Sunday, October 3, 2010

Tuchague viongozi bila kuangalia vyama vyao vya siasa

Yahya Charahani

WATANZANIA wanaonyesha dalili za kuanza taratibu kukomaa kisiasa na pia wanaonekana kupenda mabadiliko kwa kuwa na viongozi waadilifu.

Mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaoendelea nchini kwa takribani mwezi mzima sasa, umeonyesha picha hiyo ambayo ni jambo la maana katika maendeleo ya nchi yetu.

Angalau mpaka sasa katika michakato mbalimbali tumeshuhudia ukomavu wa wananchi kushindana kwa hoja na kutoleteana fujo wa vurugu zisizo na maana kama ilivyokuwa wakati wa kampeni za chaguzi tatu zilizopita. Pia tunaona Jeshi la Polisi likitekeleza majukumu yake kutowabughudhi wanaohudhuria na kufuatilia kampeni za vyama mbalimbali.

Ni katika kampeni hizi ambapo tunaona ukomavu mkubwa wa jamii ya Watanzania. Asilimia kubwa ya wananchi, wasomi na wasiosoma wako huru kutoa hoja zao wazi wazi, kueleza mambo yanayowakera na wanasikilizwa siyo na vyama vyote vya siasa.

Wananchi wameonyesha kukomaa kisiasa kwa kubadilika kwa kasi na kujiondoa katika kuelemewa na mapenzi ya kivyama, badala yake wanasikiliza, wanachambua na kubainisha hoja zao.

Kwa kiasi kikubwa wanakosoa pale kwenye upungufu na kupongeza pale panapofanyika mambo mazuri, tunaanza taratibu kuepuka mapambano baina ya vyama kwa vyama na mashabiki kwa mashabiki.

Tatizo linabakia kwa upande wa wanasiasa ambao wanaonekana wanaelendeleza mambo ya kale kwa kupakana matope.

Jambo hili linapaswa kuachwa na badala yake wanasiasa wetu wajifunze kueleleza kampeni zao katika sera za maendeleo na namna ya kuitekeleza.

Kimsingi uamuzi wa kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na urais bara na visiwani, haustahili kufanyika kwa misingi ya rangi, kabila au dini.

Kwa maana hiyo Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulenge kuwachagua viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo wananchi na taifa kwa ujumla. Viongozi hao wanapaswa kuwa na nia isiyotiliwa shaka kuwa watawakwamua wananchi kutoka katika ufukara unaowakabili.

Kwa maana hiyo, Watanzania wenzangu, tusichague rais au viongozi kwa mazoea. Kama ni wa chama tawala anaonyeshe uwezo hali kadhalika kama wa chama cha upinzani ana uwezo achaguliwe ili aweze kulisaidia taifa hili kuingia katika karne nyingine ya maendeleo. Ni vizuri kubadilika kimawazo na mtazamo ili kulita mapinduzi yake kweli, kama Marekani walivyobadilisha historia ya nchi yao na dunia nzima kwa kumchagua Mmarekani mweusi, Barak Obama kuwa rais wa taifa hili kubwa na imara kiuchumi na nguvu ya kijeshi.

Nina hakika kama wangelikuwa na dhana ya mazoea na ubaguzi, Obama asingeota kuingia Ikulu hata siku moja. Suala la maendeleo ni suala pana ambalo halihitaji chama, dini wala kabila, bali linahitaji viongozi na wananchi wenye dhamira ya kutaka maendeleo.

Wakati umefika kwa watu wote wasiopenda siasa za kulumbana na za visasi, kuunga mkono siasa za maendeleo; bila kujali kabila, chama au hali. Kinachoshangaza ni kwamba, sasa hivi (wakati wa uchaguzi) zinajitokeza siasa za kuwahonga wapiga kura, vitisho kwa wananchi, uongo na hata za ushirikina ambazo ni kinyume cha maendeleo ya demokrasia nchini.

Tumaini jipya kupata viongozi sahihi na wenye nia ya kuliendeleza taifa letu, lipo kwa uchaguzi mkuu ujao ambao ukimalizika hatutausikia wala kuuona tena hadi mwaka 2015. Tumaini la kuwapima viongozi, sio kwa maneno yao tu; bali kwa matendo yao. Ni wakati wa kuwatambua kwa matendo yao.

Wanaohubiri kupinga dhuluma, huku nyuma wakishiriki na kushirikishwa kutoa rushwa ili wachaguliwe tuwatambue kwa matendo yao. Wale wanaojinadi kuwatetea wananchi huku wakiwazunguka, kisha kuwanyanganya ardhi na mali zao bila kuwalipa fidia inayostahili, pia tuwatambue kwa matendo yao. Baada ya hapo kura yetu iamue kwa haki kwa kumpa anayestahili.

*Yahya Charahani ni mchambuzi wa masuala ya jamii, siasa na utawala.

Anapatikana kwa email: charahani@yahoo.com This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
Blogu charaz.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment