Tuesday, September 7, 2010

Dr. Slaa aleta nuru mpya Tanzania

Mgombea wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dr. Willibrod Slaa amefungua safari yake ya kuelekea Ikulu kwa mkutano mkubwa wa maelefu ya wanachama, mashabiki na wananchi walijitokeza kumsikiliza Jangwani na mamilioni wengine waliofuatilia ufunguzi huo wa kampeni kwenye luninga na radio.

Dr. Slaa akiwa amezungukwa na uongozi wote wa Juu wa chama hicho na wazee wastaafu wa chama hicho alizungumza kwa hamasa kubwa kuelezea haja ya mabadiliko ya kiutawala, kimfumo na kiungozi ili hatimaye Tanzania iweze kutoka katika taifa maskini kuelekea taifa la kisasa. Hotuba ya Dr. Slaa ilitanguliwa na hotuba za viongozi mbalimbali wa Chadema ambao nao walitumia muda huo kuhamasisha wapiga kura kuchagua mabadiliko.

Tukio la kusisimua lilitokea pale mwanachama mpya wa Chadema na wakili maarufu nchini Bw. Mabere Marando ambaye ni miongoni mwa waasisi wa harakati za upinzani nchini alipoanza kuzungumza na kutaja majina na vyeo vya watu mbalimbali kiasi cha kuonekana kusisimua wananchi. Akiwa katikati ya hotuba yake matangazo yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) yakakatishwa kwa kile kilichodaiwa ni "matatizo ya mitambo". Tukio hilo lilikuja baada ya Bw. Marando kudai kuwa wizi uliotokea Benki Kuu umetokana na ushawishi wa viongozi wa juu wa serikali ya wakati hao yaani Rais Mkapa, Lowassa na Rostam Aziz.

Hata hivyo kampeni ya Chadema nao wakasita kuendelea na hotuba hadi matangazo yatakaporudi na hivyo vikundi vya wasanii vikajimwaga jukwaani kutumbuiza wakati wanasubiri hali ya ufundi itengemae. Hata hivyo baada ya muda kidogo matangazo yalirudi tena hewani na wazungumzaji wakaendelea kuzungumza.

Viongozi wengi wa Chadema waliosimama kuzungumza walionesha na kutetea kuwa kati ya wagombea wote wa nafasi ya Urais hakuna anayefaa zaidi kama Dr. Slaa na wakawasihi Watanzania kufanya maamuzi muhimu na magumu Oktoba 31. Hotuba ya Dr. Slaa ilitanguliwa kwa kuzinduliwa kwa Ilani ya Uchaguzi ya Chadema ya 2010-2015 na hotuba ya mgombea Mwenza Bw. Said Mzee.

Author: Mwanakijij

0 comments:

Post a Comment