Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; Tarehe: 8th October 2010 @
ZIARA ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa aliyoifanya Sumbawanga Mjini, imeonesha mwelekeo kwamba jimbo hilo huenda likatua mikononi mwa Chadema iwapo CCM haitajipanga upya.
Wakati hali ikiwa hivyo mkoani Rukwa, mkoani Arusha mgombea ubunge wa chama hicho Arusha Mjini, Godbless Lema, amekamatwa kwa tuhuma za utapeli na amehojiwa pia kwa tuhuma nyingine za kutishia kuua.
Kutoka Sumbawanga, habari zinasema baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walidai kuwa ziara ya Dk. Slaa juzi na jana, imetoa taswira kuwa CCM inahitaji kujipanga upya ili kulinusuru jimbo hilo.
Zilisema CCM tayari ina mpasuko wa kisiasa ambao ulijitokeza baada ya kumteua Aieshi Hilaly kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Mpasuko huo umesababishwa na kundi la wazee maarufu mjini humo, ambao ni makada wa chama hicho, kutoafiki uteuzi huo na kuelekeza nguvu zao Chadema ili inyakue jimbo hilo, hali ambayo imechangia Chadema kupata nguvu kubwa ya kisiasa.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Mkoa wa Rukwa, Said Goha, alikiri kuwa ujio wa Dk Slaa umeiongezea nguvu Chadema na kusema kazi ni kubwa na ngumu, lakini bado CCM itaibuka na ushindi kwenye jimbo hilo.
“Mimi sina muda mrefu sana kikazi, lakini hata wenyeji wanakiri kuwa haijawahi kutokea katika historia za kisiasa kuwapo mwamko na msisimko ulioonekana kuunga mkono upinzani wakati wa ujio wa Dk Slaa.
“Lakini naamini wakimpa fursa mgombea wetu, ana uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko, tofauti na watu wanavyodai,” alisema Katibu huyo wa UVCCM.
Chadema imemsimamisha Norbert Yamsebo msomi na mwanasiasa wa siku nyingi aliyetokea CCM, hali ambayo imeleta upinzani mkali miongoni mwa vyama hivyo.
Kutoka Arusha John Mhala anaripoti, kwamba Polisi inamshikilia Lema kwa tuhuma za kujipatia Sh milioni moja kwa njia ya udanganyifu na atahojiwa pia kwa tuhuma za kutishia kuua.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Basilio Matei jana alithibitisha kushikiliwa kwa mgombea huyo, baada ya kufunguliwa mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia hiyo na mlalamikaji Maimuna Lema, wa Sakina jijini humo.
Matei alisema mashitaka hayo yanaonesha kuwa mgombea huyo alijipatia fedha hizo Mei 22 mwaka huu, kwa madai ya kukombolea mzigo wake wa biashara.
Alisema katika makubaliano na mdai, mgombea huyo aliahidi kurejesha fedha hizo baada ya muda mfupi kwa kukabidhi kadi ya gari alilodai ni lake aina ya Toyota Hilux namba T140ABK ambalo baadaye liligundulika kuwa mali ya Joseph Mangilima.
Alisema baada ya wiki moja waliyokubaliana kurejesha fedha hizo kumalizika, mlalamikaji alimfuata Lema kumtaka amlipe lakini alianza kumzungusha ndipo akamweleza kuwa atamripoti Polisi.
Kamanda Matei aliendelea kusema kwamba baada ya kuelezwa kuwa atafunguliwa mashitaka Polisi asiporejesha fedha hizo, Lema alimtaka malalamikaji huyo kutofanya hivyo, kwa kuwa atamharibia katika kinyang’anyiro cha ubunge.
“Huyu jamaa ni mjanja sana, baada ya kuona anasumbuliwa juu ya madai hayo, alimtaka mlalamikaji huyo kuacha kufungua mashitaka kwa kuchelea kumchafulia katika ubunge,” alisema Kamanda Matei.
Alisema baada ya kukagua kadi hiyo ya gari, ilibainika kwamba halikuwa mali yake bali la Mangilima kutokana na kukosekana kwa maandishi yoyote yanayoonesha mgombea huyo kulimiliki.
Kamanda Matei alisema mbali na kumshikilia mtuhumiwa kwa madai hayo, Polisi pia imemhoji juu ya tuhuma za kutishia kumuua Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Arusha, Estomii Chang’a, ofisini kwake.
Alisema kumbukumbu zinaonesha tukio hilo lilitokea wiki mbili zilizopita.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment