Thursday, November 18, 2010

Mfumo wa uchaguzi unawabana wanawake

na Datus Boniface

WANAWAKE waliokuwa wagombea ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu, wamesema mazingira na mfumo wa uchaguzi nchini haumruhusu mwanamke kushiriki na kushindana na wanaume katika kugombea nafasi za uongozi nchini.

Wakizungumza katika kongamano la kutathmini ushiriki wa wanawake katika Uchaguzi Mkuu, lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kufanyika Mabibo, Dar es Salaam juzi, walisema wanawake wanapaswa kujipanga upya ili kuubomoa mfumo kandamizi wa kibepari unaohitaji kutumia fedha kwa kila kitu, ili waweze kushiriki vema katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Mwakilishi wa kamati ya wanawake wanaotoka katika vyama visivyo na wabunge, Eliana Mshana, alisema serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilipaswa kuwawezesha wagombea kwa kuwalipia mawakala wa kusimamia kura, lakini haikufanya hivyo.

“UNDP ilitupa taarifa za kimaandishi kuwa wao na mashirika ya kiraia wasingeweza kutuwezesha nyenzo za kugombea bali wangetoa mafunzo ya kutujengea uwezo, ili tuwe jasiri na kujiamini katika kugombea. Serikali ilipaswa kutuwezesha wanawake lakini haikufanya hivyo,” alisema Mshana.

Wakizungumzia changamoto zilizowakumba wanawake katika Uchaguzi Mkuu uliopita, walisema tatizo kubwa lilikuwa ni kuwalipa mawakala ambapo kila mmoja alipaswa kulipwa sh 10,000 kwa siku na kwamba wanawake wengi walishindwa kuzilipa.

Nuru Kimwaga kutoka Chama cha Demokrasia Makini, aliyegombea ubunge Jimbo la Gairo, mkoani Morogoro, alisema changamoto kubwa aliyokumbana nayo ni matumizi makubwa ya rasilimali fedha na vyombo vya usafiri ambavyo yeye hakuwa navyo.

Akizungumzia changamoto hizo, Ofisa Programu Mwandamizi wa TGNP, Anna Mushi, alisema kuna haja ya kujipanga mapema kuhakikisha raslimali zinatafutwa za kutosha kwa ajili ya kuweka mawakala katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wanawake hao wametoka katika vyama 17 ambavyo ni CHADEMA, NCCR Mageuzi, CUF, TLP, SAU, CHAUSTA, UPDP, UDP, SAU, APPT-Maendeleo, DP, Jahazi Asilia NRA, Demokrasia Makini, UMD na TADEA wakati Chama cha Mapinduzi pekee hakikuwa na muwakilishi katika kongamano hilo.

Jumla ya wanawake 190 waligombea ubunge majimboni mwaka huu wakiwepo 25 CHADEMA, 24 CCM, 15 NCCR-Mageuzi, 14 CUF , 14 UDP, 14 UPDP, 12 TADEA, 11 DP na 10 UMD. Wanawake 557 waligombea udiwani majimboni.

0 comments:

Post a Comment