ZIKIWA zimebakia siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa ubunge katika majimbo ya Mpanda Mjini na Vijijini, mawakala 22 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wameshindwa kuapishwa, baada ya kukamatwa na polisi.
Mawakala hao wa mgombea wa Jimbo la Mpanda Kati (CHADEMA), Said Arfi walikamatwa jana majira ya saa 7 mchana katika Kijiji cha Kasulamemba, Wilaya ya Kigoma Vijijini, wakati wakisafiri kutoka mkoani Kigoma kwenda Mpanda mkoani Rukwa kuwahi zoezi la kuapishwa.
Polisi mkoani Kigoma waliamua kuwakamata mawakala hao kwa kile kinachodaiwa kuwa kulikuwa na taarifa kutoka Mpanda ambazo zilidai watu hao walikuwa wanakwenda kufanya fujo siku ya uchaguzi.
Akizungumzia kukamatwa kwa mawakala hao, mgombea ubunge wa Jimbo hilo la Mpanda Mjini (CHADEMA) Arfi, alisema mawakala hao walikuwa njiani kwa ajili ya kuwahi muda wa kuapishwa kwa vile jana ilikuwa siku ya mwisho.
Alisema kitendo cha kukamatwa mawakala wake kimemfanya apeleke majina mengine ya mawakala kwenye Tume ya Uchaguzi ili kuziba nafasi za waliokamatwa.
Alisema sababu zilizomfanya achukue mawakala kutoka Mkoa wa Kigoma ni taarifa alizokuwa nazo za kutaka kuhujumiwa kupitia kwa mawakala walioko wilayani Mpanda.
Jimbo la Mpanda Mjini, lina wagombea watatu, ambao ni Ndimubenya Ezekiel (CUF), Said Arfi (CHADEMA) na Sebastian Kapufi (CCM), lina jumla ya vituo 45.
Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumapili ya wiki hii, umekuwa na matukio mbalimbali yakiwamo ya wafuasi wa CCM na CHADEMA kupigana mara kwa mara.
0 comments:
Post a Comment