HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI DR.WILLIBROD PETER SLAA(MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
KWA
MWAKA WA FEDHA 2007/2008:
UTANGULIZI:
1: Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani kuwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2007/2008 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 43(5)(c) na 81(1) Toleo la Mwaka 2004.
2: Mheshimiwa Spika,
Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi wa Karatu walionichagua kwa kipindi cha tatu kuwa Mbunge wao. Ninawashukuru hasa kwa imani waliyokuwa nayo siyo kwangu tu, bali pia kwa Madiwani wetu wa Chadema kiasi cha kukifanya kwa mara nyingine tena CCM kuwa Chama cha Upinzani Wilayani Karatu. Tunawapongeza sana wananchi hao kwa kuona tofauti ya dhahiri kati ya uongozi wa CCM na wa Chadema. Wameona kwa vitendo maendeleo ambayo kwa miaka 40 chini ya CCM hawakuyapata. Mimi pamoja na Madiwani wangu wa Chadema tunawahakikishia kuwa hatutawaangusha na kuwa kama walivyofurahia matunda ya dhamana waliyotupa kwa maana ya Maendeleo yanayoonekana, kwa kipindi hiki pia tutafanya kila jitihada kutimiza ahadi zetu mbalimbali kwa mujibu wa ilani tuliyoiuza wakati wa kampeni.
Mheshimiwa Spika, Kwa msingi huo huo, nawapongeza pia Wananchi wa Bariadi kwa kuichagua UDP na kuifanya pia ‘Chama Tawala’ Bariadi. Natambua kuwa dhana hii ni mpya kwa wengi wetu. Katika Demokrasia halisi Chama kimoja kushinda uchaguzi kitaifa, vyama vingine vikashinda na kuwa na madaraka ya uongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa ni jambo la kawaida.
Mheshimiwa Spika, Nawapongeza kwa namna ya pekee sana Wananchi wa Pemba, ambao kwa uamuzi na hiari yao wameifanya CUF kuwa ‘Chama Tawala’ Pemba. Ni imani yangu kuwa Serikali Kuu itaheshimu daima maamuzi haya ya Wananchi na kujenga nchi ya Demokrasia ya kweli.
3: Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyosema katika Hotuba yangu mwaka uliopita, ninatoa tena mwito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na CCM kuwa njia pekee ya kupeleka maendeleo ya nchi yetu mbele ‘ni kuanzisha rasmi na kwa vigezo wazi mashindano ya maendeleo kati ya wilaya zinazoongozwa na Upinzani na zile zinazoongozwa na ‘Chama cha Mapinduzi’. Ninawapongeza vile vile Madiwani wa Chadema na wa CCM kigoma ambao wametoa funzo kubwa kwa Tanzania nzima kwa kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Madiwani Mseto, baada ya kuwa na nguvu zinazolingana. Hili ni funzo kwa vile wako wanaofikiri hakuna uwezekano wa Serikali ya Mseto Tanzania hata kabla ya kufanyia marekebisho makubwa Katiba na Sheria zetu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
Mashindano haya yatatoa kwa Wananchi nafasi ya kupima utendaji kati ya Halmashauri zinazoongozwa na CCM na zile zinazoongozwa na vyama vingine. Huu ndio ukomavu wa kisiasa na demokrasia katika nchi yetu na ishara ya wazi kuwa Serikali na Chama Tawala kitaifa kweli vimedhamiria kimatendo kuruhusu mfumo wa vyama vingi nchini tofauti na hali ya sasa ambapo viongozi wa vyama vingine “wananunuliwa” au kurubuniwa kwa mbinu chafu.
Mheshimiwa Spika,
Haya yalitokea hivi karibuni kule Kigoma, au lile tukio la aibu na la kihistoria ambapo Mgombea U-Meya kwa tiketi ya CCM Bwana Nashon Bidyanguze alifanya jaribio la kumtorosha Diwani wa Chadema Bi Bahati Shabani Rehani toka Kigoma hadi Dar-Es-Salaam kwa malengo ya kisiasa. Mtego uliowekwa na Bi Bahati kwa kushirikiana na uongozi wa Chadema Makao Makuu ndio uliozuia jaribio hilo. Jambo hilo ni kinyume kabisa na maadili mema. Kwa bahati mbaya Mgombea U-Meya huyo wala hakuchukuliwa hatua au ya kinadhamu au ya kimaadili na chama chake licha ya kukiabisha na kuliaibisha taifa zima kwa kitendo hicho.
4: Mheshimiwa Spika,
Napenda kumshukuru Mhe. Edward Lowassa,(MB), Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Mizengo Pinda Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Manaibu wao, Makatibu Wakuu pamoja na wataalamu wote kwa Bajeti iliyowasilisha Bungeni hivi punde. Napenda kuwapa pia pole kwa kazi kubwa wanayoifanya katika mazingira magumu.
5: Mheshimiwa Spika,
Nitakuwa mtovu wa shukrani iwapo sitakushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie hekima na busara na kuwapatia nguvu na afya mnazohitaji katika kuliendesha vizuri Bunge letu.
MASUALA YA JUMLA YA BAJETI MWAKA WA FEDHA 2007/2008:
6: Mheshimiwa Spika,
Kabla sijaanza kujadili Hotuba ya Waziri Mkuu, naomba nitoe maelezo yafuatayo:-
(i) Ninawasilisha ndani ya Bunge lako Tukufu maoni ya chombo kinachojulikana kama ‘Kambi ya Upinzani”. Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inatambuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kifungu cha 11 hadi 13 na pia kifungu cha 83A, Toleo la 2004.
(ii) Kambi ya Upinzani imetafakari kwa kina maana halisi ya maneno ‘Vyama vya Upinzani’, au Kambi ya Upinzani na kugundua kuwa maneno haya yana maana hasi katika mila na desturi za mwafrika tofauti na neno ‘Opposition’. Kilichofanywa na Kanuni ya sasa ni kuchukua tafsiri ya neno la kiingereza ambayo katika falsafa ya mwingereza haina maana sawa na ‘kupinga’ kama neno hilo linavyoeleweka kwa mwafrika. Kwa wenzetu mara nyingi badala ya neno ‘opposition’ hutumika zaidi ‘ Minority Party’ kwa nia ya kuepuka tafsiri hiyo hasi ya neno ‘opposition’.
7: Mheshimiwa Spika,
Kwa vile suala la jina, ni uchaguzi wa mwenye jina hilo, tunawasilisha kwako kuwa Kambi ya Upinzani imebadilisha jina lake na sasa itakuwa inaitwa ‘KAMBI YA USHINDANI’ na tunapenda tutambulike hivyo. Maana halisi ni kuwa Vyama vya siasa huwa vinashindana kwa lengo la kutaka kuingia kwenye Utawala. Vinakwenda kwa wananchi kushindanisha Sera na Ilani zao. Hivyo dhana ya Upinzani haiko kwa vile hakuna anayempinga mwenzake bali Vyama vinashindana. Ni imani yetu kuwa Ofisi yako itapokea jina hili jipya na itakuwa ndiyo jina rasmi la Kambi yetu. Kwa vile jina Vyama vya Upinzani halitajwi popote kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Sheria ya Uchaguzi wala Sheria ya Vyama vya Siasa hatuoni kuwa badiliko hili linaweza kuwa na kikwazo.
8: Mheshimiwa Spika,
Vyama vyetu pia moja moja au katika umoja wao, vinaweza kwa wakati wao kuchukua jina hilo au jina lingine lolote linaloendana na falsafa na fikra za mwafrika. Hadi hapo Kanuni zitakaporekebishwa, tutaendelea kutumia neno ‘Kambi ya Upinzani’, lakini ikieleweka kwa tafsiri hii ya Ushindani na siyo “Kupingana”.
9: Mheshimiwa Spika,
Hii ni bajeti ya pili tangu Serikali ya Awamu ya Nne iliposhika uongozi wa nchi yetu. Kambi ya Upinzani inatoa maoni yake kwa kufanya tathmini ya Malengo na Mwelekeo wa kazi za Serikali katika vipindi mbalimbali vya nyuma ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa kipindi cha tangu waliposhika madaraka. Pamoja na tathmini hii ninapenda niseme machache kuhusu Bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha kwa ujumla na maoni yetu kuhusu majibu yake ndani ya Bunge hili 22 June, 2007.
a) Mhe. Spika ni kweli Kanuni zetu Toleo la 2004, hazisemi kitu kuhusu Bajeti ‘Mbadala’. Hili lilisema wazi katika Hotuba ya Bajeti ya Waziri Kivuli. Hatukutegemea kama hili litakuwa na mjadala tena.
b) Mhe. Spika, hata hivyo anayebishia dhana ya Bajeti mbadala ni yule asiyefahamu utendaji kazi wa Bunge katika mfumo wa Vyama Vingi. Bajeti mbadala kwa kifupi ni Maoni ya Kambi isiyo madarakani kuwa tungekuwa sisi na ridhaa ya kutawala tungelifanya mambo kwa utaratibu huu. Bajeti ya Kiongozi wa Upinzani ilifanya hivyo na si zaidi.
c) Mhe.Spika, mawazo ya kuwa hakuna Bajeti mbadala hadi uwe serikalini ni mawazo potofu ya watu wasioenda na wakati, na wala hawafuatilii kinachoendelea duniani. Mifano hai iko Zambia, Mauritius, Uganda na India ambako kamati yako ndogo,( Kamati ya Ndugai) Mhe. Spika ilipata fursa ya kutembelea na kujionea utendaji kazi katika mabunge hayo.
d) Mhe. Spika, Maoni ya Kambi ya Upinzani yaliyowasilishwa na Waziri kivuli yanaonyesha kuwa Kambi ya Upinzani ingelikuwa Serikalini ingeliweza kukusanya Tshs Trilioni 5.3 badala ya Trilioni 3.5 inayokusanywa na Serikali sasa. Bajeti ya Kambi ya Upinzani ni ziada ya Trilioni 2.2. zaidi ya ile ya Serikali.
e) Mhe.Spika, Na hizi ni fedha ambazo Serikali ingelikuwa makini ingezikusanya kutoka Rasilimali zetu za ndani, mathalan mali asili, madini yetu na vito, mifugo yetu, udhibiti wa misamaha ya kodi, kutekeleza na kusimamia sheria zilizoko vizuri zaidi. Hakuna hata senti moja ya mfadhili katika ziada hii.
f) Mhe.Spika, mapato haya yangeongezeka kufikia Trilioni 5.3 bila kumgusa mwananchi wa kawaida zaidi ya kiwango cha kodi anazolipa sasa. Hii ina maana kuwa kwa mapendekezo ya Kambi ya Upinzani tungeweza kutekeleza mipango mingi zaidi ya maendeleo kuliko ilivyo katika Bajeti ya Serikali.
g) Mhe. Spika huu ndio ubunifu uliokosekana kwa upande wa Serikali. Mtu yeyote aliyesikiliza na kutafakari mawazo mbadala au upande wa pili wa shillingi asingelishindwa kutambua kuwa Maoni ya Kambi ya Upinzani yanapunguza utegemezi kwa wafadhili kutoka asilimia 42 ya sasa ya Serikali ya CCM kufikia asilimia 31.8. Kuna uzalendo zaidi ya huu?
