Sunday, October 3, 2010

Oktoba 31 tusiichague serikali ya buibui

“WALTER, mbona watawala wamezidisha ahadi?” hilo ni swali nililoulizwa na msomaji wa makala yangu.

Swali hilo ndilo linalonifanya nianze kupata mwangaza kuwa Watanzania hivi sasa wamepata mwaka wa masuala yanayogusa taifa
Ni mwamko huo ndiyo utakaowafanya wachague viongozi makini na wala si wale wenye kutoa ahadi ambazo miaka nenda miaka rudi hazitekelezeki.

Buibui ni mdudu anayesifika sana kwa kujenga utando wenye kuvutia. Ni bingwa na ukimkuta kazini akijenga, unaweza kudhani atajenga ghorofa. Lakini mwisho wa yote hujenga wavu tu usioweza kusitiri hata maungo wala mayai yake.

Buibui mara nyingi hutumia utando wake kuwanasa wadudu wachovu kama inzi na mbu wadogo, lakini wakati mtego wake huo akiusifia na kuuona mali, wadudu kama viwavi, dondora, kereng’ende hukata wavu wake na kupeta.

Nimeanza na mfano huu kwani ndio unaofanana kabisa na serikali ya sasa inayomaliza muda wake kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani hapo Oktoba 31!

Kabla ya kuingia madarakani mwaka 2005 mgombea urais kwa sasa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya kikwete alituahidi angetuondolea kadhia za rushwa, umaskini, ubabaishaji, utegemezi na mengine mengi.

Alituahidi kwa ari mpya, kasi mpya, na nguvu mpya huku akisema serikali yake ingelisafisha taifa lakini kwa hali ilivyo hivi sasa ameshindwa na badala yake amelichafua zaidi taifa.

Alituahidi angepambana na ufisadi na wezi wa fedha za umma achilia mbali umaskini ambao kimsingi husababishwa na majanga tajwa. Ajabu hivi leo, kama alivyo buibui, badala ya kutuonyesha alipojenga ili tusitirike anajenga utando (ahadi) ambazo ndizo zimetufanya maisha bora yetu tuliyoaahidiwa kuwa ndoto.

Wale watu wanaofanya uharibifu wa ufisadi, bado hadi sasa wanazidi kupeta na wanazidi kuubomoa utando wa Buibui huku mwenyewe akikodoa macho na kutoa kila aina ya visingizio.

“Nawapa muda wajirekebishe, mara oh ni ajali ya kisiasa” kauli kama hizi zinaonyesha namna kiongozi wetu alivyoshindwa kutimiza ahadi yake ya kuwakamata wanaotafuna rasilimali za nchi kwa manufaa yao.

Tunaona utando wa kuwanasa i-nzi (wala rushwa wadogo ), Kereng’ende na Manyigu bado wanaendelea kutuumiza huku yeye buibui akifanya nao shirika!

Kwa muda wa miaka mitano tumeshajifunza na tumeshaona ahadi zipi hazijatekelezwa na kwa nini zimeshindikana, Oktoba 31 mwaka huu ni jukumu letu tuchague watu safi wenye dhamira ya kupambana na ufisadi badala ya wale wanaonufaika na kuukumbatia.

Kwa wale wenye kumbukumbu watakumbuka siku si nyingi zimewahi kuripotiwa taarifa kuwa kuna fedha zilizokuwa zikitoka kuchapishwa Ujerumani, zikachotwa na wajanja. Ajabu habari ile haikupewa uzito wowote na vyombo vya habari, achilia mbali gazeti tafitishi la Thisday!

Japo hadi leo wapo watu wanaohoji kwa nini fedha zilichapiswa karibu na kipindi hiki cha uchaguzi? Kusema kweli mambo haya sasa yamekuwa mazoea ndani ya nchi yetu! Kila kukicha watu wanabuni namna ya kufanya ufisadi
Inatia kichefuchefu na hasira kuona hata wale viongozi tuliowaamini wangelinda na kuiweka nchi yetu kwenye hali nzuri na usalama, sasa wanaibomoa na kumezwa na ufisadi. Ni lazima tujiulize ni sababu zipi zitakazotufanya tukirudishe chama tawala madarakani.

Tukihoji chama hiki na serikali yake kuwa wako wapi mafisadi wakubwa? Watuonyeshe walipo akina Kagoda, Richmond na wengineo ambao walikwapua mabilioni ya fedha ambayo yanetumika kuboresha huduma muhimu za kijamii.

Ni jambo la kushangaza na kutia aibu kwa taifa kuendelea kuwaheshimu na kuwapa vyeo watawala waliotumia madaraka yao kuhujumu rasilimali za taifa kwa kuingia mikataba ya kinyonyaji.

Ni nchi pekee ambayo watu wanaiba halafu tume inayoundwa kuwachunguza ina mkono wao ambapo mwisho wa siku hutoa taarifa za kusafishana pasi na kuona aibu mbele ya jamii.

Mifano ipo mingi ya namna wanavyosafishana sina haja ya kutaja hapa. Tumeshuhudia juhudi za makusudi za kuzilinda kampuni za kitapeli za Meremeta, Deep green na nyinginezo ambazo zinasingiziwa kuwa ni za jeshi na matumizi ya fedha ilizopewa hayapaswi kujulikana hadharani.

Tujiulize wako wapi watuhumiwa tuliambiwa walishirikiana na watu wa nje kukwapua mabilioni ya rada ambao Serikali ya Uingereza ilishatueleza bayana kuwa tulilanguliwa.

Wito wangu kwa Watanzania wapenda nchi yao mwezi huu uwe ni wa kupambana na ufisadi kwa vitendo na si kwa kauli za kisanii kama ilivyozoelezaka.

Tupige kura ya ‘HAPANA’ kwa wote walioteuana kwa rushwa ili kulipana fadhila huku umma wa Tanzania ukiendelea kuzama kwenye umaskini wa kutupwa.

Tumeahidi kupelekwa nchi Kanani huku watu walewale wakiendelea kutuaminisha kwamba eti watatupeleka kanani, kumbe wanachokifanya sasa wanataka kutupeleka motoni!

Tusikikubali kuyumbishwa na maneno ya mmakada wa chama tawala ambao kila kukicha wamekuwa wakitoa propaganda za kulinda uovu uliofanywa na wenzao kwa nia ya kulinda heshima ya chama.

Wapo na wengine waliopitishwa kwa milango isiyo halali ili kwenda bungeni kutetea tena biashara kama zile za Richmond, Dowans na madudu mengine. Je, hawa wanapaswa kweli kwenda bungeni ili wakaibe tena na kuhatarisha usalama wetu zaidi?

Tukifanya kosa hili hatutastahili msamaha hata kidogo Oktoba 31, tusijaze wachumia tumbo katika ofisi zetu, mimi na wewe hebu tujiulize kwa nini kwa mfano hadi leo mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, kwanini bado yupo kwenye ofisi za umma na wakati alishahusishwa kwa kuibeba Richmond?

Je, mtu kama huyu anaweza kuifanyia nini nchi zaidi ya kuiangamiza? Cha ajabu serikali ile ile iliyotuaminisha 2005 ingetuvusha na kutupeleka Kanani ili tupate yale maisha bora hadi leo imegoma kumuwajibisha licha ya kuhusishwa na tuhuma hizo!

Kuirudisha serikali hii madarakani, si sawa na kumkaribisha chatu nyumbani ili amalize watoto wako? Au tujiulize serikali hii ina tofauti gani na mbwa anayewarudi watoto wake au fisi anayemla mwenzake?

0 comments:

Post a Comment