Saturday, October 2, 2010

Slaa: Umasikini hauondolewi kwa bajaji

Joyce Joliga na Beatusi Kagashe, Songea

DK Slaa

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema umasikini wa Watanzania hauwezi kuondolewa kwa kuwanunulia bajaji akibeza ahadi hiyo ya ununuzi wa pikipiki za magurudumu matatu iliyotolewa na Jakaya Kikwete kwa ajili ya wajawazito huku yeye akitembelea gari la Sh400 milioni.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Songea katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi ya Majengo huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wakipasa sauti kuimba "rais, rais, rais".

Dk Slaa alisema bajaji si msingi wa kuwaondelea umaskini wa Mtanzania na kwamba yeye binafsi hawezi kuahidi chochote kwa kuwa si afisa miradi na kwamba kuahidi miradi ambayo ipo katika michakato na inasubiri utekelezaji, ni kuchezea akili za Watanzania.

Mbunge huyo Karatu anayemaliza muda wake alisema CCM imefikia mwisho na ndiyo maana inaahidi ahadi zisizokuwa za msingi ambazo yeye hawezi kuziahidi kwa wananchi na kuwa Chadema itashugulikia matatizo ya msingi ambayo marehemu Baba wa Taifa aliyashugulikia.

Aliyataja mambo ya msingi ambayo atayashughulikia iwapo wananchi watamchagua kuwa rais kuwa ni umaskini uliokithiri kwa Watanzania ambao kiongozi wa serikali ya awamu ya kwanza aliupiga vita lakini viongozi waliomfata baada yake wameshindwa kushugulikia.

Alirejea tena ahadi yake ya kupunguza bei za vifaa vya ujenzi na kuwafanya wananchi wajenge nyumba bora za kuishi, akiahidi kuwa miaka mitano ijayo Tanzania itakuwa na nyumba zilizoezekwa kwa bati.

Alisema jambo jingine la msingi ambalo atalishugulikia ni elimu na kufafanua kuwa msingi wa umaskini wa Mtanzania unatokana na kutopata elimu na hivyo serikali yake itahakikisha inasimamia ili watoto wote wapate elimu ya awali kwa kuwa elimu ya Mtanzania imekuwa ikididimia kuanzia chini.

“Tanzania ya wakati wa Nyerere, elimu ilikuwa bure na mimi baba yangu alikuwa mfanyakazi kwa mzungu na nimesoma na kuitwa daktari, lakini Tanzania ya sasa si ya Nyerere... tumeshindwa kugawana kidogo kilichopo. ilkiwa mtanichagua kuwa rais, nitatumia raslimali zilizopo kuhakikisha Watanzania wote wanasoma elimu inayowawezesha kupata kazi,” alisema.

Mgombea huyo alitambua mchango uliotolewa na unaoendelea kutolewa na madhehebu ya dini hasa Kanisa Katoliki katika elimu na kusema bila mchango huo wananchi wengi wa Songea wasingepata elimu.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alidai kuwa Kikwete amejialika kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) utakaofanyika mjini Songea kuanzia Jumapili.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Songea, Dk Slaa alisema kuwa Kikwete hajaalikwa ila katumia mabavu yake kuhudhuria mkutano huo.

“Hii ni rushwa ya hali juu ambayo inapingana na Sheria na Gharama za Uchaguzi aliyosaini mwenyewe,” alisema Dk Slaa.

Katika mkutano huo wananchi waliwazidi polisi nguvu na kusogea karibu na jukwaa kumsikiliza Dk Slaa.

Alidai Kikwete ni fisadi kwa sababu ufisadi umemkaa kichwani mwake na rohoni mwake ndio maana matendo anayofanya hayaendani na juhudi za kuacha rushwa kama anavyosema.
“Ndani ya walimu hao kuna usalama wangu wa taifa humo ndani, watasema yote atakayojadili,” aliongezea Dk slaa.

Alidai kuwa usalama wa taifa wamweleze Kikwete ukweli wa hali halisi ya siasa inavyokwenda ili asije pata presha siku ya matokeo.

“Ni aibu siri ya mkubwa inapovuja... ndani yao wameparanganyika na Watanzania wameamua mabadiliko hivyo hakuna anayeweza kuwazuia,” alisema Dk Slaa akimwomba atambue alama za nyakati kwani atatia aibu mbeleni.

Pia alibeza safari za Kikwete kwenda nchi za nje na kurudi na ahadi neti na walimu wa “peace corps” ambao walianza kufanya kazi nchini tangu mwaka 1960.

Alisema ni aibu kwa rais kusifika nje wakati wananchi wake hawaoni cha kumfanya apate sifa hizo kutokana na matatizo waliyonayo.

“Mwanaume gani unasifiwa na jirani yako wakati mke na watoto wako wako ndani wanataabika kwa shida ambazo hawajui zitaisha lini,” alisema Dk Slaa.

Alisema serikali ya CCM inatengeneza mazingira ya rushwa kwa wananchi wake kwani mishahara yao nikidogo sana isiyoweka kidhi mahitaji yao ya kila siku.

Alimponda mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi kwa kukosa kufanya mambo ya maendeleo katika jimbo lake kwa miaka 10 ya uongozi wake.

Naye Mgombea ubunge wa ubunge Songea Mjini kwa tiketi ya Chadema, Mbogoro Aswald alisema uchaguzi wa mwaka huu ni vita kati ya uadilifu na ufisadi, giza na mwanga.
Aliwaomba wananchi wasichague chama bali mgombea atakaye waletea maendeleo.

GAZETI MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment