Saturday, November 13, 2010

Marando akubali matokeo

MWANANCHI GAZETI

Habel Chidawali, Dodoma
ALIYEKUWA mgombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Chadema, Mabere Marando, amekubali matokeo yaliyompa ushindi mpinzani wake, Anne Makinda wa CCM na kwamba, lakini anakwenda kujenga chama kwa ajili ya mapambano ya mwaka 2010.

Mabere alikuwa kwenye kinyanga’anyiro hicho na kubwagwa na Makinda anayekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Spika wa Bunge la Tanzania tangu nchi ipate uhuru.

Marando alipata kura 53 sawa na asilimia 16.2 ya kura halali zilizopigwa, ambazo ni 327 huku Makinda akipata 265 sawa na asilimia 81.03, kura tisa ziliharibika.

“Nimeshindwa na ninamtakia kazi njema yenye ufanisi wa hali ya juu, dada yangu Makinda kwani ninajua kwenye Bunge hili atapambana na changamoto kubwa, hivyo anapaswa kujiandaa kikamilifu, na sasa ninarudi kuijenga upya Chadema,” alisema Marando.

Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Rolya kwa tiketi ya NCCR Mageuzi kati ya mwaka 1995 hadi 2000, alisema CCM kilimfanyia fitina kwa kuwaita wabunge wake na kuwaasa wasimchague siku moja kabla ya uchaguzi.

Pia, Marando aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

“Jana (juzi) watu wa CCM waliitisha kikao cha nguvu na kusema ni lazima kuchagua chama, sio uwezo wa mtu hali ambayo iliwafanya wabunge wengi kushindwa kunipigia kura japokuwa waliamini kabisa kuwa nina uwezo mzuri tu wa kuongoza bunge zaidi ya Makinda,” alisema.

Alisema iwapo Mungu akijalia, mwaka 2015 Chadema kitaingia na nguvu kubwa zaidi kwenye bunge hilo, ingawa alitahadharisha kuwa kinachotakiwa ni kujipanga, vinginevyo wanaweza kupoteza zaidi.

Wakati huohuo, jana katika ukumbi wa bunge palitokea kioja wakati wagombea wakiomba kura, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alihaha ukumbi mzima kutafuta kipaza sauti cha kutumia kuuliza swali.
Ole Sendeka alipewa nafasi na msimamizi wa uchaguzi huo, Anna Abdallah, kuuliza swali lakini kipaza sauti cha mezani kwake kiligoma kuwaka ndipo alipoanza kuhaha ukumbi mzima.

Hata hivyo, licha ya kuhaha ukumbi mzima alishindwa kutimiza azma yake, baada ya Abdallah kumweleza kuwa swali hali halikustahili kumuulizwa.

0 comments:

Post a Comment