Sunday, October 3, 2010

Tamko la Msajili wa Vyama vya Siasa limechelewa

KATIKA ukurasa wa kwanza wa gazeti hili tumechapisha habari kuhusiana na kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, akiwaonya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bibile Fellowship, Zachary Kakobe na mtabiri maarufu Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein.

Tendwa aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa Askofu Kakobe na Sheikh Yahya wamekuwa wakitoa kauli ambazo zinahatarisha amani kwa taifa.

Alisema Askofu Kakobe katika mahubiri yake kutoa elimu ya uraia kanisani kwake, ni kitendo kinachoonyesha wazi amejiingiza katika kampeni za kisiasa na kusahau kazi yake ya kuwahudumia wana kondoo neno la Mungu.

Alisema viongozi wa dini, wanatakiwa kutoa elimu ya kiroho ambayo itawapa mwanga waumini wao ili waepukana na maovu na si kugeuza madhabahu kuwa uwanja wa siasa.

Alisema kitendo cha Sheikh Yahya kutoa utabiri wake kwa kupitia kipindi chake cha nyota kinachoonyeshwa na moja ya vituo vya televisheni jijini Dar es Salaam, kinaonyesha wazi kukipigia kampeni moja ya chama kati ya vyama viwili vyenye nguvu, jambo ambalo ni mwelekeo wa uvunjifu wa amani.

Alisema kitendo cha Sheikh Yahya kusoma nyota na kutoa utabiri, sasa kinaonyesha wazi kuhatarisha amani.

Alisema kitendo cha Sheikh Yahya kuendesha kipindi katika moja ya runinga nchini na kuonyesha kupendelea chama kimoja kati ya viwili vinavyochuana vikali hivi sasa, inaashiria wazi anakipigia debe chama kimoja wapo.

Tendwa amesema utabiri huo hauna faida kwa taifa, bali ni kwake, hivyo anapaswa kuacha kuwachanganya wananchi.

Lakini Tendwa hakuishia hapo, alikwenda mbali zaidi kuzitupia lawama baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikitoa taarifa za mgombea gani anaongoza kupendwa.

Sisi tunasema licha ya Tendwa kutotaja taasisi hiyo, ni ukweli usiopingika kuwa Kampuni ya Synovet ndiyo imekuwa ikitoa matokeo ya uchunguzi wao.

Katika matokeo ya hivi karibuni, taasisi hiyo ilitoa matokeo ambayo yanaonyesha mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, anaongoza akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Leo tumelazimika kuandika maoni haya kwa uwazi zaidi na kusema kauli hii Tendwa amechelewa kuitoa, kwani tafiti nyingi zimekwisha kutangazwa.

Tumeshangazwa na hatua hii kwa sababu katika siku za karibuni watabiri wa nyota wamefikia hatua ya kusema wagombea wawili; Dk. Slaa na Jakaya Kikwete wakatabiliwa na kifo, lakini hatukusikia karipio kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa au Jeshi la Polisi nchini.

Sisi Tanzania Daima tunachukua fursa hii kuvitaka vyombo vya dola kuwa makini na utabiri au mafundisho mabovu yanayotolewa.

Tunamalizia kwa kusema, tumesikitishwa na ukimya wa Tendwa, kwani wote tunakumbuka jinsi tulivyosikia mtabiri wa nyota alivyowahi kusema kuwa yuko tayari kumuongezea ulinzi wa nguvu za giza Rais Kikwete ili asifuatwefuatwe na maadui zake.

0 comments:

Post a Comment