Tuesday, September 7, 2010

Kwa nini hofu ya upadre wa Dk. Slaa haina msingi

Lula wa Ndali-Mwananzela
Septemba 1, 2010

KWA muda mrefu sasa vyombo kadhaa mbalimbali vya habari na watu binafsi vimekuwa vikieneza habari kuwa Dk. Wilibroad Slaa ni Padre wa Kanisa Katoliki na kuwa kwa vile aliwahi kuwa Padre (kuhani) ndani ya Kanisa hilo ina maana kuwa hadi leo hii yeye ni padre kama walivyo mapadre wengine.

Kutokana na madai hayo ya kuwa Dk. Slaa bado ni padre hivyo hastahili kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengi wanaosema mambo haya wanaonyesha kutokujua mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya upadre na jinsi gani mtu anaweza kuwa padre na akauacha na kuwa mlei kama walei wengine.

Kanisa Katoliki linazo Sakramenti saba ambazo ni Ubatizo, Kipaimara, Komunio (Ekaristia), Upatanisho (Maungamo), Ndoa, Upadrisho (Ukuhani) na Mpako wa Wagonjwa.

Sakramenti hizo saba zipo ambazo zinatolewa mara moja tu kwa mtu na nyingine ambazo zaweza kurudiwa. Tunaposema "kutolewa mara moja" maana yake ni kuwa mtu anapopatiwa uwezo na nguvu za kuanza kupokea neema za sakramenti hizo hilo hufanywa mara moja tu na hairudiwi tena (isipokuwa kama hakuna uhakika kuwa alishapokea mara hiyo ya kwanza). Hizi ni Ubatizo, Kipaimara na Upadrisho.

Nyingine ni zile ambazo mtu anapokea mara ya kwanza lakini katika maisha yake ya kila siku anarudia kupokea mara kwa mara kwa kadiri inavyohitajika. Hizi ni Ekaristia na Maungamamo japo nazo huanza kupewa mara moja tu na kutoka hapo ni kuendelea kuchota neema zake kwa taribu zinazotakiwa. Na zipo ambazo hufanywa upya kabisa kama vile hazijawahi kufanywa kabisa; hizi ni ndoa na mpako wa wagonjwa.

Si kusudio langu kuelezea theolojia ya sakramenti hizo ila nataka kuzungumzia hili ambalo linaonekana kuwashinda watu kuelewa. Jambo hili kwa wengine wanalipa ugumu usiostahili kwani unahitaji kukaa chini kwa sekunde chache tu kuelewesha na wewe mwenyewe ukajikuta unapata ule wasaa wa kusema “aha! Nimekuelewa”. Hata hivyo, natarajia kutokueleweka kwa baadhi ya watu kwa sababu aidha ni wagumu mno kuelewa au wana wepesi wa kusahau.

Ni kweli Dk. Slaa alipewa Sakramenti ya Upadrisho ndani ya Kanisa Katoliki baada ya kumaliza maandalizi yake ya kazi hiyo. Upadre si kama kazi nyingine ambazo mtu "anasomea"; si sawa na udaktari, uwakili au uhasibu. Upadre ni Sakramenti ya Ukuhani ambayo mtu anaandaliwa kuiingia na kuitumikia. Ndiyo maana kimsingi kabisa, hata mtu ambaye hajasomea kabisa mambo ya theolojia na falsafa anaweza akapewa Upadrisho endapo haja kama hiyo inatokea.

Lakini kwa miaka mia nyingi Makanisa (Mashariki na Magharibi) yamekuwa yakiwaandaa wale wanaotaka kuingia katika "Daraja Takatifu" kwa mafunzo maalumu ya mambo ya dini, falsafa, utawala n.k Ukiondoa mafunzo ya Theolojia ya Katoliki mafunzo mengine ya falsafa, utawala, au elimu nyingine yoyote ni sawa kabisa na mafunzo yanayotolewa katika vyuo vikuu vingine.

Mtu akishapata daraja ya Ushemasi wa Mpito (hatua ya kwanza kabla ya upadre) na baadaye Upadre basi anakuwa ni "Kuhani Milele kwa mfano wa Melkizedeki" na hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kufanywa kuondoa daraja hilo. Hii huitwa "alama isiyofutika". Ni alama ile ile ambayo inapatikana katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara ambapo mtu akishabatizwa ubatizo wake hauwezi kurudiwa tena kwani alama hiyo ya neema haifutiki. Kama vile wakristo wote waliobatizwa nao wanayo alama ya kudumu ya ukristo wao. Hata Mkatoliki anapoacha dini, kuhamia dhehebu jingine au kuhamia dini nyingine alama hii ya ubatizo haifutiki.