h) Mhe.Spika, licha ya mbwembwe za Mhe. Waziri, hajaweza kukosoa kwa hoja yoyote Maoni ya yaliyowasilishwa na Kambi ya Upinzani. Kwa bahati mbaya kabebwa na ushabiki wa kisiasa, ambao kimsingi hausaidii Taifa letu wala wananchi wetu.
i) Mhe.Spika, tunawaachia Watanzania wachambue mchele kutoka pumba. Tunaamini Ujumbe umefika na ndiyo lengo la maoni ya Kambi ya Upinzani, kuwaonyesha Watanzania kuwa “Inawezekana tukiwa na uzalendo, tukiipenda nchi yetu, tukiwa wabunifu na tukiacha kufanya kazi kwa mazoea”.
j) Mhe. Spika, hoja siyo usitoze kodi, na wala wananchi wasilipe kodi. Hoja ni kuwa kuna kiwango cha kuwakamua watu maskini. Waziri amesahau kuwa serikali hii hii, miaka michache tu iliyopita ilifuta ushuru wa “Upe” wa shs 2,000/ kwa vile wananchi wengi walikuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule kwa ajili ya shs 2,000. Ushuru huu ukaitwa ‘ushuru na kodi zenye kero’. Leo unawapiga kodi lukuki, tena Kwa njia mbaya kama kupandisha kodi ya mafuta ya aina zote, ambayo kimsingi inaathiri gharama zote za maisha.
k) Mhe. Spika, Mhe. Waziri amesahau kuwa asilimia 35.4 ya watanzania wako katika kiwango cha chini cha ‘Mahitaji ya Msingi’ yaani katika kila watu 100, watu 35.4 ni maskini wa kutupwa. Nyumba za kulala wasiwasi, chakula cha kubangaiza na hata mavazi yao. Hawa ndio watu ambao Mhe. Waziri anataka waendelee kukamuliwa wakati kuna vianzio vingine vingi tu vinavyoweza kuliingizia Taifa mapato mengi. Hapa tatizo ni “Mind Set”, ni kufanya kazi kwa uzoefu au kukosa uzalendo kama tulivyosema.
l) Mhe. Spika, kwa kifupi huwezi kuongeza tu kodi kwa mwananchi wakati kuna vianzio vingi vimeachwa nje; wakati udhibiti wa fedha hauko imara; wakati mabilioni yamekaa tu kwenye akaunti zilizofungwa miaka mingi na mengine mengi.
m) Mhe. Spika, Maoni ya Kambi ya Upinzani siyo tu yameonyesha vipaumbele vile vile vilivyoonyeshwa na Serikali, bali tumeongeza kipaumbele kingine ambacho Serikali haikuona yaani ‘Utawala Bora’. Wakati Bajeti ya Serikali imetoa asilimia 18 Kwa elimu, Mapendekezo ya Kambi ya Upinzani ni asilimia 20, Miundo mbinu tumeipa asilimia 21 karibu mara tano ya Bajeti ya Serikali, kilimo tumekipa asilimia 12 badala ya 6.2 ya Serikali na kadhalika. Serikali isiingize itikadi katika masuala ya kitaifa? Tunahitaji kwa pamoja, kulikomboa nchi yetu kutoka lindi kubwa la umaskini.
Serikali itupe majibu kwa hoja, wakati wa ushabiki wa kisiasa umepita, kwani wakati tunaendelea na ushabiki wa kisiasa dunia haitusubiri, inaenda mbele. Tunaisihi Serikali na wabunge wenzetu wa CCM tufanye kazi kwa uzalendo. Wananchi tunaowasemea ndio hao hao watakaowachagua tena mwaka 2010. Tuwaonee huruma.
n) Mhe. Spika, Waziri wa fedha hatimaye alisema ‘Kambi ya Upinzani haina Uzoefu’. Ukweli ni kuwa Alhamisi wakati waziri anasoma Bajeti yake alikuwa amegawa vitabu vya Bajeti Volume 11 yenye cover Pink. Baada ya kusoma Bajeti yake amegawa Volume 11 nyingine safari hii yenye Cover Blue.
o) Mhe. Spika, vitabu hivi viwili vinatakwimu tofauti. Chukua mathalan Kasma ya 25 Ofisi ya Waziri Mkuu. Kitabu Pink wakati anasoma Bajeti yake ilikuwa na Makadirio ya Matumizi ya Jumla ya (Net Total) 4,011,489,000.
p) Mhe. Spika, kitabu kilichotolewa baada ya Bajeti (Blue) kwa Kasma hiyo hiyo, kina jumla ya (Net Total) 3,372,489,000. Vote 37 Ofisi ya Waziri Mkuu, nayo vivyo hivyo. Kitabu kinaonyesha jumla ya Tshs 12,332,530,800 wakati kitabu Blue kinaonyesha Tshs 10,442,530,800. Sasa ipi ni ipi?
q) Mhe.Spika, huu ndio utaratibu anaosema Waziri unaeleweka? Huu ndio uzoefu anaosema Waziri anao kuliko Kambi ya Upinzani? Je, Waziri anafahamu kuwa kwa taarifa zilizoko yeye ni waziri wa kwanza tangu uhuru aliyewachanganya Wabunge kwa kutoa vitabu viwili kwa matumizi ya aina mmoja na wala hajaomba hata msamaha kwa wabunge kwa makosa hayo? Waziri anajua kuwa sababu moja ya hali hiyo ni kutokuwa makini wakati wa maandalizi kiasi cha kutokuweka fedha kwa miundo mbinu hadi Kamati ya Fedha na Miundombinu (ambamo na wapinzani wapo) ziliposhinikiza kupatikana kwa fedha hizo.
r) Mhe.Spika, wakati mwingine uungwana ni muhimu na hauna gharama licha ya kwamba unajenga kuheshimiana na kuaminiana.
10: Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Bajeti iliyowasilishwa na Waziri Kivuli ni kielelezo kamili, ninapenda kusisitiza kuwa maoni yetu kwa Bajeti , ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyoko kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, ni kama tulivyoeleza hivyo sitahitaji kurudia kuchambua tena Bajeti hiyo. Badala yake nitajielekeza sasa kwenye maeneo machache muhimu ya utendaji wa Serikali, maeneo ambayo Serikali inayaombea fedha za Matumizi. Mhe. Spika pale inapotakiwa tutatoa Maoni yetu mbadala, kutaka maelezo kamili kutoka Serikalini na au kuitaka Serikali kuchukua hatua mahususi.
11: Mheshimiwa Spika,
Waziri wa Fedha alitoa majibu yake ndani ya Bunge hili na mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni, na kwa kuwa alizungumza zaidi kisiasa bila kujibu hoja za msingi, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, tunaitaka Serikali sasa ituhakikishie yafuatayo:
a) Serikali sasa ikanushe au itoe Tamko kuwa kiwango cha Magogo kilichouzwa China cha cu.mita 18,316 X $150 kwa Taaarifa za Tanzania, ambapo vitabu vya China vinaonyesha cu.mita 108,605 x $ 450 na kuwa kwa kiwango hicho cha under-declaration, Serikali imepoteza $ 40.6 Millioni ( sawa na Tshs 52.8 billioni). Hiki ndicho kigezo cha uhakika kama taarifa ya Upinzani ni ya kweli au si kweli, kuna uzoefu au hakuna, na wala si maneno tu ya kisiasa. Serikali isipige siasa wakati nchi inateketea.
b) Iwapo takwimu hizo ni sahihi, au kama Serikali haina taarifa kamili kama alivyokiri Waziri wa Mali Asili na Utalii, je Serikali inakubali kuwa kulikuwa na uzembe katika kusimamia rasilimali zetu? Na je wahusika wa uzembe huo wamechukuliwa hatua gani au watachukuliwa hatua gani ikizingatiwa kuwa Mhe. Meghji alikuwa ndiye Waziri wa Mali Asili na Utalii kwa wakati huo? Haiwezekani kuwaadhibu wananchi kwa kodi isiyo lazima wakati Serikali inaacha makusudi kuchukua hatua za udhibiti na usimamizi kama walivyokabidhiwa dhamana.
c) Serikali itoe maelezo ya kina, ambayo Waziri Meghji hakujibu, kwanini takwimu za Soko la Dunia zinaonyesha mauzo ya Tanzanite ambayo inapatikana Tanzania tu, kuwa $ 400 Millioni, wakati takwimu za Tanzania zinaonyesha $ 16 Millioni tu. Je Serikali inasema nini kuhusu kukosekana kwa mkakati wa udhibiti wa mapato ya Serikali ambao umeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Tshs 100 Billioni kama tulivyoeleza kwenye maoni yetu?
d) Je Serikali inasema nini, kwa takwimu hizi tu bado kuna haja ya kumkamua mwananchi wa kawaida kupitia kodi ya Mafuta? Serikali ilichofanya ni kiini macho kwa kuhamishia kodi ya Mafuta ya Taa ya shs 4 kwenye Kodi ya Mafuta aina ya Petroli na Dieseli. Serikali inafahamu kuwa kusafirisha Mafuta ya Taa unahitaji Dieseli na kama gharama ya Dieseli iko juu, hata ya Mafuta ya Taa haitashuka. Mwananchi wa kawaida ndiye atakayeendelea kuathirika.
e) Mhe. Spika, Japo sihitaji kutetea vyombo vya habari, lakini duniani kote Vyombo vya Habari ni mhimili wa Nne, baada ya Bunge, Utawala, na Mahakama. Ndio wenye kudodosa na mara nyingi huwa wa kwanza kugundua mapungufu ya Serikali kutokana na taaluma yao ya Uandishi, (hasa Investigative Journalism). Vyombo vinavyosimamia utendaji wa Serikali, mathalan Wabunge hutumia Taarifa hizo kwa kuitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa mambo yaliyoko kwenye vyombo hivyo vya Habari kujua ukweli. Waziri Mkuu analiambiaje Taifa sasa kuhusu hili? Je Vyombo vya Habari visiandike mambo hata kama yana ukweli na manufaa kwa Taifa hili kwa vile tu hayaifurahishi Serikali? Je, Serikali anayoisimamia sasa iko tayari kutangaza rasmi kuwa vyombo vya Habari vinafanya kazi pale tu vinapoisifu na kuipigia debe Serikali? Kambi ya Upinzani ilidhani Serikali makini, ni ile ambayo inapogundua kasoro fulani tu kupitia chombo cha Habari, mara mmoja inachukua hatua na kufuatilia kasoro hiyo.
12: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani imefarijika sana kuwa Mhe. Waziri wa Fedha amekiri kufahamu Taarifa niliyoitoa hapa Bungeni kuhusu Ubadhirifu mkubwa ndani ya BOT unaomgusa Govana wa Benki Kuu, pamoja na Wafanya biashara wengine wakubwa akiwemo Mbunge kupitia kampuni anayoimiliki.
13: Mheshimiwa Spika,
Wakati akichangia hoja ya BOT siku ya tarehe 20 June, Mhe. Mzindakaya alitoa tuhuma nzito dhidi ya wabunge, na ni nanukuu “ “……kama kuna mambo mazito na ambayo Mbunge angependa kuyasema, mimi nafikiri kuhutubia habari za Internet haitoshi kuwa ndio ushahidi sahihi kwa sababu baadhi ya mambo tunayoyafahamu sisi wengine tumefayafanyia research… ..kwanza takwimu si sahihi. Takwimu sio dola milioni 200, ni dola milioni 131, ndio takwimu sahihi.
Pili, baadhi ya wafanyabiashara wanaweza wakatumia ujanja wa kuwatumia Wabunge waje wawasemee mambo yao au tofauti zao katika biashara. Na jambo hili linahitaji kuliangalia…bahati nzuri habari hii naijua kutoka kwa mhusika mwenyewe…”
14: Mheshimiwa Spika,
Hapa mambo kadhaa yanajitokeza na kwa kuwa yamesemwa Bungeni ni vema nikayazungumzia pia Bungeni.
(i) Mhe. Spika Kwanza kabisa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kifungu cha 49(7), na ninaomba kunukuu “Mbunge hatazungumzia jambo lolote ambalo yeye mwenyewe ana maslahi ya kifedha nalo, isipokuwa baada ya kutaja jinsi anavyohusika, na kiwango cha maslahi hayo”. Mheshimiwa Mzindakaya hakutamka lolote kuhusu maslahi yake katika jambo hili.
(ii) Mhe. Spika, utafiti wetu unaonyesha kuwa mwaka 2004 Mhe. Mzindakaya alichukua mkopo kwa shughuli zake binafsi wa Tshs 9.7 Billioni Benki ya Standard Charter kwa kudhaminiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambako Gavana wa Benki ndiye kiongozi mkuu na ndiye mhusika mkuu katika tuhuma zilizotajwa. Hivi sasa, mwaka huu wa 2007, baada ya miaka 4 ya deni hilo kutokulipwa Benki Kuu sasa kama mdhamini imewajibika kuilipa Benki ya Standard Charter.
(iii) Mhe. Spika, hivi sasa, Mhe. Mzindakaya ameomba adhaminiwe na BOT mkopo mwingine tena wa Tshs Billioni mbili (2). Mkopo huo uko kwenye hatua ya kujadiliwa na BOT, ama kuidhinishwa ama la. Mhe. Spika, hapa ieleweke kuwa hatuzungumzii uhalali au vinginevyo wa mkopo wa Mhe. Mzindakaya. Tunazungumzia kukiukwa kwa kanuni ya Bunge, na tunazungumzia dhana anayotaka kujenga Mhe. Mzindakaya dhidi ya baadhi ya Wabunge kwa Watanzania. Haya yote mawili na mambo mazito sana.
(iv) Kauli ya Mhe. Mzindakaya ambayo kimsingi ilielekezwa kwangu Kwa vile ndiye niliyenukuu taarifa ya Internet, inataka kutoa dhana kwa watanzania kuwa baadhi ya Wabunge, nikiwemo mimi hatufanyi ‘Research’ (yaani utafiti) ila yeye tu ndiye anayefanya ‘Research’. Hili ni tusi Kwa Bunge hili, Kwa Watanzania waliotutuma tuwasemee, na linalenga kuupotosha umma wa Watanzania kuwa kuna wabunge wanakurupuka tu kusema mambo bila kufanyia utafiti.
(v) Kauli yake ni tuhuma nzito hasa anapojenga uwezekano wa baadhi ya wabunge na nina nukuu ‘…kutumika na Wafanyabiasha wa nje wawasemee mambo yao au tofauti zao za kibiashara’. Hii inajenga dhamira potofu kwa watanzania kuwa kuna wabunge, hawana dhamira yao wenyewe, hawajui wanalolifanya ila wanatumika kama chombo, dhamira ya kutumika pia linaweza kueleweka kuwa wananunuliwa.’ Hii ni kauli nzito sana kusemwa dhidi ya mbunge yeyote, wa upinzani au wa Chama Tawala, kwa sababu wote ni wabunge kama Mhe. Mzindakaya, tumechaguliwa na Wananchi wetu kama Mhe. Mzindakaya.
(vi) Mhe. Mzindakaya hajaeleza kwanini awe na mawazo hayo potofu, au kwa vile yeye ni Tajiri na sisi wengine anadhani ni malofa hivyo ni rahisi kuhongwa na kununuliwa? Lakini hata yeye utajiri mbona kaupata kwa fedha alizokopa kwa mdhamana wa BOT ambazo Watanzania wote matajiri na maskini, sasa wanazilipa kwa kodi yao kupitia BOT?
(vii) Mhe. Mzindakaya anajikanyaga pale anapokiri kuwa Takwimu sahihi ni Dola 131Millioni na siyo dola millioni 200 ambazo hata hivyo mimi nilitaka Serikali ithibitishe. Au Mhe. Mzindakaya anaona ni halali Dola 131 Millioni zikiibiwa ila siyo Dola 200 Millioni? Kama takwimu zake zinathibitisha upotevu huo ni vipi Mhe. Mzindakaya anayejulikana kulipua mabomu hapa Bungeni, mtetezi wa wanyonge, leo awageuke wanyonge na kuwa msemaji wa Serikali katika kumtetea Gavana wa BOT.
(viii) Mhe. Spika, hapa tukisema, Mhe. Mzindaka anasukumwa na fadhila aliyopewa na Gavana kwanza kumdhamini mkopo wake wa zaidi ya Billioni 9, kulipiwa deni hilo na sasa anataka Gavana huyo huyo amdhamini tena mkopo wa Billioni zingine 2 tutakuwa tumekosea? Nawaachia Watanzania kutoa hukumu ya nani hafanyi Utafiti kati yetu sisi na Mhe. Mzindakaya, nani mtetezi wa wanyonge kati yetu sisi tunaoanika hadharani taarifa za uozo ndani ya Benki kuu na Mhe. Mzindakaya ambaye analenga wazi kuuficha. Waheshimiwa Wabunge, uzalendo hauna gharama, unahitaji dhamira safi tu, mtu uwe msafi mwenyewe, na uwe tayari kujitoa sadaka unapotaka haki na ukweli.
(ix) Mhe. Spika, kwa yeyote mwenye kuhitaji taarifa zaidi anaweza kwenda BOT, ni mali ya Serikali na kwa utaratibu wa kawaida akathibitishe niliyoyasema kuhusu mkopo wa Mhe. Mzindakaya.
(x) Mhe. Spika, Kauli hiyo ya Mhe. Mzindakaya inazidi kutoa utata. Kuna nini Benki Kuu? Jambo linalothibitisha uharaka wa uchunguzi wa kina. Kama hilo halitoshi, taarifa nyingine za uozo ndani ya BOT zinazidi kuibuka kila kukicha.
(xi) Mheshimiwa Spika, Magazeti yote Nipashe, Mtanzania, Mwananchi ya June 24, 2007 yamemnukuu Mhe.Rais wetu akipiga kelele kuhusu ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha za umma, matumizi mabaya ya ofisi kwa maslahi binafsi. Kambi ya Upinzani kama tulivyokwisha kumwahidi Rais, tuko nyuma yake na tunamwunga mkono katika vita hii. Kambi ya Upinzani inawaomba Waheshimiwa wabunge wote wa CCM, wote wenye nia njema, tuweke itikadi zetu pembeni, tumwunge mkono Mhe. Rais wetu katika hili.
15: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inazidi kustashwa na taarifa za kiwango cha ubadhirifu na hujuma, mathalan Malipo yenye mashaka makubwa ya 40 Billioni kama ilivyoripotiwa na Gazeti la Daily News, (Daily News, Issue no. 0856-3812 na 9315 la 22 June 2007, p.1), tena Gazeti la Serikali, na taarifa hiyo mpaka sasa haikukanushwa.
16: Mheshimiwa Spika,
Haiingii akilini mwa mtu yeyote kuwa Kampuni ya Kagoda Agricultural Ltd ilisajiliwa tarehe 29 Septemba, 2005 na ndani ya wiki zisizozidi nane tayari ilikuwa imeishapewa fedha zaidi ya shilingi 30.8 Billioni kupitia External Service Debt Account na Benki Kuu, ambayo Gavana ndiye msimamizi mkuu.
17: Mheshimiwa Spika,
Taarifa hiyo bado inaonyesha kuwa mikataba 9 ilisainiwa tarehe 18 na 19 Oktoba na makampuni 12 ya nje chini ya mkataba na Kampuni ya Kagoda Agricultural Ltd. Pamoja na kasoro zilizojitokeza kwa mujibu wa Taarifa ya Wakaguzi ni kuwa nyaraka zilizotumika hazionyeshi makampuni yao (letter head), majina yaliyotumika kwa wakopaji hao yanatia mashaka, walioweka saini kwa niaba ya Serikali za Ujerumani, Italia, Uingereza, Japan, Yugoslavia, Ufaransa na Marekani hayakuweza kutambulika kabisa na Mkaguzi alipowasiliana na Makampuni husika. Kuna haja ya kufahamu undani wa Kampuni hii, je wamiliki ni hawa tu walioorodheshwa katika daftari la Brela au kuna vigogo nyuma yake? Je ni suala la Rushwa? Kama hakuna yote hayo fumbo hili linaelezwaje? Huu ni msingi mwingine unaohitaji uchunguzi wa kina kabisa.
18: Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ibara ya 63(2) Bunge hili, kwa niaba ya Watanzania wote, ndio chombo pekee cha juu cha kuisimamia Serikali. Pamoja na kwamba majibu ya Mhe. Waziri wa fedha hayakuridhisha kabisa, na ni matusi kwa Bunge kama mwakilishi wa Wananchi katika kuisimamia Serikali yao, Kambi ya Upinzani sasa;-
(i) Kama kweli dhamira ya Serikali yetu ya kudhibiti ubadhirifu kama inavyosimamiwa kidete na Rais wetu, hatua za haraka sana zinahitaji kuchukuliwa kunusuru rasilimali za Taifa letu. Kwa utaratibu wa kawaida katika mazingira ya aina hii, kwenye ofisi zote na kwa ngazi zote, mhusika husimamishwa mara moja kuruhusu uchunguzi. Hapa Waziri anasema kuwa uchunguzi utakaofanyika utakamilika mwisho wa mwaka 2007. Hiki ni kichekesho. Kambi ya Upinzani inaomba sana kwa hili Wabunge wote tushikamane bila kujali itikadi zetu, tupiganie maslahi ya nchi yetu. Hakuna anayeichukia Serikali, kwa vile Serikali ikiisha kuchaguliwa itakuwepo hadi uchaguzi mwingine, lakini Serikali itusikilize pia kilio chetu kwa niaba ya Wananchi.
(ii) Mhe.Spika, Taarifa niliyoitoa Bungeni kuhusu tuhuma inayomhusu Gavana wa Benki Kuu inamhusisha Gavana moja kwa moja, au kwa uzembe katika upotevu au matumizi mabaya ya fedha za Serikali ndani ya Benki Kuu. Taarifa hiyo haiishii hapo, inamtaja mkewe Anna Muganda kuwa mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Time Mining, ambayo ndiyo iliyokuwa inaendesha kampuni ya Meremeta, na hatimaye imeuzwa kwa bei ya kutupa, na baada ya BOT kulipa dhamana ya zaidi ya Dola za marekani 100,000, kabla ya kuuzwa kwa Rand Gold, ambako Anna Muganda mke wa Gavana pia ni Mwenye hisa. Watanzania tunajiuliza hapa kuna nini? Serikali kila ikihojiwa Bungeni haitoi majibu kama alivyojibu waziri wa Fedha Bungeni juzi. Wakurugenzi wa Alex Stewart waliolipwa zaidi ya Dola za marekani 65 millioni nao walitoka Time Mining ambako Ana Muganda anahusika.
(iii) Mhe. Spika, haya yote yametokea kwa bahati mbaya? Vivyo hivyo kwenye External Debt Service Account, au kwenye Bank M, ambayo inasemekana imeandikishwa bila kufuata utaratibu na inamilikiwa na wamiliki walioonyeshwa kwenye waraka niliowasilisha wiki iliyopita. Mmoja wa wamiliki hao anasemekana kuwa Gavana Balali kupitia Kampuni yake na mkewe Anna Muganda, inayoitwa Napster Group iliyosajiliwa Uswizi. Mhe. Spika kwa haya nchi yetu inateketea. Kwa hili tunaomba watanzania wote watuunge mkono, ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa wabunge ambao dhamira zao ni safi, wana uzalendo wa kweli, tuungane ili kuokoa siyo tu jina la nchi yetu, lakini pia rasilimali zake nyingi zinazoteketezwa bila huruma.
(iv) Watanzania wote pamoja na wabunge wa CCM, tuungane kwa pamoja, hatuna sababu ya kugombania fito wakati nyumba tunayojenga ni mmoja. Kama tulivyosema awali, suala hili halihitaji kuangaliwa kwa jicho la kiitikadi, na kwa hili kwa niaba Watanzania ninamwomba Mhe. Waziri Mkuu asiwaite wabunge wa CCM kwenye kikao cha kuwafunga mdomo kama ilivyoripotiwa hapo juu. Tunaomba uzalendo tu utawale kuanzia kwa viongozi wetu wa juu, hadi kiongozi wa ngazi ya chini kabisa. Hivyo basi,
(a) Tunamwomba kwa heshima kubwa Mhe. Gavana Daudi Balali ajiuzulu kwa hiari yake, ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika na kubaini ukweli wa taarifa hizi zilizozagaa kila mahali, zenye athari si tu kwa jina lake lakini pia kwa jina na heshima ya nchi nzima, ikiwa ni pamoja na kuharibu jina la Bunge hili iwapo litashindwa kusimamia jambo hili zito.
(b) Iwapo Gavana Balali atashindwa kuchukua heshima ya kujiuzulu, basi Serikali imsimamishe mara mmoja ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika. Si vema, uchunguzi ufanyike mhusika yuko Ofisini, na kwa vyovyote vile Uchunguzi utakaochukua mwaka mzima, ni njia ya wazi ya kutengeneza mazingira ya kuvuruga uchunguzi.
(c) Wabunge tunaomba kabisa kwa hili tuungane. Najua ugumu wa nyie kutuunga mkono, kama magazeti yalivyoandika wiki hii, tunajua mnafungwa midomo, lakini tunawaomba wekeni dhamana mbele kabla ya maslahi ya vyama vyetu, na pia uwakilishi unahitaji kujitoa sadaka, hata kama mtakaangwa kisiasa lakini waliowapigia kura watawaona nyie ni mashujaa.
(d) Mhe. Spika, hapa ninasukumwa zaidi na msemo wa kiswahili kuwa ‘Machozi ya wanyonge huwa hayaanguki ardhini bali huanguka mionyoni mwao na kwa hivyo Mungu kuotoka mioyo hiyo husikia kilio chao’.
(e) Mhe. Spika wanyonge wanalia sana kuona rasilimali zao zinaangamia wakati wao wamesongwa na mizigo ya kodi, michango lukuki, lakini wengine wakijinenepea.
(f) Nchi yetu ina historia ndefu ya kuunda Tume nyingi za uchunguzi. Mara chache sana taarifa hizo zinatolewa hadharani kwa maelezo kuwa Taarifa ni za mwenye kuunda Tume. Huu ni mtazamo potovu. Haiwezekani kuwe na kilio cha wananchi, fedha za wananchi zitumike kufanya uchunguzi kisha taarifa inakuwa siri.
(g) Kambi ya Upinzani basi inapendekeza kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge, Kifungu cha 104, iundwe Kamati Teule ya Bunge kutimiza jukumu letu la kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba. Kwa utaratibu huo tutakuwa tumelinda heshima ya Bunge letu, ambalo sasa watu wengi wanazidi kuona kuwa inalinda maslahi ya Chama Tawala, na au inageuzwa kuwa Rubber Stamp’ na kuacha kutekeleza majukumu yake ya msingi. Mhe. Spika kama niliivyosema, suala hili lisiangaliwe kwa jicho la vyama bali liwe suala la uzalendo na utaifa zaidi.
19: Mheshimiwa Spika,
Maswala haya ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu, na hivyo tunapenda kupata majibu ya kina na siyo majibu ya kisiasa na kishabiki ambayo hayana manufaa wala kwa Taifa letu wala kwetu binafsi isipokuwa kama tuna maslahi yaliyojificha.
HALI YA KISIASA NCHINI:
20: Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla hali ya ulinzi na Usalama, na ya siasa nchini ni shwari kama inavyoelezwa na Serikali. Kambi ya Upinzani inapenda kuwapongeza Jeshi letu la Polisi kwa namna ya pekee kwa jinsi walivyoweza kudhibiti ujambazi, hasa ujambazi wa silaha za moto. Kambi ya Upinzani inatoa mwito kwa Watanzania wote kushirikiana na Jeshi la Polisi katika masuala yote yanayohusu usalama wetu na wa Mali zetu, kwani bila ushirikiano wa raia wema Jeshi la Polisi hawataweza kudhibiti uhalifu kila mahali na kila wakati kutokana na idadi yao na uduni wa nyenzo.
MASUALA YA HAKI ZA BINADAMU:
21: Mheshimiwa Spika,
Moja ya malengo makuu kwa mwaka wa Fedha 2007/2008 ni pamoja na “Kuwezesha na kudumisha hali ya Utawala Bora wenye kuzingatia Demokrasia, usawa na Haki” (Rasimu, Fungu 56, kif.4(ix)). Waziri Mkuu ndiye msimamizi mkuu wa Shughuli zote za Serikali na mratibu wa Wizara, Idara na vyombo vyote vya Serikali za Mitaa. Kambi ya Upinzani inadhani Ofisi ya Waziri Mkuu ina nafasi kubwa sana katika kusimamia, kuimarisha, kukemea na hata kurekebisha pale ambapo kuna dosari katika masuala yote ya Utawala Bora na Haki za binadamu katika nchi yetu. Utawala Bora na Haki za Binadamu zisipoheshimiwa na kusimamiwa kikamilifu yote tunayofanya yanapoteza maana, kwani maendeleo yote ni kwa ajili ya Binadamu.
22: Mheshimiwa Spika,
Vigezo vya hali shwari ya ulinzi na usalama siyo udhibiti wa majambazi peke yake kama tunavyofikiri mara nyingi. Kuna mambo mengi yanayoweza kuwafanya wananchi au mali zao zisiwe salama. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:
(i) Kuendelea kwa mauaji yanayotokana na “Imani za kishirikina” bado yanaisumbua nchi yetu. Matukio mbalimbali ya mauaji ya aina hii yameendelea kuripotiwa katika Vyombo vya Habari kama ilivyotokea kwa mtoto Musswadi Hemedi wa Wilaya ya Moshi, ( Mwananchi, 3 Februari, 2006, uk. 3), au yaliyosababishwa na bwana Akabula Luhende wa Bukoba (The Citizen, 1st May, 2006), au mama Tarita Katwiko(56) Manyoni aliyekatwa mapanga kutokana na imani za kichawi au kishirikina, (LHRC Database,2006).
Mhe.Spika, Kama inavyoonekana matukio haya yako sehemu mbalimbali za nchi nzima. Yameripotiwa Mbeya, Kagera, Shinyanga, Njombe na penginepo. Utafiti wa Kituo cha Haki za Binadamu unaonyesha kuwa mauaji ya aina hii yameongezeka kwa asilimia 13 ya makosa yote dhidi ya Haki za Binadamu katika mwaka 2006 (Tanzania Human Rights Report, 2006, p.19).
Mhe. Spika, tuko karne ya Sayansi na Teknolojia, lakini bado tunaendekeza ushirikina. Wahanga wakubwa wa uhalifu huu ni akina mama (wazee) na watoto. Kambi ya Upinzani inadhani Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, inahitaji kuongeza jitihada zaidi katika kusimamia sheria ya ‘The Witchcraft Act, cap 18 (R.E.). Sheria hii ikisimamiwa vizuri na vyombo vyote husika, tunaweza kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu.
(ii) Mhe.Spika, Matukio ya unyanyasaji unaotokana kwa sehemu kubwa na maamuzi ambayo hayapangwi vizuri na Serikali pia yameripotiwa katika taarifa mbalimbali kwa kipindi cha 2006. Baba na Mama lishe wengi wamekuwa wahanga wakuu wa maamuzi haya ya zimamoto ya Serikali. Watu hao hufanya shughuli ambazo zimetambuliwa chini ya Sheria ya Nguvu Kazi, tena wanalipa ushuru wa serikali, wamejikuta wakiondolewa bila mpango au utaratibu makini.
(iii) Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani haina tatizo kuwa na miji safi, iliyopangwa kwa utaratibu makini. Lakini, mara nyingi maamuzi mengi yametolewa kisiasa kuwaondoa mathalan Wamachinga jijini Dar-Es-Salaam ambao wamehamishwa bila maandalizi ya kutosha kule wanakohamishiwa, au wachimba kifusi waliojikuta ghafla wamepoteza ajira kwa amri ya kupiga marufuku maeneo yao.
(iv) Mhe. Spika, tatizo hapa ni utaratibu mbovu, maamuzi ya kisiasa ambayo hayakuandaliwa vizuri yenye athari kwa maisha ya binadamu, athari kwa elimu ya watoto wao, na athari nyingine nyingi. Hali hii imesababisha mapambano kati ya polisi na machinga au makundi hayo. Kwa siku za hivi karibuni tumeanza kuona migomo ambayo haikuwepo katika historia ya nchi yetu. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa makini yanapofanyika maamuzi yenye athari kubwa kuokoa maisha na mali za watanzania. Tusipodhibiti hali hii tutazalisha ufa mkubwa utakaokuwa msingi wa migogoro mikubwa huko mbele.
a) Mwezi Machi 2006 Serikali ilitoa agizo kwa jamii ya wafugaji wanaoendesha shughuli zao katika bonde la Usangu/Ihefu wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kuondoka katika eneo hilo la hifadhi. Kuondoshwa kwa wafugaji Mbarali na sehemu zingine inatokana na tuhuma kwamba ‘wafugaji ndio chanzo hasa cha uharifibu wa mazingira nchini’. Wafugaji hao waliondolewa wao na mifugo yao kwa kutumia vyombo vya dola. Tafiti na taarifa mbalimbali zimetolewa, zikionyesha uwepo wa unyanyasaji mkubwa,viongozi wa Serikali Kuu na Mitaa wamefanya mambo mengi kinyume na taratibu na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mifugo mathalan, mtu mwenye ng’ombe 400 kupoteza mifugo yake kwa kufa na kubakia na 40 tu, au kulazimika kuwauza ili kulipa faini, au gharama za kuwapitisha, mathalan Daraja la Mkapa kuna taarifa kuwa kwa Lorri moja wafugaji wamelazimika kulipia hadi Tshs 300,000, tena bila risiti, Mkuu wa wilaya ya Mbarali kuwalazimisha kuwauza mifugo kwa bei chini ya Bei ya soko, Mkuu huyo huyo waliposhindwa kuondoka katika muda mfupi uliotolewa aliagiza wakamatwe wao na ngombe zao. Wakalazimika kulipa faini ya shs 10,000 kwa kila kichwa cha ng’ombe. Sasa fikiria mtu mwenye ngombe zaidi ya 1,000 amelipa kiasi gani. Alijiandaa vipi kwa fedha nyingi kiasi hicho kama si kwa kuuza ng’ombe wake kwa bei ya kutupa? Serikali kushindwa kufanya maandalizi ya miundombinu, utaratibu wa chakula na madawa kabla ya kuwahamisha nakadhalika. Kule walikoenda kulazimika kutoa fedha ili waonyeshwe mahali pa kufikia, (Taz. Taarifa ya Utafiti ya HakiArdhi na wenzake).
23: Mheshimiwa Spika,
Hayo yote yanaonyesha matukio ya uvunjwaji wa makusudi wa haki za binadamu na ukosefu wa utawala bora. Matokeo ya jumla ya uvunjwaji huo wa haki za binadamu ni uporaji na upotevu wa mali, kukosekana utawala bora na rushwa iliyokithiri, kusambaratika kwa familia, kuwanyima elimu watoto waliokuwa shule, kuwanyima huduma za kimsingi na muhimu kwa binadamu, kusababisha kwa ghafla kuporomoka kwa uchumi wa wafugaji hao.
24: Mheshimiwa Spika,
Matukio kama haya yametokea Geita, Tarime, Bulyankulu, ambapo vijiji vizima vilihamishwa na kutokomea, kwa ajili ya kuwapisha wawekezaji. Wawekezaji sawa. Lakini haki za msingi za Wananchi wetu je? Tumefika mahali kweli hata utu wa binadamu tunauweka rehani kwa ajili ya wawekezaji? Wakati hayo yanafanyika hakuna maandalizi ya kutosha ya kuwahamisha wala utaratibu unaoeleweka wa kuwafidia wananchi wetu. Hali sasa imefikia mahali Bunge haliwezi tena kukaa kimya. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali:-
(a) Kwa vile Tume ya Serikali imefanya uchunguzi wa kina Taarifa ya Tume hiyo itolewe hadharani. Uchunguzi huu umefanyika kwa Fedha ya Watanzania wote wakiwemo wafugaji walioathirika. Hivyo ni haki yao kujua matokeo ya uchunguzi.
(b) Serikali ikubali kufanya haraka tathmini ya upotevu wa mali na iwalipe fidia wote walioathirika. Kuendelea kuchelewa kuchukua hatua ni kuendelea kuwaletea mateso makubwa ya kiuchumi na kisaikolojia.
(c) Serikali ianzishe mjadala wa wazi wa kitaifa juu ya mustakabali wa makabila ya wafugaji. Ikumbukwe kuwa jamii ya Wabarbaig maeneo yao yalitwaliwa na kufanywa Wheat Complex kule Hanang, yapatayo Ekari zaidi ya 100,000 miaka ya 1970. Kitendo hicho cha Serikali bila maandalizi ya mahali pa kuwahamishia imefanya jamii hiyo kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya haki za binadamu.
25: Mheshimiwa Spika,
Suala la Adhabu ya Kifo (Death Penalty), bado halijafanyiwa kazi ya kutosha na Serikali yetu. Bado Serikali yetu imeendelea kushikilia adhabu hii katika sheria yetu ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) na kuendelea na adhabu ya kifo chini ya “The National Defence Act, Chapter 132 (RE). Kuna makosa makuu matatu ambayo adhabu yake ni ‘Kifo” kwa mujibu wa Sheria zetu, yaani Mauaji ya kukusudia (Sect. 197 Penal Code), Uhaini (Sect.39 na 40 Penal code) na Makamanda wa Jeshi wanaonyesha tabia mbaya mbele ya adui (misconduct) National Defence Act, cap 192.
26: Mheshimiwa Spika,
Taarifa kamili ya Wahalifu wangapi wamehukumiwa adhabu ya kifo imekuwa vigumu kupatikana. Lakini Waziri wa Katiba na Sheria alitoa taarifa kwenye Kamati ya Bunge kuwa Mhe. Mkapa mwishoni mwa kipindi chake aliwapunguzia wafungwa wote waliohukumiwa kufungwa na kuwa na kifungo cha maisha, yaani kwa kipindi chake chote toka 1995 hadi 2005(Taarifa kwa Kamati. FY 2006/2007 uk.4). Kwa utafiti wa LHRC, kwa mwaka 2006 watuhumiwa 21 walihukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama ya Rufaa Tanzania (Tanzania Human Right Report, sic, p.10.).
27: Mheshimiwa Spika,
Kama tulivyosema mwaka jana, adhabu hii, kwanza inakuja wakati mfungwa amekwisha kukaa jela kati ya miaka 7 hadi 10 kabla ya hukumu. Hii inathibitishwa na hukumu kadhaa za Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mahakama Kuu, Registry ya Bukoba ya 18 March, 2006 ambapo alihukumiwa adhabu ya kifo baada ya miaka rumande 12. Tarehe 10 May, 2006 Mahakama Kuu Dar-Es-Salaam nayo ilimhukumu mtu kifo baada ya miaka 9.
28: Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri basi, kwanza wamekaa rumande kwa muda mrefu bila kujua hatima yao. Pili, hata baada ya hukumu wanakaa tena miaka 10 kama ilivyoonekana katika uamuzi wa Rais Mkapa kuwabadilishia hukumu baada ya miaka 10 .Wakati wote huo bila kujua hatima yao. Kila siku inayokucha wakidhani ndiyo siku ya kunyongwa, jambo ambalo ni mateso ya kisaikolojia kwao na kwa familia zao na ambayo ni sawa na kutumikia “adhabu mbili’.
29: Mheshimiwa Spika,
Isitoshe, utafiti wa kitaalam unaonyesha kuwa ‘kuondoa uhai wa mtu kwa njia ya adhabu ya kifo haimsaidii yeyote kwa vile si tishio tena kwa aliyeuawa (deterrent) wala kuwa tishio kwa wenye nia ya kua kwani hakuna ushahidi wa kitaalam kuonyesha kuwa uhalifu huu unapungua kutokana na adhabu hii (Taz. The Fact Sheet, Death Penalty Does not deter Crimes”, http://www.nodeathpenaltywi.org).
30: Mheshimiwa Spika,
Tatizo lingine ni kuwa adhabu hii pale inapokuwa imetekelezwa haiwezi tena kurekebishwa hata kama itaonekana kuwa aliyehukumiwa siyo huyu (alibi) kama ilivyothibitishwa Ireland ambapo aliyefungwa kwa mauaji alikuja kuthibitika miaka 16 baadaye kuwa siye aliyehusika. Je angelikuwa amenyongwa haki zake zingekuwaje? (Time Magazine, 2004, Pg. 34).
31: Mheshimiwa Spika,
Utafiti wa kisayansi uliofanywa na LHRC unaonyesha kuwa asilimia 68 ya Watanzania ya waliohojiwa walisema adhabu hii ‘ibadilishwe kiwa kifungo cha maisha’ na asilimia 32 tu ndio waliosema adhabu hii iendelee (Utafiti ulifanyika kwa njia ya mahojiano ya Field Monitors, Kumbukumbu za Library, Taarifa ya Vyombo vya Habari,na Field Survey iliyohusisha wilaya zote Tanzania Bara, Taz.LHRC, HRM Unit Data base,2006).
32: Mheshimiwa Spika,
Tarehe 10 hadi 17 Shirika la International Federation for Human Rights (FIDH) kwa kushirikiana na Taasisi ya Legal and Human Right Centre ya Tanzania walitembelea magereza yetu. Taarifa hiyo inayoonyesha kuwa asilimia kubwa ya wafungwa wako tayari kujirekebisha. Taarifa hii inashabihiana kabisa na barua iliyoandikwa na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, mwezi Februari, 2006 kwa Mhe Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu kuwa kweli walihusika na mauaji katika mazingira mbalimbali na wamehukumiwa na mahakama mbalimbali.
Lakini baada ya kusubiri kutekelezwa kwa hukumu yetu kifo kwa miaka kati ya 10 na 15 na kusamehewa na Mhe Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu…., tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi hiyo ya Maisha aliyotuachia.Tunakuhakikishia Mhe. Rais, kuwa uwasamehe wale wenzetu waliokaa gerezani kati ya miaka 10 hadi 30 na kuwabadilishia kifungo cha maisha. Mhe. Rais, hatuna taasisi ya kututetea, sisi ni wahalifu lakini tumetubu….tumejirekebisha sana” Mhe. Spika ni kweli hawa wanaweza kuwa wahalifu wa mauaji. Lakini mwenye dhamana ya mwisho ya Maisha ya Binadamu ni mwenyezi Mungu.
33: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inamsihi Mhe. Waziri Mkuu, aliingilie suala hili yeye mwenyewe, na kusukuma taratibu zinazohusika za kufanyia marekebisho Sheria zetu ili adhabu hii ifutike katika vitabu vyetu vya Sheria.
34: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani kutokana na mafunzo tuliyopata mwaka 2001, inaitaka Serikali iingilie kati mazungumzo yanayoendelea kati ya CUF na CCM na kutoa msukumo unaotakiwa kufikia ukomo wa mazungumzo hayo mapema. Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye pia Rais wa wananchi wa upande wa Tanzania visiwani. Hivyo jambo lolote linaloweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi hii, Mhe. Rais hawezi kukaa mbali akawa mtazamaji tu. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ichukue hatua ya haraka ili suluhu ya kweli ya mgogoro wa Zanzibar ipatikane na misingi ya amani, uelewano, mshikamano, na upendo iweze kujengwa upya kati ya wanachama wa CUF na CCM kwa upande mmoja, na kati ya wananchi wetu kwa ujumla wao. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani hairidhishwe na kasi ya mazungumzo hayo, na wakati mazungumzo yanademadema, uvumilivu wa wananchi nao unayoyoma. Tuipende nchi yetu na tuwe wepesi wa kuchukua hatua pale maslahi ya Taifa yanapohusika.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI:
35: Mheshimiwa Spika,
Mwezi Decemba, 2007 tutakuwa tumekamilisha miaka miwili kamili tangu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Taarifa mbalimbali sasa zimetoka, mathalan Taarifa ya Tume ya Uchaguzi (NEC), Taarifa ya TEMCO, Taarifa ya Waangalizi mbalimbali wa kimataifa wakiwemo, Waangalizi wa Bunge la SADC(SADC-PF). Kutokana na Taarifa hizi mambo mbalimbali yamejitokeza na ninapenda kuyagusia kwa kifupi tu. Mambo haya ni kama ifuatavyo:
(i) Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka kufahamu sasa ni lini Serikali itawasilisha Mabadiliko makubwa ya Katiba baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, na hivyo kutoa haki kwa Watanzania wanaotaka kugombea au Urais, Ubunge au Udiwani bila kulazimika kupitia chama chochote cha siasa. Serikali yetu inajitangaza kuwa inaheshimu Utawala wa Sheria na sisi tuna amini hivyo. Hatutegemei basi kuwa Serikali itakuwa inachukua njia za mkato kukwepa tena Uamuzi huo muhimu wa Mahakama, kama ilivyofanya huko nyuma. Mabadiliko makubwa ya Katiba yanayowashirikisha Wadau wote, yataondoa aibu tunayopata sasa ya Mahakama kutengua sheria zetu kwa yale mambo yanayoitwa “unconstitutional”. Tusisubiri na kesi nyingine na nyingine tuchukue hatua ya kufanyia Mabadiliko Makubwa Katiba yetu kutokana na mabadiliko makubwa yanayotokea katika nchi yetu, kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kambi ya Upinzani inategemea maelezo ya Kina katika eneo hili.
(ii) Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Kwa ujumla Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni hatua nzuri katika kufanya Uchaguzi uwe wa huru na haki kama litatumika vizuri, kwa uwazi, na misingi yenyewe ya Daftari kutumika kama inavyotakiwa. Pamoja na uzuri huo, kuna mambo yamejitokeza ambayo Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali yarekebishwe mara moja. Mambo haya ni:- a) Kwa vile hakuna utaratibu wa kurekebisha Daftari hilo mara kwa mara kabla ya Uchaguzi, vijana wapatao 11,000 wamekoseshwa haki yao ya kupiga kura katika Uchaguzi mdogo wa Tunduru. Ni vema utaratibu wa kurekebisha Daftari ukaangaliwa upya na ikiwa lazima Sheria husika irekebishwe. Katika enzi hizi za Teknolojia hakuna sababu ya uchelewashaji kama inavyoonekana sasa. Ikumbukwe kuwa kila siku kuna vijana wanafikia umri wa miaka 18 ambayo ni umri wa kupiga kura.
(iii) Mheshimiwa Spika, Hili ni suala la kikatiba, na hatudhani kuna haja ya mtu kwenda mahakamani kudai haki hii. Tunaamnini Serikali itachukua hatua ya haraka kurekebisha jambo hili. Wananchi wengi wanaoishi nchi za nje pia walinyimwa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa vile tu Sheria zetu hazitambui njia za kisasa za kupigia kura. Iwapo nchi kama Mozambique wananchi wao wanaoishi nchi wanapiga kura Kambi ya Upinzani haioni ni kwanini Tanzania ishindwe kuwapa haki za kikatiba wananchi wake. Tusisubiri wakati wa Uchaguzi, Sheria husika zirekebishwe mara moja, na ikumbukwe tarehe 12 April 2006, Mhe. Rais wetu alipokuwa Namibia aliwaahidi Watanzania walioko Namibia kuwa ‘Watanzania walioko nje wanaweza kupiga kura ifikapo 2010 (Daily News, 13 April,2006). Ni imani yetu kuwa ahadi ya Mhe. Rais haitaachwa ipite bila kufanyiwa kazi.
(iv) Mhe.Spika, Kambi ya Upinzani imefurahishwa na Uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu suala la Takrima kutokana na Shauri no. 77 ya 2005 iliyofunguliwa na LHRC, LEAT na NOLA dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hukumu hiyo ya kihistoria ilitolewa na Mhe.Jaji N.Kimaro, S. Massati na T.Mihayo tarehe 24 April, 2006. Pamoja na hukumu hiyo nzuri, na kwa kuwa Serikali hadi sasa haijakata rufaa hadi sasa, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo kwa sasa ndiyo yenye dhamana ya masuala ya uchaguzi, iwasilishe Bungeni haraka iwezekanavyo kurekebisha Sheria zote zinazohusiana na suala la Takrima hasa Sheria ya Uchaguzi ya Cap.343 RE 2002).
(v) Mhe. Spika, Mahakama kuu ilielekeza kuwa sheria iliyokuwepo awali kabla ya kuruhusu Takrima ilitosheleza kutofautisha “ Matumizi ya lazima ya uchaguzi na yale yenye mwelekeo wa rushwa ( judgment, pages 38-40). Mathalan, ni utamaduni upi wa kiafrika ambapo mgeni anayekuja nyumbani kwako ndiye anayekukirimu? Lakini kukirimiwa na mwenyeji, (mwenye nyumba) hakuna anayelalamikia hata kidogo. Rushwa ikifutwa kwenye uchaguzi, kimsingi, itawafanya viongozi wa kisiasa wawajibike zaidi kwa majimbo yao, kwani dhana ya kuwanunua wapiga kura kwa vitu vidogo vidogo itafutika kabisa.
(vi) Mhe. Spika, ulimwengu mzima sasa hivi uko makini kuona wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika nafasi zote za maamuzi na hasa Bungeni na kwenye Baraza la Madiwani, utendaji wa ngazi zote. Tunafurahi kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi chache zilizovuka asilimia 30 iliyowekwa na Wakuu wa Nchi za SADC kupitia Azimio lao la mwaka 2000. Tanzania leo ni Wanawake 75, ikiwa ni asilimia 30 Wanawake na asilimia 69.72 wanaume. Hili ni jambo la kupongezwa , na mathalan Bungeni hili pale lilipokubali kufanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 66(1)(b). Kwa vile Wakuu wa Nchi za Afrika AU nao pia wameweka Azimio sasa la kupandisha asilimia hiyo hadi kufikia 50%. Kambi ya Upinzani haina Tatizo kabisa na pendekezo hilo na tunaunga mkono. Hata hivyo, Kambi ya Upinzani inapenda kutoa tahadhari.
(vii) Mhe. Spika, Suala hili si suala la Chama cha Mapinduzi peke yake. Taarifa tulizonazo sasa ni kuwa mkakati wa utekelezaji wa azimio hilo unaandaliwa na CCM na Serikali zake tu. Badiliko hili linagusa masuala mengi sana ya nchi, yanagusa mustakabali na muundo wa utawala katika nchi yetu na hivyo, suala zito kama hili si la kujadiliwa na Chama kimoja tu. Kama ni suala la Sera karibu vyama vyote viliisha kukubali na kuunga mkono azimio la Wakuu wa AU, hivyo hatuoni kwanini mjadala wa suala hilo usifunguliwe kwa Taifa zima.
(viii) Mhe.Spika, Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri Mkuu, ambaye Ofisi yake ndiyo yenye dhamana ya Masuala ya Uchaguzi, na mratibu wa Vyama vyote, aitishe mapema iwezekanavyo Vyama vyote vya Siasa, akishirikisha pia wadau mbalimbali wakiwemo Vyama vya hiari na madhehebu ya dini kwa lengo la kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu suala hili zito. Utulivu na amani katika nchi vinapatikana kwa kuwa na siasa Shirikishi.
(ix) Mhe.Spika, Tunapenda kutoa tahadhari kuwa Siasa zinazogawa wananchi, zinazobagua wananchi na kuacha mawazo mbalimbali ya wadau nje ya maamuzi ya msingi ndiyo msingi mkubwa wa migongano na migogoro katika nchi za wenzetu. Tuepuke nyufa na migongano kwa kushirikishana kujenga Tanzania imara, yenye wananchi wenye kupendana na wenye mshikamano. Tukichezea amani tuliyonayo tutakuja kujuta sote.
(x) Mhe. Spika, baadhi ya changamoto zilizoripotiwa na Taarifa mbalimbali tulizotaja hapo juu, ikiwemo Taarifa ya NEC ni pamoja na
a) Jeshi la Polisi, likiongozwa na Ma RPC na Ma OCD kuingilia masuala ya Uchaguzi hasa kwa kuzuia mikutano ya Kampeni,(NEC, pages 71 na 79),
b) Vurugu zilizotokea katika maeneo hasa ambako Upinzani ulionekana na nguvu, na Jeshi la Polisi na FFU kuwa msingi wa vurugu hizo. Polisi wanasemekana kutumia nguvu hata pale ambapo haikuwa lazima kwa mfano kutumia silaha za moto. Ijulikane kuwa hakuna anayepinga Jeshi la Polisi na FFU kulinda amani au kuweka mazingira mazuri. Lakini taarifa zinaonyesha hata pale wananchi walipokuwa watulivu, wamefuata taratibu zote, Jeshi hilo lilifika na kutishia, kuwatawanya watu waliokuwa wanafanya shughuli zao za kampeni kwa utaratibu uliokubalika. Maeneo kama Bariadi, Bukoba, Musoma, Tarime, Karatu na Zanzibar yametajwa na Taarifa zote.
c) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya uchunguzi wa kina kwa kushirikisha na watu walio huru, mathalan Majaji wa Mahakama Kuu kujua sababu za msingi za vurugu hizo kwa lengo la kupata mapendekezo ya kuondokana na matatizo hayo katika chaguzi zijazo.
d) Mhe. Spika, Serikali yenye nia njema ya kujenga Demokrasia ya Kweli itafanya kila linalowezekana kufanya uchaguzi kuwa wa huru na wa haki, na kurekebisha dosari zote zinazojitokeza katika uchaguzi mmoja, kuwachukulia hatua wale wote wanaochafua sifa njema ya nchi kwa kusababisha vurugu wakati wa uchaguzi kwa kufanyia marekebisho sheria pale inapoonekana dosari za kisheria ndiyo sababu ya matatizo yanayojitokeza.Mhe.Spika, Ni imani yetu Serikali haitasubiri Uchaguzi mwingine ili kuzifanyia kazi dosari hizi.
e) Mhe. Spika, Taarifa ya NEC pia inaonyesha kuwa vyama vingine havikuweza kufanya Kampeni vizuri kwa kukosa rasilimali fedha. Ni imani yetu kuwa ili demokrasia ikomae vizuri, Serikali iangalie uwezekano wa kutoa Ruzuku kwa shughuli za uchaguzi kwa fomula itakayokubalika na wadau na Serikali tukizingatia kuwa hizi ni fedha za walipa kodi wa Tanzania, na hivyo ni lazima zitumike vizuri.
SERA YA MAKAO MAKUU KUHAMIA DODOMA:
36: Mheshimiwa Spika,
Mwaka wa Fedha 2006/2007 Katika Kitabu cha Maendelo cha Bajet, yaani Volume lV Sub sub vote, 1003 na kifungu kidogo zaidi 6510 Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makao Makuu ilitengewa Tshs 427,945,000 .Kazi zilizofanyika ni usafishaji wa mifereji ya maji taka, ujenzi wa uwanja wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square), ununuzi na ujenzi wa mabanda mawili katika uwanja wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma.
37: Mheshimiwa Spika,
Mwaka wa Fedha 2007/2008 Ofisi ya Waziri Mkuu wamepewa kwa ajili ya CDA jumla ya Shs 1.6billioni. CDA wamepewa Jumla ya Shs 1.7billioni kwa Mishahara ya Watumishi (Taz Randama ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Fungu 37 Kasma 6510 uk 67). Yaani zaidi ya fedha walizopewa kwa shughuli za kustawisha Makao Makuu. Kazi wanazotarajia kufanya ni pamoja na pamoja na kumalizia ukarabati wa Nyerere Square, kusafisha mifereji ya maji, kuotesha miti, kukarabati barabara za Manispaa ya Dodoma na kupima viwanja.
38: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatambua kuwa kuhamisha Makao Makuu ni Sera ya Chama cha Mapinduzi, na hatuna sababu ya kuhoji mambo ya Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo Sera hiyo iliyopitishwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, haijatekelezwa au imetekelezwa kiwango kidogo sana tangu ilipotangazwa 1973 kwa Tangazo la Rais, no.230. Kwa takwimu hizi hakuna mkakati wowote wa muda mfupi wala wa muda mrefu wa kutekeleza sera hiyo kikamilifu. Wakati huo huo, Taifa linaathirika sana na sera hii kama ifuatavyo:-
b) Mhe. Spika tangu mwaka 2001 tuliambiwa ndani ya Bunge hili kuwa Wizara 5 zimehamia Dodoma. Tunataka Waziri Mkuu alithibitishie sasa Bunge hili toka uamuzi huo wa kuhamia Dodoma ni Wizara ngapi zimehamia Dodoma kikamilifu?
c) Mwaka huu wa Fedha Ofisi ya Waziri Mkuu imeidhinishiwa Tshs l, 633,999,000 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dar-Es-Salaam (Taz. Kasma ya 6351 Randama ya Wizara Fungu 37). Mwaka jana zilitengwa Tshs Billioni 1 kwa ajili ya kuchora ramani majengo hayo. Kambi ya Upinzani inataka kufahamu, ni kwa nini fedha hizo zisitumike katika kujenga Ofisi nzuri ya kisasa Dodoma badala ya kukarabati jengo la tangu wakati wa Wajerumani, ambalo sasa hata ukarabati wake umekuwa wa ghali. Je, kwa mtindo huo azma ya kutekeleza Sera ya CCM ya kuhamia Dodoma bado ipo, iwapo kiongozi wa Shughuli za Serikali ndiyo kwanza anaimarisha Ofisi yake Dar-Es-Salaam?
d) Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani inataka pia kufahamu wakati Kasma ya 270104 ujenzi wa Jengo, Tshs 3,305,353,000 inaonekana kwenye Kitabu cha Bajet Volume 11 inatofautiana na Kasma ya 6351 iliyotajwa hapo juu, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kasma 6351 zinaonekana wapi, kwani vitabu vya Hazina havimsaidii kabisa Mbunge kutambua fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya nini kwa vile vifungu vimetajwa kwa jumla jumla tu.
e) Mhe. Spika, Kwenye Randama Kasma ya 310801 nayo imeombewa Tshs 829,819,600 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu dodoma na Dar-Es-Salaam. Tupatiwe ufafanuzi wa kina kuhusu kasma hizi zinazojirudia rudia?
f) Mhe. Waziri aliondolee wasiwasi Bunge hili kuwepo au kutokuwepo matumizi mabovu ya Fedha za walipa kodi kutokana na viongozi wa Serikali, wa kisiasa na watendaji, kuwa na nyumba mbili Dodoma na Dar-Es-Salaam, zote zikigharimikiwa na Serikali kinyume na kanuni za fedha za Serikali.
g) Mhe. Waziri wakati wa Majibu yake pia, alihakikishie Bunge hili ukweli au vinginevyo, wa Taarifa kuwa Wale viongozi waliohamia Dodoma, ambao kwa sababu karibu Serikali yote bado iko Dar-Es-Salaam, wanalazimika kukaa Dar-Es-Salaam muda mwingi na muda wote huo hulipwa posho ya safari (‘per Diem’) tofauti na kama wangelikuwa wanaishi na kufanyia kazi Dodoma, jambo ambalo linaichukulia Taifa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwenye shughuli za Maendeleo.
h) Mhe. Spika, Kambi ya Upinzani inataka pia kuelezwa kwa kina iwapo taarifa hizo ni za kweli Serikali inalielezaje Taifa hili kwanini walipa kodi waendelee kugharimia Sera ya Chama cha Siasa ambayo haitekelezwi inavyotakiwa na wala hakuna mkakati mpango unaoeleweka wa kuitekeleza?
i) Mhe. Spika, ieleweke wazi kuwa Kambi ya Upinzani haina tatizo kabisa na kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma. Kambi ya Upinzani inakerwa na Sera ambayo miaka nenda rudi haitekelezwi lakini fedha zinatumika. Kazi nyingi zinazofanywa na CDA kimsingi zingeweza kufanywa na Manispaa ya Dodoma kama ilivyo katika miji mingine bila kikwazo. Ni dhahiri kuwa huhitaji kuunda mamlaka kwa ajili ya kusafisha mifereji ya maji, kutengeneza barabara ndogo ndogo, au kupima ploti. Hizi ni kazi zinazofanyika na Manispaa au mamlaka ya Jiji kama ilivyo Dar-Es-Salaam, Tanga, Mwanza, Mbeya au Arusha. Kazi hizo zikiunganishwa na Mamlaka ya Jiji au Manispa unaookoa zaidi ya Shs Billioni 1.7 ambazo zingeweza kupunguza makali ya Wananchi katika ujenzi wa Sekondari, ujenzi wa Zahanati.
MAJUKUMU YA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
39: Mheshimiwa Spika,
Serikali za Mitaa ni vyombo muhimu sana katika uongozi wa nchi kwa vile vyombo hivi viko karibu na watu na ndiyo ngazi inayokutana na wananchi kuliko ngazi nyingine zote. Katika hotuba yangu ya mwaka jana nilizungumzia mambo mengi ikiwa ni kuhusu namna ya kuimarisha vyombo hivi. Ninaomba nirudie tena machache mwaka huu, kwa lengo la kutoa mchango wa Kambi ya Upinzani katika kujenga Serikali imara za Mitaa na hivyo kujenga Demokrasia ya kweli nchini mwetu. Mambo haya ni kama yafuatayo:-
(i) Mhe. Spika, kama tulivyosema, Wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa Vijiji, Madiwani na viongozi ambao mchana kutwa na usiku kucha wako kazini kusimamia programu zote zinazobuniwa na Serikali.
(ii) Mhe. Spika, Programu za kupiga vita Umaskini mathalan Mkukuta au Mkurabita. Wenyeviti wa Vitongoji, vijiji na Madiwani ndio injini ya kutekeleza mipango yote ya maendeleo kama vile Mipango ya MMEM, TASAF,MMES, Mpango wa kuboresha Kilimo (ASDP), Mpango wa Maji, na kwa ujumla mipango yote iliyobuniwa kitaifa. Wanatakiwa pia kubuni mipango na miradi inayohusiana na maeneo yao. Hawa ndio walinzi wa amani na usalama katika maeneo yao. Ni dhahiri basi, hawa ni viongozi muhimu sana katika nchi yetu.
(iii) Mhe.Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kubuni ‘mpango maalum’ wa kuwawezesha viongozi hawa kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia vizuri zaidi rasilimali nyingi zilizopelekwa chini na Serikali kuu kupitia Programu hizi za kitaifa. Si mara nyingi kusikia viongozi hawa wakienda Semina, Warsha au kongamano, lakini sisi viongozi wa juu kila wakati tuko kwenye Semina, kuanzia Mawaziri, Makatibu wakuu na Wabunge. Ni vema sasa tukapunguza Semina katika ngazi ya juu na tukazielekeza chini. Katika ngazi yetu hata tukipewa Maelekezo kwa nyaraka tunaweza kutekeleza maelekezo hayo bila kuhitaji Semina za gharama kama zile “Semina elekezi za Ngurundoto”.
(iv) Wenyeviti wa Vitongoji, vijiji, na Madiwani wawekewe mpango mzuri wa kuwapatia kipato cha uhakika, angalau kwa kiwango cha kima cha chini cha Mshahara Serikalini. Haiwezekani mtu anayesimamia fedha na rasilimali nyingi kama zinavyopelekwa fedha za Program zilizotajwa na yeye maisha yake yawe ya kubangaiza. Siku za karibuni magazeti mengi yameripoti ubadhirifu unaofanywa katika ngazi za Vijiji. Yote haya kimsingi ni kwa sababu nafasi za vishawishi zimekuwa nyingi zaidi, tofauti na huko nyuma ambapo programu zilikuwa zinatekelezwa na kusimamiwa na ngazi za wilaya. Vijiji viko chini ya 13,000 kata ziko kama 2,500.
(v) Mhe. Spika, tukiwa na nia hatutashindwa kuwalipa angalau mshahara wa kima cha chini viongozi hawa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tukisimamia vizuri fedha nyingi kama zinavyoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kila mwaka, na kubuni vianzio vipya kama vilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli wa Fedha, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa tutapata fedha za kutosha kuwalipa hawa viongozi wetu kwa kuanzia bila hata kwenda kuomba fedha kwa mfadhili. Wafadhili wakitusaidia itakuwa ni nyongeza. Mhe. Spika, dhamira ndicho kitu kinachotakiwa.
(vi) Watendaji wa Kata ambao ni waratibu wakubwa wa maendeleo, wanaosimamia ‘Amani’ katika maeneo yao, wanamsaidia Mkurugenzi wa Wilaya (DED) katika utekelezaji wa majukumu yake. Hawa, wanahitaji vyombo vya uhakika vya usafiri mathalan pikipiki. Ni vema Serikali ikabuni mpango wa kudumu (sustainable) wa kuwasaidia Watendaji hawa kupata vifaa hivi, hata kama ni kwa kuwakopesha kama tunavyofanya kwa Wabunge na kukata kwenye mishahara yao. Kmsingi hawa ndio wanaofanya kazi nyingi zaidi kuliko hata Makatibu Tarafa ambao tumewapatia pikipiki tayari. WEO wako karibu zaidi na maeneo ya kazi, na Makatibu tarafa wana umuhimu wa uratibu tu. Uratibu hauna tija iwapo mzalishaji hana tija.
(vii) Serikali itazame upya sheria na 7 na 8 ya Mwaka 1982 na kuweka wazi zaidi majukumu ya Wakuu wa Wilaya, kama kufuta nafasi hizo zimeshindikana, ili kuleta tija zaidi kati ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya (DED) ambaye ndiye mwenye Wataalam na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambaye kimsingi ina viongozi wakuu wasiozidi 3. Ni kichekesho kufikiri kuwa watu 3 wanaweza kuwa na utaalam wa aina zote kuweza kusimamia Wataalam zaidi ya 100 walioko chini ya Ofisi ya Mkurugenzi na Mtendaji wa Halmashauri. Matokeo ni kuwa Wakuu wa Wilaya ndio wamekuwa wakitekeleza majukumu ya Wakurugenzi kwa kutembelea vijiji na Wakurugenzi kubaki maofisini au kuhudhuria Semina za nje, kutokana na mgawanyo usio wa wazi wa majukumu. Eneo hili linahitaji kuangaliwa haraka sana.
(viii) Sheria zinazoongoza Serikali za Mitaa pamoja na Sheria ya Regional Administration inayounda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zirekebishwe haraka sana kuendana na mabadiliko makubwa yanayotokea sasa na kwa kuzingatia Mpango wa Maboresho, ambao sasa uko karibu mwaka wa 8. Matunda ya Maboresho bado hayajaonekana pamoja na kuwa fedha nyingi sana za Wafadhili na za ndani zimetumika katika Semina na Warsha za Maboresho.
(ix) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kufahamu kwa kina kauli ya Serikali juu ya mapendekezo haya.
(x) Kambi ya Upinzani pia inapenda kupata tathmini ya kina ya Mpango wa Maboresho, ukionyesha malengo yake na mafanikio na matatizo tuliyokutana nayo, na mpango mzima umegharimu fedha kiasi gani za ndani na ngapi za nje.
(xi) Kambi ya Upinzani inayotaarifa kuhusu Program ya Mafunzo kwa Ushirikiano na Serikali ya Japan ambapo Ma Ras na baadhi ya DED walihudhuria kwa awamu kadhaa kule Japan. Taarifa tuliyonayo ni kuwa kutokana na Programu hiyo mapendekezo mengi ya msingi yalifanyika mathalan:
a) Mgawanyo mzuri zaidi wa Majukumu ya madaraka kati ya Serikali kuu na Serikali za Mitaa. Hapa kwetu bado Serikali za Mitaa japo zinatajwa na Katiba lakini, kiutendaji bado ni “Field Agents” wa Serikali Kuu, na maamuzi yake yanaweza kuingiliwa wakati wowote na Serikali Kuu. Japan hilo haliwezi kutokea kwa vile wameunda Machinery kabisa ya kusuluhisha migogoro kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, na mahusiano baina ya Serikali hizi yanalindwa kabisa kwa Sheria ya Bunge.
b) Serikali za Mitaa zina Mamlaka kamili. Hapa kwetu tunaziita Serikali, lakini kiutendaji hazionekani kama Serikali. Makusanyo yote yanakusanywa na Serikali kuu, lakini mgawanyo asilimia 60 unaenda Serikali za Mitaa na asilimia 40 tu ndiyo inayobaki Serikali Kuu.
(xii) Kutokana na Program hiyo basi, je Serikali imepanga kutumia vipi uzoefu waliopata Ma RAS na Ma DED hao? Hatua gani inafuata sasa baada ya kuwa Tathmini ya Program hiyo imefanyika? Serikali itatoa lini kwa Bunge hili Taarifa hiyo ya Tathmini ili lifahamu Matokeo ya Program hiyo, kwani wahusika waliporudi walitakiwa kufanya Semina kwenye maeneo yao ili elimu hiyo iwafikie watu wengi na kwa taarifa yetu kazi hiyo haikufanyika.
BAJETI YA 2007/2008 NA MAENEO YA VIPAU MBELE:
40: Mheshimiwa Spika,
Vipaumbele vilivyowekwa vinakubalika kwa vile ndiyo msingi wa maendeleo. Ndiyo maana hata katika Bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani vipaumbele hivyo hivyo viliwekwa na kuongezea Utawala Bora kama eneo muhimu sana. Utawala Bora, hasa uwazi na uwajibikaji vikikosekana, yote mengine yaliyowekwa kama vipaumbele vitaporomoka. Fedha zitaibiwa, zitatumika vibaya, hapatukuwa na uwazi, na matokeo yake ni kuwa kazi zitafanyika nusu nusu tu. Kambi ya Upinzani inataka kutoa rai kuwa ili tufanikiwe, ni lazima tuondokane na dhana ya itikadi.
41: Mheshimiwa Spika,
Maendeleo hayajui itikadi. Barabara ni barabara tu utoke chama gani. Maji hayana sura, na wananchi hawatajali ni chama bali wataangalia nani kawaongoza kupata maji. Hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ndiyo Mratibu wa Vyama vya Siasa, ni vyema ikaandaa utaratibu wa kujenga imani kwa Watanzania kufanya kazi pamoja kwa ujumla wao bila kujali itikadi zao. Ni imani yetu, kuwa Waziri Mkuu atakuwa kiungo kati ya Serikali na Vyama kama malengo ya Ofisi yake yanavyoeleza, na atapanga mapema iwezekanavyo kukutana na vyama vya Siasa ili kubadilishana mawazo na viongozi wa Vyama mbalimbali vya siasa.
MAMBO YA JUMLA:
46: Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kuwa mwaka 2007 Taifa letu lilikumbwa na janga la Ukame. Wote tunaomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la aina hiyo tena. Kutokana na hali hiyo hatua mbalimbali zilichukuliwa kulinusuru Taifa letu na athari ya ukame huo. Baadhi ya hatua za kunusuru zilipigiwa kelele sana na Wananchi na makundi ya wadau mbalimbali. Ni katika hatua hiyo, TAKUKURU, Taasisi ya Rushwa ilichukua hatua ya kuchunguza misingi ya malalamiko hayo.
47: Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kutambua hali hiyo, Kambi ya Upinzani imestushwa sana na Tamko la TAKURU. Tamko hilo lilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Takuru, tarehe 11 May, 2007, na kwa kifupi inatoa ifuatavyo:
(i) Kuwa mchakato mzima wa kumtafuta mzabuni wa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ambako kampuni ya Richmond iliibuka mshindi, ulikuwa wa wazi na hakukuwa na mazingira yeyote ya rushwa.
(ii) Mchakato mzima, mbali ya kuwa wazi na shindanishi, hakukuwa na ushahidi wowote uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe wala upokeaji wa kamisheni kwa watendaji kama ilivyokuwa inadaiwa.
(iii) Hakuna ushahidi wowote, uliopatikana kuthibitisha ofisa yeyote Serikalini kumiliki hisa au kuwa na madaraka katika kampuni ya Richmond Development Company.
(iv) Hata hivyo:
a) Uchunguzi umethibitisha kwamba mapungufu
yalikuwepo, hata hivyo mapungufu hayo yalikuwa ya kawaida na hakuna hasara iliyosababishwa na mapungufu hayo.
b) Kampuni yenyewe ya Richmond haikuwa na uwezo, na ilikuwa imeegemea kampuni kubwa ya Pratt and Witney yenye uzoefu mkubwa.
48: Mheshimiwa Spika,
Taarifa hiyo ya TAKUKURU inasikitisha kwa sababu badala ya kutoa majibu ya kuridhisha inazua masuali mengi zaidi; Masuala haya ni:-
(i) Taarifa inakiri kuwa kulikuwa na mapungufu, lakini haitaji mapungufu yapi
(ii) Taarifa inaeleza kuwa mapungufu haya ni ya kawaida na hayakusababisha hasara kwa Serikali. Tunashangaa mapungufu haya ni yapi wakati Taarifa iliyotolewa ya TANESCO inaonyesha kuwa Mitambo iliyonunuliwa na Tanesco yenye kutoa Megawati 100 kama hiyo iliyodishwa, ina thamani ya dola za marekani 134 millioni na wakati huo huo Richmond wamelipwa Billioni 172. Taarifa haielezi hii tofauti inatoka wapi na je hii si hasara kulipia mitambo ya kukodi kwa bei kubwa kuliko bei ya soko, na isitoshe, kwa bei hiyo ya Billioni 172 ingepatikana mitambo ya kununua na siyo ya kukodi.
(iii) Taarifa ya TAKUKURU inaeleza kuwa Kampuni ya Richmond ilisajiliwa Tanzania 12 Julai, siku kadhaa baada ya kusaini mkataba na TANESCO (Mkataba huo unasemekana kwa taarifa hiyo, ulisainiwa 23 Juni 2006, jambo linalotia utata zaidi je, ni halali kwa shirika la Umma kuingia kwenye Mkataba na kampuni ambayo haikusajiliwa?
(iv) Utata mwingine ni pale ambapo awali kampuni zote zilizoomba Tenda hiyo zilikataliwa kwa vile hazikuwa na uwezo (capacity). Baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea, Kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na uwezo ikateuliwa, bila taarifa kufafanua kama Tenda ilitangazwa tena, jambo ambalo kwa dhahiri kama halikufanyika ni kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma.Taarifa inasema TANESCO walikuwa wametoa tahadhari kuhusu uwezo wa Kampuni ya Richmond lakini ushauri huo haukusikilizwa.
(v) Bado watanzania hawajapata pia maelezo ya kina kuhusu Kampuni ya Dowans ambayo nayo imesemekana kumbwa na matatizo makubwa.
49: Mheshimiwa Spika, kutokana na utata huu kwenye Taarifa ambayo inaelekea inajikanganya, na pia haionyeshi uchunguzi huu wa PCCB ulifanyika vipi, nani waliohojiwa, na sababu za Mkataba kusainiwa kabla ya kuandikishwa Kampuni hazikupewa majibu. Kutokana na sababu hiyo, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali:-
a) Kuiwasilisha Bungeni taarifa Kamili ya TAKUKURU (PCCB) ili waheshimiwa wabunge waweze kuisoma, kuitafakari, na kuichambua Taarifa hiyo ili wajiridhishe na Taarifa hiyo. Fedha zilizotumika ni fedha za umma, hivyo ni haki ya wawakilishi wa wananchi kujuridhisha na taarifa hiyo.
b) Serikali ilieleze Bunge hili Tukufu na Taifa kwa ujumla ni kwa nini tumelipa Tshs 172 Billioni kama kwa fedha hizo hizo au chini yake tungeweza kununua mashine kama hizo za kumiliki sisi moja kwa moja, na tusingeliwajibika kulipia ‘Capacity charge’ ambayo sasa tunawajibika kuilipa tutumie umeme au tusitumie umeme wao. Serikali iwe wazi ni hasara kiasi gani Taifa limepata kutokana na kuingia mkataba na Kampuni isiyo na uwezo?
c) Kama kulitokea mapungufu, Bunge hili lielezwe waliohusika na mapungufu hayo ni kina nani, na je wamechukuliwa hatua gani?
d) Kwa vile Mkataba huu ulikuwa wa dharura kutokana na ukame. Na hadi mvua ziliponyesha Kampuni ya Richmond haikuweza kutoa umeme uliotakiwa. Ni kwanini katika hatua hiyo Serikali haikuvunja Mkataba na Richmond na hivyo kuokoa fedha nyingi za Serikali na wananchi?
50: Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Ushindani inapenda kupata Taarifa na majibu ya kina kuhusu hoja hizi.
Sasa naomba nikushukuru tena kwa kunipa fursa hii, na pia nawashukuru waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kunisikiliza. Mwenyezi Mungu atupe hekima na Baraka kwa manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Nawasilisha.
……………………….………………………
Dr. Willibrod Peter Slaa (MB),
Jimbo la Karatu,
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-
OFISI YA WAZIRI MKUU/TAMISEMI.
25 June, 2007, Dodoma.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment