Barnabas Lugwisha
HAKUNA ubishi kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetokea kuwa kipenzi cha wananchi, maana mioyo ya Watanzania wengi imevutiwa na umakini wa viongozi wa chama hicho.
Ukitaka kuhakikisha hilo, rejea siku ile ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya kura za udiwani, ubunge na urais kwa kuyaangalia matokeo kwenye kata za vigogo ambazo baadhi yake ni Oysterbay, Masaki na Mbezi Beach.
Huko ni kwa waliofaidi matunda ya nchi hii na hata kufikia hatua ya kugawana nyumba za serikali. Lakini wote hao wameungana na walalahoi kwa kuipa kura CHADEMA.
Binafsi nasema, vigogo walioiunga mkono CHADEMA, hongereni sana kwani kwa mara ya kwanza mioyo yetu imeunganishwa na sera makini za CHADEMA.
Hata hivyo kwa bahati mbaya, kule kwetu Kiwalani, ndani ya Jimbo la Segerea alikoshinda Dk. Makongoro Mahanga, kura zetu zilipotea.
Katika vituo 37 tulikotumbukiza kura zetu, ilikuwa ni hasara tupu, kwani ofisa mtendaji wetu (jina tunalihifadhi), alitutangazia kuwa kura zetu zimepotea. Tulinyamaza kwa kuwa viongozi wetu walituasa tudumishe amani.
Mpendazoe umo mioyoni mwetu kwa kuwa tulikupa kura zetu, ila wajanja wamezichakachua. Inshallah siku moja utatinga mjengoni!
Turejee kwenye mada, Je, chama hiki kimekuwa mwandani wetu kirahisi? Jibu ni hapana:
Hadi kukonga nyonyo za Watanzania viongozi wakuu wa chama hiki wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, walihenyeka, wamezunguka huku na kule, kuanzia Mwanza hadi Mtwara, kote huko wamekuwa wakitoa elimu ya uraia sanjari na sera za chama chao.
Nakumbuka ni katikati ya mwaka 2003 nikiwa mwandishi wa gazeti la Mtanzania na The African, naambiwa na mabosi wangu niambatane na CHADEMA katika ziara ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, niliambatana na Waheshimiwa mzee Philemon Ndesamburo, Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa na Grace Kiwelu, ambao wote hao walikuwa ni wabunge katika majimbo, Kiwelu alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Narejea nyuma kutokana na mafanikio makubwa sana ambayo chama hicho kimeyapata achilia mbali uchakachuaji wa hali ya juu wa kura za chama hicho uliotokea kufuatia uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.
Katika ziara hiyo ambayo ilikuwa ni ya kukitangaza chama na kutoa elimu ya uraia nilijifunza mengi na nikiyaakisi kwa sasa unatimia msemo wa ‘ukitaka cha uvunguni sharti uiname.’
Tulifika Iringa, Mbeya na kwingineko, leo ni mabadiliko makubwa ambayo nimeyaona kutoka kitambo, CHADEMA imepata mbunge Iringa mjini ambako kulikuwa na wana CCM watiifu mno.
Jambo lililonishanganza ni kwamba katika ziara hiyo, eneo hilo lilikuwa gumu kwa chama hicho, kiasi cha kuwakatisha tamaa viongozi wa CHADEMA katika mikutano yao ya Iringa mjini.
Mathalani, Iringa mjini, ulifanyika mkutano wa hadhara maeneo ya stendi pale, jina la uwanja silikumbuki, katika mkutano huo wananchi wengi walijitokeza lakini cha ajabu kila walipokuwa wakisalimiwa na kiongozi aliye hutubia kwa kauli mbiu ya CHADEMA, wananchi hao walikuwa kimya ama waliitikia kwa mashaka, ni dhahiri walionyesha utii kwa chama tawala.
“People’s power, People’s Power, People’s Power (kimya).” “Aisee hawa watu ni wagumu sana,” alisikika akisema mzee Ndesamburo aliyekuwa akiwasalimia wananchi hao.
Aisee hawa watu ni wagumu sana, kumbe mzee huyu hakugundua kwamba miaka saba baadaye chama chake kitaaminika kiasi cha kupata mbunge katikati ya watu hao wagumu.
Narejea nyuma kidogo kwa sababu ninapenda niwakumbushe Watanzania wenzagu kwamba maisha unavyoyapanga na unavyotaka yawe ndivyo yanavyokuwa.
Hakuna muujiza katika maisha kwamba utapata maziwa na asali bila kufanya kazi, haiwezekani! Viongozi hawa wa CHADEMA wamemenyeka sana, walitembea nchi nzima kwa gharama zao kuwaelewesha Watanzania sera za chama hicho, kuna walio waona wanapoteza muda, lakini kuna waliowaona kama wakombozi wa baadaye wa taifa hili.
Kuna mahali tulipita katika ziara hiyo tukielekea Tarafa ya Makongorosi, nje kidogo ya Jiji la Mbeya, eneo tajiri kwa madini ya dhahabu, lakini lililotopea katika lindi la umaskini.
Nakumbuka ilinibidi kupanda juu ya mti ili nipate mtandao wa simu.
Tukiwa njiani kuelekea eneo hilo, tulikutana na bibi mmoja wa makamo, Mbowe alimuuliza maswali mbalimbali, moja ya maswali hayo nalikumbuka, lilikuwa ni jina la rais wa Tanzania kwa wakati huo (2003).
“Jina la rais ni Nyerere (alikuwa ni Rais Mkapa), alijibu bibi huyo.” Mbowe alitikisa kichwa na kusema, ‘kazi ipo.’
Kazi ipo, kwani mbali na kuwaeleza ukweli juu ya umuhimu wa mabadiliko, imekichukua chama hicho takiriban miaka 18 tangu kuanzishwa kwake kukubalika, hasa kwa Watanzania, na kuwa chama kikubwa rasmi cha upinzani ndani ya mioyo ya Watanzania.
Tukirejea Iringa na Mbeya, sehemu ambayo kila mara baada ya mikutano ya elimu kwa umma viongozi wa CHADEMA walikuwa wakiitwa polisi na kukumbushwa kuzingatia mambo fulani fulani, ilimradi tu kuwabana, leo hii imekuwa ni vituo vikuu vya upinzani katika njia kuu hiyo ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Leo hii ni faraja kubwa sana kutambua kwamba nguvu, rasilimali na elimu ya uraia waliyoitoa viongozi hawa wa CHADEMA havikupotea bure.
Havikupotea bure, kwa sababu ilihitaji ujasiri wa hali ya juu kujitolea kusafiri nchi nzima katika safari zilizopewa majina mbalimbali kama ‘Operesheni Sangara’ ilimradi kuwaelezea Watanzania umuhimu wa mabadiliko katika taifa letu.
Dk. Slaa alitumia muda mwingi kuwaelezea namna ambavyo wana Karatu wanafaidi matunda ya jasho lao, kwa maana ya maendeleo, baada ya kuichagua CHADEMA na hatimaye kuunda halmashauri. Zilikuwa ni hadithi nyingi za kuwaomba Watanzania wabadilike.
Leo hii, Watanzania wameusikia mwangwi kutoka Karatu, Moshi, Kigoma, Mbeya, Iringa, Mwanza na Arusha.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment