Sunday, November 14, 2010

Viongozi wenye kashfa wajiuzulu

Mhariri,
NI ombi kwa wanasiasa kwamba katika maisha yao ni vizuri wakawa na kawaida ya kuachana na madaraka hasa pale wanapokuwa na kashfa kwani kujiuzuru kwao kunaweza kusaidia kuwaimarisha kisiasa kuliko kung’ang’ania kama ambavyo wengi wanafanya.

Kwa mfano sijafurahishwa kabisa na namna ambavyo Andrew Chenge alivyomtupia maneno aliyekuwa spika, Samuel Sitta kwamba ameharibu bunge na vitu kama hivi.

Ikiwa kama yeye alilenga kugombea nafasi ya uspika hakuwa na sababu ya kumnenea mabaya Sitta, kwani kati ya yeye na Sitta, ni nani ambaye katika jamii anaonekana wazi kulalamikiwa zaidi na jamii.

Sisi wananchi sio wajinga, mbunge huyu anakabiliwa na kesi mauaji ambayo bado haijatolewa hukumu. Kwanini CCM wasingeacha kwanza mahakama ikamwachia huru na ndipo aruhusiwe kugombea ubunge? Je haki iko wapi mtu ambaye analalamikiwa au ana kesi kama hivi, anamtangaza mwingine kwamba ni mbaya na hafai kuliongoza tena bunge.

Amegombea wananchi tumekaa kimya, haya kapita anaanza kuleta malumbano na wengine ambao hata hawakuwa na matatizo, kisa alimhukumu na kutomtetea alipohusishwa na ufisadi.

Wananchi tulichokisoma hapa ni tatizo la kuwa na ugomvi wao wawili na ugomvi huo ameupeleka katika maslahi ya nchi, hili ni kosa kubwa. Ndio maana wananchi sasa wanafahamu kuwa sheria, miiko na taratibu za kazi/uongozi zipo kwa ajili ya makapuku tu.

Lakini si kwa viongozi wateule. Kwani kosa la kuua iwe kwa bahati mbaya au vinginevyo si swala dogo la kulichukulia juujuu, kana kwamba ni kesi ya wizi wa kuku wa jirani.

Viongozi wenye mamlaka ya kusimamia maadili ya ki utu ya kawaida, wanapo shindwa au kufumbia macho kutoa maamuzi ya kusimamia utawala bora, basi ujue hao viongozi ni kinyume ya viongozi waadilifu, waung wana, wastaarabu .

kwani hawa watakuwa wamejaa kiburi, umimi, uzandiki, unafiki na ni vigumu kufanya kitendo cha kistaarabu kama kujiuzulu. Au kutoshiriki katika uongozi kwani tayari miiko, maadili anayotakiwa kuwa nayo kiongozi hawanayo tena.

Masanja,
Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment