Wednesday, November 17, 2010

Barua kwa Rais Kikwete - Wagombea Binafsi

31 Mei 2006

Barua kwa Rais Kikwete - Wagombea Binafsi

MAAMUZI YA MAHAKAMA KUHUSU WAGOMBEA BINAFSI NA UMUHIMU WA KUBADILI MFUMO WETU WA UCHAGUZI

Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ikulu,
Dar es Salaam.


Ndugu Rais,

Kwanza naomba nikupe pongezi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Kiongozi wa nchi yetu. Inawezekana kuwa tayari nimeshakupa hongera tulipokutana pale Dodoma siku uliyomwapisha Waziri Mkuu Ndg. Edward Lowassa au vile vile tayari umekwisha pongezwa na Mwenyekiti wangu wa chama cha CHADEMA ndg. Freeman Mbowe pale Diamond Jubilee. Hata hivyo, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuwasiliana na wewe kama Rais kwa barua, nimeona ni bora nikupe hongera zangu tena.

Vile vile nikutie moyo kwa kazi unayofanya. Umeanza kazi kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya ili kuleta Mabadiliko ya kweli na Uhuru wa kweli kwa jamii ya Watanzania.

Kwamba timu yako nzima ya uongozi inafanya kama wewe ni suala la mjadala mwingine. Sina shaka hata kidogo kuwa Waziri Mkuu na Spika wa Bunge letu tukufu wanaendana na ari yako. Ninaamini watakusaidia vya kutosha. Nina imani kubwa sana na viongozi hawa licha ya changamoto kadhaa ambazo ninaamini ni matatizo ya kimfumo (systematic inherent problems) tu ambayo hata sisi tungefanikiwa kupata ridhaa ya Watanzania na kuongoza taifa letu tungekutana na changamoto hizo. Nikisema sisi, ndugu Rais, nina maana CHADEMA.

Ndugu Rais, barua hii ni yangu binafsi kama kijana mwenye kulipenda taifa langu na bara langu la Afrika. Kwa kuwa nina ofisi ya kitaifa, kama Mbunge, nakuomba uchukulie barua hii kama inatoka kwa Mbunge kwenda Rais wa nchi ambae ni sehemu ya pili ya Bunge.

Barua hii ina mawazo ya kujaribu kusaidia kutokana na changamoto iliyopo mbele yetu kufuatia hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu kuruhusu wagombea binafsi wa uongozi wa nchi yetu. Wagombea binafsi maana yake ni wagombea wasio na vyama vya siasa. Wanaweza kuwa ni wanachama wa vyama, lakini hawana dhamana ya vyama vyao wanapogombea na kisha kuchaguliwa kuwa viongozi.

Ndugu Rais, kuwa na mgombea binafsi haina maana kuwa mgombea huyu hatakuwa na udhamini wa aina fulani. Mfano, Kikundi cha Wafanya biashara wa zao fulani (mfano Tumbaku kule Urambo) wanaweza kudhamini watu kadhaa, wakagombea udiwani, wakashika “majority” ya Halmashauri ya Wilaya. Maana yake ni kuwa maamuzi yote ya Halmashauri ya Wilaya Urambo yatakuwa chini ya kundi hili. Hii inawezekana. Inawezekana pia hata kwa ngazi ya Ubunge. Sina uhakika katika ngazi ya Urais. Lakini sina haja ya kukuhadithia alichofanya Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi.

Ndugu Rais, Vyama vya siasa vimewekewa masharti ya kuandikishwa. Kuna sheria inayopelekea vyama kusajiliwa na kuna ofisi ya Msajili wa vyama anaeratibu vyama vyote ikiwemo chama chako, CCM. Hata kama mmoja wa wajumbe wa secretariat ya chama chako alinukuliwa akisema Msajili wa vyama ni karani tu, lakini ofisi hii ina majukumu makubwa sana ya kuhakikisha taifa halimeguki kisiasa. Ingawa nina mawazo tofauti, kwamba ofisi hii ingeweza kuwekwa chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya muundo wa sasa. Lakini hii sio hoja kwa sasa.

Kiufupi ni kwamba vyama vinaratibiwa. Katiba zao na hata kanuni zao za uteuzi wa wagombea wa nafasi zote zipo kwa Msajili. Msajili aweza kufuatilia kuona kama chama kinafuata taratibu zake na anao uwezo wa kuonya.

Ndugu Rais, nchi haiwezi kuwa na ofisi ya kuratibu wagombea binafsi. Nidhamu yao Bungeni na hata katika Mabaraza ya madiwani haitaweza kushughulikiwa na vyama. Hawa hawana vyama!

Ndugu Rais, sio nia yangu hata kidogo kushauri kuwa tusiruhusu wagombea binafsi. Hii itakuwa ni kuzuia uhuru wa Mtanzania kushiriki katika uongozi wa nchi. Mahakama imesema ni kinyume na Katiba. Katiba ambayo sote tumeapa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea. Kiapo tulichokula ni kikubwa sana na lazima tuheshimu kiapo. Hata hivyo, suala hili ni lazima tuliangalie kwa mapana yake.

Mara baada ya mahakama kutoa hukumu nilinukuliwa na magazeti ya hapa nyumbani na moja na Ghuba (Gulf Times) na lingine na Marekani (The Herald Tribune). Nilisema kuwa maamuzi ya mahakama yanatutaka tufanye mabadiliko makubwa ya mfumo wetu wa siasa. Maamuzi ya mahakama yanaweza kuudhoofisha mfumo wa vyama nchini kwetu.

Uzoefu wangu unaonesha kuwa Watanzania hawapendi vyama. Sio manazi wa vyama vya siasa. Hawaoni kama vyama vinawawakilisha. Wanaona vyama kama vikundi tu vya watu wenye madhumuni ya kutawala. Hawaoni vyama kama Asasi muhimu za kujenga demokrasia na kutoa sera mbadala. Ndio maana kati ya Watanzania milioni 16 waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2005, ni Watanzania milioni tano tu ndio wanachama wa vyama. Hata wewe ndugu Rais, umechaguliwa na Watanzania milioni 9 wakati chama chako kina wanachama milioni tatu tu!

Kwa hali hii ya udhoofu wa vyama kutokukonga nyoyo za Watanzania, wagombea binafsi wanaweza kuvuruga kabisa mfumo wa vyama. Hii ni hatari ninayoiona. Ni hatari kweli kweli. Ni hatari kwa sababu, nchi inaweza kukatika kwa matamshi tu ya mtu ambae hana chombo cha kumdhibiti. Vyama vinadhibiti wanachama wake.

Ndugu Rais, mimi binafsi nina maoni yafuatayo ili kuimarisha Demokrasia katika nchi yetu kufuatia hukumu ya mahakama kuu. Mapendekezo yangu haya yanaweza kuwa sehemu ya mjadala wa kitaifa uliouahidi wakati ulipolihutubia Bunge mwishoni mwa Disemba 2005.

* Serikali ikubaliane na maamuzi ya Mahakama:

Mabadiliko ya Katiba yapelekwe Bungeni na kuondoa vizuizi vya Watanzania kugombea uongozi kwa kudhaminiwa na vyama. Sheria ya Uchaguzi ifanyiwe marekebisho na kuweka masharti kadhaa ya kufuata kwa mgombea binafsi. Mfano, mgombea mtarajiwa kupata wadhamini 50 kutoka kila kata iliyopo katika Jimbo, kama anagombea Ubunge na wadhamini 20 kutoka kila Mtaa/Kijiji katika Kata kama anagombea Udiwani. Kama anagombea Urais, apate wadhamini 1000 kutoka kila Mkoa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

* Mfumo wa Uchaguzi urekebishwe na kuruhusu mfumo mchanyato wa uwiano wa kura na mfumo wa “first-past-the-post”:

Ndugu Rais, mfumo wetu wa uchaguzi unataka Wabunge na Madiwani kupatikana kutoka katika majimbo na kata tu. Wabunge wanawake hupatikana kwa uwiano wa kura za Wabunge nchi nzima na Madiwani wa wanawake kutokana na uwiano wa viti vya udiwani ambao kila chama kimepata.

Lakini Wabunge Wanawake hawana mamlaka ya kisheria kwa eneo maalumu. Kwa sasa ni rahisi kusema kuwa wanatoka mikoani, lakini hii ni kwa sababu tuna chama kimoja kikubwa na hivyo kupata kura za kuenea mikoa yote. Huko mbele, tena na hawa wagombea binafsi, itatokea mikoa ambayo haitapata wabunge wanawake kwa sababu kura hazitotosha kwa chama kimoja kugawa wabunge kila mkoa. Umefikia wakati sasa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi ili kuingiza uwakilishi wa uwiano.

Napendekeza kama nchi tutafakari mambo yafuatayo yanayohusu mabadiliko ya mfumo wa kisiasa wa nchi yetu:

1. Wabunge wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi watokane na Halmashauri za Wilaya za sasa. Mfano, badala ya Wilaya ya Manispaa ya Kinondoni kuwa na Wabunge watatu, iwe na Mbunge mmoja tu. Halmashauri ya Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji ndio iwe Jimbo la Uchaguzi. Katika ngazi hii wagombea wasio na vyama waruhusiwe pamoja na wale wenye vyama.

Kwa hali ya sasa tutapata Wabunge 119 kutoka kundi hili. Idadi yao itaongezeka kutokana na kuongezeka kwa Halmashauri zitakazoundwa pindi mahitaji yanapotokea. Haitakuwa tena kazi ya Tume za Uchaguzi kuunda Majimbo ya uchaguzi bali vile vigezo vya kuunda Halmashauri (Baraza la Madiwani) vilivyopo kisheria (Local Government Authorities Acts) ndio vitatumika.

2. Wabunge 231 watokane na kura za uwiano. Vyama vya siasa vitapata viti kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama kimepata katika Mkoa. Chama cha siasa ni lazima kiwe kimepata kwanza asilimia tano ya kura zote zilizopigwa katika Mkoa husika ili kigawiwe viti. Kwa hiyo kila chama kitatengeneza orodha ya wagombea wake kwa kila Mkoa na kuipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Orodha hii iwe katika hali ambayo kama jina la kwanza ni Mwanaume la pili awe Mwanamke, hali kadhalika kama jina la kwanza ni Mwanamke katika orodha la pili liwe la mwanaume. Mikoa itapata idadi ya Wabunge kutokana na vigezo maalumu, mfano idadi ya watu n.k. Jambo la kuzingatia tu ni kwamba idadi ya sasa ya Wabunge katika mikoa isishuke baada ya mabadiliko haya (no region shall be left worse off).

Mfano Mkoa wa Kigoma una Jumla ya Wabunge saba wa Majimbo. Iwapo tukibadili mfumo kama ninavyopendekeza hapa, kutakuwa na wabunge wanne wa kuchaguliwa, kutoka Halmashauri za Wilaya Kasulu, Kibondo na Kigoma na Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji. Hivyo wabunge watatu watagawiwa kwa vyama kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama kitapata.

Kwa mapendekezo haya tuna uhakika wa kuwa na Wabunge wanawake zaidi ya theluthi moja katika Bunge. Lakini pia tutakuwa na uhakika kwamba kila Mkoa utakuwa na Mbunge au Wabunge wanawake.


Ndugu Rais, mabadiliko haya ya mfumo wetu wa Uchaguzi yana faida nyingi sana. Moja ya faida ni kuvigeuza vyama vyetu vya siasa kutoka katika kushindanisha watu tu, bali pia kushindanisha sera. Kwa sababu wananchi watakuwa wanapiga kura mbili. Kura moja ya chama na kura nyingine ya ama diwani au Mbunge na Rais. Kura ya chama ndio itatufanya kupata wabunge wa uwiano. Wala hatutatumia mfumo mmoja kuzalisha mfumo mwingine. Bali kila mfumo utazalisha Wabunge kuunda Bunge letu.

Vyama vikianza kushindanisha sera tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana kama nchi katika kuimarisha mfumo wa demokrasia na kwa kweli hatutokuwa na wasiwasi wa vyama kudhoofika kutokana na wagombea Binafsi kuruhusiwa.

Demokrasia ndani ya vyama itaimarika kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha vyama vinapata wawakilishi wake katika Orodha ya Mikoa kidemokrasia. Pia pale Bungeni uliahidi kutengenezwa kwa “code of conduct” ambazo zitakuwa binding kwa kila chama ili kuimarisha demokrasia ndani ya vyama.

Ndugu Rais, najua una majukumu mengi ya Kitaifa. Sitaki nikuchoshe na barua yangu hii.

Hata hivyo, sisi hatutokuwa wa kwanza kufuata mfumo huu wa uwiano. Ndugu zetu wa Msumbiji wanafanya hivi. Pia Afrika ya Kusini, Ujerumani, Uswidi na hata India.

Mfumo huu, pia unaweza kumaliza matatizo ya kisiasa ya Zanzibar kwani kila kura itakuwa na thamani. Wawakilishi wa Zanzibar watatokana na kura za kila chama. Kura za Wapemba walio CCM na za Waunguja walio CUF zitahesabika. Hivyo, ile hali ya Pemba yote kutoa Wawakilishi au Wabunge wa CUF tu au Unguja yote kutoa Wawakilishi au Wabunge wa CCM tu itaondoka. Hali hii pia inaweza pelekea kupatikana kwa vyama vingine vyenye wawakilishi au Wabunge kutoka Zanzibar, kwani ushindani utakuwa ni wa sera za vyama na sio watu.

Ndugu Rais, naomba utafakari mawazo yangu haya. Ninaamini kuwa ni muhimu kufanya mabadiliko ya mfumo wa siasa. Kesi ya Mtikila sio sababu pekee ya mabadiliko, bali tunakokwenda hatuwezi kukwepa mabadiliko kwa faida ya demokrasia ya nchi yetu.

Kwa leo naomba niishie hapa. Nakutakia kila la kheri katika kazi.

Kwa ruhusa yako nina nakili barua hii kwa Spika wa Bunge letu Tukufu na pia kwa wasaidizi wako muhimu. Pia nina nakili barua hii kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala.

Wako mtiifu,

Zitto Z. Kabwe (Mb)
Kigoma Kaskazini.

Nakala:
Ndg. Samuel Sitta (Mb)
Spika wa Bunge.

Ndg. Edward Lowassa (Mb)
Waziri Mkuu.

Ndg. Kingunge Ngombale Mwiru (Mb)
Waziri (OR) Siasa na Uhusiano wa Jamii.

Ndg. Mary Nagu (Mb)
Waziri wa Katiba na Sheria.

Ndg. Willibrod P. Slaa (Mb)
Katibu Mkuu, CHADEMA.

0 comments:

Post a Comment