Tuesday, September 7, 2010

Uchaguzi wa wabunge: Tuchague ujana wa moyo dhidi ya umri


Godfrey Dilunga
Septemba 1, 2010

VYAMA vya siasa, hasa vinavyoaminika kuwa na nguvu ya kisiasa nchini vimepania kupata idadi kubwa ya wabunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Vyama hivyo pengine vimepania hivyo kwa gharama yoyote. Ikibidi kuhujumu demokrasia na hasa mchakato wa kupiga na kuhesabu kura. Kila chama kipaumbele chake ni kupata wabunge wengi.

Katika mazingira ya kawaida, kutwaa madaraka ndiyo lengo la msingi la chama cha siasa. Lakini kwa upande wa mpiga kura, lengo la msingi si kukiwezesha chama kutimiza ndoto hiyo kienyeji au kiholela.

Fikra za mpiga kura zinapaswa kutangulia ndoto hizo. Wakati chama kikilenga kupata wingi wa wabunge, mpiga kura anapaswa kufikiri namna ya kuwezesha nchi (sio chama cha siasa) kupata wabunge bora na makini.

Kwa kadiri changamoto za kidunia zinavyoshika kasi, mpiga kura wa Tanzania anapaswa kufikiri, kupigania na kuhakikisha nchi inapata wabunge bora na makini.

Mpiga kura anapaswa kuitazama nchi na si chama cha siasa wakati akielekea kumchagua mbunge. Matakwa ya wakati yanalazimu wapiga kura kuchagua ubora dhidi ya wingi.

Tuchague wingi wenye ubora na si wingi wa idadi. Na kwa mantiki hii ya wingi wenye ubora dhidi ya wingi wa idadi, chama kilichoteua wagombea bora na makini ndicho kinastahili.

Jiulize mpiga kura, umepania nini katika Uchaguzi Mkuu huu? Je, umepania kuongeza idadi ya wabunge wa chama chako bila kigezo cha ubora na umakini?

Kama umepania hivyo, kura yako haitajenga mustakabali bora wa Taifa. Kura yako ni kikwazo kwa ustawi wa Taifa.

Kura yako ni usaliti na kwa hiyo utakuwa msaliti wa Tanzania iliyokusudiwa na waasisi wake. Utakuwa msaliti. Msaliti dhidi ya mchakato wa kujenga Tanzania yenye mustakabali unaotabirika.

Kama nilivyoeleza awali, ni dhahiri, vyama vya siasa vimepania kupata wingi wa wabunge. Wamepania kupata wingi dhidi ya ubora ikibidi.

CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na vyama vingine vinataka idadi kubwa ya wabunge. Wanatamani hivyo bila hata kujali katika baadhi ya maeneo hawajateua wagombea kwa kigezo cha ubora na umakini.

Wanatarajia mavuno tofauti na mbegu walizopanda. Katika baadhi ya majimbo kwa kuzingatia kigezo cha umakini na ubora, vipo vyama vimepanda bangi vikitarajia kuvuna mtama.

Kwa mantiki hiyo, mpiga kura anapaswa kuing’oa mbegu hiyo ya bangi inayokusudiwa kuoteshwa jimboni mwake kwa kuinyima kura. Hivyo basi, hapaswi kuchagua kwa kuzingatia uanachama, urafiki au ushabiki.

Uanachama hauna maana kwenye Uchaguzi Mkuu kwa sababu inayotumika kupiga kura si kadi ya chama, ni kadi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Sheria zote za Uchaguzi hazitambui mpiga kura kwa kadi yake ya chama, ushabiki au urafiki wake na mgombea. Sheria zinatambua kitambulisho cha kura. Kitambulisho cha Tanzania si chama.

Kwa mantiki hiyo, hupaswi kuisaliti Tanzania kwa kuchagua mgombea wa ovyo eti kwa sababu anatoka kwenye chama chako.

Tuchague mgombea bora si mgombea wetu au mgombea wao. Tuchague mgombea makini si mgombea wa chama chetu au chama chao. Tumchague Mtanzania si mwana-CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi.

Tuingie kwenye Uchaguzi tukiwa na dhana kwamba mgombea bora na makini jimboni ni mgombea huru (binafsi). Ubora na umakini wake umemfungua kamba za chama au itikadi.

Kiwewe cha vyama kupata wingi wa wabunge bila ubora kisiathiri fikra zako mpiga kura. Maslahi ya mpiga kura yanahifadhiwa, kulindwa na kutetewa kwa kadiri ya ubora na umakini wa aliyechaguliwa.

Kwa vyovyote, mgombea bwege kwa kigezo cha ubora, umakini na uadilifu ataendeleza ubwege huo ndani ya Bunge au popote madaraka hayo yatakapolazimu kutumika.

Tunapomchagua mgombea bwege kwa kigezo cha ubora, umakini na uadilifu, tafsiri inayojitokeza ni wapiga kura husika kuingia kwenye kundi hilo.

Jimbo husika litakuwa limeingia katika rekodi ya kuwa na wapiga kura wengi wasio na ubora, umakini na uadilifu.

Daima mpiga kura atanufaika kwa ubora wa mbunge aliyemchagua. Hivyo basi, wakati chama kinapigania wingi wa wabunge, mpiga kura pigania ubora, umakini na uadilifu. Ni uchaguzi wa ubora, umakini na uadilifu dhidi ubwege.

Ikimbukwe, hatuchagui wajumbe wa vikao vya chama cha siasa. Vikao ambavyo havina nafasi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunachagua wajumbe wa mhimili wa Taifa.

Kwa nini ugeuke mfano wa mchwa anayetafuna mhimili (nguzo) wa Taifa kwa kuchagua mbunge asiye bora, eti kisa ni kulinda maslahi ya chama?

Kwa lugha nyingine unafanikisha chama chako kugeuka mchwa anayetafuna mhimili wa Taifa. Mpiga kura, usikubali kuwa mchwa na kukiwezesha chama chako kuwa mchwa.

Kumbuka tunachagua mbunge. Tunachagua kiongozi wa dola anayeingia katika chombo nyeti, chenye mamlaka ya kuhoji, kubadili, kurekebisha, kuamua tuelekee wapi kwa niaba yetu.

Kutokana na uzito wa chombo hicho ni muhimu kuchagua ubora, umakini na uadilifu na si kinyume chake. Chama kilichopitisha wagombea wasio na ubora hakipaswi na hakistahili kuhurumiwa.

Wingi wa watu wasio na bora ndani ya Bunge, hauna mantiki ikilinganishwa na wingi wa watu wenye ubora ndani ya Bunge.

Tusibabaishwe na malengo ya vyama, tubabaikie malengo na mustakabali wetu kama wapiga kura. Kwa vyovyote vile, malengo na mustakabali wetu unapaswa kujikita katika ubora, umakini na uadilifu.

Tuviadhibu vyama vilivyopitisha wagombea mabwege kwa kigezo cha ubora, umakini na uadilifu. Tunawajua wagombea hao kwa sasa tunaishi nao vijijini au mijini.

Na kutokana na kuwajua, tudadisi ubora wao kwa kujibu swali kwamba: Je, mgombea husika ni mnafiki aliyetayari iwe usiku au mchana, hadharani au ufichoni kutelekeza maslahi ya wananchi ili kunusuru maslahi ya chama chake?

Wakati huu wa kampeni tumsake mbunge bora kati ya orodha ya wagombea kwa kuweka majina yao katika mzani wa maslahi ya chama dhidi ya wananchi.

Hatupaswi kuelekea sanduku la kura eti kuchagua mgombea kijana dhidi ya mzee, mwanamke dhidi ya mwanamume, mzoefu dhidi ya asiye na uzoefu. Tukachague mgombea bora.

Tuwatazame wagombea bora si kutokana na ujana au uzee. Umri kisiwe kigezo nambari moja. Na hapa tukumbushane maneno ya aliyekuwa Mke wa Rais wa Umoja wa Kisovieti, Michael Gorbachev, Raisa.

Raisa Gorbachev ambaye alipata umaarufu mkubwa kwenye jukwaa la kimaitaifa, akitajwa kuimarisha haiba ya mumewe katika medani za uongozi, aliwahi kuchambua mantiki ya umri kwa kutafsiri ujana.

Mhadhiri huyo wa Sosholojia aliyefariki mwaka 1999 kwa saratani ya damu (leukaemia) aliwahi kueleza kuwa ujana bora ni ule wa moyoni. Ujana bora si umri.

Kwa hiyo mwenye mvi anaweza kuwa kijana moyoni katika mantiki ya utumishi uliotukuka, umakini, uadilifu na ubora wa kupigiwa mfano.

Hivyo ndivyo Raisa ambaye alipata kuandika kitabu maarufu kilichoitwa Tumaini (Hope), mwaka 1991 kikieleza masuala ya kale na marejeo yake, anavyotafsiri ujana katika mantiki murua.

Kwa ujumla, tuchague mgombea bora. Mgombea kijana moyoni na si kijana kwa umri. Ubora na umakini wa tutakayemchague kuwa mbunge ndiyo ubora na umakini wetu wapiga kura. Ukichague asiyefaa na wewe pia hufai.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Simu:
0787-643151


0 comments:

Post a Comment