Monday, November 22, 2010

Dk Bana: Chadema wana hoja ya msingi

Sadick Mtulya
MKUU wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, amesema Chadema kina hoja ya msingi kushinikiza uundaji katiba mpya na kwamba, tatizo lipo njia wanayotumia.
Kauli ya Dk Bana inakuja ikiwa ni siku chache, baada ya wabunge wa Chadema kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia, kuashiria kuzindua rasmi.

Chadema ilifaya hivyo ikiwa ni hatua yao kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kushikiza uundaji wa katiba mpya, Nec na uundaji Tume ya uchunguzi wa yaliyoajiri uchaguzi mkuu uliopita.
Kufuatia kitendo hicho, wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi waliibuka na maoni tofauti.
Akizungumza katika kipindi cha ‘Tuongee Siasa’ kupitia Kituo cha Televisheni cha Star Tv jana, Dk Bana alisema madai ya chama hicho yana msingi.
“Madai ya Chadema ni ya msingi, lakini tatizo ni njia waliyotumia kutozingatia utamaduni wa Watanzania katika kudai haki,’’ alisema.

Dk Bana alisema Chadema imetumia njia hasi ambayo kimantiki itajenga tabia kwa wananchi wa kada tofauti kususia vikao au mikutano itakayokuwa inaitishwa na viongozi.
“Kama njia hii itakubalika katika jamii, itafikia hatua hata wanafunzi watatoka nje ya darasa wakati mwalimu akiwa anafundisha, kwa hoja kwamba hawamtaki jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Watanzania na hatari kwa mustakabali wa baadaye wa taifa,’’ alisema.

Kuhusu Katiba, alifafanua kwamba kulingana na mabadiliko ya wakati, Katiba ya sasa ambayo ilitungwa mwaka 1977, haikidhi haja na tija ya Watanzania inastahili kutungwa upya.

“Kulingana na wakati, inahitajika katiba mpya itakayokidhi haja na tija kwa Watanzania wote, Katiba ambayo itatoa fursa zaidi kwa wananchi kuweza kuwajibisha viongozi,” alisema na kuongeza:
“Itatoa fursa ya kujadiliwa zaidi kwa masuala ya muundo wa muungano, uteuzi wa mawaziri, uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi za serikali, uwepo wa tume huru ya uchaguzi, rais kupunguziwa madaraka na mambo mengine.’’

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amenukuliwa akisema uamuzi wao ulizingiatia demokrasia na kwamba, ulipeleka ujumbe mzito kwa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa ili kuibua mjadala wa kitaifa juu ya umuhimu wa masuala hayo matatu.

chanzo : gazeti mwananchi

0 comments:

Post a Comment