbeya.
Baada ya hapo mwaka 1991 hadi 2000 alijihusisha na biashara za ng`ombe mkoani Dodoma. Mwaka 2000 hadi 2006 alikuwa katibu wa wafanyabiashara wa mchele kata ya Ubaruku na 2005 hadi 2010 amekuwa diwani wa kata ya ubaruku kupitia chama cha TLP.

0 comments:

Post a Comment