Monday, August 30, 2010

Slaa: Matokeo yataishangaza dunia

Chadema kimesema kitaishangaza dunia kutokana na matokeo ya kura za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu kwa kushinda kwa kishindo katika nafasi zote.

Aidha, chama hicho kimesema kinatarajia kushinda katika nafasi nyingi kuanzia udiwani, ubunge na urais kwa kuwa dalili za ushindi huo zimeanza kuonekaka kutokana na watu kuikubali ilani yake.


Kauli hiyo ilitolewa jana katika viwanja vya Kimara Suca, jijini Dar es Salaam, na mgombea wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa, wakati akizindua kampeni za mgombea ubunge jimbo la Ubungo, John Mnyika, pamoja na madiwani wa jimbo hilo.


Alisema CCM kijiandae kwa kubwagwa na kumtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kuacha kuudanganya umma kwamba wana nafasi ya kuendelea kuitawala nchi, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.


“Mwaka huu tutaishangaza dunia kwa kukiondoa madarakani CCM... kwa kuwa Watanzania wamechoka kuburuzwa na wako tayari katika mapambano ya kuleta mageuzi,” alisema Dk. Slaa.


Alisema Chadema ikishinda hakitavunja Muungano kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali kitaboresha kwa kuunda serikali tatu ambazo ni, Serikali ndogo ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika ambayo itashughulikia masuala ya Tanzania Bara na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, itakayoshughulikia masuala ya ulinzi, fedha na mahusiano ya kimataifa.


Mbali na hayo, alisema taifa liko kwenye msiba kwa muda wa miaka 50 sasa ambao ni maradhi na umaskini uliokithiri.


Kwa upande wake, Mnyika alisema wakimchagua kwenda kuwawakilisha kwa miaka mitano ijayo, amejiandaa kutatua matatizo sugu ikiwemo, ajira, elimu, miundombinu, maji, ardhi na afya.


Mnyika aliwataka wananchi waamke kwa kuchagua madiwani wa Chadema ambao wataweza kupambana na ufisadi wa fedha za halmashauri yao ya Kinondoni.



CHANZO: NIPASHE

1 comments:

Mabble said...

Hii ni kweli kabisa, tunachoomba ni kuona vyombo vya habari, taasisi za serikali, waangalizi wauchaguzi wa ndani na nje ya nchi wanafanya kazi zao inavyostahili na kwa uaminifu. Hatutakubaliana kabisa na wizi wa kula kwa namna yoyote ile. Na hii tuomba liwe angalizo kwa serikali na chama kilicho madarakani, kuhakikisha hawavitumii kwa namna yoyote ile na kwa maslahi yoyote yale. Mungu ibariki Tanzania, Mungu kibariki chama kinachopigania haki na ustawi wa jamii yetu Watanzania.

Post a Comment