HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA TAIFA YA BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA) JOHN MNYIKA AKIFUNGUA MKUTANO WA WAWAKILISHI WA WANAVYUO VIKUU VYA MKOA WA DAR ES SALAAM KATIKA VIWANJA VYA MAKAO MAKUU YA CHAMA KINONDONI JUMAPILI TAREHE 25 JULAI 2010
Vijana wenzangu wanavyuo;
Wageni waalikwa na wanahabari;
Ni mara yangu ya kwanza leo kuhutubia vijana wenzangu toka Kamati Kuu ya chama katika kikao chake cha tarehe 25 mpaka 26 Aprili 2010 iliponiteua kuongoza Kamati ya taifa ya BAVICHA katika kipindi hiki mpaka uchaguzi wa vijana utapofanyika baada ya uchaguzi mkuu.
Nimeupokea wajibu huu kwa moyo mkunjufu kwa kuwa umenikumbusha kipindi nilichokuwa Mkurugenzi wa Vijana na hakika ni jukumu muhimu kwa chama hiki cha kizazi kipya wakati huu ambapo ubunifu, uwingi na uthubutu wa vijana unahitajika kuwezesha mabadiliko katika taifa letu.
Awali ya yote naomba tusimame kwa dakika moja ya ukimya kuwakumbuka mashujaa waliomwaga damu yao na kutangulia mbele ya haki wakiwa katika wajibu wa kulinda na kutetea ardhi ya nchi yetu na watu wake.
Nashukuru tumekutana leo tarehe 25 Julai ambayo ni siku ya mashujaa nchini kujadili matendo ya kishujaa yaliyofanywa na yanayokusudiwa kufanywa katika taifa letu.
Tunakutana leo kwa sababu ya tendo la kishujaa la mtanzania mwenzetu Dr Wilbroad Slaa kukubali ombi la kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tendo hili la kishujaa la kuachia jimbo la uchaguzi ambalo alikuwa ana uhakika wa kuletetea na badala yake kugombea nafasi ya urais ambayo baadhi ya watu wametafsiri kama ni ‘kuuawa ama kujiua’ kisiasa.
Kama vile mashujaa walivyokubali kupoteza maisha yao kulilinda na kulitetea taifa, ndivyo ambayo Dr Slaa ni shujaa wa demokrasia na maendeleo kwa kufanya tendo ambalo linaweza kutafsiriwa kuwa ni kutishia maisha yake ya kisiasa hususani katika bunge kwa kuamua kugombea nafasi ya Urais kutokana na kuweka mbele maslahi ya taifa kwanza.
Mashujaa wa aina hii huwa hawafi kwa kuwa fikra zao hukumbukwa milele, uamuzi wa Dr Slaa kujitokeza kugombea wakati huu utaandika historia mpya kwa taifa la Tanzania. Uamuzi huu wa kishujaa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo misingi ya CHADEMA ambayo inaweza kueleweka vizuri zaidi kupitia bendera anayoipeperusha.
Bendera ya CHADEMA ina rangi nne; nyekundu, nyeupe, bluu bahari na nyeusi. CHADEMA ikiwa ni chama kinachothamini mashujaa wa nchi hii imeweka rangi nyekundu katika bendera yake ambaye imefafanuliwa vizuri katika katiba na kanuni za chama kwamba ni ishara uzalendo na upendo kwa taifa.
Leo tarehe 25 Julai wakati sisi tukiwa hapa kwenye mkutano huu viongozi wa kiserikali wako kwenye viwanja vya mnazi mmoja wakifanya maadhimisho ya kinafiki ya kuwakumbuka mashujaa kwa maneno huku kwa vitendo wakiwa wamewasahau na kusahau misingi waliyoisimamia.
Tunu za taifa hili zilizoko kwenye ngao ya taifa ni “Uhuru na Umoja”, hata hivyo tunavyozungumza hivi sasa uhuru huu umetoweka kwa nchi kuwa tegemezi na rasilimali kwa sehemu kubwa kuuzwa kwa bei ya kutupwa kwa wageni huku sehemu kubwa ya watanzania ikiwa hainufaiki na matunda ya uhuru kutokana na kufungwa na kongwa za umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Tanzania imegeuzwa chanzo cha malighafi ghafi, soko la bidhaa duni toka nje chini ya soko holela na watawala kukiunga misingi ya uongozi.
Kwa upande mwingine misingi ya umoja inazidi kutetereshwa kutokana na kupuuzwa kwa utawala wa sheria, kumea kwa ubaguzi na kupanuka kwa matabaka katika jamii kwenye sekta mbalimbali iwe ni afya, elimu na hata mifumo ya haki hali ambayo ni tishio kwa ustawi na usalama wa nchi yetu. Hali hii inahitaji mashujaa kujitokeza kutanguliza mbele uzalendo na upendo kwa taifa ili kulikomboa taifa kwa kuleta mabadiliko ya kweli ya uongozi na mfumo mzima wa utawala.
Dr Slaa ametimiza wajibu huo kwa kusimamia ukweli, uwazi, uadilifu na amani kama rangi nyeupe katika bendera ya CHADEMA inavyowakilisha hususani kupitia kazi yake bungeni, katika jamii na jimboni Karatu katika kipindi cha utumishi wake. Hata hivyo baadhi ya mambo hayajaweza kutekelezwa na serikali iliyopo madarakani kutokana na dola chini ya CCM kutekwa na mafisadi na kuwa na mfumo legelege wa uongozi uliofilisika kidira na kimaadili.
Umefika wakati sasa wa Shujaa huyu kuinuliwa kupewa wajibu mkuu zaidi katika nchi yetu wa kuwa Rais wa Tanzania aweze kuunda serikali na kusimamia utekelezaji ili kurudisha nchi kwa wananchi. Ndio maana tunaunga mkono uamuzi wa Kamati kuu ya chama iliyoketi tarehe 20 Julai kumwomba kugombea urais ili ajaze fomu na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama tarehe 20 Agosti 2010.
Na kabla ya kuanza kuutekeleza wajibu huo akiwa ikulu, uchaguzi ambao kampeni zake zinaanza rasmi tarehe 20 Agosti mpaka 30 Oktoba kabla ya kupiga kura tarehe 31 Oktoba ulipaswa kuwa na mgombea wa uwezo wa Dr Slaa ili uwe sehemu ya mchakato wa kuiwajibisha serikali wakati wote wa kampeni. Dr Slaa akiwa mgombea urais uchaguzi utakuwa ni mchakato wa pekee wa kusambaa kwa elimu ya uraia kwa umma, kuunganisha watanzania bila kujali itikadi katika kuleta mabadiliko, kuibua uozo uliopo na kutoa sera mbadala zenye kuleta tumaini jipya la watanzania kupitia chama na uongozi mbadala. Mchango huu wa kishujaa kwa taifa utapanda mbegu ya mabadiliko ya kisiasa na kuliondoa taifa kutoka kwenye lindi la mazoea ya ufisadi kwa kuhamasisha utamaduni wa uwajibikaji.
Katika kampeni hizo kama sehemu ya dhamira ya pamoja ya kuondoa ukiritimba na hodhi ya chama kimoja kwenye vyombo vya maamuzi Dr Slaa kuwa mgombea urais kwa uzoefu na makini atazunguka nchi nzima kuwanadi wagombea udiwani na ubunge na kuwaongeza nguvu ili tuweze kuwa na wakina Dr Slaa wengi zaidi wazee kwa vijana katika halmashauri na bungeni.
Viongozi hawa mbadala wataweza kujenga taifa lenye kutoa fursa na kutumia vizuri rasilimali za taifa iwe ni mali asili, kodi, utaalamu na vipaji vya watanzania katika kuwezesha maendeleo ya mwanachi kwa ujumla na taifa kwa ujumla kupitia chama mbadala. CHADEMA ikiwa ni chama mbadala kinatambua umuhimu wa kutumia vyema rasilimali katika sera zake na misingi yake, hivyo Dr Slaa atapeperusha bendera ya chama rangi ya bluu bahari ikiwa inawakilisha haki na rasilimali za taifa hususani maji.
Maneno yoyote ya kupingana mwelekeo huu wenye kutanguliza taifa kwanza iwe ni kwa nia njema inayosukumwa na hofu ya ombwe la Dr Slaa bungeni au mashaka ya pengo lake Karatu ama dhamira mbaya ya wapambe wa Kikwete za kuhadaa nafsi za watanzania yanapaswa yapingwe kwa matendo ya wote wenye kuitakia mema nchi yetu kwa kumuunga mkono Dr Slaa kwa hali na mali.
Ndio maana napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza vijana wenzangu wasomi wa vyuo vikuu mlioona mbali kabla hata ya kamati kuu kukaa tarehe 20 Julai kwa kutumia ubunifu na uthubutu wa kuweka saini (petition) ya kumwomba kugombea. Naamini kamati kuu ilizingatia kuwa demokrasia ni utawala wa watu kwa ajili ya watu na kukubaliana na wito wenu na wa makundi mengine katika jamii wakiwemo wanachama wa CHADEMA wa kumuomba kugombea.
Tanzania bila CCM inawezakana kila mtu akitimiza wajibu; hivyo nashukuru kwamba baada ya kufanikisha hatua ya kwanza leo mmeomba kukutana nasi kwa hatua ya pili ya kujadiliana namna ya kufanikisha ushindi.
Hivyo ukiondoa hotuba hii ya ufunguzi leo hakutakuwa na mada za viongozi badala yake tutasikiliza kutoka kwenu mawazo yenu na namna ambavyo mmejipanga kumuunga mkono Dr Slaa katika azma ya kuleta mabadiliko tunayoyataka.
Karibuni katika viwanja vya ofisi ya chama chenye fikra za kuamini katika falsafa ya “Nguvu ya Umma” ambayo inakilishwa na rangi nyeusi katika bendera yetu ambayo ni ishara ya utu wetu: kwamba umma ndio wenye mamlaka juu ya viongozi; umma ndio wenye wajibu wa kuamua hatma ya maisha yao na ya taifa; na umma ndio unaopaswa kunufaika na rasilimali za nchi yetu.
Ni falsafa hii hii ndio tutakayotumia kuwezesha ushindi wa Dr Slaa na ushindi wa wabunge na madiwani mbadala kwa vijana kuwa mstari wa mbele kugombea ama kuunga mkono wagombea ikiwemo kutafuta na kulinda kura kwa kupitia pia falsafa ya Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA) kwamba: Vijana; Nguvu ya Mabadiliko.
Serikali yenye woga wa mabadiliko inayotawala kwa hujuma imetoa waraka na kuziingilia ratiba za vyuo husasani vya umma na kufanya vifunguliwe baada ya uchaguzi kwa hoja kanyaboya na hivyo kukwamisha baadhi yenu kupata haki ya msingi ya kikatiba ya raia ya kupiga kura pamoja na kuwa mlishajiandikisha tayari. Aidha ratiba hii ina dalili zote za kukwepa mshikamano wa wasomi wakati wa uchaguzi kwa kila mtu kuwa likizo katika hali inayoweza kutafsiriwa kuwa ni mpango wa ‘wagawe uwatawale’.
Hata hivyo, ni wakati wa vijana kuwaambia watawala kuwa ‘hatudanganyiki wala hatugawanyiki’, uamuzi wenu wa kukukutana wawakilishi wa wanavyuo mbalimbali kabla ya kutawanyika ili kuunganisha nguvu ya pamoja umefanyika katika wakati muafaka.
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba dhima ya wasomi na kama wajibu wa mtu aliyepewa chakula aweze kupata nguvu ya kwenda kuleta chakula kwa ajili ya wengine katika kijiji chenye njaa; mtu kama huyo asiporudi ni msaliti.
Ni wajibu huu ndio unaopaswa kuwasukuma maeneo yoyote ambayo mtakuwa muifuatilie fursa yenu ya kupiga kura na kufanya hivyo, lakini mnawajibu mkubwa zaidi wa kutafuta kura nyingine nyingi zaidi kwa kuwaelimisha watanzania wengine na kuongoza harakati za mabadiliko ya kweli.
Katika kushinda uchaguzi vipo vipaumbele vinne ambavyo naomba nivitaje kwa kadiri ya umuhimu wake kama sehemu ya kuibua majadiliano yetu siku ya leo; mosi, mgombea; pili, ajenda; tatu, oganizesheni na nne; rasilimali.
Kwa upande wa Urais mgombea tayari tunaye ambaye anasubiri tu kuthibishwa na mkutano mkuu baada ya michakato kukamilika; wa upande wa ubunge na udiwani pia katika maeneo mbalimbali ya nchi wapo wagombea wamejitokeza ingawa milango bado iko wazi kwa kuwa tarehe ya mwisho ya uchukuaji na urudishaji fomu ndani ya chama ni tarehe 9 Agosti kabla ya uteuzi wa kiserikali Agosti 19. Kwa bahati njema pia sehemu kubwa ya wagombea ni vijana wenzetu na wazee wenye kutaka mabadiliko. Hivyo mnawajibu wa kwenda kuwaunga mkono wagombea katika maeneo ambayo mnakwenda.
Kipaumbele cha pili ni ajenda za kisiasa ambazo katika uchaguzi huwekwa katika ilani. Tayari kamati kuu ya chama imepokea rasimu ya ilani na mchakato wa kuiboresha unaendelea kwa kuzingatia mawazo na maoni mbalimbali unaendelea mpaka itakapopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama Agosti 12 mwaka huu. Hivyo, nyinyi kama vijana wasomi wa kada za mbalimbali mna wajibu wa kushauri hoja za kuwekwa kwenye ilani katika sekta mbalimbali ambazo mmezisomea na mnaendelea kuzisomea kwa kuzingatia pia hali halisi ya taifa na watanzania kwa sasa. Majadiliano ya leo yatawezesha kuanza kupokea maoni yenu si tu ya kuchambua hali ilivyo chini ya uongozi wa CCM bali pia kupendekeza CHADEMA ifanyeje pindi ikiingia katika uongozi ama ni Tanzania ya namna gani mngependa ijengwe na chama mbadala. Pamoja na kuwa CHADEMA inazo sera zake na mwaka 2005 ilikuwa na ilani ambayo mnaweza kuirejea kupitia www.chadema.or.tz bado tunaamini kwamba chama cha siasa kina wajibu wa kuwasikiliza wananchi badala ya kujifungia na kuandaa ilani zisizosingatia hali halisi ya taifa.
Kipaumbele cha tatu ni oganizesheni ya kampeni ikiwemo mikakati mbalimbali ya kujipenyeza katika jamii kwa kutumia mbinu na timu mbalimbali. Hivyo, natarajia kikosi hiki kitasambaa katika maeneo mbalimbali na kutumia ubunifu, nguvu, uwingi na uthubutu wa vijana kufanya kampeni za kipekee kama ambavyo mtabadilishana mawazo katika mkutano wa leo. Tanzania bila CCM inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu.
Kipaumbele cha nne ni rasilimali, izingatiwe kwamba tayari CCM imeshaanza na imejipanga kutumia nyenzo ikiwemo za dola/serikali na fedha nyingi zikiwemo za ufisadi na ubadhirifu katika kulazimisha ushindi kwa ushahidi wa nyaraka ambazo binafsi ninazo mpaka sasa ambazo zitatolewa katika wakati muafaka. Ni wajibu wetu kushirikiana kuwaumbua kila mahali mipango yao ya kiharamia lakini ni wajibu wetu pia kutumia mbinu mbadala na rasilimali mbadala za kukabiliana na hali hiyo. Rasilimali mbadala kwa kutumia nguvu ya umma ni pamoja na vijana wasomi kama nyinyi kujitolea utaalamu wenu, muda wenu, vipaji vyenu na nguvu yenu kuwezesha maandalizi, kampeni na ulinzi wa kura. Haya ni kati ya mambo ambayo ni muhimu mkayatafakari katika mkutano wa leo.
Historia ya duniani inaonyesha kwamba mchango wa vijana na wanafunzi ni wa muhimu sana katika kuanguka kwa tawala za kidikteta, za kibaguzi na za kifisadi. Historia kama hii inapaswa kuandikwa nchini mwetu kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi ili kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.
Tuyafanye hayo tukitambua kwa pamoja kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa Ari, Nguvu na Kasi (ANGUKA) zaidi. Kwa falsafa ya chukua chako mapema(ccm), ya chama cha mafisadi(ccm); Tanzania yenye neema haiwezekani. Tuunganishe nguvu kurudisha nchi kwa wananchi; Tanzania bila CCM inawezekana kupitia chama mbadala na uongozi bora.
Natangaza kwamba mkutano huu umefunguliwa rasmi na tuko tayari kuwasikiliza; Vijana, Nguvu ya Mabadiliko.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment