Edwin Mjwahuzi na Victor Kinambile, Nzega
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa, ameahidi kuwalipa mafao yao wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ndani ya siku 100 kama akichaguliwa kuwa rais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.
Slaa aliyasema hayo jana kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Polisi, eneo la Uzunguni, mjini Nzega mkoani Tabora.
"Nimesikitishwa sana baada ya kuona taarifa inayowaonyesha wazee hawa wakipingwa na kunyanyaswa kwa kumwagiwa maji ya kuwashwa na polisi baada ya kuziba barabara ya Kivukoni jijini Dar es Salaam juzi (Ijumaa) kwa sababu ya kudai fedha zao," alisema na kuongeza:
Wastaafu hawa wanadai fedha ambazo zilishalipwa na Serikali ya Uingereza ambazo ni Sh117 billioni, polisi wanakuja na magari yao kuwatawanya kwa kuwamwagia maji,”.
Wazee wa hao walifunga barabara hiyo kwa mara ya pili baada ya Mahakama Kuu kuahirisha kesi yao ya madai ya mafao ambapo iliwalazimu Jeshi la Polisi kuwatawanya na baadhi yao kuwakamata.
Dk Slaa alisema anaishangaa Serikali ya Awamu ya Nne kwa kudharau kauli ambayo ilitolewa bungeni kipindi cha Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba aliposema wameshatenga pesa kwa ajili ya kuwalipa wastaafu hao.
"Pindi nitakapoingia madarakani ndani ya siku 100 nitahakikisha malipo yote ya wastaafu hayo yanalipwa na wale waliokula pesa yao zitawatokea puani,” alisema
Alisema ni laana kuona wazee wanadhalilishwa kwa kupigwa na kusumbuliwa wakati muda huu wanatakiwa wapumzike majumbani mwao.
Pia Dk Slaa aliwasihi wananchi wa mjini Nzega wadumishe amani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu waachane na mambo ya ugomvi hata kama akatokea mtu au kikundi cha watu kikataka kuwafanyia fujo wawapuuze.
"Akitokea mtu akakupiga shavu la kushoto mgeuzie na kulia kisha ondoka, ila ikifika siku ya kupiga kura lipiza kwa kuchagua viongozi wa Chadema ndio wapenda amani,"alisema
Alisema Nzega ina madini ya kutosha, lakini wananchi wanashindwa wayauze wapi hivyo akichaguliwa atahakikisha anajenga soko kubwa la kudumu ambalo litasaidia uuzwaji wa madini wilayani hapo.
“Hakuna soko kubwa hapa hivyo mkininchagua lazima nilijenge kwani kama madini yapo tunashida gani sisi Tanzania matajiri bwana, lazima nilijenge soko liwe mfano hapa Nzega,”alisema Dk Slaa.
Mbali na soko hilo aliongeza kuwa wakulima watapata fursa ya kusindika mazao yao wilayani hapo na sio kupeleka nje ya mkoa kama inavyofanyika kwa sasa.
Mgombea huyo wa urais alisema anazihitaji sana kura za wafanyakazi ili wamuunge mkono aweze kuingia Ikulu.
Alisema atahakikisha akiibiwa kura anatumia vijana wake kujua kura zilizoibiwa zimeenda wapi, lakini hawezi kutangaza vita kamwe.
Wakati huo huo, umati mkubwa wa wananchi walijitokeza katika miji ya Ndala, Nzega na Kahama kumlaki mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Slaa ambapo shughuli mbalimbali za kijamii za hospitali, misa makanisani na baadhi ya vyuo katika maeneo zilisimama.
Akiwa katika Kijiji cha Ndala, Dk Slaa misa za kanisani katika eneo hilo ambalo ni la misheni ya Kanisa Katoliki zilisimama kutokana na kelele na nderemo zilizokuwapo na hivyo kuahirishwa hadi alipomaliza mkutano.
Huduma za matibabu katika hospitali ya misheni ya eneo hilo pia zilisitishwa kwa muda na kuendelea baada ya yeye kuondoka kutokana na sababu hizo za kelele.
Mjini Nzega wananchi walikuwa na shauku la kumuona mgombea huyo ambapo walijitokeza kwenye uwanja huo wa Polisi tangu saa tatu asubuhi wakimsubiria mpaka alipowasili kwa kutumia helikopta yake muda wa saa saba mchana.
Dk Slaa aliwasili kwenye uwanja huo akiwa na mchumba wake, Josephine Mushumbusi ambapo wananchi hao walimkimbilia wakitaka kumshika mkono, lakini walinzi wake walijaribu kuwazuia kwa lengo la kulinda usalama wa mkono wake wa kushoto asije ukatoneshwa.
Katika hatua nyingine, akiwa wilaya ya humo alisababisha waumini wa KKKT kukatiza misa, pia huduma katika hospitali ya Nzega kusimama kwa muda kwenda kumsikiliza Dk Slaa akinadi sera zake.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment