Wednesday, September 8, 2010

Chadema: Hatutaki siasa za maji taka

Na Waandishi wetu
8th September 2010


Wasema wanakwenda kwa umma
Mume wa Josephine aenda kortini




Mgombea urais kupitia chama cha CHADEMA, Dk. Willibroad Slaa.


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakina muda na siasa za majitaka na kimefunga mjadala kuhusu ndoa ya mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. Willibroad Slaa.
Chadema ilisema mjadala na hoja zinazotolewa kuhusu suala hilo ni muendelezo wa kile kilichoelezwa kuwa ni `siasa za majitaka' kauli iliyoasisiwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Sitta alitumia kauli hiyo kujibu mapigo ya kundi la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) za kumzushia kashfa zisizokuwa na msingi.

Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema jana kuwa chama hicho kinakabiliwa na kazi ya kutafuta ridhaa ya wananchi, ili kishughulikie mambo yenye maslahi kwa jamii.

Tunayaangalia matatizo yanayowakabili Watanzania na kutafuta ridhaa ya kuiongoza nchi, tumefunga mjadala kuhusu suala hilo,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Lissu, alisema Chadema italizungumzia suala hilo ikiwa litafikishwa mahakamani.

Alisema chama hicho kina orodha ya uchafu na vimada wa wagombea wa urais wa vyama vingine (hakuwataja), lakini hawajawazungumzia jukwaani kwa vile hayana maslahi kwa Watanzania.
Lissu alisema kuna mambo binafsi kadhaa ya baadhi ya wagombea urais, ikiwemo matatizo ya afya yanayojulikana chanzo chake, lakini Chadema haiwezi kuyazungumzia jukwaani ama kuyatumia kama njia ya kupata kura.

Hatutaki hata kuzungumzia ‘status’ ya ukimwi kwa baadhi ya wagombea, ana wake wangapi, ana vimada wangapi...nani anakwenda nje kubadilisha damu kila miezi sita, hatutazungumzia siasa za chumbani kama wanavyotaka tufanye, kwa sababu hayatatatua matatizo tuliyonayo,” alisema.
Alisema mambo mengine yenye umuhimu kwa jamii na ambayo Chadema inawajibika kuyazungumzia ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Lissu alisema chama hicho kitaendelea kuzungumzia mustakabali wa taifa ikiwemo wizi unaofanywa na vigogo wa serikali ikiwemo upotevu wa Sh. bilioni 772 zilizoelezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2007/2008.

Naamini kabisa kwamba Watanzania wanahitaji kufahamu kwa nini hawapati elimu bora, kwa nini mama wajawazito wanakufa wakati wa kujifungua, kwa nini wao ni masikini wakati Tanzania ina rasilimali lukuki,” alisema.

Ninaamini pia kuwa Watanzania hawako tayari kukimbilia kwenda kuangalia huo mtaro wa maji machafu…wanataka kuleta yale waliyomfanyia Mrema (Lyatonga), mwaka 1995, yale ya Frederick Sumaye na mashamba yake na yale Salim na kaka yake wa Oman,” alisema.

Mwaka 2005 Mrema alizushiwa kashfa ya kuzaa na kumtelekeza mwanamke aliyejulikana kwa jina la Angelina Mosha (marehemu).

Pia aliyekuwa miongoni mwa wana-CCM waliotaka kuteuliwa kuwania urais mwaka 2005, Dk. Salim Ahmed Salim, alizushiwa kuwa mwarabu na kwamba alikuwa na ndugu zake huko Oman.
Lissu aliongeza kuwa sheria haitaji sifa za mgombea urais katika suala la ndoa “kwamba awe na wake wangapi au mke, mahawara au asiwe nao.”

Alisema Dk. Slaa amezushiwa tuhuma hizo kwa kuwa ameonekana kuwa tishio kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk. Slaa ana ‘record’ nzuri, amekuwa sauti kuu kwa maslahi ya taifa bungeni, sio mla rushwa, kwa hiyo wameona waingie chumbani kwake kwa sababu hawawezi kumkamata kwenye rushwa,” alisema.
Alisema baadhi ya watu walizusha kwamba Chadema ni chama cha Wachaga, Dk. Slaa ametumwa na kanisa Katoliki na sasa wameamua kuingia kwenye masuala yake binafsi baada ya kukwama kwenye hoja hizo za awali.

Dk Slaa afunguliwa kesi mahakamani
Wakati huo huo, shauri la madai limefunguliwa jana Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam na Aminiel Chediel Mahimbo, akimtaka Dk. Willibroad Slaa amlipe fidia ya Sh. bilioni moja.

Mahimbo anamtuhumu Dk. Slaa ambaye ni mgombea urais kupitia Chadema, kuwa amemnyang'anya' mke, Josephine Mkatunzi Mushumbusi.

Kesi hiyo ilifunguliwa jana kwa niaba ya Mahimbo na kampuni ya uwakili ya Amicus kupewa namba 122 ya mwaka 2010.

Mahimbo alifafanua katika madai yake kwamba katika fedha anayodai, Sh. milioni 200 ni ya maumivu maalumu na Sh. milion 800 ni ya kufidia kitendo cha mlalamikiwa kumpunguzia hadhi na heshima mbele ya jamii.

Aidha, Mahimbo alidai kuwa, Septemba 7, 2002, alifunga ndoa ya Kikristo na mwanamke huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), usharika wa Kijitonyama na waliishi sehemu mbalimbali hapa Dar es Salaam ikiwemo Kimara Baruti.

Alidai kwamba ndani ya ndoa yao, walifanikiwa kupata watoto wawili, Upendo aliyezaliwa Mei mosi 2003 na Preciuos aliyezaliwa Machi, 14, 2007.

Vivuli vya vyeti vya ndoa na vile vya kuzaliwa watoto hao vimeambatanishwa.
Pia alidai kuwa ndoa yao bado ni halali kwa kuwa haijawahi kutenguliwa.
Aidha alifafanua kuwa mwanzoni mwa mwaka huu, mkewe alianza safari za mara kwa mara, kitendo kilichosababisha asiwepo nyumbani kwao kwa muda mrefu.

Mahimbo alidai kwamba aliamini kuwa safari hizo zilitokana na kuongezeka kwa shughuli za mkewe, kwani ni mfanyabiashara anaeendesha kampuni iitwayo Green World Clinic.
Aliendelea kudai kwamba, mlalamikiwa amemtambulisha Mushumbusi kama mkewe kwa tarehe na sehemu tofauti.

Vivuli vinavyoihusu habari hiyo katika magazeti mbalimbali vimeambataishwa.
Pia alidai kuwa mahusiano ya kingono kati ya mlalamikiwa na mke wake yamemdhalilisha, yamemhuzunisha, yamemshushia hadhi mbele ya jamii, hivyo kupata maumivu maalum.

Chadema kumshitaki JK kwa umma
Chadema kimeuchambua uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, uliotupilia mbali pingamizi lao dhidi ya mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Chama hicho kimesema uamuzi wa Tendwa umetolewa kwa misingi ya kisiasa zaidi kuliko kisheria.
Tamko hilo limetolewa na Chadema ikiwa ni siku moja baada ya Tendwa kutupilia mbali malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi yake na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika, Agosti 30, mwaka huu.

Katika malalamiko hayo, Chadema walitaka Rais Kikwete aenguliwe katika orodha ya wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, kwa madai ya kuvunja Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 wakati wa kampeni za CCM zinazoendelea hivi sasa.

Wakili wa Chadema Mabere Marando, alitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari jana.
Kwa maoni yetu sisi ni kwamba, Tendwa alitoa maamuzi ya kisiasa na siyo uamuzi wa kisheria,” alisema Marando, ambaye pia ni mjumbe wa timu ya kampeni za uchaguzi za chama hicho.
Alisema Sheria ya Gharama za Uchaguzi, imempa Msajili madaraka yanayomfanya kuwa mfano wa ‘nusu mahakama’, hivyo kiutaratibu anawajibika kufuata misingi ya kubadilishana malalamiko kabla hajatoa maamuzi yake.

Kutokana na hali hiyo, alisema baada ya Chadema kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi ya Msajili, CCM walipopeleka majibu yao, kisheria Tendwa aliwajibika kuwapelekea Chadema majibu hayo ya CCM na kuwapa fursa ya kuyajibu.

Hata hivyo, alisema mpaka jana Tendwa alikuwa hajawapelekea majibu hayo ya CCM, ambayo alisema ni haki yao kuyapata na kuyasemea chochote kama inabidi, kwa vile wao ndio waliofungua kesi kwake.
Alisema pia, katika malalamiko yake, Chadema waliwasilisha ushahidi, CCM wakatoa majibu, lakini katika uamuzi wa Tendwa, hakuna popote panaposema kwamba CCM walipeleka ushahidi wowote kwake.

Sisi ushahidi tulioupeleka amesema katika hukumu hiyo, wameleta magazeti haya, na haya na haya. Lakini upande wa CCM, Tendwa hakusema kwamba, walijitetea kwa ushahidi huu katika kutujibu,” alisema Marando.

Pia alisema katika uamuzi wake, Tendwa amefanya jambo, ambalo ni kinyume cha sheria juu ya watu wanaofanyia maamuzi malalamiko au kesi kwa kutamka kwenye uamuzi wake kuwa amejitafutia ushahidi yeye mwenyewe, aliouita “utafiti”.

Alisema kwa jinsi wanavyomfahamu Tendwa, hawana shaka kwamba, aliomba serikali impe mambo aliyotaka kuyatumia katika uamuzi wake.

Tulijua kwamba, na Ngwilizi aliwahi kusema Jangwani kwamba, Tendwa hana ubavu wa kufanya maamuzi sahihi ya kisheria. Utafiti huu kwa kuwa hakueleza ameufanya utafiti namna gani, na tunajua ofisi ya Tendwa ilivyo, bila shaka alikwenda kwa Kikwete ili aweze kumjazia jazia sehemu, kumzibia zibia mashimo ili afikie uamuzi ambao ameufikia sasa,” alisema Tendwa.

Alisema hali hiyo inathibitisha kwamba, Tendwa hakuwa na nia ya kufanya uamuzi wa kisheria tangu mapema.

Marando alisema jambo lingine la msingi la kisheria, ni kwamba Tendwa amejiongezea tafsiri katika sheria ili maamuzi yake yaweze kuunga mkono CCM.

Alitoa mfano wa ahadi ya Rais Kikwete katika kampeni ya ununuzi wa meli katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Tendwa katika ukurasa wa 24 wa uamuzi wake alisema ahadi hiyo inatokana na ilani ya CCM.

Hata hivyo, Marando alisema kwa mujibu wa nukuu ya Tendwa, ilani ya CCM inasema: mojawapo ya ahadi zao ni ‘kuendeleza huduma za uchukuzi kwenye maziwa kwa kuimarisha Bandari za Kigoma, Mbamba Bay, Mwanza, Bukoba na Nansio’ na kwamba, katika kipengele hicho, hakuna ahadi ya meli mpya katika maziwa hayo.

Lakini kwa makusudi kabisa Tendwa akapanua tafsiri ya maneno ‘uchukuzi kwenye maziwa’ ili zile ahadi za meli za Kikwete ziingie katika ahadi ya kwenye ilani ya CCM. Ni makusudi tu kama mwanasheria aweze kuibeba CCM katika kutushinda sisi,” alisema Marando.

Alisema kuhusu Sh. bilioni 5, ambazo Rais Kikwete ameahidi kukilipa Chama cha Ushirika cha Nyanza na vyama vingine vya ushirika, Marando alisema Tendwa katika ukurasa wa 23 amenukuu sehemu ya ilani ya CCM inayosema:

Ili kuendeleza ushirika, katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2010-2015) CCM itaielekeza serikali kutekeleza yafuatayo: Kusimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya ushirika na programu mbalimbali za kuendeleza sekta ya ushirika.”

Alisema Tendwa amechukua kipengele hicho na kukiingizia tafsiri kwamba, ilani ya CCM inamhusu Rais Kikwete kuahidi kulipa madeni ya Nyanza na kubeba madeni ya vyama vya ushirika yanayotokana na fedha za wananchi.
Kwa tafisiri hizi za Tendwa, ni kwamba ameruhusu Kikwete kutoa ahadi ambazo, kwanza hazimo katika ilani…,” alisema.

Alisema katika uamuzi wake, Tendwa anasema sheria ya Gharama za Uchaguzi inayozuia kushawishi watu kumpigia kura mgombea kwa njia za hongo, ametafisiri kwamba maana ya ‘kushawishi’ na ‘hongo’ ni kufanya mambo hayo kisirisiri gizani.

Kuhusu nyongeza ya mshahara kutoka Sh. 135,000 kima cha chini hadi sh. 235,000 iliyotangazwa na Rais Kikwete, alisema majibu ya CCM yaliyomo kwenye uamuzi wa Tendwa, yanasema serikali haijaongeza mshahara kima cha chini.

Alisema Tendwa alikwenda mbali zaidi na kudiriki kumnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Hawa Ghasia, kuunga mkono jambo hilo, wakati si kweli.

Marando alisema kutokana na hali hiyo, kuna njia mbili mbadala chini ya sheria hiyo, moja ni kwenda mahakamani hivi sasa kuomba marejeo ya maamuzi hayo ya Tendwa.
Nyingine ni kufungua kesi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Kuhusu njia ya kwanza, alisema amewashauri viongozi wa Chadema kwamba kwenda mahakamani kuomba marejeo haina uhakika kama uamuzi utatoka kabla ya kampeni hazijaisha.
Alisema hofu inatokana na hivi karibuni kushutumiwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan, kwamba hataki aongee mambo ya mahakamani nje ya mahakama.

Hivyo alisema hana uhakika kwamba, kama watapokea na kushughulikia marejeo yao haraka na Rais Kikwete aondolewe katika kampeni kabla ya Oktoba 31, mwaka huu.

Kuhusu njia ya pili, alisema Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inaruhusu kufungua kesi, lakini inapingana na Katiba ya nchi, ambayo inatamka kwamba, uchaguzi wa rais hauwezi kulalamikiwa mahakamani baada ya kutangazwa mshindi.

Hiyo njia pia tutaitafakari baadaye kwa sababu pia tunaweza kuamua kwamba tusi-challenge kutangazwa kwake lakini tunaweza kwenda mahakamani kuomba tamko la mahakama kwamba vitendo alivyotenda kwa mujibu wa sheria hii alipanga,” alisema.

Aliongeza, “tunaweza kufanya hivyo baada ya uchaguzi, lakini hiyo njia kwa sasa siwezi kuifikiria sana kwa sababu naamini Slaa atamshinda Kikwete,” alisema Marando.
Tunaendelea kumshitaki katika mahakama ya umma, kuwaomba wasimpigie kura kwa sababu haaminiki,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kampeni za Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema kwa vile wanajivunia nguvu ya umma, mambo yote hayo wanayarudisha kwao.

Chadema ilidai kwamba Rais Kikwete akitumia nafasi yake ya urais, aliongeza au kuahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kwa kupandisha kima cha chini kutoka Sh. 135,000 hadi Sh. 235,000.
Pia aliahidi kulipa Chama cha Ushirika cha Nyanza Sh. bilioni 5 ili kilipe madeni ambayo kinadaiwa na kuahidi kuwa serikali itachukua madeni yote ya vyama vya ushirika.

Pia, Rais Kikwete aliahidi watu wa mkoa wa Kagera kununu meli mpya kubwa na ya kisasa zaidi itakayotumiwa na wananchi wa mkoa huo na wengineo kusafiri kati ya Bukoba na Mwanza.

Chadema ilidai kuwa vitendo hivyo vimekatazwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa madai kwamba vilikuwa na nia ya kushawishi wafanyakazi kama wapigakura kumpigia kura Rais Kikwete kutokana na nyongeza hiyo ya mishahara, kushawishi wananchi wa kagera na Mwanza wanaotumia usafiri wa meli katika Ziwa Victoria kumpigia kura.

Habari hii imeandikwa na Restuta James na Elisante John, Singida na Muhibu Said na Raphael Kibiriti wa SJMC, Dar es Salaam.




CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment