HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI DR.WILLIBROD PETER SLAA (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA KWA
MWAKA WA FEDHA 2010/2011
UTANGULIZI:
1: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani kuwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2010/2011 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) (7) , Toleo la Mwaka 2007.
2: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuwashukuru sana wananchi, na wapiga kura wangu wa Wilaya ya Karatu ambao kama kawaida wameendelea kuniunga mkono wakati wote kwa njia mbalimbali na hasa kwa mshikamano wao wa kuijenga wilaya yetu.
Nawashukuru sana, na hasa kwa kuionyesha Tanzania nzima kuwa kumbe maendeleo yanawezekana hata bila CCM. Nachukua fursa hii kuwahakikishia kuwa nitaendelea kuwatumika kwa akili, moyo na uwezo wangu wote.
3: Mheshimiwa Spika, Nachukua fursa hii pia kuwashukuru Watanzania wote kutoka kona zote za Tanzania wenye mapenzi mema ambao kwa maelfu wamendelea kutuunga mkono na kujifunza kutoka Karatu katika jitihada zao mbalimbali za kujiletea maendeleo. Kwa wapenzi wetu wote, Mwenyezi Mungu awarudishie mara mia kwa upendo wenu.
4: Mheshimiwa Spika, nitakuwa nimekosa fadhila iwapo sitatoa shukrani kwa Chama changu CHADEMA, chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Freeman Mbowe, Mwenyekiti (T). Chadema ndio kimeniwezesha kufika hapa Bungeni. Kwa waliofikiri kuwa ubunge unapatikana kwa njia ya CCM tu, natumaini wameona kuwa Ubunge unapatikana pia kupitia kambi ya Upinzani. Watanzania waache tu hofu na uwoga, Tanzania ni yetu sote. Vyama vyote vya siasa ni “milango na madirisha”tu ya kuwahudumia. Haitoshi kulalamika kila mwaka, mabadiliko yanawezekana kila mmoja akifanya na kutimiza wajibu wake.
5: Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Kambi ya Upinzani wakiongozwa na Mhe. Hamad Rashid Mohamed, (Mb) Mbunge wa Wawi na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa msaada walionipa wakati wote katika kipindi chote cha miaka mitano tunayoelekea kumaliza sasa kama Kambi ya Upinzani.
6: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe. Mizengo K.P.Pinda (Mb) Waziri Mkuu, Mhe. Celina O.Kombani (Mb) Mawaziri wa Nchi, na Naibu Waziri na Makatibu Wakuu kwa kuandaa Bajeti hii wakisaidiana na Wataalam wao wote, na kwa ushirikiano walionipa wakati wote katika utekelezaji wa majukumu yangu mbalimbali hapa Bungeni na kwa Jimbo langu la Karatu.
7: Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, napenda kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu na kuliweka katika medani ya kimataifa kwa ubora, uongozi wa kasi na viwango vya juu na kuwa kielelezo cha kweli cha demokrasia katika nchi. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie hekima na busara na kuwapatia nguvu na afya mnazohitaji katika kuliendesha vizuri Bunge letu hasa katika kipindi hiki cha lala salama.
MAJUKUMU YA UPINZANI NA KAMBI YA UPINZANI:
8: Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ya Tano na ya mwisho kwa Serikali ya Awamu ya Nne. Kwa kuwa hii ni Hotuba yetu ya mwisho kwa Bajeti hii, tutafuata zaidi mfumo wa tathmini ya utendaji wa Serikali kwa kutathmini bajeti hii na Bajeti zilizopita za Serikali.
9: Mheshimiwa Spika, Kazi ya msingi ya kikatiba ya Kambi ya Upinzani siyo kuipigia makofi Serikali ya Chama Tawala bali kuangalia zaidi mapungufu katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwaonyesha wananchi kwanini waendelee kuichagua Serikali iliyoko madarakani au kwa nini wasiiondoe kwa njia ya Sanduku la kura kama hawajaridhika na utendaji wake.
10: Mheshimiwa Spika, Watanzania wanahitaji pia kuonja yale yanayopendekezwa kutolewa na vyama vingine. Huu ndio mchezo wa demokrasia japo katika demokrasia “Changa” ukitamka hivyo wengine wanaona huo ni uhaini. Tathmini yetu itafuatiliwa na maoni ya Kambi ya Upinzani.
11: Mheshimiwa Spika, Iwapo vyama vya Upinzani vitaipigia makofi Serikali ya Chama Tawala, basi vyama hivyo vitakuwa wasindikizaji tu siku zote, wakati na lengo lenyewe la kuvisajili ni kutengeneza ushindani wa sera na utendaji katika kuwaletea matumaini mapya wananchi kwa njia ya uchaguzi wa mara kwa mara na pale Chama Tawala kinaposhindwa kutekeleza matumaini ya Wananchi, wakiondoa kwa njia ya Uchaguzi na kujaribu Chama kingine. Ndio maana ya utajiri wa vyama vya siasa.
12: Mheshimiwa Spika, Demokrasia yetu sasa siyo changa tena baada ya miaka takriban 20 ya Mfumo wa vyama vingi hivyo wananchi wana uwezo wa kuona, kutafakari na kufanya maamuzi yao wenyewe kutokana na Taarifa sahihi wanazopata. Wananchi baada ya miaka takriban 50 wamekwisha kuona jinsi kila kukicha wanavyoendelea kuwa masikini, na wakati huo huo wamekwisha kuona na kuonja baadhi ya matunda ya mfumo wa vyama vingi japo kwa uchache.
13: Mheshimiwa Spika, Hotuba hii inalenga kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuonyesha wapi Chama Tawala kimeshindwa kufikia malengo yake, na wapi upande wa upinzani japo hauna Serikali umeweza kuisukuma Serikali kwa kiwango cha kuwafanya wananchi kunufaika.
14: Mheshimiwa Spika, kwa miaka minne iliyopita Kambi ya Upinzani imekuwa ikichangia mawazo mbadala kwa kina na kwa mapana. Lengo ni kutoa mchango wetu katika kuleta maendeleo katika nchi yetu na kumnufaisha mwananchi wa kawaida. Hii ingewezekana tu iwapo Serikali ingelikuwa sikivu na kutekeleza “Vizuri” angalau baadhi ya ushauri, na au kuchukulia hatua baadhi ya mambo ambayo Kambi ya Upinzani imekuwa ikishauri.
15: Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Hamad Rashid (MB), imezungumzia kwa kirefu mapungufu ya kibajeti na kupendekeza Bajet mbadala ya Kambi ya Upinzani. Sipendi kuyarudia hayo yote.
16: Mheshimiwa Spika, Kauli , Sera, na Ilani ya chama Tawala inapimwa kupitia vigezo vya Bajeti na utekelezaji wa Bajeti hiyo kwa kila mwaka. Vigezo vya kisiasa haviingii sana katika upimaji huu, kwani kama kauli mbiu ni “Maisha Bora kwa kila Mtanzania” basi tathmini yetu itajikita kama kweli katika kipindi cha Miaka mitano Maisha Bora yamepatikana kwa kila mtanzania au la! Vigezo muhimu katika hali hiyo ni vya kawaida kabisa yaani hali ya kawaida ya maisha ya mwananchi inavyokua.
17: Mheshimiwa Spika, Katika Tathmini hii pia nitatumia Taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha aliyoitoa Machi,2010 kwa vyombo vya Habari akitoa Tathmini ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM akielezea mafanikio ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Desemba, 2005 hadi Desemba 2009.
18: Mheshimiwa Spika, Mathalan, wananchi wengi wameacha kunywa chai kwa vile Sukari sasa imekuwa bidhaa ya anasa wastani wa Tshs 1,200/= hadi 1,800/-wakati mwaka 2005 ilikuwa shs 500/= hadi 600/=, mikate iliyokuwa kimbilio la walala hoi hasa mijini imekuwa haishikiki tena kwa vile bei ya mkate unakimbilia shs 1,500/= hadi 2,000/=. Nyama inazidi kuwa hadithi ya kusadikika kwa Watanzania wengi kwani bei ya kilo inakimbilia zaidi ya shs 4,500-5,000/- katika maeneo mengi. Mchele ambao ukiacha mahindi unakuwa chakula cha Watanzania wengi unakimbilia Tshs 1,500/ kwa kilo.
19: Mheshimiwa Spika, hali inakuwa ngumu pale ambao bei ya kila kitu kimepanda maradufu, na kipato cha Mtanzania kimebaki pale pale, na nguvu ya Mwananchi kununua nayo ikishuka kwa kasi kubwa kutokana na kuporomoka kwa thamani ya Shillingi ya Tanzania. Serikali makini ni ile isiyotafuta visingizio bali hutafuta kila siku namna ya kupunguza makali hayo kwa wananchi wake. Ndio maana ya “all Politics is local” visingizio vya hali ya uchumi wa dunia hauwahusu wananchi, kwani waliiweka/ajiri Serikali kwa lengo pekee la kushughulikia maswala yao.
20: Mheshimiwa Spika, Pale Serikali inaposhindwa kupunguza makali hayo ndio inaitwa “Serikali imeshindwa kulinda maslahi ya ndani ya Wananchi wake”. Katika hali hii Taarifa za Serikali za kuwa Wastani wa kipato cha Mtanzania (per Capita) kwa mwaka 2008 ni Tshs 682,737.7 inapoteza maana. Watu wenye kipato hicho wasingelishindwa kununua angalau sukari na mchele! Hata hivyo Watanzania wenyewe ndio wanajua kama wanapata kipato hicho au hizo ni Takwimu za vitabuni tu! (Taarifa ya KM- Wizara ya Fedha).
21: Mheshimiwa Spika, tamko la Serikali la Uchumi kukua litakuwa na maana tu iwapo Watanzania wanapata chakula vizuri, wanalala vizuri, mishahara ni mizuri, lakini si kwa vitabu kuonyesha takwimu kubwa kubwa za uchumi kukua. Wananchi hawali takwimu za vitabuni, wanahitaji mahitaji yao muhimu kwa maisha yao ya kila siku. Kwa kigezo hiki ni dhahiri Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kukidhi kigezo muhimu cha kuwapatia Watanzania Maisha Bora katika miaka minne iliyopita.
22: Mheshimiwa Spika, lazima Bunge kama mwakilishi wa Wananchi lichukue nafasi yake kusimamia maslahi ya Watanzania na kulinda haki zao, Kwa kusimamia vizuri fedha, mali na rasilimali za nchi yetu. Wabunge ni Wawakilishi, lakini huku vijijini kuna baba zetu, mama zetu, Dada zetu, kaka zetu, shangazi zetu na kadhalika. Wao ndio wanaojua jinsi maisha yalivyo magumu, na ndio wanaotupima kwa vigezo vya bei nilizotaja hapo juu.
23: Mheshimiwa Spika, Dola moja ya Marekani inayokubalika kimataifa kama kigezo cha umaskini wa kutupwa, na kwa msingi huu tukiwa wa kweli katika takwimu zetu, Watanzania wengi zaidi ya asilimia 16 iliyotajwa katika “Hali ya uchumi” watakuwa katika kundi hili ambalo haliwezi tena kula nyama, kununua sukari, kununus mchele na hata maharage kilo sasa ni zaidi ya Shs 1,000 hivyo hata chakula ambacho ni cha mtu wa chini sana watashindwa kukinunua.
24: Mheshimiwa Spika, haya ni “Maisha Magumu” sana kwa watanzania hao kwa kigezo chochote kile na hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania tangu tupate uhuru.
25: Mheshimiwa Spika, Hili si swala la kisiasa. Maisha Bora ni pamoja na kujua kama kila mtanzania amepata mlo wa uhakika, amelala mahali pazuri, amepata huduma nzuri, hasa Afya na Elimu, na huduma zote za kijamii zinazostahili kutolewa na Serikali. Maisha Bora ni pamoja na kuona kama hali ya Mtanzania ya uchumi imeboreka kwa kiasi gani katika kipindi kinachotathminiwa. Hivi ndivyo vigezo tutakavyotumia katika tathmini hii, na ninaamini hili ni jukumu letu la kikatiba. Watanzania nao wana haki ya kujua mustakabali wa nchi yao kwa kusikiliza upande wa pili wa shilingi bila ushabiki wa kivyama au kisiasa tu.
26: Mheshimiwa Spika, Wananchi hawali siasa, bali wanahitaji kitu cha kuingia kwenye matumbo yao waweze kuishi vizuri kama binadamu, wanahitaji mahili pazuri kujikimu japo siyo magorofa ambayo hata wengine hata kuyaona tu hawajaona wala hawatarajii kuyaona. Kigezo kingine cha kupima maendeleo ni kupima tulikotoka, tuliko leo, na hasa katika tathmini ya miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kigezo cha kipato binafsi ambacho kinamgusa mtu mmoja mmoja. Mheshimiwa Spika, ni vema tukaeleweka vizuri.
27: Mheshimiwa Spika, Si kwamba tunapotoa tathmini hii hatuoni mambo yaliyofanywa na Serikali zetu chini ya TANU/CCM/ASP tangu tulipopata uhuru. La hasha. Tunachosema ni kuwa kwa rasilimali tulizonazo tungeliweza kufanya zaidi sana, tungeliweza kufanya mambo mengi bila kumbughudhi mwananchi kama tungeliweza kulinda vizuri rasilimali tulizonazo na kuzielekeza vizuri kwenye maeneo muhimu yanayomnufaisha mwananchi.
28: Mheshimiwa Spika, Huu ndio mgogoro siyo kwamba kambi ya Upinzani haina macho kuona yaliyofanyika. Lakini kwanini tupoteze muda kuzungumzia vitu ambavyo kila mmoja anaona na wengi tunakubaliana kuwa havikidhi hali? Ndio maana kila mara tumesema kuwa Vipaumbele vya Serikali vinakasoro, na hata pale inapoonekana fedha zinasemekana zimetengwa, kimatendo hali siyo hivyo.
VIPAUMBELE KATIKA BAJETI YA SERIKALI 2010/2011:
29: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu na hata Mhe. Waziri wa Fedha, katika hotuba yake kifungu cha 38 cha Hotuba, anaweka bayana Misingi na Shabaha za Bajeti kwa mwaka 2010/2011. Baadhi ya misingi hiyo ni pamoja na kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa mapato kwa kuhusisha vyanzo vipya; kuimarisha udhibiti na usimamizi wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali; kuendelea kuchukua hatua ya kudhibiti misamaha ya kodi ili kuongeza mapato; kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Kauli mbiu ya Kilimo Kwanza na kuanzishwa kwa vitambulisho vya Taifa.
30: Mheshimiwa Spika, Kauli hii ya kisiasa ni kauli tamu sana katika masikio ya Watanzania. Kwa bahati mbaya Watanzania wengi wanafikiri Bajeti ni Hotuba ya Waziri, na kwa kawaida hawafanyi utafiti wa kina kujua kauli hii ya Waziri inatafsiriwa vipi katika takwimu za Kibajeti.
31: Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine, tena napenda kuwashauri sana Watanzania, kabla ya kuipongeza au kuichana chana bajeti ni vizuri wakaangalia Takwimu za kibajeti yaani fedha zimetengwa kiasi gani na kwa ajili ya nini, taarifa ambayo inapatikana katika kitabu cha kwanza hadi cha Nne ya Vitabu vya Bajeti.
32: Mheshimiwa Spika, nitatoa mifano michache kuona kama Kauli hii tamu ya kisiasa inawiana na kilichoko katika vitabu vya Bajeti. Kitabu cha Nne, Public Expenditure Estimates Development Votes, kwa mfano mwaka 2009/2010 Wizara ya Kilimo ilitengewa Jumla ya Tshs 92,694,254,000 na mwaka 2010/2011 imetengewa Tshs 103,952,371,000.
33: Mheshimiwa Spika, Ni kweli kuna ongezeko la Tshs 11,258,117,000. Lakini ikumbukwe kuwa mwaka 2009/2010 Dola ya Marekani ilikuwa inabadilishwa kwa $1= Tshs 1200, leo $ 1 ni sawa na Tshs 1,450 Hivyo uwezo na nguvu ya manunuzi ya Shillingi imeshuka kwa zaidi ya Tshs 250 hivyo kwa fedha hizo kazi unazofanya inaweza kufanana na zile za mwaka jana au hata chini ya hapo.
34: Mheshimiwa Spika, muhimu zaidi ni kuona fedha hizo zimetengwa hasa kufanya kazi gani ndani ya kilimo, na je zitakazofika kwa mkulima kufanya shughuli za kilimo hasa ni kiasi gani? Kasma ya 43 ndiyo inayojibu swali hili. Kifungu kidogo cha 2002 ndicho kinatengewa fedha kwa ajili ya vifaa vya kilimo ( Agricultural Mechanization,) Tshs 497,850,000. ASDP ambayo inaonyesha kuwa kwa shughuli za ASDP ambayo ndio yenye kunufaisha kilimo mmoja kwa mmoja ni Tshs 97,595,807,000 tu Matumizi mengine ni Tshs 149 Billioni.
35: Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kabisa hiki ni kiwango kidogo sana katika jumla ya Bajeti ya trillioni 11. Uwiano huu hauonyeshi dhahiri kuwa Kauli ya Kilimo kwanza haioani na fedha zilizotengwa. Vivyo hivyo kwa kutazama Kasma zilizotengwa chini ya Halmashauri za Wilaya nazo hazionyeshi uwiano huo.
36: Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa vipaumbele ndio vinavyoitafuna nchi. Serikali isiyoweka vipaumbele kwa wananchi wake ni dhahiri ni Serikali isiyojali wananchi wake wenyewe. Mfano halisi ni msamaha kwa Makampuni makubwa ya Madini, wakati inawatoza wananchi wake waendesha Pikipiki na Bodaboda ambao wanafanya biashara ya kujitafutia tu chakula. Wakati imetoa misamaha mikubwa ya zaidi ya Billioni 700, lakini wafanyakazi wake inawaondolea kodi ya asilimia 1 tu ambayo ni ndogo sana.
37: Mheshimiwa Spika, Hivyo hoja ya kwamba Serikali haiwezi kuongeza mishahara si ya kweli, kama Serikali ingelipanga vizuri vipaumbele vyake. Taarifa kamili kuhusu mishahara itatolewa na Waziri wetu kivuli wa Wizara husika
KUPANUA WIGO WA MAPATO:
38: Mheshimiwa Spika, Mapato ya Serikali yaani jumla ya Makusanyo yote yanaonekana katika kitabu cha Kwanza yaani “Volume l Financial Statement and Revenue Estimates” (for the Year from 1st July, 2010 to 30th June, 2011). Makusanyo yote yameonyeshwa kwa mfumo wa asili, na miaka yote mfumo huu unafanana. Kitabu hiki kinaonyesha kuwa Vote 21 ‘Hazina’ Trillion 5.4 ya mapato yote yatapatikana kwa njia zile zile za kawaida, Bia, Sigara, Vinjwaji Baridi vinaonyeshwa kuwa ndio vilivyongezewa kodi. Kodi ya Mauzo na hata kodi ya magari.
39: Mheshimiwa Spika, Uchambuzi huu na Taarifa za TRA zinaonyesha kuwa Sehemu kubwa ya Kodi inalipwa na Wafanyabiashara (wenye TIN) wasiozidi, 570,000 kwa nchi nzima, na kati ya hao asilimia zaidi ya 75 wanatoka Dar-Es-Salaam. Wafanyakazi wa Serikali na Sekta Binafsi wanaolipa kodi ni takriban 1,000,000.
40: Mheshimiwa Spika, hivyo mzigo mkubwa wa kodi unabebwa na idadi ndogo sana ya Watanzania. Huo ndio mfumo uliokuwepo siku zote na unaendelea kuwa hivyo. Ni dhahiri maneno matamu yaliyoko katika Hotuba ya Serikali ya kupanua wigo wa mapato hayako kwa matendo.
41: Mheshimiwa Spika, wala Serikali haionekani kutafuta kodi kwenye maeneo mapya ambayo yangelipunguza sana mzigo wa kodi kwa walipa kodi wachache ambao kila mwaka wanabebeshwa mzigo huo huo, au wananchi ambao ndio walaji wa mwisho kila mwaka kubebeshwa mzigo wa kulipa kodi kupitia mfumo wa VAT.
42: Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kuwa watu wachache sana wanaendelea kubeba mzigo mkubwa lakini usiotosheleza mahitaji ya maendeleo na badala yake Taifa linazidi kuwa Tegemezi. Serikali ingelikuwa makini ingelifanyia kazi pendekezo lake au kauli yake yenyewe, la kuwa na Wigo mpana wa kodi, watu wengi zaidi wangeligawana mzigo na hivyo mzigo usionekane kumwelemea mtu mmoja mmoja.
43: Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 21, Kifungu kidogo cha 2007 ambayo inahusika na Kodi ya Mapato, kwenye mapato, faida na ‘Capital gains’ inayonyesha Taifa linapata kiasi cha Tshs Billioni 463,070,200.00 tu. Kodi kutoka kwa Wafanyikazi takriban 1,000,000 inakisiwa kuwa Tshs 44,325,000.00. VAT kwenye huduma mbalimbali itaingizia Taifa kiasi cha Tshs 229,822,900.00, wakati Kodi kwenye biashara ya nje inategemewa kuingiza tu kiasi cha Tshs 96,394,800.
44: Mheshimiwa Spika, kwa nchi inayoingiza karibu kila kitu hata Sindano ya kushona na “vifungo” vya nguo, ni dhahiri kabisa kuwa kiasi hiki ni kidogo sana na inaashiria mambo mengi ikiwa ni pamoja na under-declaration, under-invoicing, na au udanganyifu wa wazi na viashiria vya rushwa katika Idara husika.
45: Aidha, Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi wanafikiri kuwa kodi pekee mwaka huu ni zile zilizoko kwenye kodi iliyopanda ya Sigara, Bia, na vinywaji baridi tu. Watanzania wengi hawana elimu ya kodi. Kodi za vinywaji na Sigara zinakatwa toka kiwandani hivyo watu wengi hawajui kuwa wavuta sigara, wanywaji wa bia na soda ndio wenye kulipa hizo kodi.
46: Mheshimiwa Spika, hivyo ni muhimu Watanzania waelewe kuwa siku zote kodi kwenye sigara, bia na soda inapopanda wao ndio wanaozilipa japo hawalipi moja kwa moja, kwani kodi hizo zinakuwa ndani ya bei ya Sigara, bia na Soda na sukari. Lakini isitoshe, Watanzania wanalipa kodi kupitia VAT ya asilimia 18 yaani kwa kila shs 100 wanalipa kodi ya shs 18 Serikalini kupitia gharama za simu za mikononi ambazo sasa watumiaji wake wanakadiriwa kuwa 18 Millioni.
47: Mheshimiwa Spika, jambo ambalo watanzania hawajelewa ni kwamba kodi inayopandishwa katika bidhaa wao ndio wanaolipa, wafanyabiashara wao ni njia ya kuikusanyia Serikali fedha hizo tu.
48: Mheshimiwa Spika, Kuongezeka kwa mara kwa mara kwa vinyaji kunawalazimisha wananchi wengi wageukie vinywaji vya kienyeji na hasa Gongo ( Moshi, changaa au kwa jina lolote linalojulikana- pombeni ambayo siyo tu kwa sheria zetu ni harama lakini pia ni hatari kwa afya za Raia wetu).
49: Mheshimiwa Spika, asilimia 20 ya Ushuru kwenye mafuta aina ya Petroli (Diesel –Kifungu cha 21 kifungu kidogo cha 2) nayo inaathiri moja kwa moja mwananchi wa kawaida kwa kuwa bei ya Petroli nayo itaendelea kuathiri gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usafiri wa binadamu. Ni kweli kuwa bei ya Mafuta (Petroli na Diesel) katika soko la dunia nayo imepanda kwa mara nyingine tena.
50:Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imeshindwa kubuni namna ya kukata makali hayo kwa njia bunifu kama vile “ Stabilization fund” ambayo nchi nyingine zinafanya. Tanzania tumeachia mzigo wote kwa mlaji wa mwisho ambaye kwa bahati mbaya asilimia 98 ni wananchi wa kawaida wa mijini (wakiwemo wafanyakazi ambao mshahara wao ni kiduchu mno) na wa vijijini.
51: Mheshimiwa Spika, hivi sasa wananchi wengi wamepata mwamko wa kujenga nyumba za kisasa na kuondokana na hali mbaya ya nyumba, za majani, udongo, na kadhalika. Mwamko huo unapata kikwazo kikubwa kutokana na Bei ya bati, cementi na misumari kuendelea kuwa juu.
52: Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ingeliweza kupunguza makali haya kwa kupunguza asilimia 18 ya VAT angalau ishuke hadi 16 kulingana na nchi nyingine za Afrika Mashariki, katika Bei ya Bati, Cementi, Nondo na hata kodi na ushuru mbalimbali kwenye vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na bidhaa za mbao za ujenzi. Kwa mtindo huu, japo kuna dalili ya kuendelea na ujenzi, ni watu wenye hela ndio wenye uwezo wa kujenga na watanzania walio wengi wataendelea kuwa watazamaji katika shughuli za maendeleo. Bila maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
USIMAMIZI NA UDHIBITI WA MAPATO:
53: Mheshimiwa Spika, kitakwimu inaonekana fedha nyingi sana zinaenda kwenye miradi mbalimbali hasa ngazi ya Wilaya. Maswali mengi ya kujiuliza ni kama tunapata thamani halisi ya fedha zinazoelekezwa kwenye miradi hiyo? Isitoshe, Maneno, Usimamizi na Udhibiti yaliyotamkwa mwaka huu kama ilivyo miaka mingine yamekuwa wimbo wa kila Siku.
54: Mheshimiwa Spika, taarifa za CAG za kila mwaka ni ushahidi wa wazi kuwa Serikali pamoja na kutamka maneno haya matamu, imeshindwa kutekeleza lengo lake hili. Taarifa za kila mwaka zinaonyesha upotevu wa mabilioni ya Shillingi, lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa.
55: Mheshimiwa Spika, taarifa za CAG zinaongezewa nguvu na Taarifa za Kamati 3 za Bunge ambazo zimethibitisha matumizi makubwa na mabovu ya Fedha za umma. Kwa mwaka wa Fedha wa 2008/2009 ambao ndio ukaguzi wa mwisho wa CAG na pia Kamati za Bunge za Hesabu, Kamati hizo zimetoa taarifa zake Bungeni na Serikali makini inatakiwa kuwa imeisha kuchukua hatua na wahusika wa ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma nao wanatakiwa kuwa wamechukuliwa hatua.
56: Mheshimiwa Spika, Kutokuchukua hatua kwa mapendekezo ya Chombo cha kikatiba yaani Taarifa ya CAG ikipewa nguvu na Maazimio yanayotokana na Kamati za Bunge ni udhaifu mkubwa sana kwa Serikali. Utashi wa Serikali wa kuchukua hatua haujaonekana kama ulivyothibitishwa na utekelezaji wa Maazimio ya nyuma mathalan, Aliyekuwa Balozi wa Tanzania Malawi aliyefanya shopping ya gari kwa kubeba fedha kwenye begi na kununua Gari Dubai bila utaratibu wowote wa manunuzi ya umma (tender) , na Gari lenyewe likiwa limetembea zaidi ya km 700,000. Gari hilo halikufanya kazi likarudishwa Dar-Es-Salaam kwa fedha za umma.
57: Mheshimiwa Spika, Balozi huyo hatimaye aliishia kukatwa tu fedha kidogo tu wakati anastaafu. Taifa linapoteza mabilioni ya Fedha, na kisha linaendelea kuimba kuwa ni “ Taifa Maskini”, linaenda kuomba fedha kwa wahisani lakini halichukui hatua kwa wahusika wa ubadhirifu huo, japo hatua iliyochukuliwa katika Halmashauri ya Bagamoyo inatia moyo, na hapa kwa namna ya pekee kwa mara nyingine ninapenda kumpongeza kwa dhati sana Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambao wamesimamia vizuri zoezi hili. Ni imani yangu pia zoezi lililoanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mkinga nayo itachukuliwa kwa umakini mkubwa na hatimaye wahusika wote kufikishwa mbele ya Sheria.
KUPUNGUZA GHARAMA ZISIZO ZA LAZIMA:
58: Mheshimiwa Spika, Eneo lingine ambako tumeonyesha udhaifu mkubwa ni katika ni pale ambapo Bajeti yetu Mwaka 2010/11 siyo tu inaendelea kuwa Tegemezi bali tumelazimika kukopa fedha kwa kinachoelezwa kuwa Wahisani wamejitoa kwa kuwa hatukutimiza masharti.
59: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni masharti yapi ambayo wahisani hao wameweka. Tanzania ni nchi ambayo tangu wakati wa Mwalimu imekataa kupewa masharti. Lakini je, Masharti hayo ni ya aina gani? Ni vema Taifa likajua masharti hayo ili pia tufahamu ni nani hasa marafiki zetu.
60: Mheshimiwa Spika, Lakini iwapo masharti hayo ni ya usimamizi wa uchumi wetu, hata Kambi ya Upinzani tutawaunga mkono kwani tusingelipenda uzembe, ufisadi wala wizi ndani ya Serikali yetu kwa manufaa ya watanzania. Mheshimiwa Spika Serikali ni mtumishi wa Umma, na ni lazima maadili ya uendeshaji wa Taifa yaheshimike kwa manufaa ya wote.
61: Mheshimiwa Spika, hatua ya kukopa mwaka huu ndani na nje tena kutoka vyombo vya kibiashara, si jambo zuri kwa uchumi wetu kwani inaashiria pia kuwa tutapaswa kulipa kwa masharti ya kibiashara. Kama tunakopa kulipia Mishahara (Recurrent Expenditure). Hali hii haikubaliki kabisa, na kama hatua hiyo imefikiwa kutokana na uzembe wa Afisa kutotekeleza masharti yaliyokubaliwa ni vema Bunge likafahamishwa na Afisa huyo achukuliwe hatua zinazostahili kwa kuliingizia Taifa hasara ya Tshs takriban Billioni 200/.
Baadhi ya mikopo hiyo ni yenye masharti yasiyo nafuu ya Tshs Billioni 797,720/- (kufidia pengo lililotokana na wahisani kujitoa).
62: Mheshimiwa Spika, Mikopo kwa shughuli za maendeleo ni jambo la kawaida, na Kambi ya Upinzani haina pingamizi iwapo tu mikopo hiyo itasimamiwa na kutumika vizuri. Lakini kukopa kwa kuendeshea shughuli za Serikali yaani kulipa mishahara, posho mbalimbali, mafuta na kadhalika si jambo linalokubalika hata kidogo. Mikopo mingi itakuja kulipwa miaka 30/40 ijayo hivyo si vyema kuwabebesha watoto na wajukuu zetu mzigo wa kulipia mikopo ambayo hawatakuwa wameonja matunda ya mikopo hiyo hata kidogo.
63: Mheshimiwa Spika, kuna msemo wa mitaani kuwa “mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake”. Iwapo Serikali imeona hakuna fedha kupitia njia za kawaida, wala misaada basi ilitakiwa kukata na kupunguza matumizi yake kuliko kuliingiza Taifa katika madeni ambayo hayana tija kwa Taifa. Madeni yote ya uendeshaji kwa kawaida hayana Tija.
64: Mheshimiwa Spika, Mwaka jana tulipiga kelele kuwa chai na vitafunio ofisini vilikuwa na Bajeti kubwa kuliko hata fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mahakama Kuu kwa nchi nzima. Tunashukuru kuwa kilio chetu kimesikilizwa kwa kiasi fulani. Hata hivyo kuna maeneo ambayo bado yangeliweza kupunguzwa zaidi, mathalan Kasma ya 410501 ununuzi wa Vyombo vya Nyumbani. Ni lazima Serikali itueleze ni kwa nini vyombo hivi vinanunuliwa kila mwaka na hata kama ni hivyo, mbona vilivyochakaa haivonekani kuingizwa kwa upande wa maduhuli ya Serikali kama mapato? Kuna mchezo gani hapa?
65: Mheshimiwa Spika, Serikali lazima iwajibike kwa wananchi na kutoa ufafanuzi wa kina kunapotokea matumizi ya namna hii ambayo ni mabilioni kwa Serikali nzima. Mifano hai ni ofisi ya Waziri Mkuu, Kasma ya 410501. Vivyo hivyo kwa kasma ya 410502 Ununuzi wa Samani, mapazia na Mazulia Kifungu ambacho nacho kinaenda kwenye mabilioni ya Fedha.
66: Mheshimiwa Spika, Hali hii bado iko kwenye Wizara na Idara zote, mathalan Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kasma ya 210503 kwa ununuzi wa chakula na viburudisho, au kasma ya 410500 “kitchen Applicances, utensils and crockery”. Swali la msingi ni kuwa vitu hivi vilikuwa kwenye Bajeti ya mwaka 2009/2010. Je ni kwa nini vinanuliwa tena kupitia bajeti ya 2010/2011? Na iwapo ni hivyo vilivyochakaa vimekwenda wapi? Je Samani na hasa mazulia na fenicha zinachakaa kwa mwaka mmoja tu? Au watumishi wenye stahili wameongezeka? Iwapo hivi ndivyo mbona Idara zimebakia zile zile? Kunahitajika maelezo ya kina.
67: Mheshimiwa Spika, hali hii haiwezi kabisa kukubalika katika nchi ambayo inakiri katika Takwimu yake yenyewe kuwa watu zaidi ya 12.9 Millioni wanaishi chini ya mstari wa Umaskini (below poverty line) unaotambulika duniani ( yaani ni maskini wa kutupa –ambalo ni ongezeko la watu 1,500,000 kati ya 2001/2008 (HBS 2007). Yaani tumekuwa na maskini wengi zaidi kuliko mwaka 2001.
68: Mheshimiwa Spika, hii ni hali ya kutisha, na Serikali kwa Takwimu hizi tu inapaswa kuwa makini zaidi na kuondoa aina zote za matumizi ya anasa na kupanga mikakati imara zaidi ya kuwanyanyua hawa ndugu zetu Watanzania millioni 12,9 ambao ni maskini wa kutupa. Katika vigezo hivi vyote ni dhahiri, Serikali ya Chama cha CCM haiwezi kusema kuwa imepata mafanikio. Ni ajabu kama kuongeza Maskini, badala ya kufuta umaskini inaweza kuhesabika kama ni mafanikio.
69 Mheshimiwa Spika, kwa rasilimali na utajiri mkubwa tulionao, hali ya Mtanzania inatakiwa kuwa bora zaidi iwapo atawekewa utaratibu mzuri, mikakati mizuri ya ajira, na matumizi bora ya rasilimali yenye kumjali zaidi Mwananchi . Hali ya sasa ya matumizi ya Rasilimali za Taifa haionyeshi dalili hiyo, na tusipokuwa makini, Madini, magogo yataisha na Taifa litabaki halina rasilimaili ya kuendeleza vizazi vijavyo.
70: Mheshimiwa Spika, Je, tumefaulu katika kumletea Mtanzania Maisha Bora, ambayo ndio ilikuwa Kauli Mbiu nzito wakati wa Kampeni za Uchaguzi 2005. Kwa Bahati mbaya, hakuna anayezungumzia tena kauli hiyo, hata Viongozi wenyewe wa CCM wameitekeleza.
71: Mheshimiwa Spika, wakati tunahesabu maisha ya Watanzania kwa vitu kama Radio, Baiskeli na kochi, wako Watanzania wanaotuhumiwa kukwapua mabilioni ya hela, wamejenga maghorofa, wakiwa watumishi wa Serikali, na mishahara yao inajulikana, posho zao wakisafiri zinajulikana na sio wafanyibiashara lakini wanaogelea katika starehe ya ajabu wakati watu million 11hata mlo wao wa siku ni shida. Ni lazaima Serikali ya awamu ya nne itafute vigezo vingine kuelezea ufanisi, kwa vyovyote si hivi ambavyo vinawagusa wananchi walio wengi.
72: Mheshimiwa Spika, aidha, Kambi ya Upinzani pia katika uchambuzi wake wa kina inabaini kuwa Serikali haijaweza kabisa kusimamia Safari za nje. Haiwezekani, Haina mantiki kabisa kila Wizara, na katika kila Wizara takriban kila idara na kitengo inatenga mamilioni ya Fedha kwa ziara za nje na za mikoani.
73: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inadhani sasa umefika wakati wa kufanya tu zile ziara zenye Tija. Hivyo ndivyo wanavyofanya wenzetu siyo tu nchi za Ulaya lakini hata nchi kama Ruanda, Mozambique, Namibia ambazo zimetupiku sana kwa maendeleo, japo nchi hizo zote zimetoka kwenye mazingira ya Vita miaka michache tu iliyopita. Siyo tu hao wenzetu walikuwa kwenye vita, bali Tanzania ilikuwa katika mstari wa mbele katika ukombozi au kuleta amani kwa nchi hizo. Siri yao ni nini?
74: Mheshimiwa Spika, hakuna siri kubwa kama usimamizi thabiti wa mapato ya nchi na matumizi yake. Jambo hili linahitaji sana utashi wa Kisiasa siyo tu wa kutoa matamko matamu lakini pia wa kuchukua wakati mwingine maamuzi na hatua ngumu. Tanzania tuko nyuma sana katika hatua hii.
75: Mheshimiwa Spika, Mathalan, kwa wale tuliopata uzoefu wa kusafiri kwenda nje ya nchi, mara ngapi tumesafiri na Mawaziri tena kutoka nchi hisani, wakisafiri katika ndege Daraja la Kawaida (Economy class) wakati sisi tunaotegemea msaada toka kwao hata wa kulipa mishahara yetu tumepanda Daraja la Wafanyabiasahara wakubwa (Business Class). Hatutegemei Waziri Mkuu wetu asafiri katika Economy class. Lakini tunahitaji kuthibiti zaidi ziara hizi. Hatua ya kwanza ya kuthibiti ni Si kila mwaliko, au kila safari inayojitokeza lazima tuende na siyo kila mkutano tunaoalikwa lazima tuende.
76: Mheshimiwa Spika, Serikali ichague mikutano muhimu na yenye Tija kwa nchi yetu. Na fedha za ziada ziwekezwe kwenye maendeleo zaidi. Mheshimiwa Spika uwiano wa Bajeti ya Matumizi ya Kawaida ambayo mwaka huu ni Trilioni 5.9 dhidi ya Matumizi ya Maendeleo ya 3.8 ni sherti uangaliwe upya.
77: Mheshimiwa Spika, Matumizi yasiyo ya lazima yathibitiwe, na matumizi yasiyo na tija ya moja kwa moja nayo yaondolewe na vyanzo vipya vibuniwe kuwatoa Watanzania kwenye aibu hii ya kuitwa “Nchi maskini”. Mkakati tuliojiwekea wa 2025 unaelekea dhahiri hautawatoa katika Umaskini iwapo tutaendelea kwa mwendo huu tulio nao.Nio maana matumizi katika ziara kwa mfano isiyo na tija ya moja kwa moja lazima kuthibitishwa na mamlaka fulani. Ni kwa sababu hiyo Mauritius, Zambia, Uganda, Safari zote za Mkuu wa nchi, zinathibitishwa na Bunge, na kila ziara nje ya zilizopitishwa na Bunge, zinahitaji “Retrospective Approval”(kibali cha Bunge cha Baadaye), baada ya hoja ya msingi kujengwa na Serikali.
78: Mheshimiwa Spika, kauli ya Mwalimu kuwa wakati wenzetu “Wanatembea sisi lazima tukimbie”, ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kusukuma maendeleo yetu, lakini ni dhahiri Mwalimu ameondoka na Kauli yake hiyo. Ni vigumu sana kufikiria maendeleo wakati wenye Diploma na cheti cha Chuo kikuu ni asilimia 0.6.
79: Mheshimiwa Spika Serikali na washabiki wa CCM watuelewe tunapozungumzia takwimu hizi. Hakuna Mtanzania anayetakiwa kuwa na ushabiki wa kisiasa kwa Takwimu hizi na wote tunatakiwa tulie kwanza, tuweke vichwa pamoja ili tuelewe ni vipi tunajikwamua katika hili. Ni aibu kwa Tanzania yenye amani, utulivu kuwa na takwimu hizi, wakati wenzetu wa Ruanda, Uganda, Mozambique waliotoka kwenye mazingira ya vita wanazungumzia Takwimu za juu zaidi.
80: Mheshimiwa Spika, hakuna asiyejua kuwa Tanzania haina utaratibu wowote wa udhibiti wa fedha chache zilizoko na zinazohitajika sana kusukuma mbele maendeleo yetu ya nchi iwe katika ujenzi wa madarasa, Zahanati na vituo vya afya au miundombinu. Tunajisifia kuwa na idadi kubwa ya madarasa lakini Taarifa ya CAG na Kamati inaonyesha jinsi idadi kubwa ya madarasa haya inavyokosa sifa, na hivyo baada ya muda si mrefu tusipokuwa waangalifu hatutakuwa na madarasa kwa vile yatakuwa yamechoka. Hii haina maana kuwa kuna madarasa mazuri sana kati ya hayo. Mheshimiwa Spika, Wanaharakati na vyombo vya habari vimechambua sana ziara za Rais, na Tija yake sina sababu ya kuzirudia hapa.
TAARIFA ZA CAG NA KAMATI KUTOFANYIWA KAZI:
81: Mheshimiwa Spika, hatuwezi kumaliza eneo hili la udhibiti bila kufanya marejeo kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali. Tangu Ofisi ya CAG ilipoanzishwa imekuwa ikilalamika miaka yote kuhusu matumizi yasiyo yakinifu ya fedha.
82: Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais alionyesha utashi mkubwa wa kiasiasa pale alipowaita viongozi wakuu wakiwemo Wakuu wa Mikoa (RCs), Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri kujadili Taarifa ya CAG.
Kambi ya Upinzani iliamini kuwa maagizo ya Rais yangelisimamiwa kikamilifu na watendaji wake, na pale ambapo hayasimamiwi kikamilifu, hatua madhubuti zingelichukuliwa. Hali imekuwa si hivyo hata kidogo kiutendaji. Nikitoa mfano wa mwaka 2009, Kamati za za Bunge za Mahesabu zimetoa Taarifa zake Bungeni, na Bunge kupitisha Azimio kukubali mapendekezo ya Kamati hizo.
83: Mheshimiwa Spika, Kimsingi CAG amekuwa wakati wote akitoa Taarifa, lakini Taarifa hizo zimekuwa hazifanyiwi kazi. Ushahidi ni mavitabu na mavitabu na hakuna taarifa yoyote ya utekelezaji iliyo wazi. Kama ingelikuwepo CAG angeliziona na kwa kuwa haziko tunaamini kuwa hakuna hatua iliyochukuliwa. Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kama Rasilimali za Taifa hili zingelisimamiwa na kudhibitiwa inavyotakiwa leo hali yetu ya uchumi isingelikuwa tofauti na Malaysia au Singapore ambapo wakati wa uhuru walikuwa na hali ya uchumi kama ya kwetu. Watanzania lazima wajiulize Tananzia kuna nini? Rasilimali nyingi sana, ardhi kubwa sana, maji mengi sana, lakini watanzania Maskini wa kutupwa. Serikali lazima itupe jibu.
84: Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani kwa miaka minne iliyopita tumekuwa tukitoa Bajeti mbadala lakini hakuna hatua zilizochukuliwa japo, Waziri Mkulo jana wakati wa kuhitimisha amesema kuwa “tungelimpelekea mapema”, tumpelekee mara ngapi?
85: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ilitegemea kuwa Serikali, kwa maana ya Hazina, Tamisemi, na Wakurugenzi husika wangelichukua hatua mara moja kuhusu maeneo yaliyobainishwa kuwa na Ubadhirifu. Hali imekuwa kimya, Kamati za Bunge zimezunguka takriban mikoa yote gharama za Wananchi, lakini matokeo yamekuwa kama hakuna lililotokea.
86: Mheshimiwa Spika, Serikali kwa ujumla wake imenyamaza kimya, karibu maeneo yote, ukiacha tukio la Bagamoyo na sasa la Muheza/Mkinga ambayo nayo tunaamini yatasimamiwa kikamilifu. Kamati ya LAAC imefika kwenye maeneo, inakuta hakuna nyumba ya mwalimu iliyojengwa lakini vitabu vya Halmashauri vinaonyesha mradi umekamilika asilimia 100 (mfano wa Nyumba ya Mwalimu Migombani, Monduli- Nyumba iliyoko imejengwa Asilimia 100 na TANAPA) Kisima cha maji ambacho hakipo Manispaa ya Arusha, Mradi wa Umwagiliaji Halmashauri ya Morogoro ambapo CAG amefanya kazi nzuri hadi kuwataka waliosababisha hasara siyo tu walipe hasara hiyo bali pia mamlaka husika iwachukulie hatua za kisheria na kinidhamu.
87: Mheshimiwa Spika, hali hiyo ya udanganyifu, ubadhirifu, matumizi yasiyo mazuri ya rasilimali, majengo yasiyofuata ramani na ubora, imejitokeza katika miradi mingi kama ilivyoonyeshwa na Taarifa ya Kamati ya LAAC iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu.
88: Mheshimiwa Spika, Mifano ya Miradi hiyo ambayo matumizi yake au hayakuridhisha kabisa, au miradi haipo lakini fedha imetumika ni pamoja na miradi ya Shule ya Msingi Mlongo Kisiwani Mafia, Stendi ya Basi Manispaa ya Songea, stendi ambayo haipo kabisa lakini fedha zimetumika, Zahanati ya Ndagoni ambapo ujenzi umesimama na fedha kuliwa; Mradi wa ujenzi wa Nangaramo (Nanyumbu ambapo mradi umejengwa lakini hautumiki na fedha za umma zimefungwa humo ni dhahiri mipango haikuwa makini na wala hapakuwa na upembuzi yakinifu, au Mradi mkubwa wa maji Newala uliogharimu Tshs Millioni 172 lakini hauwezi kutumika kwa miaka mingi ijayo kwa ukosefu wa Umeme, na wananchi wa vijiji 11 wataendelea kutazama matenki 11 matupu bila manufaa yoyote kwao.
89: Wakati huo huo Mheshimiwa Spika, Halmashauri nchini hazijajibu hoja mbalimbali za ukaguzi, zenye thamani ya Tshs Billioni 91,101, 051, 978.40, Kamati ya LAAC ilikwisha kutoa Taarifa Bungeni kuwa japo ni kweli fedha hizi si lazima ziwe zimeibiwa, lakini kinachotokea ni kuwa Wakiisha kupita wakaguzi, wahusika wanaenda kununua receipt bandia mitaani, na kuwaita tena wakaguzi kwa ukaguzi wa pili.
90: Mheshimiwa Spika, Mtindo huu usipokomeshwa fedha nyingi zitaendelea kuibiwa, na risiti bandia kuwasilishwa kwa uhakiki na wakati huo hakuna kazi inayofanyika. Hali hii iligunduliwa pia na Kamati ya LAAC hivi karibuni kwa kupiga simu kwenye Kampuni iliyodhaniwa imetoa bidhaa lakini kampuni hiyo kukanusha kabisa kuhusika.
91: Mheshimiwa Spika, Billioni 91 kwa wale wasiofahamu ni fedha nyingi kiasi gani, ni sawa na Madarasa ya Sekondari 65,000 kwa thamani ya Tshs 14 Millioni kwa darasa. Kiasi hiki kinahusu Halmashauri 126 tu. Halmashauri nyingi zimeshindwa kujibu hoja za miaka ya nyuma kabisa ya CAG yenye jumla ya Tshs 32, 903,395, 306 amabayo nayo ni sawa na Madarasa 2,350 kwa gharama ya Tshs 14 Millioni kwa Darasa, au ni sawa na Shule zilizokamilika Madarasa 16 kila mmoja, Shule 146. Wilaya ya Kongwa peke yake haijashughulikia hoja za thamani ya Tshs 6,813,262,872. ambazo thamani yake zinatosheleza kujenga Sekondari 30 bila mchango wa mwananchi hata mmoja.
92: Mheshimiwa Spika, nimeeleza haya kwa kuwa hii ni hali ya kutisha. Kambi ya Upinzani haina nia ya kumkebehi yeyote, wala kuingiza ushabiki. Inaumizwa na hali halisi, na tunaumia tuapoona watu wanaingiza siasa kwenye mambo yasiyotaka siasa.
93: Mheshimiwa Spika, CAG pamoja na kuwa anafanya kazi kwenye mazingira magumu sana, hana watumishi wa kutosha, hana vifaa na nyenzo za kazi za kutosha, lakini anafanya kazi nzuri sana. Anatoa Taarifa iliyo sahihi bila hila. Lakini hakuna ushirikiano wa kutosha kwa upande wa Uongozi wa Serikali, wahusika hawachukuliwi hatua, au zikichukuliwa kesi nyingi, kama Kamati ya LAAC ilivyogundua zinaishia njiani kwa kuhujumiwa na Watendaji wa Halmashauri kwa kutokupeleka ushahidi na nyaraka za kutosha mahakamani. Hali hii isipothibitiwa Taifa letu litaendelea kuimba wimbo wa Nchi maskini,
94: Mheshimiwa Spika, hadi leo hii, mamlaka husika hazijachukua hatua, imebaki kimya kana kwamba hakuna lililotokea. CAG amekagua, Kamati yako ya Bunge imekagua na kutoa Taarifa Bungeni. Hayo yote yanatumia fedha za wananchi wa Tanzania hao hao wanaokosa huduma. Mamlaka imekaa tuli kana kwamba hakuna lililotokea na mambo ni shwari tu.
Mheshimiwa Spika, hali hii haiwezi kuvumiliwa katika nchi inayojiita ‘Maskini’ miaka 50 baada ya uhuru. Kambi ya Upinzani nayo inajiuliza baada ya wahusika kukaa kimya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Shughuli za Serikali au Mhe. Rais, kwanini nao pia wamekaa kimya? Kuna nini katika mfumo wa Serikali, na kwa utaratibu huo kauli za “mitaani” kuwa uwizi na ubadhirifu huo ni cheni hadi ngazi ya TAMISEMI na Hazina tutashindwaje kuiamini?
95: Mheshimiwa Spika, Ni imani yangu kuwa Waziri Mkuu au Waziri wa Nchi, Tamisemi atatolea ufafanuzi wa kina hali hii. CAG mwaka jana amefanya siyo tu ukaguzi wa kawaida bali pia alifanya Ukaguzi Maalum (Special Audit) zipatazo 9 na ameenda mbali kufanya Ukaguzi wa Ufanisi na kupendekeza hatua mahususi za kuchukua. Wahusika wamekaa kimya tu rasilimali zinaangamia, umaskini unazidi kukua na kukithiri, na wananchi wanazidi kupoteza matumaini kila kukicha. Ukaguzi wa Ufanisi wa Babati ulihusu maeneo ya Mafuriko, na Taarifa ile ingelifanyiwa kazi, athari iliyoletwa na Mafuriko ya Kilosa huenda isingelitokea au isingelikuwa kubwa kiasi hicho.
96: Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nchi Utumishi, aliwahi kueleza kuwa kulikuwa na Watumishi “hewa” zaidi ya 3,000 kwenye Pay Roll ya Serikali. CAG na Kamati ya LAAC wamethibitisha pia kuwa wako watumishi wengi waliostaafu, waliofariki, walioacha kazi, waliofukuzwa majina yao bado hayajaondolewa kwenye Orodha ya Watumishi wa Serikali. Hawa hawapo duniani, au hawapo kazini lakini wamekwisha kulipwa kwenye akaunti zao. Hivyo hizi fedha zimepotea.
97: Mheshimiwa Spika, Watumishi wote Wilayani kwa utaratibu wa sasa wanalipwa na Halmashauri. Hivyo, hakuna maelezo yeyote kwa majina hayo kutoondolewa kwenye Orodha, wakati kila mwezi Afisa wa Halmashauri anapeleka Orodha ya Watumishi Wizarani. Taarifa zote za kifo, kuacha kazi, ziko wilayani. Hivyo Mishahara hewa kutokea ni dalili ya uzembe na au uwizi ambayo ni lazima ichukuliwe hatua mara mmoja kuokoa fedha nyingi zinazopotea. Kwa mwaka 2008/2009 Fedha ambazo hazikurudishwa hazina ni Billioni 1,755,207,927 kwa mamlaka ya Halmashauri za Wilaya peke yake.
98: Mheshimiwa Spika, hizi ni fedha nyingi sana na kama zingelielekezwa kwenye ujenzi wa madarasa ni sawa na madarasa 125 au shule za Sekondari 7 zilizokamilika za madarasa 16 kila shule. Lakini fedha hizi zimelipwa kwa watumishi hewa. Serikali imejua hilo, Waziri wa Utumishi alitangaza mwenyewe kuhusu Watumishi hewa, lakini Taifa halijajulishwa tena kuhusu hatua mahususi zilizochukuliwa dhidi ya waliosababisha hali hiyo, iwe ya kinidhamu au kisheria.
99: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inadhani Serikali haijawa na mpango mkakati mahususi wa kudhibiti hali hii kuokoa fedha nyingi za walipa kodi, tukisema hili pia tunakebehi? Taifa hili tuache ushabiki, tataendelea kudidimiza Taifa, na watoto na wajukuu zetu watatuhukumu. Tusiogope kusema ukweli pale unapostahili alimradi hatuyasemi kwa ushabiki. NI vema na Serikali wakati wa kujibu ijibu hoja kwa hoja badala ya ushabiki na kuwa tu “defensive” yaani “kujitetea kwa kujitetea tu”. Ni kwa kuweka vichwa pamoja tutaokoa rasilimali chache za Taifa.
100: Mheshimiwa Spika,Taarifa nyingine zinazoonyesha kuwa hakuna udhibiti imara ni Taarifa kuwa kwa mwaka 2008/9 Jumla ya Tshs 2,526,117587 zinazohusu Halmashauri 33 tu zilizolipwa bila kuwa na hati za Malipo. Halmashauri nyingine 62 zilifanya malipo yenye thamani ya 5,313,071,671 zikiwa na nyaraka pungufu.
101: Mheshimiwa Spika, halmashauri zetu zote kwa sasa zina Wahasibu wenye sifa, zina Wakaguzi wa Ndani na zina ikama zilizokamilika za Wahasibu wasaidizi. Hakuna sababu kabisa, isipokuwa kuna uzembe na hila za uwizi ndio maana nyaraka hizo au hazionekani wakati wa ukaguzi au zinaonekana pungufu. Halmashauri nyingi ziko kwenye Mfumo wa uhasibu wa EPICOR lakini hata pale ambapo mfumo huo umefungwa na Computer kuwekwa wahusika wanaacha kuzitumia bila sababu za msingi.
102: Hali hii inatia mashaka makubwa na kuashiria dalili isiyo nzuri. Japo CAG amelalamikia hali hiyo muda mrefu sasa lakini hakuna hatua inayochukuliwa na fedha zinaendelea kuteketea na Taifa linaendelea kulalamika kuhusu “Umaskini”.
103: Mheshimiwa Spika kutokuwa na nyaraka au nyaraka zisizozokamilika za malipo ni kinyume na Agizo no 5 (c) la Memoranda ya Fedha za Serikali ya Mitaa ya mwaka 1977. Ukiukwaji huu wa makusudi wa Memoranda unafahamika, na madhara ya kutokuwa na nyaraka nayo inafahamika lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Kambi ya Upinzani inasema, ni vizuri sasa Waziri husika akatoa maelezo ya kina ya hali hii ya kuweka Kanuni na hatimaye Kanuni hizo hazisimamiwi? Viongozi wa chini wako wapi? Ngazi ya Mkoa, Wilaya, na hata Wizara hawaoni hali hii? Tatizo liko wapi? Tumekwisha kusema Madiwani wapewe Break Down ya matumizi, ni imani yangu TAMISEMI itakuwa imeziandikia Halmashauri ili swala hilo litekelezwe ili Madiwani wawe na uwezo wa kusimamia na kudhibiti matumizi katika eneo lao kwa kuwa na Taarifa zinazowawezesha kusimamia.
104: Mheshimiwa Spika, Wilaya nyingi zimeingia kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii. Watanzania wengi au wanachangia Mfuko huo kwa jinsi Wilaya ilivyoweka katika Sheria zake ndogo. Kwa ujumla wale ambao hawachangii wanatakiwa kulipa Tshs 1500. kwa kituo cha Afya, na shs.1000. kwa Zahanati. Fedha hizo hazirekodiwi vizuri na CAG ameshindwa kuzikagua. Hata hivyo, katika Wilaya ya Karatu tuliwahi kufanya Test ndogo kwa ukaguzi wa dharura. Tulikuta kwa mwezi mmoja upotevu wa zaidi ya 100 Millioni. Hii ni baada ya kuondoa watoto na wazee na wale wote wanaotibiwa bure.
105: Mheshimiwa Spika, Kamati ya Madiwani iliundwa, na kutoa Taarifa kwenye vikao vyote vya maamuzi na hatimaye Mkurugenzi kuachiwa kuchukua hatua. Hakuna hatua iliyochukuliwa. Mheshimiwa spika, Millioni 100 kwa Mwezi ni hela nyingi sana. Hii ni hali ya kutisha. Watendaji na Serikali wote wanajua kuwa kutokutengeneza Taarifa sahihi ya Mfuko huu ni kinyume na Agizo la 84(iii) ya Memoranda ya Fedha za Serikali za Mitaa. Uvunjifu huu umeachwa muda wote bila kukemewa!
106: Mheshimiwa Spika, kwa mtindo huu je ni kweli Tanzania inastahili kuitwa nchi maskini, au tunaifanya Tanzania kuwa Maskini kwa nguvu. Hapa sijaongelea rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu yaani madini ya kila aina ambayo nayo hatutumii vizuri, tunawapa misamaha ya ajabu ajabu, kinyume kabisa na Taarifa ya Kamati tuliyounda na kuihudumia kwa zaidi ya Tshs Billioni 2. Ni dhahiri kwa mtu yeyote makini hali hii haiwezi kuingia akilini kabisa. Sijazungumzia rasilimali ya Bahari/Maziwa na Samaki tulio nao, sijagusia Misitu na Ardhi ambayo sasa inauzwa kwa bei ya kutupa, na wakati mwingine ni wananchi wenyewe wanauza ardhi yao bila kuangalia madhara ya siku zijazo.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2009” NA MWELEKEO
WA UCHAGUZI MKUU 2010:
107: Mheshimiwa Spika baada ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya fedha na usimamizi au udhibiti, sasa niseme kidogo kuhusiana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2009. Mheshimiwa Spika, Oktoba, 2009 ilikuwa ni uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa viongozi wa ngazi ya Kijiji, Kitongoji na Mtaa. Uchaguzi huo kama tulivyotabiri haukuwa wa huru na haki kwa sababu mbalimbali nitakazoeleza hapa chini.
108: Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri Serikali yetu, japo kwa mdomo inazungumzia la kutaka kuona unafanyika uchaguzi huru na haki lakini matendo ya viongozi wetu mbalimbali, kuanzia TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya ambao ndio walikuwa Wasimamizi wakuu wa Uchaguzi, walionekana dhahiri kuwa “wakiendeshwa” na mamlaka nje ya mamlaka zao. Aidha ilikuwa dhahiri kabisa kuwa Serikali ilikula njama na Chama Tawala. Viashiria ya wazi ni kuwa:
i) Vyama vilishirikishwa na kwa pamoja tulikubaliana kutengeneza Kanuni ambazo tunaweza kuziita Sheria Mama. Baada ya Kanuni TAMISEMI ilitengeneza kitu kilichoita “Mwongozo” ambao ulikuja kuwa na nguvu kuliko hata Kanuni zenyewe tulizokubaliana.
109: Mheshimiwa Spika,Wakati Kanuni inatamka kuwa “ Mgombea wa nafasi ya Uongozi atadhaminiwa na kiongozi wa Chama cha Siasa”, Mwongozo uliotengenezwa na TAMISEMI ulisema “ …atadhaminiwa na kiongozi wa ngazi ya “chini kabisa” ya chama cha siasa”. Vyama vingine, ngazi za chini kabisa, mathalan ngazi ya “msingi” kwa Chadema sio ngazi ya uongozi bali ni ngazi ya uratibu tu hivyo haina mamlaka ya kudhamini.
110: Mheshimiwa Spika, Katika utendaji, Wasimamizi wasaidizi wakashikilia maelekezo ya Mwongozo na kukataa maelezo mengine yeyote. Hata tulipoijulisha TAMISEMI tuliambiwa Wasimamizi watajulishwa lakini hakuna kilichotokea. Matokeo na athari ya hatua hiyo ya kisheria ni kuwaondoa (disfranchise) wagombea wengi wa vyama vya Upinzani, mathalan Chadema. Athari yake ni kuwa wagombea wetu wengi waliondolewa kutokana na mchezo mchafu. Hali hiyo pia imetokea kwa Wagombea wa CUF.
ii) Chadema tuliletewa kitabu cha Mipaka ya Vijiji, vitongoji na Mitaa, siku moja baada ya CCM kumaliza zoezi la kura ya maoni. Mtu yeyote mwenye akili atajiuliza imewezekanaje kufanya kura ya maoni wakati mipaka haijulikani? Maelezo pekee ni kuwa TAMISEMI ilikula njama ya kutoa Taarifa kwa CCM hivyo CCM ikaitumia Taarifa hiyo katika kura zake za awali, wakati vyama vingine tulianza kujipanga baada ya kujua mipaka.
111: Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya awali nilieleza jinsi Waziri Celina Kombani alivyoshinikizwa katikati ya Uchaguzi hadi kumhamisha Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Karatu katikati ya Uchaguzi. Taarifa zote tunazona simu zilikuwa zanapigwa tunazo mpaka muda walipowasiliana. Ni hali ya hatari sana Waziri ambaye kimsingi Uchaguzi uko chini yake anapoagizwa na Chama kimoja kwa vile tu ni chama Tawala. Mheshimiwa Kombani amejitetea kwenye vyombo vya Habari kuwa Yule Mkurugenzi amehamishwa kwa kuwa alikuwa Afya.
112: Mheshimiwa Spika, Ninatoa “Challenge”, kuwa Mheshimiwa Waziri atoe vyeti vya Afya, kwa vile kiongozi anayeondolewa kwa sababu za Afya kwanza awe ameomba yeye, na pili kama Serikali inamwondoa iwe kwa Vyeti vya Daktari. Wakati wa kudanganyana umepita, Sheria na kanuni tunazifahamu. Serikali inayopaswa kulinda kanuni na Sheria inapokuwa ya kwanza kuzivunja, hali inakuwa mbaya sana. Ni dhahiri kitendo hiki peke yake kinaufanya uchaguzi ule usiwe wa huru na haki, lakini pia inaondolea Tanzania Sifa ya kuwa nchi inayothamini demokrasia japo inahubiri sana Demokrasia ndani na nje ya nchi.
113: Mheshimiwa Spika, ni dhahiri hali hii siyo ya kistaarabu, haistawishi utawala bora wala misingi ya demokrasia. Hali hii inaondoa kabisa dhana ya kuwa TAMISEMI inaweza kuwa “impartial” na kusimamia uchaguzi bila kupendelea . Hoja ya Upinzani ya kuondoa Uchaguzi huo chini ya TAMISEMI inapata mantiki, na tunasisitiza Uchaguzi ujao uondolewe kabisa chini ya TAMISEMI na uwekwe chini ya TUME ya TAIFA ya Uchaguzi, yenyewe japo inalalamikiwa kwa mambo mengine lakini haijaonyesha “upendeleo wa wazi” kiasi hicho.
114: Mheshimiwa Spika, Hivyo, Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Yusuf Makamba kuwa “CCM imepita bila kupingwa katika nafasi 24,000 ni lazima iangaliwe kwa umakini, siyo sahihi, na inapotosha kwani uchaguzi haukufanyika katika mazingira yanayofanana. Aidha taarifa kuwa matokeo hayo yanaashiria CCM ndiyo chama kinachopendwa kinapotosha.
115: Mheshimiwa Spika, Katika hili lazima tuseme kwa ukali wote kuwa CCM imecheza faulu kubwa kwa kuwa wao ndio “Linesmen, Refereee na Mchezaji”, ikajiamulia aina ya mchezo inayotaka. Mheshimiwa Spika, nchi hii ni yetu sote. Kuna Siku watanzania wataamka, watakataa udanganyifu huu wa wazi, watakataa kunyanyaswa. CCM dhahiri sasa kwa kung’ang’ania uongozi inataka kutupeleka pabaya, na nikumbushie tu, nchi jirani ambako kila siku tunasikia siyo shwari, ni kutokana na vitendo vya aina hiyo.
116: Mheshimiwa Spika, uchaguzi huo unaashiria nini kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani baadaye Mwaka huu? Mheshimiwa Spika, tayari kuna dalili zinazoashiria kuwa hila za namna hiyo zinaanza kuandaliwa, ikiwa ni pamoja na Maadili yanayoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo pamoja na mengine yanalazimisha Chama ambacho hakitasaini kitafutwa kugombea. Ni dhahiri vyama vinakataa kuweka saini kwa vile kuna mambo ya msingi ambayo hatujakubaliana na si utawala bora kulazimisha vitu ambavyo kwenye maziringira yetu hayafai, na hatua hiyo inaweka masharti ambayo hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano haiweki.
117: Mheshimiwa Spika, Maeneo mbalimbali kila kukicha tunasikia matukio ya rushwa ndani ya Chama cha Mapinduzi japo kifungu cha 25 ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi tuliyopitisha tu juzi inatakiwa idhibiti hali hiyo. Watu wanapita kwenye vilabu, wananunua pombe, wanatoa hela, wanatoa jezi kwa vijana bila utaratibu unaojulikana, na kadhalika.
118: Hali hii mheshimiwa Spika haiathiri Wagombea wa Upinzani tu, bali pia wa CCM. Kinachoathirika ni maadili ya Taifa, hivyo swala hili lisiangaliwe tu kwa jicho la Vyama vya Siasa. Lakini pia, kutokuchukua hatua ni dalili ya wazi kuwa CCM haina tena uwezo wala dhamiria ya kudhibiti Rushwa ndani yake. Mtu anayeingia kwa kununua wapiga kura kwa jezi, pombe na hela ni dhahiri hawezi kupiga vita rushwa na wala hawezi kusimamia maendeleo na Rasilimali ya Nchi hii. Ni vizuri wananchi wakawa makini na watu wa aina hiyo.
119: Mheshimiwa Spika ikumbukwe “Rushwa ni Adui ya Haki”, ni dhahiri wabunge wakipatikana kwa Rushwa watashindwa kuwatetea Wananchi maskini iwe ni kwenye kero zao mbalimbali, ushauri au hata kusukuma mbele maendeleo yao. Ni imani yangu, nia ya Mhe. Rais ya kusukuma hadi ikatungwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi haitavurugwa na watu wasiozingatia maadili, ndani ya Vyama, lakini na hata wasiozingatia Sheria
yenyewe.
120: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imekuwa ikipokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali yanayohusiana na vitendo vya viongozi wa CCM kuwafuata kwenye nyumba zao, kuwataka wawaonyeshe kadi zao za kupigia kura, wanaandika namba hizo kwenye fomu au daftari zao. Kinachoudhi ni usumbufu, wakati mwingine usiku wa watu hasa wasio wanachama au wapenzi wa CCM kufatwa na kulazimishwa kutaja namba zao za kadi za Kupigia kura.
121:Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inafahamu kuwa Kadi ya kupigia kura ni mali ya Mpiga kura, na mwenye mamlaka ya kuiomba au kutaka chochote kifanyike kwenye Kadi hiyo ni Tume ya Taifa peke yake na hakuna mtu au mamlaka nyingine yeyote inayohusika. Kwenye Uchaguzi mdogo wa Bussanda na Biharamulo Kadi za wapiga kura zilichukuliwa kwa nguvu, tulitoa majina na taarifa kamili polisi lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
122: Mheshimiwa Spika, Hivyo, ni vema Serikali ikatoa Tamko na kuwataka viongozi wa CCM wa ngazi zote za chini kuanzia Mkoa, kwani mkoa wa Arusha kwa mfano zoezi hilo analiongoza Katiba wa Mkoa Mary Chatanda mwenyewe. CCM iandikishe wanachama wake, lakinii iache kufuata wananchi ambao wanahakika si wanachama wao, na waache tabia ya kuwaamsha wananchi kiholela.
123: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani haina shida CCM kuandikisha watu wao wanavyotaka alimradi hawaingilii uhuru wa wanachama wa vyama vingine, na au hata watanzania wasio na vyama. Vurugu hiyo imesababisha damu kumwagika Busanda na Biharamulo, ni imani yangu kuwa CCM inayokuwa mstari wa mbele kuhubiri uchaguzi wa amani na utulivu haitakaa kuona damu ya mtanzania hata mmoja itamwagika kama ilivyotokea kwenye Uchaguzi mdogo wa Kiteto, Tarime, Bussanda na Biharamulo. Amani inatengenezwa haiteremki tu kutoka mbinguni. Wala amani haiji kwa kuhutubia na kutoa maagizo ambayo hayafuatiliwi kiutendaji. Jeshi la Polisi nalo litakiwe kusimamia Sheria na kuacha kubeba chama chochote cha Siasa.
124: Mheshimiwa Spika, matatizo yameishaanza kujitokeza sasa kwa mfano Wilaya ya Temeke ambako OCD wa Mkoa wa Temeke ameweka amri ambayo ni kinyume na Sheria kuwa vyama vinavyotaka vifanye mkutano vipeleke maombi kwa Mkuu wa Wilaya. Mfano halisi ni siku ya 10June, ambako Chadema walipeleka “Taarifa” ya Mkutano kwa OCD kama sheria inavyotaka lakini akakataa kuipokea, na kuagiza iende kwa Mkuu wa Wilaya. Afisa wetu alipoenda kwa Mkuu wa Wilaya hakumkuta lakini akaambiwa na DAS kuwa huo ndio utaratibu.
125: Mheshimiwa Spika, viongozi wasiofuata sheria za nchi ndio wanaosababisha fujo na vurugu nchini. Ni vema Serikali iwafunze vizuri wasiipeleke nchi pabaya kwa matakwa tu ya watu wachache. Huu ndio mwanzo wa kuvurugika nchi iwapo kila mmoja anajiwekea sheria zake. Ni imani yangu kuwa tumejifunza kutoka kwa majirani zetu, na ni imani ya Kambi ya Upinzani kuwa misingi yote ya amani katika uchaguzi itafuatwa kikamilifu.
UTAWALA BORA NA DEMOKRASIA NCHINI:
126: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, na hata kwenye Kitabu cha Hali ya Uchumi, kazi iliyofanywa na Serikali katika eneo hili imefafanuliwa, mathalan Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kufungua ofisi za Mashtaka na Upelelezi katika Mikoa ya Shinyanga, Lindi na Mtwara. Hii ni hatua nzuri. Pia Katika Hali ya Uchumi Serikali imeeleza kuwa kesi za Rushwa kubwa 15 zilifunguliwa mahakamani.
127: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini japo hii ni hatua mojawapo, Utawala Bora ni zaidi ya hapo. Mahakama zisipokuwa karibu na Wananchi kwa umbali unaofikika misingi yenyewe ya utawala bora haitakuwapo. Mahakama zimekuwa na usumbufu mwingi, kesi zinachelewa sana mpaka maana ya haki inapotea. Wananchi wadogo wanashindwa kuzifuata haki zao kutokana na umbali mkubwa na hasa kesi zinapopigwa tarehe za mara kwa mara watu wa hali ya chini wanafika kukata tama na kupoteza haki zao.
128: Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Mabaraza ya Kata yenye kushughulikia hata baadhi ya kesi za Jinai. Lakini Serikali hadi leo haijatoa maelekezo ya kina jinsi mabaraza hayo yatakavyoendeshwa. Jambo ambalo limefanya kesi za ardhi kuwa kero zaidi kuliko hata awali. Gharama za kufungulia kesi katika Baraza ni kubwa mno ambayo wananchi wa kawaida hawawezi, mathalan 20, 000 kufungua file, wakati mahakama ya mwanzo kesi inafunguliwa kwa shs 1,500 tu.
129: Mheshimiwa Spika, ni wakati sasa Serikali itazame upya utaratibu huu ulioanzisha mabaraza haya, mamlaka yao, uendeshaji wao, ikiwa ni pamoja na usimamizi. Baadhi ya Wenyeviti wa Mabaraza ya Wilaya wameguuka kuwa miungu watu, na wanahukumu kesi wanavyotaka, wakati mwingine bila hata kuwasikiliza mashahidi inavyotakiwa.
130: Mheshimiwa Waziri niko tayari kukupa majina ya wahusika wanaolalamikiwa kwa kesi za aina hiyo. Vyombo hivi vimeundwa kutoa haki, na vyombo vya haki vinapogeuka kuwa kinyume madhara yanakuwa makubwa zaidi na wananchi wanapoteza imani kwa Serikali yao moja kwa moja.
131: Mheshimiwa Spika, katika Maeneo mengi, TAKUKURU ni sehemu ya matatizo, na mfano ni matukio yaliyotokea Kijiji cha Chemechem, Wilayani Karatu, ambako wananchi wamelalamikia jinsi viongozi wa kijiji hicho walivyotafuna rasilimali za kijiji hicho, na TAKUKURU wamefika mara kadhaa, lakini hakuna hatua inayochukuliwa wala hakuna Taarifa.
132: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo imefika kwa Mkurugenzi Mkuu ambaye naye aliahidi atashughulikia lakini hadi sasa ni kimya zaidi ya miaka miwili . Kijiji kinaangamia TAKUKURU ipo na wanalipwa mishahara kwa kodi ya Wananchi hao hao. Mheshimiwa Spika, hatuingilii utendaji wa Takukuru, lakini mambo yanapokuwa hayaendi ni lazima tuyaseme hapa Bungeni kama chombo kinachosimamia Serikali na vyombo vyake vyote. (Katiba Ibara ya 63(2).
133: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora, Mheshimiwa Sofia Simba akifuatana na Mary Chatanda Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, alitembelea Wilaya ya Karatu mwezi May, 2010, Wananchi wa Karatu walifurahi sana kwa vile wanatembelewa na Waziri wa Utawala Bora wakiamini kero zao kuhusu utawala Bora zitapata ufumbuzi. Cha kushangaza Mheshimiwa Spika, Mhe. Waziri, pamoja na mengine na kwa kushirikiana na Mary Chatanda, walianza kuwachochea Wananchi wa kijiji cha Gyekurum Lambo kuwa waandamane kugomea kijiji chao kuingizwa katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Karatu. Waziri wa utawala Bora, ambaye pia ni mwanasheria alipaswa kulinda Sheria. Mheshimwia Waziri Mkuu, wakati ukiwa waziri wa Tawala za mikoa ndio ulitangaza Mamlaka ya Miji midogo 55 nchi nzima. Wakati Tangazo hilo linatolewa Halmashauri husika wala hazikuulizwa. Leo Waziri anashawishi wananchi waandamane, badala hata ya kuwashauri wachukue hatua za kisheria kupinga hatua hiyo. Waziri ni sehemu ya Serikali.
134: Mheshimiwa Spika, Wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kulikuwa na mawasiliano ya kina na Tamisemi na hata Waziri Celina Kombani. Sasa Serikali hiyo hiyo inajikanganya na kushawishi wananchi kugoma. Ni dhahiri kwa hatua hiyo tu, ni dhahiri Serikali CCM haina utawala Bora, na kama inadhani inao haina Waziri anayestahili Wizara hiyo, na kwa kuwa Wizara hiyo matunda yake ndiyo hayo inatumia bora fedha za Wananchi wa Tanzania kwa Wizara isiyo na Tija.
USALAMA WA RAIA NA MALI ZAO:
135: Mheshimiwa Spika, Siku za hivi karibuni Taifa limeshuhudia matukio ya Watanzania, Raia wema kuvamia vituo vya Polisi, na kuleta madhara ya kuumiza polisi na kuharibu mali. Matukio haya yameongezeka kama vile yalivyoongezeka matukio ya Raia kufa mikononi mwa Polisi na hatimaye kutafutwa visingizio vya kila aina. Matukio haya yametokea Iringa, Arusha, Dar-Es-Salaam , Karatu na maeneo mengine mengi.
136: Mheshimiwa Spika, Tukio la aibu la hivi Karibuni lililotokea Wilaya ya Tarime, linatia aibu Taifa. Polisi kutuhumiwa kuvamia nyumba za Raia, na kuwalazimisha kuvua nguo wanawake na wanaume, na wanawake kulazimishwa kulamba sehemu za siri za wanaume shemeji zao, na mwanamke mwingine kulazimishwa kulala na mtoto wake si jambo la kawaida.
137: Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa kama ni kweli na Serikali ikakaa kimya tu. Jambo la kusikitisha, ndani ya Jeshi la Polisi bado kuna viongozi wenye mawazo ya mgando. Ni aibu kwa afisa wa Polisi ambaye hajui kuwa Tanzania ni nchi ya vyama vingi, na kuwa njia za kawaida zinaposhindikana, Raia ana haki ya kukimbilia mahali anapodhani atasaidiwa, kama walivyofanya wakina mama hawa kwa kukimbilia Chadema. Lakini Polisi anawalaumu hadharani eti ‘kwanini walienda Chadema’ kana kwamba Chadema ni chama haramu nchi hii. Nashukuru wakina mama hao hawakukata tama, walipata fursa ya kupiga kelele Chadema, na hatimaye jambo likafika hadharani kwa Taifa zima.
Mhe. Waziri Mkuu, Matukio haya, japo yanafanywa na watu wachache, lakini wanachafua sura ya Jeshi letu la Polisi ambao ndani yao wako wengi tu wanaofanya kazi nzuri sana na ya kijasiri. Ni lazima Jeshi liwashughulikie hawa wachache wanaochafua jina la Jeshi.
138: Mheshimiwa Spika, matukio mengine yanayochafua jina na sura ya Jeshi letu ni pamoja Polisi kuwalinda wahalifu kama ilivyo kwenye kesi nyingi za Karatu ambapo nimekwisha kumjulisha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa. Inatisha inapofika mahali watu wanaweza kukamatwa kwa amri ya mtu binafsi tajiri.
139: Mheshimiwa Spika, Tajiri huyo akipiga watu ni halali, na hata pale anapokamatwa yeye tajiri anapelekwa na Askari kwa gari lake akiendesha mwenyewe, na kusaidiwa mahakamani kwa ‘fast track’ na akiisha kupata mdhamana anarudi na gari lake na askari huyo.
140: Mheshimiwa Spika, Hii ni sawa na kubinafsisha jeshi la Polisi kwa matajiri wachache. Marehemu Boay Gichuru aliyeuawa katika kijiji cha Qanded Karatu, ambapo raia wema wakiwemo viongozi wa kijiji wamesaini affidavit, licha ya kutoa Statement, kuwa wako tayari kutoa uishahidi popote, lakini polisi wamenyamaza. Wahusika wanatambaa mitaani kuwa wameweka polisi wote mifukoni.
141: Mheshimiwa Spika, taarifa ya mazingira ya kifo hicho imepelekwa kwa IGP na mimi mwenyewe nimemjulisha Naibu Waziri, Mambo ya Ndani wote wamekaa kimya. Taarifa za namna hii tumepokea kutoka Tarime, Bariadi, Kagera, Rukwa na meaeneo mengine mengi.
Mhe. Spika, ni vema Mheshimiwa Waziri Mkuu akafahamu kuwa matendo haya yanakatisha tamaa wananchi. Isaitoshe matukio ya namna hii yanachafua jina la Polisi lakini pia la Chama Tawala kuwa imeshindwa kusimamia haki za raia wake, na inabeba matajiri kuliko raia maskini.
142: Mheshimiwa Spika, matendo ya unyanyaswaji kama yanayofanywa na Polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Geita, katika kijiji cha Rwamgasa, Wilaya ya Geita ni vitendo ambavyo navyo havivumiliki katika utawala wa Sheria. Viongozi wa chama ambao kwa utaratibu wa kawaida,wametoa “Taarifa”kufanya mikutano yao ya chama wanakamatwa wakati hawakupewa hata ile taarifa ya “kukataliwa” hiyo mikutano basi.
143: Mheshimiwa Spika, Shinikizo la kuwakamata linatoka kwa Mkuu wa Wilaya, ambaye Sheria ya Vyama vya Siasa wala haimtambui. Wananchi wa kijiji cha Mpuguso, Wilaya ya Rungwe nao wananyanyasika sana na manyanyaso yameanza baada ya Chama cha Upinzani kushinda katika kijiji hicho. Ni vizuri Serikali ikawaelimisha maafisa wake, Wakurugenzi wa Wilaya, Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali, Maafisa wa TRA, na Uhamiaji. Hakuna anayekataa viongozi hao kufanya kazi zao lakini wafuate maadili ya kazi zao, na wale wanaokiuka washughulikiwe inavyostahili. Nchi hii ni yetu sote, hakuna mwenye hati miliki, hivyo wananchi wote, wa jinsia yeyote, rangi yeyote, imani ya dini yeyote na itikadi yeyote wote tuna haki sawa na hakuna aliye juu ya mwingine. Serikali inawajibu wa kusimamia usawa huu bila upendeleo au ubaguzi wowote ule.
MASUALA YA UFISADI NA UWIZI WA MALI YA UMMA:
144: Mheshimiwa Spika, Mwaka wa 2007 mimi pamoja na Wenzangu na kwa kushirikiana na Wabunge wa Kambi ya Upinzani nilitoa pale Mwembe Yanga, “List of Shame”, iliyokuwa yenye majina ya watu tuliowatuhumu kuhusika na Ufisadi mkubwa katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na Ufisadi ndani ya BOT. Kwa kuwa baadhi ya Kesi ziko mahakamani sitaki kuzungumzia zile kesi ambazo ziko Mahakamani tayari. Hata hivyo ninapenda kueleza kuwa wengi wa waliokuwa ndani ya Orodha hiyo ya Watuhumiwa wa Ufisadi walitishia kunipeleka mahakamani. Nami nikasema wawahi kwenda mahakamani kwa vile Taarifa nyingi zingeweza kutoka hadharani.
145: Mheshimiwa Spika, Mwaka 2007 Shirika mmoja la Uingereza lilitangaza kufanya Mkutano wa “Economic Forum”, ambao ungelifanyika Hoteli ya Kempinski, na kutangazwa katika Gazeti la “The Economist”.Waandalizi wa mkutano huo walitangazwa kuwa ni pamoja na Bwana Yusuf Manji, ambaye walimtaja kama ni moja wa nguzo kubwa ya uchumi wa Tanzania, na pia angelikuwa mtoa mada mmojawapo. Nilipotakiwa maoni yangu na waandishi wa Habari nikapinga sana kuwa huyo Bwana hawezi kuwa nguzo ya Uchumi wa Tanzania kwa vile anahusishwa na kutumiwa mambo mbalimbali katika uchumi wa Tanzania.
146: Mheshimiwa Spika, Kufuatia kauli hiyo kwenye Gazeti, Bwana Yusuf Manji alinifungulia Kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Civil Case, na. 140 ya mwaka 2008 Yusuf Manji ( Plaintiff vs Dr. Willibrod Peter Slaa, Defendant) kwa kosa la kumchafulia jina.
147: Mheshimiwa Spika, Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu, kuwa nimeshinda kesi hiyo. Nashukuru kuwa haki ya Watanzania inalindwa. Katika uamuzi wake, Jaji G.P. Shaidi, aliotoa tarehe 14 Januari, 2010 amekataa(rejected not dismissed) kesi hiyo katika hatua ya PO. Kwa maneno yake mwenyewe , Jaji anatamka “ Under the circumastances, of this Case, I hold the view that the plaint as drafted does not fully disclose cause of action against the defendant, I therefore reject it under Order V11 Rule 1 of the Civil Procedure Code.
148: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru sana Mhe. Tundu Lissu, Wakili wangu aliyesimamia kesi hiyo mpaka haki ikapatikana katika hatua ya PO, yaani kabla hata kesi yenyewe haijasikilizwa. Kwa ushindi huo ninapenda kuwasisitiza Watanzania wawe majasiri kulinda heshima ya Nchi yetu, kulinda Rasilimali za Taifa hili kwa gharama yeyote, na nina hakika tukisimamia ukweli Mungu atalinda Taifa lake kwa njia ya majasiri wachache. Ninaipongeza pia mahakama kwa kusimamia ukweli na haki.
UBADHIRIFU/RUSHWA NA UFISADI:
149: Mheshimiwa Spika, Masuala ya Rushwa na ufisadi yameisumbua nchi yetu kwa muda sasa. Wako watu wanaosema tuache kuzungumzia Ufisadi bali tuzungumze maendeleo. Ukweli ni kwamba huwezi kuwa na maendeleo kama Rushwa na ufisadi havitapigwa vita kwa hali na mali. Iwapo fedha Wananchi watalipa kodi, na watu wachache wakazitumia kwa njia ya kifisadi, Shule haziwezi kujengwa, Zahanati hazitajengwa wala Zahanati hazitapata dawa, barabara nazo hatiajengwa na kadhalika. Ni kwa msingi huo, Tunaoamini kuwa Ufisadi na ubadhirifu wa mali ya Umma tunashikia Bango kuwa swala la Ufisadi ni lazima Serikali ichukue hatua madhubuti.
150: Mheshimiwa Spika, ndani ya Bunge hili Tukufu Kambi ya Upinzani imeendelea mwaka hadi mwaka kuuliza maswali ambayo hayajapata majibu. Mwaka huu ninarudia tena, kuuliza na kutaka maelezo ya kina kuhusu Ufisadi uliofanyika kupitia Kampuni ya Deep Green Finance Company Ltd, ambayo ilisajiliwa 18 Machi 2004 kwa Taarifa za Brella wanahisa waanzilishi wakiwa ni Mawakili Protase R.G.Ishengoma na Stella Ndikimi wa Kampuni ya IMMA Advocates.
151: Mheshimiwa Spika, Mawakili hao walihamisha hisa zao kwa Kampuni ya Needbank Ltd na Nedbank Africa Investment Ltd tarehe 15 April, 2005. Tarehe 1 Mei 2004 siku ya Sikukuu, Kampuni hiyo ilifungua Akaunti benki ya NBC, Corporate Branch, Akaunti na 011103025840 na haikuingiza hata senti moja katika akaunti hiyo kwa zaidi ya Mwaka mmoja. Kati ya Tarehe 1 August, na December, 2005 Kampuni hii ilipokea jumla ya Billioni 10,484,005 815.39 kutoka BOT.
152: Mheshimiwa Spika, Billioni 10 kutoka BOT kwenda kwa Kampuni tusiyoijua na Serikali haitaki kutolea Taarifa inaleta mashaka na wasiwasi mkubwa kuhusu uwajibikaji wa Serikali yetu. Serikali imekataa kujibu hoja hizi, na Bunge hili na Watanzania tunahitaji kujua Kampuni hii ni ya nani, kwa dhahiri siyo ya kijeshi, na hivyo hakuna usiri wowote.
153: Mheshimiwa Spika, jinsi fedha zilivyohamishwa kwa siku, tarehe, kiasi na njia iliyotumika niliwasilisha katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2008/2009. 154: Mheshimiwa Spika, Tanzania imefikishwa mahali kwenda kukopa fedha kwenye Benki ya Kibiashara wakati tuna fedha zetu zilizotoka Benki Kuu, imepelekwa kwenye Kampuni tusiyoifahamu na Serikali haitaki kutoa jibu. Kimsingi hii ni dharau kubwa kwa Watanzania, na Serikali imekiuka kabisa misingi ya Uwajibikaji na misingi ya Katiba kuwa madaraka ya Serikali yenyewe yanatoka kwa Wananchi.
155: Mheshimiwa Spika, Kampuni ya pili ambayo Kambi ya Upinzani na Watanzania wanataka kujua ukweli ni Kampuni ya Tangold ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius tarehe 05 April, 2005 Ikiwa na Hati ya Usajili na 553334 na kupata Global Business Licence( C2/ GBL) tarehe 08 April,2005. na kupata Hati ya Kutimiza Masharti hapa nchini tarehe 20 February 2006. Hata hivyo Mhe. Spika, Taarifa zilizoko ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporate Branch, no. 0lll03024840 iliyofunguliwa Tarehe 1 January, 2003, yaani miaka miwili kabla Kampuni hiyo haijasajiliwa Mauritius na takriban miaka 4 tangu imepata Hati ya ‘Kutimiza Masharti’ Tanzania.
156: Mheshimiwa Spika, Serikali inaweza kukataa kujibu maswali haya, inaweza kutumia ubabe, lakini kuna siku itafika Taifa haliwezi kukaa kimya, majibu lazima yatapatikana tu.
157: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu sahihi kwa vile ndani ya Bunge lako hili Tukufu Serikali imekuwa ikitoa Kauli tofauti, mathalan, wakati aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, wakati ule Mhe. Karamagi, analieleza Bunge kuwa TANGOLD ni mali ya Serikali kwa asilimia mia moja, Taarifa ya Kamati ya Bomani inaeleza kuwa Kamati hhiyo iliarifiwa kuwa TANGOLD ni mali ya watu Binafsi? Isitoshe, tumeuliza na hatujapata majibu, Kifungu cha 7 cha Memorand ya Usajili inasema kuwa wenye hisa wanaweza kuhamisha ‘share zao’ kwa baba, mama, mke, watoto wapwa…….” Swali ambalo halijapata majibu na lazima sasa lipate majibu ni je Serikali inao watu hao?
158: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndani ya Bunge hili amekataa kujibu maswali yanayohusu Meremeta. Kambi ya Upinzani haitachoka kuweka na kuingiza kumbukumbu hizi ndani ya Hansard ya Bunge. Mheshimiwa Spika, Naomba kuwakumbusha Watanzania kuwa Kampuni ya Meremeta, inayotuhumiwa kwa matumizi ya Tshs 155 Bilioni, ambayo ni zaidi ya Bilioni 133 za EPA, iliandikishwa Uingereza ikiwa na Hati ya Usajili na 3424504 ya Tarehe 19 August,1997 na kupata Hati ya Kutimiza Masharti (Certificate of Compliance) nchini Tanzania kama Tawi la Kampuni ya Kigeni yenye na 32755 ya tarehe 3 Oktoba, 1997.
159: Mheshimiwa Spika, kinachoshangaza katika Kampuni hii ni kuwa wenye hisa wake tofauti na Bunge lilivyoelezwa mara nyingi (Hansard, Karamagi na Meghji Bajet Speech 2007), ni Triennex (PTY) Ltd ya Afrika Kusini yenye hisa asilimia 50%, Msajili wa Hazina mwenye hisa asilimia 50% kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni mbili za London Law Services Ltd wa Temple Avenue, wenye hisa 1% na London Law Secretarial Services Ltd ambao anuani yao ni sawa na hao wenzao, nao pia wana hisa 1%. Jeshi la Wananchi halitajwi mahali popote. Hata kama Meremeta ni Kampuni ya Jeshi, ni Kampuni iliyokuwa inafanya Biashara kwani kuchimba dhahabu Buhemba, ni Biashara ya Madini na siyo siri ya Kijeshi. Hivi ni nini Serikali inaficha kuhusu Kampuni hii. Hata kama kuna Siri,
160: Mheshimiwa Spika, ni kwanini Taarifa ya Siri isitolewe kwa Kamati maalum ya Bunge au Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ulinzi.
161: Mheshimiwa Kambi ya Upinzani haioni kuwa ni sahihi Taarifa ya Kampuni ya Umma isitolewe kwa Bunge kwa utaratibu wowote ule. Kambi ya Upinzani haitaacha kufanya utafiti hadi ukweli wote ujulikane kuhusu Kampuni hii. Tshs Billioni 155 ambazo MEREMETA inatuhumiwa, ni fedha nyingi sana za Wananchi, na bila kupata maelezo ya kina basi, ni dhahiri kuwa Serikali itakuwa inaficha ukweli fulani.
162: Mheshimiwa Spika, Ni imani ya Kambi ya Upinzani, kuwa safari hii, Serikali angalau itakuwa tayari, basi kutoa maelezo japo mafupi, na au kama haiko tayari kutoa taarifa hiyo hadharani, basi angalau kwa Kamati ya Bunge ya Uongozi, ya Mambo ya Nje na Ulinzi au Kamati yeyote ile ambayo Serikali itaona inafaa.
163: Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Ukaguzi wa EPA, uliofanywa na Ernest and Young katika kifungu cha 3.20, 3.23, na 3.24, kinatamka wazi uwepo wa “fraudulent supporting documents submitted to support claims” Yaani ufisadi uliotumika ni pamoja na kutumia hati za kugushi katika kutoa fedha kutoka BOT; malipo ya viwango visivyo sahihi au kutumia viwango visivyo sahihi vya kubadilisha fedha (yaani incorrect amounts and incorrect exchange rate). Ukaguzi ulionyesha kuwa kati ya Tshs 133 Billioni malipo ya zaidi ya 90.3 Billioni yalifanyika kwa kutumia Hati za kugushi (invalid and fraudulent supporting documents), nyaraka hizi zimeonyeshwa katika kiambatanisho C ikionyesha na majina ya Makampuni husika, ikiwa ni pamoja na Kagoda Agriculture ltd ambayo peke yake ilichukua zaidi ya Billioni 40.
164: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekaa kimya kabisa kuhusu Kampuni ya Kagoda, Kambi ya Upinzani imelazimika kueleza kwa kirefu tena kilichojiri kupitia Kagoda, taarifa mbalimbali zilizoko kuhusu kampuni hii na sura ya ufisadi inayoonekana wazi. Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyosajiliwa nchini chini ya Sheria ya Makampuni Sura ya 212 tarehe 29 September, 2005 na kupata Hati na 54040. Wakurugenzi waliosajiliwa wa Kagoda ni watu wawili wenye anuani za Kipawa Industrial area, Plot no 87 Temeke Dar-Es-Salaam, na P.O.Box 80154 Dar-Es-Salaam, kinyume na utaratibu wa usajili Brella ambao unahitaji wakurugenzi wa Makampuni kujisajili kwa kuonyesha anuani ya mahali anapoishi na siyo Sanduku la Posta.
165: Mheshimiwa Spika narudia tena, ni lazima Serikali ilieleze Bunge kwa niaba ya Watanzania wote undani wote kuhusu Kampuni ya Kagoda, na hatua zipi imechukua au inafikiria kuchukua dhidi ya Kampuni na watendaji wake na au watendaji na viongozi wa Serikali waliohusika angalau hatua za kiutawala na au kinidhamu. Hiyo pia ni kwa watendaji wake ambao labda hawakuwa makini wakati kampuni ya Kagoda iliposajiliwa, jambo linaloleteleza kuwa vigumu kwa kampuni hii kujulikana hasa ni mali ya nani, iwapo hivyo ndivyo ilivyo.
UFISADI KUPITIA UNUNUZI WA RADA YA JESHI:
166: Mheshimiwa Spika, leo ni takriban miaka 9 tangu Kambi ya Upinzani ilipopinga ununuzi wa kinachoitwa Radar ya Jeshi, ndani ya Bunge lako Tukufu, na hatimaye kupinga upitishwaji wa Bajet na kutoka nje. Kumbukumbu za Hansard zinaonyesha kuwa Kambi ya Upinzani wakati huo ikiongozwa na Mheshimiwa Lwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Mjini, ilitoka nje ya ukumbi ambao leo ni ukumbi wa Msekwa kuonyeshwa kuchukizwa kuburuzwa na Serikali na Wabunge wa CCM ambao walitumia turufu ya uwingi wao kupitisha Bajeti hiyo. Kambi ya Upinzani inamshukuru sana aliyebuni na kutengeneza mitambo ya Hansard ambayo siyo tu inarekodi kilichosemwa ukumbini bali pia kama kuna kicheko, makofi na hata kuzomewa kama ilivyotokea siku hiyo.
167: Mheshimiwa Spika, Miaka 9 baadaye, Kambi ya Upinzani inaona fahari kubwa, tulichokisimamia siyo tu kimeelekea kuthibitika lakini imekuwa ni hadithi dunia nzima, na imehusishwa na kitendo kikubwa cha ufisadi au rushwa au uwizi wa mali ya Umma. Ufisadi huo umejadiliwa ndani ya Bunge la Uingereza (House Commons) mara kadhaa na uchunguzi kuanzishwa na Shirika la Upelelezi la Uingereza la Serious Fraud Office (SFO). Wakati wenzetu wa Uingereza, ambao tunao mfumo unaofanana sana wa Sheria.
168: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inayo furaha ya pekee kusikia kuwa Serikali iliyokuwa imekanusha kata kata kuwa hakuna ufisadi wa aina hiyo, ndio inayotuma wataalam wake kwenda kudai mgawo wa Serikali ya Tanzania baada ya Serikali ya Uingereza kutamka kuwa itatoa mgawo huo kwa NGO.
Mhe. Spika, kwa jambo kubwa kama hilo, Kambi ya Upinzani inaona ingelikuwa jambo la Busara kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliarifu rasmi kitu gani kinaendelea kuhusu sakata hilo? Isitoshe, Sakata hilo linahusu pia bei ya Radar hiyo kupandishwa kuliko bei yake halali.
168: Mheshimiwa Spika, Hii maana yake ni kuwa kuna fedha za Walipa kodi wa Tanzania imetumika vibaya, Serikali ya Tanzania imeingia hasara kwa kulipa bei kubwa kuliko bei halisi. Je wahusika walioliingizia Taifa wamechukuliwa hatua gani. Mheshimiwa Spika, Maswali haya yanagusa hadhi na heshima ya Serikali ya Tanzania hivyo ni imani yangu kuwa Serikali haitakuwa na kigugumizi kuwaeleza Watanzania kilichojiri, hatua zilizochukuliwa au zinazotarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliosababisha hasara hiyo.
169: Mheshimiwa Spika kwa Taarifa tulizonazo, SFO walifanya upelelezi wa tuhuma za Rushwa (kickback) zinazoihusu Kampuni ya kwao ya BAE. Hata hivyo kulinda heshima ya nchi yao, wakamaliza swala hilo nje ya Mahakama kwa kukubaliana BAE kulipa fine, kwa kosa la “kutokutunza kumbukumbu vizuri” badala ya Tuhuma ya awali iliyokuwa ikichunguzwa ya Rushwa.
170: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa SFO walikuwa wakishirikiana na Tanzania katika upelelezi, na kwa kuwa walikwisha kuwa Wasilisha kwa Mwanasheria wa Serikali kwa Barua yao yenye Kumb. SPC01/D/MC ya tarehe 21 Machi 2001, majina ya wahusika wote wa kashfa hiyo kwa upande wa Tanzania, Kambi ya Upinzani inataka kufahamu Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani au inachukua hatua gani sasa baada ya SFO kumaliza kazi kwa upande wa kwao? SFO wamekwenda mbali zaidi, kiasi cha kuonyesha Fedha hizo zilikopelekwa na viongozi pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania katika Akaunti za nje Uswisi, Lichtenstein na hatimaye katika kisiwa cha New Jersey, Uingereza.
171: Mheshimiwa Spika, Iwapo Serikali ya Tanzania haijachukua hatua yeyote hadi sasa je ni sababu gani za msingi zimefanya Serikali yetu kutokuchukua hatua? Mheshimiwa hali hii ya usiri katika mambo ya umma ndio unaoleta hisia kuwa Serikali yetu haina uwazi, haisemi ukweli katika masuala yanayoihusu Rasilimali na mali za Taifa letu. Ni imani yetu kuwa Serikali itatoa Taarifa ya kina kwa Bunge lako Tukufu ili Taifa liweze kufahamu kinachoendelea. Hizi ni fedha za Wananchi, na Serikali inawajibika kwa Wananchi, Kambi ya Upinzani haioni kabisa msingi wa usiri huu. Hata hivyo, haya yametendwa na Serikali au ilikuwa inafahamu na kama haikufahamu basi inapaswa kuwa chukulia hatua hao wote walioliingizia Taifa hasara hii kubwa.
HALI YA SIASA NCHINI:
172: Mheshimiwa Spika, kwa mtu yeyote mnyofu, mkweli na anayefanya upembuzi yakinifu wa hali ya siasa ya Tanzania atakubali leo kuwa hali ya siasa ni tete katika maeneo na nyanja nyingi. Tusijidanganye kwa kusema kila mara kuwa hali ya kisiasa nchini ni ‘shwari’. Tusipojiangalia na kuwa makini tutakuwa tunacheza mchezo wa Mbuni wa ‘kuficha kichwa kwenye mchanga’.
173: Mheshimiwa spika, kila kukicha kuna taarifa ya mgomo kwenye shirika hili au lile kutokana na wafanyakazi au kunyanyasika, au kunyimwa haki zao, au kubaguliwa. Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli wa Msukosuko wa Kifedha wa dunia, ni vema waajiri wakaa na wafanyi kazi wao na kupanga pamoja namna bora ya kuhimili msukosuko huo ambao unaelekea kwisha.
174: Mheshimiwa Spika, Waajiri wasiachiwe kufanya maamuzi kufanya maamuzi ya kiimla ya kusimamisha wafanyikazi wao. Ninapenda kutoa pia wito wa jumla kwa vyama vyote vya Wafanyakazi kusimamia haki za Wananchi kwa mujibu wa Katiba zao kwani malalamiko haya ya kutelekezwa na vyama katika maeneo ya kazi tunayapata karibu kila mahali.
175: Mheshimiwa Spika, Hali katika Vyuo vyetu vikuu si shwari. Chuo Kikuu cha Dodoma ina hali isiyokawaida ya unyanyasaji unaofanywa kwa misingi ya kisiasa. Mheshimwia Spika, nashukuru kuwa tarehe 13 June, 2010 Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano akiwa amevalia rasmi katika mavazi ya CCM alipokea maandamano ya Wanafunzi. Nimefarijika sana na maandamano hayo. Ni imani yangu kuwa manyanyaso katika Chuo hicho kwa vijana wanachama wa vyama vya upinzani sasa utaisha na vijana wanaweza kufanya siasa kwa uwazi bila kunyanyaswa. Vijana hao walishiriki katika maandamano wakiwa katika Sare za CCM na Mheshimiwa Rais naye akiwa katika Sare rasmi akawapokea na kuwahudumia. Iwapo hiyo inawezekana, basi kumbe wana haki ya kushiriki kwenye shughuli za vyama wanayochagua wenyewe bila kulazimishwa. Nnaamini sasa ukurasa mpya umefunguliwa kwa vijana wetu kushiriki kikamilifu katika Shughuli mbalimbali za Siasa pale wanapoamua kufanya hivyo na kwa kuzingatia Sheria za nchi.
176: Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya ajabu kukataza ushiriki wa vijana wake katika shughuli za Siasa. Wanavyuo ni watu wazima, wana miaka zaidi ya 18 inayotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kufanya shughuli za kisiasa, tena hao ndio wanaoandaliwa kuwa viongozi wa miaka ijayo. Kuwa zuia kushiriki katika siasa ni kuwa nyima haki zao za kisiasa. Mwalimu Nyerere alianza Siasa akiwa mwanafunzi, na bila ushiriki wake katika Siasa, si ajabu Tanganyika isingelikuwa imefika hapa tulipofika leo. Ni muhimu vijana wakawa huru kushiriki shughuli za siasa, ili wapate ujuzi na uzoefu watakaohitaji katika maisha yao ya baadaye.
177: Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka jana (Hansard), nilieleza kuwa nimeletewa barua mbili rasmi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Singida vijijini, wakati ule Mama Bernadetha Kinabo, akiwaandikia Watendaji wote wa wilaya yake, kuwa mtendaji yeyote atakayeshirikiana na Kambi ya Upinzani atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu. Lakini wakati huo huo barua ya pili, anayowaandikia Watendaji wa Vijiji na wa Kata, inawaagiza Watendaji hao watoe, shs 12,000 kwa kila kijiji ajili ya kuwasafirisha wajumbe wa Halmashauri Kuu wanaotoka Mkoa wa Singida kwenda kwenye Mikutano ya kitaifa ya CCM.
178: Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kabisa hapa kuna “double standard”, watakaoshirikiana na Upinzani watachukuliwa hatua, lakini siyo tu inaruhusiwa kushirikiana na CCM bali pia kuchangiwa fedha kutoka fedha mfuko wa kijiji ambazo zinatokana na jasho au mchango wa kila mmoja wana ccm na wa upinzani, na hata wasio na vyama kabisa.
179: Mheshimiwa Spika, Serikali iwe makini na kuingiza ubaguzi kupitia watendaji wa Serikali ni jambo la hatari sana. Tunataarifa pia kuwa Wafanyibiashara wanalazimishwa kuchangia Kampeni za Chama cha Mapinduzi. Kuchangisha mwananchi yeyeyote ni sawa. Lakini kulazimisha ni kinyume kabisa na sheria za nchi hii. Ni imani yangu kuwa Serikali itatoa miongozo sahahi ili haki siyo tu itendeke bali pia ionekane inatendeka .
180: Mheshimiwa Spika, hali hiyo ikiachiwa kuendelea itakuwa vigumu, kuamini kuwa Tanzania ni nchi ya Demokrasia ya kweli, labda ya mdomo tu na mbele ya Taasisi za kimataifa ili kuendelea labda kupata misaada yao. Kambi ya upinzani inapenda kueleza masikitiko yake sana na pia kulaani vitendo hivi vya kulazimisha wananchi kuchangia au kufanya mambo ya kukipendelea Chama cha Mapinduzi na hasa kama vina baraka ya viongozi wa ngazi ya juu. Mfano wa hivi karibuni ni wa Waziri wa Utawala Bora Sofia Simba ambaye kwa kushirikiana na Mary Chatanda Katibu wa Mkoa wa Arusha, waliwalazimisha viongozi wa CCM Kijiji cha Gyekurum Lambo,Wilaya ya Karatu, kuvamia eneo la kijiji/mtaa na kujenga banda la mashine ya kusaga ambayo kwa mujibu wa ahadi hiyo atatoa Mhe. Sofia Simba.
181: Cha kusikitisha, Mheshimiwa Spika ni kuwa eneo lililoshinikizwa ni eneo au mahali pasipofaa kwa kazi hiyo kwa kuwa eneo hilo liko mbele ya ofisi na karibu kabisa na uwanja wa mikutano wa Wananchi. Waziri wa Utawala Bora anadhaniwa kukuza na kulinda utawala Bora na utawala wa Sheria. Lakini kwa Mhe. Sofia Simba ni tofauti yeye ndiye anayeenda kuchochea uvunjifu wa Sheria kama alivyowahutubia wananchi wa Gyekurum Lambo, akidhani anabomoa ngome ya Chadema. Kumbe hafahamu Karatu. Wajinga ndio waliwao.
182: Mheshimiwa Spika, kama matendo hayo hayana baraka za viongozi wa juu, ni imani yetu kuwa wahusika hawa watachukuliwa hatua kwa kuichafulia jina CCM. Serikali na nchi yetu kwa ujumla. Vitendo hivi kutoka kwa watendaji wa Serikali vinashushia hadhi Serikali, wanaonekana kama viongozi wasio na maadili na wala hawajui wanalofanya na badala yake wanawachanganya wananchi. Ni imani yangu kuwa kwa kuwa Waziri Mkuu kiongozi wa Shughuli za Serikali yuko hapa, atakemea vitendo hivyo na kujenga heshima ya Serikali yake.
183: Mheshimiwa Spika, kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuna taarifa mbalimbali za uonezi na unyanyasaji unaofywa na wananchi wakati mwingine kuchukua sheria mikononi mwao. Matukio ya Wananchi kuvamia vituo vya polisi na wakati mwingine kuondoka na wahalifu, au kuwapiga hadi kufa yameendelea hata mwaka huu kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa ya Mwaka 2007/8 ya Tume ya Haki za Binadamu.
184: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika hotuba yangu mwaka 2006, 2007, 2008 na mwaka huu, pia ninaomba nigusie kuwa wananchi katika maeneo mengi ya vijijini wanapata unyanyaswaji mkubwa kutoka polisi na mahakama. Kwenye maeneo haya au wananyimwa haki, hawasikilizwi au wanadaiwa rushwa wazi wazi. Mahali pengine viongozi hasa ma -VEO bado wanawapiga wananchi, au wanawaweka kwenye lock up zisizostahili kama vile kuwaweka kwenye maghala ya mbegu yenye dawa. Wilaya kama Bukombe, Kishapu na zilikutwa hazina mahakama za Wilaya na wananchi wake kuhangaika sana kufuata huduma za mahakama wilaya nyingine, tena kwa gharama kubwa na wakati mwingine kukaa lock up muda mrefu kwa vile ni vigumu kupata wadhamini katika mazingira ya wilaya hizo za mbali.
185: Mheshimiwa Spika, manyanyaso haya yamejitokeza tena katika Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu “Kutozwa gharama kinyume na taratibu/Rushwa. Mheshimiwa Spika, Tume ya Haki za Binadamu ni chombo cha Serikali. Ziara zake zinagaharimikiwa kwa kodi ya wananchi. Kambi ya Upinzani inategemea kuwa safari hii Serikali itatoa Kauli kali dhidi ya manyanyaso haya ambayo dhahiri yako chini ya uwezo wa Serikali kuyakomesha. Mheshimiwa Waziri Mkuu alieleze Bunge hili ni hatua gani Serikali inachukua kukomesha manyanyaso haya.
186: Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa kwa Taarifa ya mwaka 2009 kuna bado unyanyasaji unaotokana na maamuzi mabovu katika ngazi ya Halmashauri za miji, manispa na wilaya, kama vile utekelezaji usio na mpango wa kuwaondoa Wamachinga na Mama na Baba lishe ambayo imewasababishia upotevu wa mali, na kuwarudisha katika lindi kubwa la umasikini na upotevu wa mali pamoja na wengi kukosa kazi na hivyo familia zao kuathirika sana .
187: Mheshimiwa Spika, suala hili nalo liko chini ya uwezo wetu kuliweka sawa. Hatuhitaji fedha kigeni hata kidogo, inatakiwa mipango sahihi na bora tu kuwahudumia wananchi wetu hawa, ambao kwanza katika mazingira ya kawaida wanahitaji msaada wajikwamue katika hali yao ya kiuchumi. Kwa kuwafukuza fukuza, na kumwaga mali zao kidogo tunawafukarisha zaidi, jambo ambalo ni kinyume kabisa na dhana na sera ya Taifa ya Mkukuta.
188: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa mwongozo na maelekezo stahiki kwa Halmashauri za Miji na majiji kusimamia utekelezaji bora wa Mipango miji na kuondoa usumbufu. Mji au Halmashauri itakayoshindwa kutekeleza maagizo hayo ichukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria ikiwa lazima.
189: Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inarudia tena rai yake ya kuitaka Serikali kutazama upya mapema iwezekanavyo sheria na 7 na 8 hadi 11 kwa na kuzihuisha na sheria za Fedha ya Umma na Manunuzi ya umma kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika Serikali za Mitaa na kuondoa migongano iliyoko sasa. Naipongeza sana Serikali kwa kukubali kuwa na mfumo maalum wa wakaguzi wa Ndani hadi ngazi ya Taifa jambo ambalo tunaimani litaimarisha sana usimamizi na udhibiti wa Fedha na rasilimali za umma katika ngazi ya Halmashauri. Ni imani yangu Sheria inayohusu Mkaguzi wa Ndani itawasilishwa Bungeni katika Bunge hili la 20 angalau kupitia Written Laws Miscellaneous Amendment. Hii ni kutokana na umuhimu wa Wakaguzi wa Ndani( Internal Auditors) katika kusimamia fedha za umma na rasilimali mbalimbali za Taifa letu katika ngazi ya Halmashauri, Wizara na Idara zinazojitegemea.
190: Mheshimiwa Spika, ni imani ya Kambi ya Upinzani kuwa kwa vigezo hivi tumejaribu kuonyesha maeneo mbalimbali ya udhaifu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali. Kwa tathmini hii na kwa Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani iliyowasilishwa na Mhe. Hamad Rashid(Mb) wa Wawi na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, ni dhahiri kuwa kuna mapungufu mengi sana katika utekelezaji wa Sera, Ilani na Kauli ya CCM. NI dhahiri kuwa umaskini wetu haukuletwa na Mwenyezi Mungu bali unatokana na Sera zisizo sahihi, vipaumbele vilivyopinda vya Serikali ya CCM, Kauli nyingi tamu katika maandishi lakinii zisizoendana na hali halisi katika tarakimu katika vitabu vya fedha, usimamizi usio makinii wa fedha na rasilimali za umma. Kwaa mapungufu haya, Watanzania ndio wenye kuamua kama wanaridhika na Chama Tawala, CCM ama la, Wananchi wakiwa makini, na kama hakuna mchezo mchafu, na kwa jinsi wananchi walivyochoka na CCM, Kambi ya Upinzani inauhakika ukweli utajuilikana mwezi Oktoba katika Sanduku la kura. Watanzania wanastihili kupewa Taarifa zenye kuwasaidia kuingia katika uchaguzi wakijua masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao.
191: Kambi ya Upinzani inapenda kupata Taarifa na majibu ya kina kuhusu hoja hizi. Mwenyezi Mungu atupe busara zake kama tunavyoomba kwenye Dua kila siku asubuhi.
192: Mheshimiwa Spika Naomba kwa namna ya pekee niwashukuru sana Dr. Kashillilah, Katibu wa Bunge na timu yake ya wataalamu na wahudumu wa Bunge kwa huduma nzuri waliyotoa kwa Kambi yetu kipindi chote cha miaka mitano. Ninatoa pia shukrani za dhati kwa Mratibu wa Kambi ya Upinzani ndugu Oliver Mwikila kwa kuhudumia Kambi kwa muda wa zaidi ya miaka 6 sasa, Ndugu Frank Mbuni, Mama Mahundu na Grace Secretary na Mhudumu kwa huduma nzuri walizotoa kwa kipindi chote. Mheshimiwa Spika naomba nikushukuru tena kwa kunipa fursa hii , na pia nawashukuru waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kunisikiliza.
Mheshimiwa Spika, Nawasilisha.
…………………………………………………
Dr. Willibrod Peter Slaa (MB),
Jimbo la Karatu,
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-
OFISI YA WAZIRI MKUU/TAMISEMI.
16 June, 2010, Dodoma.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment