Thursday, October 7, 2010

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VISIINGILIE UCHAGUZI MKUU; KUVURUGA AMANI

C/O TANZANIA GENDER NETWORKING PROGRAMME, MABIBO ROAD,
P O BOX 8921, DAR ES SALAAM, TEL. +255 22 2443205;2443450;2443286 Mobile 255 754 784 050 Fax. 2443244, Email info@tgnp.org, web TGNP

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VISIINGILIE UCHAGUZI MKUU; KUVURUGA AMANI

1. Oktoba 1, 2010, Vyombo vya Ulinzi na Usalama; Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Makao Makuu ya Jeshi ka Polisi vilitoa tamko, kupitia Luteni Jenerali Abdulhaman Shimbo, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, juu ya ulinzi na usalama kuhusu amani wakati wa kampeni na uchaguzi. Kesho yake, yaani Oktoba 2, vyombo vya habari nchini vilikariri tamko hilo, na hivyo kusambaza ujumbe na maudhui yake kwa wananchi na umma kwa ujumla, kama ilivyokusudiwa.

2. Katika ujumla wake, Tamko la Vyombo vya Ulinzi na Usalama linasisitiza umuhimu wa wadau wa uchaguzi kulinda amani na usalama, ambazo ni tunu za Taifa la Tanzania, hususan katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010. Tamko linawakumbusha wadau wa uchaguzi; wananchi, asasi za kiraia, mashirika ya dini na vyama vya siasa, umuhimu wa kutunza na kuenzi amani sawia na kushirikiana na vyombo vya usalama kulinda amani. Aidha wadau wanakumbushwa wajibu wa majeshi; JWTZ na polisi kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kuwa katika hali ya amani na usalama. Hili ni jambo jema kwa faida na ustawi wa taifa letu ambalo wengi wa wananchi wake bado ni maskini sana.

3. Hata hivyo, licha ya Tamko kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuenzi na kulinda amani na usalama wa taifa lao, sisi mashirika yanayotetea Usawa wa Jinsia, Haki za Binadamu na Maendeleo na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct) tumeshitushwa, hatukubaliani na tunalaani kwa jinsi na namna (mtindo) tamko la vyombo vya ulinzi na usalama lilivyotolewa, uhalali wa wahusika kutoa tamko hilo, kipindi lilipotolewa tamko hilo, mantiki yake, mwelekeo wa maudhui yake na chombo kilichotoa tamko husika kwa sababu zifuatazo:

i). Tamko la Vyombo vya Ulinzi na Usalama linakiuka, na ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977. Ibara 138 haibainishi kuwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama yatajihusisha moja kwa moja na masuala ya Uchaguzi wala kubainisha kuwa Amiri Jeshi Mkuu, yaani Rais wa Jamhuri, anaweza kutoa amri kwa majeshi ya Ulinzi na Usalama kuingilia shughuli za Uchaguzi Mkuu, au chaguzi nyinginezo. Aidha ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, haitaji wala kutambua Majeshi ya Ulinzi na Usalama kama sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kitendo cha Majeshi ya Ulinzi na Usalama kutoa tamko kupitia vyombo vya habari ni dhahiri kinalenga kutoa vitisho, kuchochea, kuingilia mchakato, na bila shaka kuvuruga Uchaguzi Mkuu unaokusudiwa kufanyika Oktoba 31. Na kama hivyo ndivyo, WanaFemAct tunalazimika kuamini kuwa tamko la vyombo vya Ulinzi na Usalama limeficha na kusheheneza malengo ya maslahi binafsi, siyo maslahi ya nchi kama umma unavyoaminishwa.

ii). Hadi sasa, zaidi ya 'vijembe' vya hapa na pale baina ya wanasiasa na vyama vya siasa vinavyoshindana na kujinadi kwa wananchi ili kupata ridhaa ya kuongoza dola ya Tanzania, hakuna wala hakujatokea tishio lolote la kuvurugika kwa amani. Vyama vya Siasa vimekuwa vikiendelea kutangaza mipango ya sera zao, vijijini na mijini, kupitia mikutano ya kampeni; wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano ya kampeni, kusikiliza na kuchambua ahadi mbalimbali zinazotolewa na wanasiasa na vyama vyao; vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti taarifa mbalimbali kuhusiana na mambo yanayojiri kwenye mikutano ya kampeni, na hata kampeni za nyumba kwa nyumba; asasi za kiraia, kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, zimekuwa zikiendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa makundi mabalimbali ya wapiga kura watarajiwa; Msajili wa Vyama Vya siasa amekuwa akiendelea kufuatilia utekelezaji wa Maadili ya Vyama vya Siasa Wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiendelea kuratibu kampeni, kusimamia manunuzi ya vifaa tayari kwa kusambazwa katika vituo 52 000 vya kupigia kura nchini kote, kuthibitisha usahihi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na kuratibu wadau wengine wa uchaguzi, kwa mfano, waangalizi wa ndani na nje wa uchaguzi. Hayo yote yakiwa yanaendelea hakujatokea tishio la kuvurugwa kwa amani wala tatizo la kiusalama. Kama hivi ndivyo, wanaFemAct tunaendelea kuamini kuwa tamko la Vyombo vya Ulinzi na Usalama lina agenda yake; ya siri. Si bure! Litakuwa ni jambo la kushangaza na kusikitisha sana iwapo Watanzania watabaini kuwa vyombo vyao vya ulinzi na usalama vimeanza kutumiwa vibaya na wanasiasa na vyama vya siasa kwa manufaa ya kikundi maslahi binafsi cha vatu wachache.

iii). Jeshi la Wananchi wa Tanzania halipaswi kujihusisha na masuala ya ndani ya usalama wa raia. Kama kweli kungekuwa na tishio la amani na usalama, basi tungetegemea kuona Jeshi la Polisi, chombo chenye dhamana ya kuhakikisha kunakuwa na hali ya usalama kwa raia na mali zao, likitoa tamko hilo; siyo JWTZ. Sasa kama hivyo ndivyo, wanaFemAct tunasikitika na kushangaa kuona Jeshi la Wananchi wa Tanzania likifanya kazi za polisi wakati askari wa Jeshi la Polisi wapo tele, pamoja na Inspekta Jenerali wao. Hali hii haieleweki na ni kinyume cha kanuni za msingi za utawala bora. Inakuwaje askari polisi waendelee kulipwa mshahara wakati kazi zao zinafanywa na wanajeshi wa JWTZ!

iv). Ujumbe unaotolewa na tamko la Vyombo vya Usalama kuwa "vimejiandaa kikamilifu kupambana na mtu, watu, kikundi, chama au taasisi yoyote... itakayochochea kuyakataa matokeo ya uchaguzi" ni kitisho cha dhahiri, si kwa vyama vya siasa na wagombea pekee, bali pia ni dhidi ya jitihada za kujenga na kuimarisha utawala bora na demokrasia kwa ujumla hapa nchiniTanzania. Ni dhahiri Luteni Jenerali Abdulhaman Shimbo anafahamu kuwa si wanajeshi wala silaha zinazoweza kulazimisha wananchi, vyama vya siasa na wagombea wao wakubaliane na matokeo ya uchaguzi bali uchaguzi unaokubalika miongoni mwa washindani na wananchi kwa ujumla kuwa umefanyika kwa kuzingatia vigezo vya msingi vya chaguzi huru na haki. Katika kutimiza hili, usimamizi imara na usiokuwa na upendeleo, na vyombo vya usalama na vyombo vya habari visivyopendelea upande wowote ni nguzo muhimu kuhakikisha washindani wa kisiasa wanakubaliana na matokeo ya uchaguzi. Yaliyotokea katika nchi za Romania, Ukraine, Zimbabwe, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na kwingineko duniani ni mifano inayotoa mafunzo ya kutosha kwa raia na wanajeshi pia. Hakika hili halihitaji tamko la Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Kama hivyo ndivyo, wanaFemAct hatuoni sababu iliyopelekea Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoa tamko lake, na hasa katika kipindi hiki ambacho kampeni zinaendelea vizuri. FemAct hatuko tayari kuona Tanzania inapitishwa ya machafuko ya kupandikiza kwa lengo la kunufaisha kirundi maslahi cha vatu wachache.

Kwa kuzingatia sababu zetu hapo juu, wanaFemAct tunapendekeza ifuatavyo:
a). Vyombo vya Ulinzi na Usalama viache mara moja kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa kuwa jambo hili linaweza kusabaisha vitisho na vurugu dhidi ya wapiga kura na wananchi kwa ujumla; kuchafua hali ya amani na usalama ambayo ni tunu ya Tanzania. Lakini iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo, basi sheria husika sharti zifuatwe, Jeshi la Polisi likiwa na dhamana ya kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

b). Wanasiasa, vyama vya siasa na viongozi waache mara moja kujitafutia ushindi kwa kutumia mlango wa nyuma. Uongozi wa dola sharti upatikane kupitia mashindano ya wazi kusaka ridhaa ya wananchi kidemokrasia katika uchaguzi unaokubalika kuwa huru na haki, siyo kutumia vyombo vya Ulinzi na Usalama kutisha wapiga kura ili kujihakikishia ushindi.

c). Vyombo vya habari viendelee kuhabarisha wananchi na wapiga kura juu ya mipango ya sera za vyama vya siasa na ahadi za wagombea kama inavyojiri katika mikutano ya kampeni.

d). Asasi za kiraia ziendelee kuelimisha wananchi juu masuala mbalimbali yanayoongeza uangavu kwa wapiga kura, na wananchi kwa ujumla juu ya sheria, taratibu, kanuni za uchaguzi, haki na wajibu wa kuhudhuria mikutano ya kampeni, kusikiliza ahadi za wagombea, kufanya maamuzi na hatimaye kujitokeza kupiga kura.

e). Wapiga kura waendelee kujibidisha kupata elimu ya mpiga kura, kuhudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa na wagombea, na kusikiliza kwa makini ahadi za wagombea wakipembua na kuchambua kati ya pumba na mchele ili kunako Oktoba 31 wafanye uamuzi kwa kihistoria kuchagua viongozi watakaoweza kushirikiana na wananchi kukwamua Taifa letu kuondokana na umaskini na kuletea Taifa heshima.


Mwisho/

FemAct

Dar es Salaam, Oktoba 6, 2010.

0 comments:

Post a Comment