Friday, September 10, 2010

Nukuu ya Leo kutoka kwa Dk. Slaa



"Simamia, Dhibiti, Wajibisha." Hii ni kauli nzito iliyotolewa na mgombea urais kupitia Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akisisitiza umuhimu wa uongozi unaowajibika na kuwajibisha, ili kuokoa raslimali za taifa na kuzielekeza katika huduma za jamii. Akasema anahitajika kiongozi anayeweza kufanya mambo hayo matatu, ili kuwezesha serikali kuokoa pesa na kuziingiza katika kulipia elimu na afya. Alitoa kauli hii mjini Ngudu, Mwanza, katika mkutano wake wa tano leo, mara baada ya kuwaeleza wananchi kuhusu sera za afya na elimu, kwamba zitalipiwa na serikali, na kwamba vyanzo vya mapato ya kulipia huduma hizo vipo, na kwamba serikali ya JK inashindwa kuyatekeleza hayo kwa sababu inaishi katika anasa. Meneo mengine aliyotembelea leo ni Itinge, Mwandoya, Hungumalwa na Mwamashimba.

Alizungumzia umuhimu wa serikali kufumua mikataba yote mibaya, hasa ya madini, inayopoteza mabilioni ya shilingi kila siku, ili kumpunguzia Mtanzania mateso yanayosababisha na uongozi usiojali wananchi. Amekuwa akisema kila mahali kuwa serikali ya sasa inakumbatia wawekezaji, inatelekeza wananchi.

Dk Slaa pia alizungumzia pia suala la mishahara ya wafanyakazi, akisema iwapo ataingia madarakani, ataiboresha kwa kufanya kima cha hini kiwe Sh 315,000; huku akiwaongezea marupurupu ma maslahi ya nyongeza katika huduma za ujenzi wa makazi bora na bima za afya. Huku akiwakumbusha hongo iliyotolewa na JK mwezi uliopita kwa kuwaingizia wafanyakazi nyongeza katika mishahara, kinyume cha bajeti iliyopitishwa na Bunge, Dk. Slaa alisema hawataiona nyongeza hiyo baada ya uchaguzi kwa kuwa si rasmi. Alisema kwamba katika majibu ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa Chadema kuhusu pingamizi walilomwekea JK wakidai ameongeza mishahara kinyemela, hakuna mshahara wowote ulioongezwa rasmi, hivyo msajili akakosa kigezo cha kisheria cha kumtia JK hatiani. Lakini nyongeza hiyo ilikuwapo. Aliwakumbusha kuwa JK alikataa kura za wafanyakazi; akasema yeye (Slaa) anazitaka. Kuhusu pesa hizo zilizoongezwa kinyemera, alimalizia kwa nukuu nyingine muhimu, akiilekeza kwa wafanyakazi: "Zimeingizwa sasa, baada ya uchaguzi hamzioni. Mlizoingiziwa...mmeliwa."

0 comments:

Post a Comment