na Walter Mguluchuma, Mpanda
MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mpanda Mjini, Said Arfi, aliyekuwa akitetea kiti hicho, ameibuka mshindi.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka Mpanda jana usiku wakati tukienda mitamboni, zilisema Arfi aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,841 dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sebastian Kapusi, aliyepata kura 8,235.
Hata hivyo, matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa leo, baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpanda, Henry Haule, kushindwa kufanya hivyo jana usiku kwa sababu za kiusalama.
“Ni kweli zoezi la kuhesabu kura limefanyika mara tatu, kwa kila mgombea kujiridhisha kutokana na mchuano kuwa mkali… msimamizi alihofia kutangaza matokeo usiku kutokana na hali ya usalama wa hapa,” alisema mmoja wa maofisa wa CHADEMA.
Alisema licha ya jana kutwa nzima polisi wenye silaha na mabomu ya machozi kuzunguka maeneo ya mji huo kuimarisha ulinzi, hali bado ilikuwa inaonekana kuwa tete.
Wakati huo huo, kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa ni kikundi cha ulinzi (Green Guards) cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanadaiwa kumvamia nyumbani kwake, Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Stella Malaki, kwa kile walichodai kuwa hawakuridhishwa wala kufurahishwa na uteuzi uliompa nafasi hiyo na kumtishia kifo.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa, Malaki alisema kamwe hatishiki wala kutetereka, kwa kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge, ambaye yuko tayari kufa akitetea msimamo wake.
“Vitisho vyote hivi ni vya kisiasa, kwani wapo baaadhi ya wanasiasa wa chama kingine wamekasirishwa na mie kuteuliwa kuwa mbunge kupitia CHADEMA mkoani hapa… mie sitishiki na niko tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea wanyonge.
“Isitoshe lazima wafahamu mimi ni mzawa wa Wilaya ya Mpanda, nimesomea shule ya sekonadari mkoani Mbeya na niliamua kugombea nafasi hii ambayo ni haki yangu kikatiba, ili ni watetee wanyonge… sasa chuki ya nini?” alihoji Malaki.
Alisema mkasa huo ulitokea juzi majira ya saa 4 usiku, ambapo yeye na mumewe aliyemtambulisha kwa jina la John Malaki, wakiwa pamoja na watoto wao wawili Happiness Bayone (30) na Emmanuel Malaki (20), ambaye alikuwa akiendesha gari la familia aina ya Chaser lenye namba za usajili T 983 AGP, wakitokea Hospitali ya Wilaya ya Mpanda na kuelekea kwao Mtaa wa Nsemulwa mjini hapa.
“Mie tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, mwaka huu, nilikuwa napata matibabu…hata wakati nilipotangazwa kuwa ni mbunge mteule kupitia CHADEMA nilikuwa nimelazwa … hivyo usiku wa jana nilikuwa natokea hospitali ya wilaya nachomwa sindano za masaa, nikashtukia navamiwa na kundi la vijana.
“Kwa kuwa leo (jana) nasafiri kwenda Dodoma kuapishwa, niliona ni busara kupitia usiku ule nyumbani kwa mgombea wa Jimbo la Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA), ili niweze kuagana naye na kumuelezea mkasa mzima,” alisema Malaki.
Alidai baada ya kuagana na Arfi, walipita Mtaa wa Kawajense wakielekea nyumbani kwao ndipo walifika mbele ya baa iitwayo ‘ Seven Hills’, walisikia sauti za miluzi na kuwaona vijana wakiwa wamevaa miwani mieusi na makoti marefu wakirukia gari lake bila kuelewa sababu ni nini.
Alisema yeye na familia yake walidhani gari lililokuwa likiwafuata nyuma kwa kasi ni la polisi wa doria, lakini walisitaajabu walipoingia nyumbani kwao na gari hilo nalo liliingia.
Alisema ghafla walishuka, aliodai walinzi wa CCM maarufu kama ‘Green Guards’, ambao walikuwa na mapanga na visu, huku mmoja wao akisikika akisema anzisha, kabla ya kuzingirwa, na kuambiwa uteuzi wake haukuwafurahisha.
“Ndipo watoto wangu waliponiomba kwa usalama wangu niingie ndani, lakini niliwakatalia nikawambia kuwa hapa ni nyumbani, nikakataa kuingia ndani kwa kuwa nilikuwa tayari kufa hadi nione nini vijana hao walikuwa wakitaka kutoka kwangu.
“Niliwaambia vijana hao kuwa pamoja na kwamba mimi ni mwanamke, siwaogopi na kama kweli wamedhamiria kuniua basi wafanye hivyo mbele ya famila yangu, msimamo wangu uliwapumbaza na kuamua kuondoka,” alisema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, alipoulizwa, alisema polisi wanafanya uchunguzi wa tukio hilo, ili kubaini vijana hao walitumwa na nani ili waweze kukamatwa.
WE HAVE MOVED TO/TUMEHAMIA WWW.UDADISI.COM
3 years ago
0 comments:
Post a Comment