Kutokana na hilo Mkatoliki huyo akiamua kurudi kwenye Imani Katoliki basi habatizwi tena zaidi ya kuungamishwa Imani ya Mitume. Alama hii ya ubatizo si kwa Wakatoliki tu, Kanisa Katoliki linatambua kama ni halali ubatizo unaofanywa na madhehebu mengine ya kikristu (japo si yote) kama vile Waanglikana na Walutheri.

Ndiyo maana Wakatoliki, kwa mfano, wakimpokea Mkristu anayetoka Ulutheri au Anglikana ambaye amebatizwa huko hatobatizwa tena kwenye Ukatoliki atapokelea tu baada ya kukiri imani Katoliki.

Hili nalo ni kweli kwa mtu analiyepadrishwa. Alama yake ya upadrisho wake ni ya kudumu na hakuna kitu ambacho yeye au mtu mwingine anaweza kufanya kuifuta milele. Hata yeye mwenyewe hawezi kuifuta kwa kutoamini au kukana uwepo wa Mungu. Ni kwa sababu hiyo mtu ambaye ameshawahi kupata upadrisho ataendelea kuwa na alama hiyo milele. Hili ni fundisho ambalo ni msingi wa kuelewa padre ambaye bado anahudumu na padre ambaye ana alama ya kudumu. Mapadre wote wanayo alama hii ya kudumu lakini si wote wanaweza kuhudumu kama mapadre.

Kwa maana hiyo, Padre wa Kikatoliki anaweza kuacha, kufukuzwa, kuachishwa kazi za kila siku za kutoa huduma ya Upadre lakini bado anabakia kuwa ni padre moyoni. Hivyo, mtu huyo aliyeacha hastahili kuitwa "Padre X" kwa maana ya mapadre ambao bado wako kwenye huduma. Ni sawa na daktari aliyeacha kazi ya udaktari au kufukuzwa udaktari au uwakili lakini bado mafunzo na uwezo wa kutoa huduma hiyo akawa bado anao japo haruhusiwi tena kufanya hivyo. Wapo watu ambao kutokana na mazoea wataendelea kumuita "daktari" japo hafanyi tena huduma hiyo.

Jambo hili ni muhimu kulielewa. Mtu ambaye ameacha yeye mwenyewe upadre bila kurejeshewa hali yake ya ulei (yaani uumini wa kawaida) kwa mujibu wa taratibu za Kanisa basi mtu huyo bado ni padre na haruhusiwi kupewa Sakramenti ya Ndoa na anafungwa na vifungo vingi zaidi.

Hata hivyo, Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kumfanya mtu aliyewahi kuwa padre kurejeshwa kwenye hali ya ulei (yaani kuondolewa kabisa kazi na haki ya kufanya kazi za upadre na kuwa muumini wa kawaida kabisa). Mtu ambaye ameondolewa upadre kwa utaratibu wa Kanisa (laicization –kufanywa mlei) na kibali cha Vatikani anaondolewa haki na majukumu yote ya mapadre wengine isipokuwa mambo mawili tu yaani useja (celibacy) na kusikiliza maungamo ya mtu aliyekaribu na kifo.

Hilo la useja linahitaji kibali kingine kuondolewa ili aruhusiwe kuoa. Hata hivyo, kwa vile padre ni padre milele basi mtu aliyewahi kuwa padre anaweza kusikiliza maungamo na kutoa msamaha kwa mtu ambaye yuko katika hatari ya kifo tu.

Kwa mfano, wamesafiri mahali na gari limepinduka na hakuna msaada wa karibu na yupo mtu ambaye ni mkatoliki (au mtu mwingine mwenye imani hiyo ya maungamano) na akaomba kama kuna padre asikilize maungamano yake basi yule aliyekuwa padre anaweza kabisa kusikiliza maungamo hayo na kumpatia ondoleo la dhambi. Japo kama na yeye atanusurika kuna utaratibu wa kutoa taarifa kwa Askofu wa eneo hilo juu ya tukio hilo bila kutoa taarifa ya kilichoungamwa.

Sasa basi, si ajabu kabisa kwa padre kufuata utaratibu na kurejeshewa hali yake ya ulei. Pindi hilo linapotokea basi padre huyo hupewa masharti yake mapya ya hali yake hiyo mpya ya jinsi gani aishi kama asiye padre.

Miongoni mwa mambo hayo ni kukatazwa kuvaa nguo yoyote ya kipadre (kama kola ya kirumi shingoni), kukatazwa kukaa katika eneo la kanisa, kunyimwa haki za matunzo atakapostaafu kama mapadre wengine, kukatazwa hata kuwa mhudumu wa komunio ndani ya kanisa ili isije kuwachanganya watu na wengine wanaopewa masharti ya kutofundisha elimu ya theolojia katika vyuo visivyo vya kikatoliki n.k Lengo ni kuhakikisha kuwa mtu huyo anabakia ni padre jina tu na si mhudumu.

Jambo kubwa, hata hivyo, ni kuwa watu wanachanganya masharti ya Sheria ya Kanisa yanayomkataza padre mhudumu kushiriki kugombea nafasi ya kisiasa. Sheria ya Kanisa namba 285 kwenye mojawapo ya sehemu zake ndogo inakataza kwa padre mhudumu kushiriki katika nafasi ya kuchaguliwa katika mambo ya siasa. Hivyo, paroko au paroko msaidizi mahali au padre mwingine yoyote ambaye bado yuko katika huduma haruhusiwi kugombea uchaguzi au nafasi ya kisiasa.

Hii kanuni hata hivyo haifuatwi wakati wote. Historia inao mapadre kadhaa ambao kutokana na matakwa yao wenyewe waliamua kushiriki katika nafasi za kisiasa wakati mwingine kinyume na maelekezo ya uongozi wa juu wa Kanisa (maaskofu wao au Vatican).

Mwaka jana huko Ufilipino Padre Edd Panlilio alitamani kuwa Rais wa nchi hiyo mojawapo yenye Wakatoliki wengi duniani. Kwa vile alikuwa bado ni padre mhudumu sheria za Kanisa zilikataza yeye kufanya hivyo. Hata hivyo, alikuwa tayari kuomba kuruhusiwa kuwa mlei ili agombee nafasi hiyo.

Mfano mzuri wa kuelewa hili ni aliyekuwa Askofu Ferdando Lugo wa San Pedro huko Paraguay. Askofu Lugo alitaka kuingia katika siasa kitu ambacho kinakatazwa na Kanuni za Kanisa Katoliki. Askofu Lugo aliomba Kanisa Katoliki limruhusu arejee katika hali ya ulei ili aweze kushiriki katika siasa lakini Kanisa lilimkatalia, yeye aliendelea kugombea na aliposhinda uchaguzi Mkuu wa Paraguay Kanisa Katoliki lilikubali kumuondolea Upadre wake na kumrejesha katika Ulei. Hivyo, Rais wa sasa wa Paraguay ni Askofu wa zamani wa Kanisa Katoliki ambaye alirejeshwa katika ulei.

Hii ina maana ya kwamba, Dk. Slaa si tu ni mlei lakini anayo haki kama wakatoliki wengine walei kushiriki katika nafasi ya uongozi kwani hajavunja sheria yoyote ya Kanisa, wala hajaenda nje ya haki zake za kikatiba. Dk. Slaa sasa hivi ni muumini Mlei kama wengine na atakapoamua kupata sakramenti nyingine yoyote ya Kanisa ataweza kufanya hivyo kwa uamuzi wake yeye mwenyewe kwani alifuata taratibu za Kanisa za kurejeshwa katika maisha ya mlei.

Hivyo, Dk. Slaa si mtumishi wa Kanisa Katoliki na si padre kwa maana ya kuwa anahaki na majukumu yote ya mapadre wengine. Yeye ni muumini mlei ambaye kutokana na nafasi yake ya kuwa aliwahi kuwa padre anabakia na haki za waumini wengine walei ndani ya kanisa hilo na vile vile uwezo wa kusikiliza maungamano ya mtu aliye katika hatari ya kifo TU.

Hii ina maana ya kwamba Dk. Slaa anayo haki kama Mtanzania mwingine bila kujali dini yake au nafasi yake katika dini hiyo kugombea nafasi ya Urais.

Hili ni muhimu kuelewa kuwa Katiba yetu haimkatazi hata padre mhudumu kugombea nafasi ya Urais au ubunge kama akitaka, makatazo hayo yako kwenye Kanisa na si kwenye Katiba yetu. Hivyo, hata kama leo akatokea padre, shehe, mchungaji n.k akataka kugombea nafasi yoyote ya ubunge basi anazo haki hizo.

Tayari tunajua wapo wasomi wengi tu wa dini zetu kubwa mbili ambao wamekwishakuingia bungeni. Dk. Slaa ameshakuwa Mbunge kwa vipindi vitatu. Wapo na wabunge wengine na hata katika nafasi nyingine za kisiasa za watu ambao wamewahi kushika elimu ya juu ya dini za Kikristu na Kiislamu na hatukuwahi kuona watu wanalalamika kuwa kwanini watu waliowahi kuwa wachungaji (au walio bado wachungaji), mashehe au walimu wa dini kuingia na kuchaguliwa kwenye siasa.

Kama tunakubali kuwa watu hao wote wameweza kutimizwa matakwa ya Katiba yetu na tukawakubali kwa nini inapofika kwenye suala la Urais tuanze kutoa sababu zisizo na kichwa wala miguu? Hivi leo kama Kikwete angekuwa ni msomi wa dini ya Kiislamu au mtu aliyewahi kuwa shehe huko nyuma kweli tungeweza kwa haki kusema kuwa hilo peke yake linamfanya asistahili kuwa Rais wetu kama tunamkubali?

Lakini jambo la mwisho ambalo linaonekana kuwasumbua watu wengine na halihitaji maneno mengi kwa sababu hapo juu tayari nimeliashiria ni hofu ya baadhi ya watu kuwa ati Dk. Slaa kwa vile aliwahi kuwa padre basi akiingia madarakani atakuwa chini ya maelekezo ya Baraza la Maaskofu au Vatican yenyewe.

Kwa vile nimekwishakusema hapo juu kuwa mtu akisharudishwa kwenye hali ya ulei hawi tena chini ya utawala, nidhamu au maelekezo ya askofu wake kama mapadre wengine kumbe Dk. Slaa hayuko chini ya Askofu wa Mbulu, Baraza la Maaskofu au Vatican kiutawala. Yuko kama Mkatoliki mwingine yoyote ambaye anaweza kwenda popote, kufanya biashara yoyote, kuishi popote na yeyote bila kulazimishwa kuulizwa au kutoa maelezo kwa mtu yeyote.

Hii ina maana ya kwamba hakuna mtu wa Baraza la Maaskofu ambaye anaweza kumuita Dk. Slaa ati ampatie maelezo au mtu ambaye anaweza kuingilia shughuli zake za kisiasa. Viongozi wa Kanisa wameachiwa eneo la kiroho tu kama ilivyo kwa wachungaji, mashehe, na viongozi wengine wa dini kwa imani ya waumini wao.

Tukikubali kuwa ati kwa vile mtu amewahi kuwa Mkatoliki basi atapokea maelekezo toka kwa uongozi wa Kanisa kwenye mambo ya kisiasa ni lazima tukubali kuwa mtu wa dini nyingine au dhehebu jingine naye ataweza kuburuzwa na viongozi wake wa dini.

Hadi hivi sasa tunaweza kuona wazi kuwa mambo kadhaa ambayo Dk. Slaa ameyafanya au kuyasema hadharani nina uhakika baadhi ya viongozi wa dini wasingependa ayaseme jinsi hiyo au wangeweza hata kumkalisha chini.

Dk. Slaa ameweza kujionyesha kuwa ni mtu wa kuthubutu, yuko huru na haangalii nyani usoni. Kama alivyozungumza siku chache zilizopita staili yake hiyo ya utawala inafahamika hata kwa mapadre na viongozi wengine wa Kanisa ambao aligongana nao wakati akiwa katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki.

Tanzania haimhitaji padre kuwa rais, Tanzania haihitaji mchumi kuwa Rais, Tanzania haihitaji daktari kuwa Rais, Tanzania haihitaji mwalimu kuwa Rais, na vile vile haihitaji shehe kuwa Rais. Hizo zote si sifa za kuwa Rais.

Tanzania inahitaji Mtanzania mwenye kutimiza masharti ya Katiba kuwa Rais na awe ni mtu mwenye uwezo wa kutuongoza tunakotaka kwenda na ambaye atakuwa tayari kutupa uongozi bora tunaouhitaji kuelekea katika safari ya ujenzi mpya wa Taifa.

Kama hilo litamhusisha mtu aliyewahi kuwa mchumi, mkuu wa wilaya, waziri wa mambo ya nje au mtaalamu wa nyota na iwe! Lakini kama itamtaka mtu aliyewahi kuwa padre basi na iwe, kwani tukianza ubaguzi kwa sababu ya maisha ya kidini ambayo mtu amewahi kuyaishi, itakuwaje kwa wale ambao leo wanagombea na wamewahi kuwa waganga wa kienyeji au bado ni waganga wa kienyeji?

Barua-pepe:


0 comments:

Post a Comment