Thursday, September 16, 2010

Dk Slaa: Tumechoka kupiga debe, sasa tunataka usukani

Tuesday, 14 September 2010 16:57

Dr Willibrod Slaa

Salim Said
KILA chama cha siasa lengo lake kuu ni kushika dola ili kupata fursa ya kutekeleza ilani yake.
Kila chama huwa kina mpango mkakati au mbinu za kutumia katika kuwahamasisha na kuwakampeni wananchi, ili wakichague chama husika na wasikichague chama kingine.

Chadema kwa kutumia mgombea wake wa urais Dk Wilibrod Slaa anasema, “Lengo langu ni kuing’oa CCM na kwa maana hiyo sina njia nyingine ya kufanikisha azma yangu zaidi ya kutafuta machafu yao na kuyaweka wazi kwa wananchi.”

Dk Slaa anataja sababu 13 zinazowapa Watanzania uhalali wa kuiondosha madarakani CCM, ili kuondokana na upigadebe ndani ya miaka 15 tangu mfumo wa vyama vingi uingie nchini.

Akizungumza katika mikutano mbalimbali ya kampeni Dk Slaa anasema umefika wakati wa Watanzania kuachana na upigadebe na kuipa Chadema usukani wa kuendesha gari kwa miaka mitano ijayo.
Akitaja sababu hizo, Dk Slaa anasema:

Sababu ya 1: Ni kwamba Rais Jakaya Kikwete amewatukana na kuwadhalilisha kinamama wa Tanzania kwa kuwaahidi kuwanunulia bajaji 400 ili kubebea wajawazito.

“JK amewatukana Watanzania, utamwekaje mama anayeumwa uchungu na hali ya bajaji ilivyo mpaka afike salama katika kituo cha afya. Lakini wakati waziri wake mwanamke akitembelea gari la Sh200 milioni anataka kuwapandisha bajaji Watanzania wanaotaka kuleta Watanzania wapya, amewadhalilisha,” anasema Dk Slaa.

Dk Slaa anasema kuwa ahadi hiyo ni hewa kwani alishaitoa bungeni wakati akizungumza na wabunge miaka mine iliyopita na hakuitekeleza.
“Kama ameshindwa kuitekeleza alipoitoa bungeni miaka minne iliyopita leo anaitoa tena, atawezaje kuitekeleza? Au atuambie kama bajaji hizi ni nyingine au ni zile zile alizoahidi 2006? Na kama ni nyingine je, zile alizipeleka wapi?” Anahoji Dk Slaa.

Sababu ya 2: CCM inapaswa kung’oka kwa sababu baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka madarakani walifuta Azimio la Arusha lililoleta umoja, upendo na kupiga vita ufisadi wakaja na Azimio la Zanzibar na kuwagawa Watanzania kimatabaka.

“Nimekaa bungeni kwa miaka mitano naomba nakala ya Azimio la Zanzibar nimeshindwa kuipata hata wazanzibari wenyewe hawana. Huu ndio mwanzo wa matabaka na ufisadi nchini,” anasema Dk Slaa.
Sababu ya 3: Tanzania hivi sasa inaongozwa na manyani wakubwa wanaoishi kwa kukwapua mali za watanzania bila ya huruma.

Anasema, “Hata baba wa taifa akifufuka leo na kuja kuona hali ya Tanzania ilivyokuwa mbaya kimatabaka katika kipato, basi atamuomba Mwenyezi Mungu afe ili arudi kaburini.”

“Makamba anasema natukana, lakini sina lugha nyingine ya kusema, fisadi ni fisadi tu na mwizi ni mwizi tu hana jina jingine, nimehangaika katika makamusi sijapata jina mbadala la mwizi” anasema Dk Slaa.
Sababu ya 4: Ni kuongezeka mara dufu kwa safari za nje za raisi Kikwete huku mabilioni ya watanzania yakipotea kwa safari hizo.

“Fedha zetu zinaisha kwa safari za nje, huku faida yake ikiwa ni chandarua hata dawa ya kupuliza hapati. Lakini nawambia watanzania ziara za JK hazijaleta faida yoyote katika uwekezaji nchini,” anasema Dk Slaa.

Anasema hamzungumzii rais kama cheo bali anamzungumzia mgombea wa CCM katika nafasi ya uraisi, hivyo anachofanya ni kumkosoa yeye na chama chake (CCM) na kueleza nini Chadema itafanya iwapo itashinda.

Sababu ya 5: Rais Kikwete aliahidi kujenga uwanja mpya wa ndege jambo ambalo hajalitekeleza hadi sasa miaka mitano imeisha na kwamba anakuja tena na ahadi kama hiyo.
“Nimezunguka mikoa yote na naendelea kuzunguka sijaona uwanja mpya bali viwanja vyote vya ndege ni kama malisho ya ng’ombe,” anasema Dk Slaa.

Sababu ya 6: Chanzo cha umasikini wa Watanzania ni wabunge wa CCM ambao wanashindwa kuwatetea Watanzania wanapokuwa bungeni.
Sababu ya 7: Rais Kikwete hafai kuwa rais tena kwa sababu hasomi na kwamba kila siku anarudia kuahidi mambo aliyoshindwa kuyatekeleza katika awamu yake ya kwanza.
“Utashangaa baadhi ya wakati anatoa ahadi ambazo alishazitoa na hajazitekeleza. Kama hii ya bajaji hata ukienda katika vitabu vya kumbukumbu ya bunge (hansard) imo, lakini unashangaa anairudia baada ya miaka mine kupita,” anasema.
Sababu ya 8: Ni kuwapo kwa matabaka makubwa katika viwango vya mishahara ya watumishi wa Umma nchini.
“Leo polisi wetu wanalazimika kuvuta kitu kidogo kwa wananchi masikini kwa sababu ya matabaka haya, mkitupa ridhaa yenu tutafumua mfumo huu ndani ya siku 100 na kuondoa matabaka,” anasema Dk Slaa.
Sababu ya 9: CCM imeshindwa kupambana na ufisadi ambao unazidi kuwakandamiza watanzania kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.

Sababu ya 10: Rais Kikwete anavunja sheria alizozisaini mwenyewe jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi.
“Kifungu 21 (1) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi aliyoisaini kwa mbwembwe nyingi, kinazuia mgombea kutoa ahadi jukwaani, Kikwete ametoa ahadi nyingi kama mgombea, je, hajui sheria,” anahoji Dk Slaa.

Sababu ya 11: Dk Slaa anasema kutokana na kutowajali watanzania CCM waliingiza kinyemela kipengele katika sheria ya gharama za uchaguzi bila ya kujadiliwa bungeni na wao walithibitisha.
Sababu ya 12: Anaitaja kuwa ni ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania kutotekelezwa ipasavyo na serikali ya CCM na ndio mana wengi mnaishi katika nyumba zilizozekewa matope.

“Mkitupa ridhaa yenu tutafuta kodi katika vifaa vyote vya ujenzi ili muweze kujenga nyumba bora kwa sababu maisha bora yanaanzia nyumbani,” anasema Dk Slaa.
Sababu ya 13: Rais Kikwete aliahidi kujenga vyumba vya madarasa 22,000 lakini kwa takwimu za serikali baada ya miaka mitano wamejenga vumba 300 tu.

“Hatuwezi kuwa na serikali inayojisifu kwa kujenga vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, huku kukiwa hakuna walimu, maabara, maktaba na maji ya kutumika katika vyoo,” anasema Dk Slaa.

http://www.mwananchi.co.tz/makala/-/4720-dk-slaa-tumechoka-kupiga-debe-sasa-tunataka-usukani

0 comments:

Post a Comment