Mussa Juma, Karatu
MGOMBEA wa urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema kuwa jukumu la kuhakikisha amani inatawala wakati wa uchaguzi mkuu si la wapinzani pekee, bali vyama vyote vinavyoshiriki.
Dk Slaa alikuwa akizungumzia kauli za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akidai kuwa kuna vyama vinahubiri vurugu na uchochezi na kuwataka viongozi wa vyama hivyo kuacha na badala yake wanadi sera zao.
Jana, Dk Slaa aligeuka mbogo na kusema kuwa damu imeshaanza kumwagiza kwenye baadhi ya maeneo kutokana na vurugu za CCM, lakini hadi sasa Kikwete amekuwa kimya.
“Jakaya Kikwete hatapona katika hili... damu za Watanzania zimeanza kumwagika Mwanza, Musoma, Hai, Mbeya, Iringa, Arusha na maeneo mengine na yeye yupo kimya kwa kuwa wanaomwaga ni CCM,” alisema Dk Slaa.
Alisema tangu ameanza ziara amejionea jinsi Watanzania wengi walivyokubali mabadiliko hivyo, kama ikitokea kura zao zikaibwa, wa kulaumiwa haitakuwa Chadema wala wapinzani, bali ni CCM.
“Jukumu la amani halipo kwa wapinzani pekee... tumeona damu inamwagika maeneo mengi na Kikwete yupo kimya; sasa naonya kama kweli hali hii ikiendelea na ajue amani inaweza kuondoka kwa kuwa haki ya wananchi inaporwa,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa pia alisema kuwa hagombei urais kwa lengo la kuwa afisa miradi anayeahidi kujenga barabara na zahanati, bali anataka kuongoza nchi.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu, ambaye amekuwa akieleza makombora yake kwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, aliuambia mkutano wa hadhara uliofurika kwenye Uwanja wa Bwawani, Karatu mkoani Arusha kuwa anataka kuwapatia Watanzania ukombozi wa kweli wa maisha yao.
“Mimi si afisa miradi au mipango wa kusema mkinichagua nitajenga zahanati, nitajenga, barabara nitanunua Bajaj," alisema Dk Slaa akionekana kumlenga mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akitoa ahadi za kujenga barabara, hospitali na kununua pikipiki za magurudumu matatu ili zitumike kubeba wagonjwa.
"Hiyo siyo kazi yangu (rais) kwa kuwa yote hayo yapo katika mipango ya serikali na mgombea yoyote atakayeshinda atatekeleza,” alisema Dk Slaa.
Alisema ahadi nyingi ambazo zinatolewa sasa na Kikwete tayari zilipangwa na serikali na Bunge lililopita hivyo kuahidi kuzitekeleza sasa ni kuwadanganya wananchi.
“Mpango wa ununuzi wa meli mpya kwenye Ziwa Victoria ulikuwepo, miradi hiyo ya Bajaj ilikuwepo na hata hili la elimu ya sekondari si mpango wa CCM uliigwa na serikali,” alisema Dk Slaa.
Katibu huyo mkuu wa Chadema aliwataka wananchi kupuuza matokeo ya tafiti za kura zilizofanywa na Redet akisema kuwa ukweli halisi unajulikana na utaonekana siku ya kupiga kura Oktoba 31.
Katika mkutano huo. Dk Slaa aliwaomba wakazi wa Karatu kumchagua mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji Israel Natse na wagombea wote wa udiwani huku wakihakikisha wanalinda kura zao.
“Mwaka 2005 waliniibia kura na nyie mnajua na hata mahakama ilikiri hivyo naomba mwaka huu mlinde kura wasiibe tena,” alisema Dk Slaa.
Mgombea huyo kesho atakuwa na mikutano kwenye miji ya Monduli mkoani Arusha, Hai, Moshi na mkoani Tanga.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment