Thursday, November 18, 2010

CHADEMA kumsusa Kikwete

Mbowe akataa kuzungumzia msimamo wao

na Mwandishi wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kinatarajiwa kutohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na uzinduzi wa Bunge la 10 utakaofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Sababu za CHADEMA kutohudhuria uzinduzi wa Bunge na kuapishwa kwa Pinda, kunatokana na msimamo wao walioutangaza wiki iliyopita kuwa hawamtambui kiongozi huyo kwa sababu matokeo yaliyompa ushindi yalichakachuliwa.

Habari ambazo zilizagaa maeneo mbalimbali mkoani hapa zilibainisha kuwa CHADEMA hawatohudhuria uzinduzi huo wa Bunge, ili kushibisha hoja yao ya kutomtambua Rais Kikwete ambaye alipata ushindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu.

Tanzania Daima, limedokezwa kuwa msimamo huo wa CHADEMA, unamaanisha kuwa chama hicho hakitahudhuria shughuli zozote ambazo Rais Kikwete atakuwa mgeni rasmi.

Msimamo kama huo uliwahi kutolewa na Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kiliwahi kutoyatambua matokeo yaliyowaingiza madarakani waliokuwa marais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour na Dk. Amani Abeid Karume.

CUF ilikataa kuhudhuria mikutano ya Baraza la Wawakilishi pamoja na ile ya Bunge sambamba na kutoshiriki kwenye shughuli mbalimbali za kitaifa zilizokuwa zikiongozwa na marais hao.

Tofauti na CUF, CHADEMA imetoa msimamo wa kutomtambua Rais Kikwete, lakini kimeweka wazi kuwa wawakilishi wake wataendelea kuwatumikia wananchi kulingana na sheria na Katiba za nchi.

Tanzania Daima, lilizungumza na msemaji wa kambi ya upinzani bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhusu tetesi hizo na kusema hayuko tayari kuzungumzia tetesi bali aliwataka wananchi wavute subira, ili waone kama watahudhuria au hawatohudhuria.

Alibainisha kuwa hawezi kuzuia mawazo ya watu au maneno yao, lakini ukweli utajulikana wakati ukifika kama wabunge wa CHADEMA wataingia bungeni wakati Rais Kikwete akilizindua na kulihutubia Bunge.

“Taarifa za CHADEMA kutohudhuria sherehe hizo umezipata wapi?....mimi naomba uvute subira ili kujua ukweli wa tetesi hizo, wanaozieneza wanajua walikozipata...muda utaamua,” alisema Mbowe.

Tanzania Daima, lilidokezwa na watu walio karibu na wabunge wa CHADEMA kuwa msimamo wao ni kutohudhuria sherehe hizo, kwani wakifanya hivyo ni sawa na kwenda kinyume na msimamo wao walioutoa mwanzoni mwa wiki hii wa kukataa kumtambua Rais Kikwete.

CHADEMA inadai kuwa Kikwete alipata madaraka kwa sababu ya uchakachuaji wa kura uliofanywa na Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kumuwezesha Kikwete kuibuka na ushindi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, leo asubuhi katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Chamwino, anatarajia kuapishwa kushika wadhifa huo baada ya kuidhinishwa na Bunge juzi.

0 comments:

Post a Comment