Sunday, 21 November 2010
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kipo tayari kukutana na serikali, chama au taasisi nyingine yoyote itakayotaka kujadiliana kuhusu hatua yao ya kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa urais na madai yao ya katiba mpya.
Katika tamko ambalo halijawahi kutokea kwenye siasa za Tanzania, Chadema ilitangaza kuwa haitambui matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai kuwa taratibu nyingi zilivurugwa kwa lengo la kumbeba mgombea wa chama tawala na ilidhihirisha msimamo wao wakati wabunge wa chama hicho walipotoka kwenye ukumbi wa Bunge mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kuanza kuhutubia.
Lakini jana mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliiambia Mwananchi kuwa wako tayari kukaa meza moja na serikali au taasisi ambayo wataiona kuwa inaweka mbele maslahi ya taifa ili kujadiliana nayo kuhusu msimamo huo wa kwanza kuweka dhidi ya rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Msimamo wa Chadema umetolewa wakati mwandishi msaidizi wa rais, Premi Kibanga akikitaka chama hicho au Mbowe kufuata taratibu zilizopo iwapo wana lengo la kweli la kutaka majadiliano.
Kibanga alisema kuwa Mbowe, kama mwanasiasa na kiongozi wa kitaifa, anazifahamu taratibu na njia za kutumia iwapo anataka kukutana na serikali. Lakini mbunge huyo wa Hai alisisitiza kuwa hawangependa majadiliano yao ya serikali yachukue sura ya kisiasa kwa kuwa kufanya hivyo hakutafanikisha kufikiwa kwa lengo wanalolikusudia. “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunalifikisha taifa hili mahali ambapo amani na utulivu utaendelea kuwepo.
Kati ya madai yetu yote hakuna jambo ambalo ni kwa ajili ya Chadema... tunayoyadai yatainufaisha CUF, CCM, vyama vingine vya siasa na wananchi wote,” alisema. Hata hivyo, Mbowe alionya kuwa mazungumzo hayo yasitawaliwe na aina ya maoni yanayotolewa na viongozi kadhaa wa CCM, yakiwemo ya katibu mkuu wa chama hicho tawala, Yusuf Makamba na katibu wa itikadi na uenezi, John Chiligati. “Hawa wameonekana kuzungumzia suala hili kisiasa zaidi wakati lengo letu sisi si kupiga siasa. Angalia hata mambo wanayosema eti tutaleta hoja ya kuwafukuza Chadema bungeni... hoja kama hiyo haina msingi kwa sababu hawana ubavu kisheria wa kufanya hivyo,” alisisitiza.
Alisema mazungumzo wanayoyalenga ni yale yatakayohakikisha kuwa madai yao yanafikiriwa kwa kina huku maslahi ya taifa yakiwekwa mbele. Alisema wanafurahi kuona kuwa kitendo chao cha kutoka bungeni wakati wa hotuba ya Rais Kikwete kimesaidia kuibua mjadala mzito nchini ambao iwapo utapewa nafasi ya kujadiliwa bila kuweka ushabiki wa kisiasa, nchi inaweza kupata mabadiliko makubwa siku za usoni.
Alitoa mfano wa wa watu kama waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani ambao walikaririwa wakisema kuwa suala la kuwa na katiba mpya ni muhimu. “Maoni kama haya, ambayo yanatoka kwa watu wazito kama hawa, yanaonyesha kuwa kitendo chetu kimeamsha mjadala wa maana kwa taifa hili,” alisema.
Alipoulizwa iwapo kitendo chao cha kutaka kukutana na serikali hakiathiri uamuzi wao wa kutotambua matokeo ya urais, alisema kuwa walishatamka tangu awali kuwa hawakatai kuwa kuna rais ingawa wanachopinga ni jinsi alivyopatikana. “Tunajua kuwa Kikwete ndiye ametangazwa kuwa rais, lakini tunachopingana nacho ni jinsi alivyoelezwa kuwa ameshinda katika uchaguzi... tunachokidai si kuwa uchaguzi urudiwe au kwamba Dk (Willibrod) Slaa atangazwe rais, la hasha. Tunalenga kuwa na mfumo bora siku za usoni ambao hautaacha shaka kwenye matokeo ya urais,” alisisitiza.
Alisema ni hatari sana kuwa na sheria ambayo hairuhusu watu kuhoji matokeo ya kura za urais katika mazingira ambamo watu wengi wanaingia kwenye kinyang’anyiro hicho. Alisema kuwa sheria ya kukataza kuhoji matokeo ya urais ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja wakati kukiwa hakuna mgombea wa kutoka vyama vya upinzani. “Wakati ule Mwalimu Nyerere ndiye kila mara alikuwa mgombea pekee, alikuwa hashindani na mtu yeyote kwa hiyo hakukuwa na mtu wa kuhoji. Wenzetu hawa wameichukua sheria hiyo na kuileta kwenye mfumo wa vyama vingi. Hauwezi kuitumia sheria hiyo hiyo wakati huu wa ushindani,” alisema.
Alisema iwapo matokeo ya uchaguzi wa ubunge na udiwani yanaweza kupingwa mahakamani, hakuna misingi ya kidemokrasia ya kukataza kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais. Alitaka serikali kuiga mfano wa Senegal ambayo ina mahakama ya katiba ambayo moja ya majukumu yake ni kusikiliza malalamiko yote kuhusiana na uchaguzi wa rais na kiongozi mpya wa nchi haapishwi hadi mahakama hiyo imethibitisha matokeo hayo. Alisema pamoja na madai ya katiba mpya, madai yao mengine ambayo wangependa yajadiliwe iwapo watakutana na serikali ni kuundwa kwa tume huru itakayochunguza matukio yote kuhusu uchaguzi wa rais.
Alisema kwa mazingira yaliyopo, tume hiyo inaweza kuundwa na Rais Kikwete lakini kwa kuwachagua watu makini ambao wanaheshimika nchini. “Watu kama hao wapo wengi tu,” alisema.
Alionya kuwa si vema tume hiyo ikachukua mrengo wa kisiasa kwani kufanya hivyo kunaweza kupotosha majadiliano. “Kuna nafasi ya Chadema au CCM kuunda tume hiyo, lakini itaonekana kuwa ni ya kichama zaidi. Pia kuna nafasi ya Bunge kuunda tume, lakini Bunge nalo lina wanasiasa ambao wana maslahi kutoka katika vyama vyao. Hii ndiyo maana tunashauri rais anaweza kuunda tume hiyo lakini kwa kuhakikisha kuwa anawateua watu ambao wanaheshimika katika jamii ambao kila mmoja anajua kuwa wanajali zaidi maslahi ya taifa,” alisema.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment