Sunday, October 3, 2010

Nilichokiona Jana Mwembetogwa Iringa

Na Maggid Mjengwa,

Iringa ni ngome ya CCM. Jana jioni Dr Slaa alitua Iringa na kuvuta umati mkubwa wa watu. Nilikuwapo pale Viwanja vya Mwembetogwa. Nini aliongea na kina nini ndani yake, nitachambua hapa kwa ufupi;

Nilifika viwanja vya Mwembetogwa saa kumi na robo jioni. Tayari Dr Slaa alishatua. Watu walikuwa wengi sana. Pamoja na uzoefu wangu wote wa kujipenyeza kwenye kundi la watu nikiwa na kamera, bado kwangu safari hii ilishindikana. Niliishia kutafuta sehemu ya juu kidogo nyuma ili walau nipate picha ya Dr Slaa akihutubia. (Picha ya kwanza hapo juu blogiini imepigwa na Francis Godwin.)

Nimekaa Iringa tangu mwaka 2004 na nimeudhuria mikutano yote ya kampeni za Urais kuanzia Jakaya Kikwete, Mbowe, Lipumba hadi Mrema, lakini niweke wazi. Mkutano wa jana pale viwanja vya Mwembetogwa umevunja rekodi zote katika kujaza watu kwa mujibu wa kumbukumbu zangu za tangu 2004. Katika chaguzi ziliopita kuna watumishi wa Serikali waliokuwa wakienda kwenye mikutano ya vyama vya upinzani kwa kunyata. Walikuwa na hofu ya kuonekana wanaunga mkono upinzani na kuonekana kwao kwenye mikutano ya akina Mbowe, Zitto na Lipumba ingetafsiriwa kuwa hawaipigii kura CCM. Jana kulikuwa na watu wa aina zote, hata makada wa CCM walifika pia.

Kwenye hotuba yake ya takribani dakika 43 Dr Slaa alijikita katika maeneo makubwa matatu;
Uchaguzi wenyewe; alianza kwa shambulizi dhidi ya Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ( JWTZ) na Polisi kwa tamko lao juu ya uchaguzi. Dr Slaa naye akasema ametoa tamko lake akiwa Njombe kushutumu hatua hiyo ya jeshi na polisi akisema kuwa ni kuwatisha wapiga kura.

Dr Slaa akagusia pia masuala ya elimu akisisitiza azma ya Chadema kutoka elimu bure kuanzia chekechea. Katika eneo hili Dr Slaa alifanikiwa pia ( kisiasa) kukwepa kutoa ufafanuzi wa ni kwa namna gani. Kuna mahali alifanikiwa sana alipojaribu kulinganisha na wakati wake alipokuwa shuleni na hali ilivyo sasa.

” Ndugu zangu, leo mtoto anakwenda shule anaambiwa abebe na ndoo!” Alisema Dr Slaa.
Niliwasikia wasikilizaji wakimalizia na ” mafagio, makwanja…”

Hapo Dr Slaa aliweza kupenya kwenye kero na matatizo ya kila siku ya wapiga kura. Na ni mambo haya ambayo wapiga kura wanayaelewa zaidi kuliko kashfa za EPA, IPTL, Deep Green na nyinginezo ambazo akina Dr Slaa na wanasiasa wengine wameshindwa kuziweka katika lugha nyepesi ikamfanya mpiga kura wa Kihesa awaelewe. Mpiga kura ambaye bado anaumiza kichwa kila siku kutafuta senti za kununulia mafuta ya taa na michango ya madawati ya watoto wake.

Dr Slaa aligusia kwa kirefu pia suala la uchumi na namna Serikali yake itakavyohakikisha Tanzania inanufaika na rasilimali zake. Kuna wakati kwenye hotuba yake alijichanganya kido aliposema wachagueni wabunge wa Chadema ili kwenye kikao cha bajeti cha Julai mwakani wapige mapanga bajeti tupate fedha za elimu na mengineyo. Dr Slaa alisahau kuwa yeye ndiye atakayeunda Serikali na lazima aonyeshe kwa wapiga kura kuwa ndivyo itakavyokuwa.
Staili ya Dr Slaa

Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumsikiliza Dr Slaa akihutubia ‘ live’.
Nguvu zake:

- Dr Slaa ana mvuto. Anavuta wasikilizaji. Anaongea kwa staili inayomfanya mtu aamini kuwa dakika ijayo ana kitu cha muhimu zaidi atakitamka. Watu wanavutika, wanabaki kumsikiliza.

- Anaongea kwa staili ya kimahubiri. Ana uzoefu katika hilo. Kuna wakati anayaacha matokeo ya anachoongea kwa Mungu na watu.

- Ametokea ndani ya CCM. Anafahamu kuwa walio wengi anaowahutubia kwa kawaida ni wapiga kura wa CCM. Dr Slaa anafahamu, wanachokitafuta wanaomsikiliza walikuwa nacho, wamekipoteza, kwa uzembe. Hata Baba wa Taifa angefufuka pale Mwembe togwa angetamka; ” Eh, hivi Dr Slaa naye amerudi CCM!”. Ndio, jana pale Mwembetogwa Dr Slaa alikuwa anazungumzia CCM ya Mwalimu.

- Dr Slaa mara kwa mara anatumia nafsi ya tatu; ” Wanasema Dr Slaa….” Anayesema hayo ni Dr Slaa.

- Hasimami mahala pamoja jukwaani. Anatembea tembea huku akigeukia hadhira yake.

- Anachangamka jukwaani. Aliweza hata kurukaruka kidogo. Inawavutia wanaomsikiliza.
Udhaifu wake:

- Anaanza hotuba yake kwa kuonyesha ana haraka kidogo. Wanaomsikiza nao wanapata ‘ stress’ ya namna fulani. Watu wanaanza kuangalia saa zao pia. Details hizo zinaweza kumtoa nje msikilizaji.

- Wakati mwingine anaonyesha jazba kidogo. Maneno kama ; ” Kama Kikwete mwanamme…” Anatakiwa ayaepuke. Yanaweza kutafsiriwa vibaya na katika nchi nyingine wanaharakati wa jinsia wanaweza kumjia juu.

- Anatoa maagizo, anatoa siku saba.. hata kabla hajaingia Ikulu. Labda angetamka zaidi ” CHADEMA tunataka’. Kuna wapigakura wanaohofia kumwingiza madarakani mwenye silika za udikteta.

- Dr Slaa hakuzungumzia KATIBA na umuhimu wa kuanzishwa kwa mchakato wa kuandika KATIBA mpya kwa nchi yetu. Wapiga kura wengi leo wameanza kuelewa kuwa KATIBA yetu ni chanzo cha matatizo yetu mengi. Haitoshi tu kubadilisha marais na vyama. Huko ni sawa na kuyatoa maji kwenye ndoo ya bati na kuyaingiza kwenye ndoo ya plastiki. Na kubadili ni kuyatoa maji kutoka kwenye ndoo ya plastiki kuarudisha kwenye ndoo ya bati! Maji ni yale yale. Ndio maana , zawadi kubwa kwa sasa kwa Watanzania katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru ni kuanzisha mchakato wa kuandika KATIBA mpya shirikishi itakayoirudisha nchi yetu kwenye reli. Na hakika imeanza kuwa KIU kubwa ya Watanzania.

- Huenda Dr Slaa hapati muda mwingi wa kutafuta taarifa zenye kuwagusa watu walio mbele yake kumsikiliza. Kuwa watu wengi walijazana pale Mwembetogwa jana kwa mtazamo wangu kunachangiwa pia na namna CCM ilivyoboronga katika kumpata mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini. Miongoni mwa waliomsikiliza Dr Slaa jana pale Mwembetogwa ni wanachama na wapenzi wengi wa CCM. Na ajabu kubwa kabisa; Dr Slaa tangu mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake hakutamka jina la ” Mama Monica Mbega”. Mgombea Ubunge wa CCM, Iringa Mjini. Hata mgombea wa CHADEMA Mchungaji Msigwa alipopewa dakika tatu na Slaa aongee, naye hakutamka jina la ” Monica Mbega” na kwanini wana Iringa Mjini wasimchague Monica Mbega.
Mengineyo;

Tatizo la CHADEMA na vyama vingi vingine vya upinzani linabaki pale pale; oganaizesheni. Wengi katika umati ule uliokusanyika pale Mwembetogwa hawajui zilipo ofisi za CHADEMA mjini. Hawawajui makada wa Chadema. Mkutano kama ule ilikuwa ni fura kwa Chadema kuwatambulisha makada wa Chadema na wapi wapenzi wa Chadema waende kupata taarifa za chama chao.

Badala yake, wengi wa waliokwenda pale Mwembetogwa kumsikiliza Dr Slaa wamerudi majumbani kwao. Na atakayewatembelea tena kuzungumzia uchaguzi ni Balozi wao wa nyumba kumi.

Naam. Demokrasia yetu bado changa. Na ishara za jamii inayotaka mabadiliko inaonekana. Tuwe na ujasiri wa kutoa maoni yetu kwa kutanguliza MASLAHI YA TANZANIA KWANZA. Hata Roma haikujengwa kwa Siku Moja.
Maggid
Iringa.


mjengwa

0 comments:

Post a Comment