Salim Said
SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), limepongeza CCM na Chadema kwa kuteua wabunge wa viti maalum kutoka watu wenye ulemavu.
Wabunge walioteuliwa na CCM, ni Magreth Mkanga na Al-Shaimar Kwegiar, huku Chadema ikimteua Rejia Mtema kutoka Mkoa wa Morogoro.
“Pia, tunakishukuru CUF kilichopitisha baadhi ya wagombea ambao ni wenye ulemavu na kupelekea kuchaguliwa kwa Salum Bar’wan kuwa Mbunge wa Jimbo la Lindi mjini,” inasomeka sehemu ya taarifa yao.
Taarifa hiyo inasema, Shivyawata haina budi kuwapongeza wananchi wa jimbo hilo waliofanya maamuzi mazito, licha ya kauli potofu ya unyanyapaa na unyanyasaji iliyotolewa na mmoja wa wapambe wa chama kimojawapo cha siasa, dhidi ya mgombea huyo wakati wa kampeni.
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa tumewapoteza waliokuwa wabunge wenye ulemavu ambao hawakupita katika kura za maoni, akiwemo Mudhihiri Mudhihir na Bujiku Sakila,” inaongeza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa: “Tunawasihi wabunge wenye ulemavu ambao wameingia kwa mara ya kwanza Bungeni, kuwa mfano kwa kuwatetea wananchi na kutoa michango mizuri ya mawazo itakayoleta maendeleo kwa Watanzania wote wakiwemo watu wenye ulemavu.”
Inafafanua kuwa hali hiyo itadhihirisha kuwa ulemavu sio kikwazo iwapo kutakuwa na dhamira ya dhati ya kuwashirikisha wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
MWANANCHI GAZETI
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment