Thursday, November 25, 2010

Serikali mpya isimamiwe

MOJA ya habari kubwa leo ni Baraza jipya la Mawaziri lililotangazwa jana na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Baraza la Mawaziri lenye jumla ya mawaziri 50 huku likiwa limefanyiwa mabadiliko ya kimuundo katika wizara mbalimbali zilizokuwepo awali, lilifafanuliwa jana na Rais Kikwete kuwa linalenga kurahisisha ufanisi wa utendaji kazi wa serikali yake.

Izingatiwe kuwa katika idadi hiyo mawaziri ni 29 na manaibu waziri ni 21, na baraza hilo limezidi kuwa kubwa zaidi kuliko lile lililopita ambalo lilikuwa na mawaziri 47.

Ikumbukwe kuwa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alikuwa akilalamikia sana ukubwa wa baraza la mawaziri lililopita huku akianisha takwimu mbalimbali zilizoonyesha kuwa lilikuwa likiongeza gharama kubwa zisizo za lazima katika uendeshaji wa serikali.

Aidha, hoja hiyo ya Dk. Slaa ilikuwa ikiungwa mkono pia na wasomi, wanaharakati na watu wa kada mbalimbali huku wakisisitiza kuwa ni muhimu kuwa na serikali ndogo yenye tija na inayobana matumizi.

Kinyume cha kilio hicho cha wadau wa siasa na masuala ya kiutawala, tunasikitika kuona Rais Kikwete ameshindwa kuwa msikivu na kurudia kuunda baraza kubwa tena kuzidi hata lile la awali.

Tunajua kuwa hoja ya Rais Kikwete kuongeza wizara na mawaziri ni kurahisisha utendaji na ufanisi wa serikali yake kama alivyoeleza jana wakati anafafanua sababu za kuigawa wizara ya miundombinu kuwa wizara mbili za Ujenzi na Miundombinu.

Hata hivyo bado tunachelea kushawishiwa na hoja hizo za rais, kwani ukweli ni kwamba mawaziri si watendaji bali ni wanasiasa wanaofanya zaidi kazi ya kuratibu na kusimamia sera ambayo inaweza kufanywa na mawaziri wachache ili mradi kuwe na watendaji bora.

Kwa mantiki hiyo, tulitegemea badala ya Rais Kikwete kuongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, angefanya mabadiliko ya mfumo wa utendaji na watendaji wenyewe ili kuwarahisishia kazi mawaziri wachache na kuokoa fedha za walipa kodi kwa manufaa ya wananchi.

Kwa dosari hiyo kubwa, ni matumaini yetu kuwa wadau mbalimbali na taifa zima, kila mmoja kwa wakati wake na kwa nafasi yake ataendelea kutimiza wajibu wa kumsihi mkuu huyo wa nchi kupunguza ukubwa wa baraza lake. Bado tunaamini ni msikivu na ataitikia kilio hiki mbele ya safari.

Pamoja na dosari hiyo, bado tunawasihi Watanzania wote kuipa ushirikiano mzuri serikali hiyo mpya iliyotangazwa jana kwani ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi na tofauti zetu mbalimbali.

Hivyo basi, tunatoa rai kwa chombo kikuu cha kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali (Bunge) kuhakikisha kuwa linashauri, kuifuatilia na kuisimamia serikali hiyo mpya ili iwajibike vizuri na kwa uadilifu wa hali ya juu kwa masilahi ya vizazi vya leo na vya kesho vya taifa hili.

Tunahitimisha kwa kuwataka wananchi wa kawaida na vikundi shinikizi, zikiwamo asasi zisizo za kiserikali (NG’Os na CSO’s) pamoja na asasi za kidini kuunga mkono rai hii ya kuipa ushirikiano serikali yetu pamoja na kuisimamia.

source : tanzania daima

0 comments:

Post a Comment