Wednesday, August 18, 2010

Dk. Slaa: Nimeshinda mafisadi

Na Mwandishi Wetu

“HUU si ushindi wangu binafsi, bali ni ushindi wa Watanzania. Ni ushindi wa wazalendo wa nchi hii, dhidi ya mafisadi. Hakika, huu ni ushindi wa wananchi wazalendo wa kweli katika taifa lao.

“Ni ushindi wa wanademokrasia, dhidi ya wahujumu wa demokrasia. Ni ushindi wa wanyonge, dhidi ya wachafuzi wanyonyaji wa taifa.”

Haya ndio maneno anayosema mbunge wa Karatu (CHADEMA), mkoani Arusha Dk. Willibrod Slaa, kuelezea hisia zake baada ya kushinda kesi aliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga ubunge wake katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Jumatano iliyopita, Jaji Robert Makaramba wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, alitupilia mbali madai yote 13 ya wanachama hao, akisema walalamikaji wameshindwa kuyathibitisha.

Walalamikaji katika kesi hiyo, ni John Bura, Joseph Haimu na Thomas Irafai. Miongoni mwa madai yao, ni pamoja na msimamizi wa uchaguzi kutoa fomu bandia Na. 21 B zinazotumika kusajili matokeo.

Walikuwa wanatetewa na Mpaya Kamara na Ezra Mwaluko, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akitetewa na Mery Lyimo na Veratas Mlay.

Jaji Makaramba katika uamuzi wake alifika mbali zaidi. Alisema “Mahakama imekubaliana na hoja za wakili wa utetezi Tundu Lissu, kwamba walalamikaji waliwasilisha nyaraka za kughushi.”

Hata hivyo, alisema ni jukumu la vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi ili kuwafikisha mahakamani waliohusika katika kugushi nyaraka hizo.

Uamuzi huo umemkosha Dk. Slaa. Hata hivyo, anasema kwamba alitarajia kushinda. “Sikuwa na mashaka na kesi hii. Madai ya walalamikaji hayakuwa na nguvu za kisheria,” anafafanua.

Anasema, “Wenzetu walighushi nyaraka. Walikuja mahakamani na nyaraka za uwongo. Walikuja na madai ambayo huwezi kuyathibitisha mbele ya mahakama.”

“Kimsingi walikuja kuidanganya mahakama. Bahati njema mahakama imeuona uwongo wao. Katika mazingira hayo, hata kama Jaji angetaka kuwabeba asingeweza, maana walikuwa hawabebeki,” anafafanua.

Pamoja na kwamba kesi hiyo imefunguliwa na wanachama watatu, Dk. Slaa anaamini kuwa mshindani wake katika uchaguzi huo, Patrick Tsere ndiye aliyekuwa anaifadhili.

Kwa nini? Anasema, “Kila kesi ilipokuwa inatajwa bwana huyu alikuwa anashinda katika viwanja vya mahakama. Alikuwa anatumia muda mwingi katika kesi ile, kuliko kufanya kazi za umma.”

“Ni kweli alitakiwa mahakamani kuja kutoa ushahidi. Alikuja mara moja na kumaliza kazi yake. Lakini kila mahakama ilipokuwa inakutana, Tsere naye alionekana katika viwanja vya mahakama. Hii ina maana kwamba pamoja na kuwa kesi ilifunguliwa na wengine, lakini yeye alikuwa amejificha nyuma yao.”

“Ufisadi upo wa aina nyingi. Kuna watu wanaibia serikali kwa kuchota mabilioni ya umma, na wengine wanalipwa bila ya kufanya kazi. Hawa wote ni mafisadi,” anasema kwa hali ya kuchukia.

Anasema, “Katika hili, Tsere anakuwa fisadi kwa kuacha kazi za serikali na kushinda mahakamani bila sababu za msingi.” Katika uchaguzi huo, Dk. Slaa alimshinda Tsere. Kwa sasa Tsere ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.

Mbali na Tsere, Dk. Slaa anamtaja Martin Thomas, kwamba alikuwa mmoja wa wafadhili wakuu wa kesi hiyo. “Huyu aliomba tenda ya ujenzi wa barabara wilayani Karatu. Baraza la Madiwani la Halmashauri, ikamfuta baada ya huko nyuma kujenga madaraja yasiyofikia kiwango,” anasema.

Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inaongozwa na CHADEMA. “Viongozi wa CCM wakamfuata Ngwilizi (Brigedia Hassani Ngwilizi) kumuomba aingilie kati. Bila utashi wa wana-Karatu Ngwilizi akaja Karatu na kutangaza kumpa zabuni Thomas.”

Anasema, “Tunaposema CCM hawawezi kupambana na ufisadi, tunasema tukiwa na uhakika na hilo. Ndiyo maana ninaposema ushindi wangu ni ushindi dhidi ya mafisadi, nina maana pana zaidi. Kwamba CCM hakina ubavu wa kupambana na ufisadi. Hiki ni chama kinachokumbatia mafisadi.”

Wakati huo, Ngiwilizi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Dk. Slaa anasema mmoja wa walalamikaji, Emmanuel Denis alikuwa mwenyekiti wa kijiji, akaingia katika ufisadi wa fedha za miradi ya kijiji hadi kufukuzwa uongozi.

Thomas Lulu alikuwa mwenyekiti wa ujenzi wa shule, lakini ni yeye anayekabiliwa na tuhuma za kutafuna fedha za ujenzi zinazofikia Sh. 10 milioni.

Anasema ni kweli ametumia muda mwingi mahakamani, badala ya kuwafikia wapigakura wake, lakini “ushindi wangu umenipa nguvu ya ziada kuwa walikuwa nami mahakamani.

“Ushindi umenipa mwamko mpya. Tumeongezewa mizigo, lakini sasa tuna ajenda mpya na tunasonga mbele, japokuwa kimaendeleo tumetumia fedha nyingi,” anasema.

Anasema, “Narudi bungeni nikiwa na mwamko mpya na nguvu mpya. Sasa nakwenda kuitumia kikamilifu nafasi yangu ya ubunge na uenyekiti wangu wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (LART).”

Dk. Slaa anafahamika vema namna alivyo mchokonozi kiasi cha kufichua mabomu mengi ndani ya serikali.

Ni yeye aliyeongoza mkutano wa hadhara wa 15 Septemba, 2007 wa vyama vinne vya upinzani ambapo alitangaza walichokiita orodha ya watu 11 watafuna nchi.

Angali na ari hiyo? “Ndiyo mabomu hayajaisha. Yapo mengi, na kwa jinsi nchi hii inavyoendeshwa, tutegemee watu wengi kuguswa. Ukombozi haujapatikana na kamwe hauwezi kupatikana mara moja.”

“Furaha kubwa tuliyonayo ni kwamba wananchi wameanza kutuelewa. Wanaelewa kuwa mapambano yangalipo, tena makubwa sana na kwamba mchango wao unahitajika.

“Siku zote wananchi walikuwa wanadanganywa kwamba tuliyokuwa tunayasema ni uzushi na kauli tu za kisiasa, sasa ukweli umedhihiri kwamba kumbe watawala walikuwa wanaficha ukweli. Ndani ya serikali kuna ufisadi mkubwa unaohitaji nguvu kubwa kuushughulikia,” anasema.

Katika orodha ya watafuna nchi, wamo mawaziri watatu waliojiuzulu, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Andrew Chenge.

Kuhusu tuhuma zinazomkabili rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Dk. Slaa anasema “kinachosubiriwa ni muda tu.”

Anasema iwe iwavyo, lazima Mkapa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Watanzania wanadanganywa kwamba rais mstaafu ana kinga ya kutoshitakiwa. Ni kweli anayo, lakini kinga yake inahusu wakati anafanya kazi zake za urais. Anapogeuka kuwa mjasiriamali, ameibeza kinga yake,” anasema.

Anasema, “Kilichomkuta Fredrick Chiluba wa Zambia, ndiyo kinachomkuta Mkapa. Walitumia vibaya madaraka waliyokabidhiwa na umma na kugeuka wahujumu.”

Dk. Willibord Peter Slaa, alizaliwa Oktoba 1948 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Kwermusl, Daud na Karatu kati ya mwaka 1958 hadi 1965.

Mwaka 1966 hadi 1977 alijiunga na Sekondari na vyuo vya seminari vya Dung'unyi Sekondari, Itanga, Kibosho na Kipalapala.

Mwaka 1977 alijiunga na Chuo Kikuu cha St. Urban kilichopo Rome Italia kwa masomo ya shahada ya juu (PhD), sheria za Kanisa Katoliki na sheria za Cv-Law.

http://www.halihalisi.co.tz/08/05/21/

0 comments:

Post a Comment