Wednesday, November 17, 2010

Unabii wa kuanguka kwa CCM utatimia hivi

19 Septemba 2007

Unabii wa kuanguka kwa CCM utatimia hivi
na
Samson Mwigamba

ITAKUWA ni mwishoni mwishoni mwa utawala wa rais wa awamu ya nne kutoka CCM. Utawala uliowapa matumaini makubwa hewa wananchi wa jamhuri hii.

Sauti zao wananchi zitapaza na kusikika kila pembe ya nchi hii kama sauti za matarumbeta yatakayopigwa na malaika watakaoambatana na Bwana Yesu wakati akirudi mara ya pili duniani kuchukua wateule, yatakavyosikika kila pembe ya dunia hata kuamsha waliolala makaburini kama inavyosimuliwa ndani ya Biblia takatifu. Wananchi watakumbuka jinsi “walivyouziwa mbuzi kwenye gunia”.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, CCM iliunda kamati iliyoongozwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wakati huo), Pius Chipanda Msekwa kwa ajili ya kupitia na kupendekeza utaratibu bora zaidi wa kupata wagombea wa chama hicho wa nafasi mbalimbali za serikali, ikiwamo urais.

Moja ya mapendekezo kadhaa ya kamati hiyo ilikuwa ni kwamba, mgombea urais kupitia CCM awe amepatikana kufikia Mei ya mwaka wa uchaguzi.

Bila shaka ni ili kujipa nafasi ya kutosha kumtambulisha mgombea wao kwa wananchi yasije yakawakumba yale ya mwaka 1995, ambako walipata tabu ya kumtambulisha mgombea asiyefahamika kwa kipindi kifupi hadi wakalazimika kumtumia Baba wa Taifa kuzunguka nchi nzima, akimnadi Benjamin Mkapa ambaye hadi leo wengi wanaamini kwamba wakati akipitishwa na chama kugombea urais, alikuwa hafahamiki kiasi cha baadhi ya watu kudhani aliyepitishwa alikuwa Kenneth Mkapa, mchezaji beki namba tatu wa timu ya Yanga wakati huo.

Hata kabla ya mwaka wa uchaguzi mkuu uliofuata, yaani 2005, pilikapilika zilikuwa zimeshaanza ndani ya chama hicho kikongwe Afrika. Kukawa na kupakana matope kwingi miongoni mwa wanachama walioonekana kuwa na nafasi na nia ya kugombea urais kupitia chama hicho.

Aghalabu kila aliyepakwa matope alisikika akisema “waliofanya hivyo ni kwa malengo ya 2005”. Ni katika wakati huu tulipoanza kuona kalamu ikitumika kwenye magazeti kuchafua baadhi ya watu na kusifia wengine. “Wenye akili” wakang’amua kuwa makusudi ya maandishi kama hayo yalikuwa ni mkakati.

Hatimaye 2005 ikawadia na muda wa kuchukua fomu za kugombea urais kupitia CCM ukawadia. Wanaume 11 waliokamilisha timu ya mpira wa miguu wakajitosa kuchukua fomu.

Wakati huu ndipo tuliposhuhudia kiwango cha juu cha kutumia magazeti kuchafuana. Katika hali ambayo binafsi sikuitarajia, mwandishi maarufu niliyemheshimu na kumpenda kwa makala zake, wa gazeti maarufu la Kiswahili ambalo nilikuwa silikosi kila Alhamisi, alitoa makala mfululizo za kumchambua kila mgombea aliyeomba kupitishwa na chama hicho kuutafuta urais.

Kama kujihami akatoa sababu ya kufanya hivyo tangu mwanzo kabisa wa makala zake, eti ilikuwa ni kwa sababu CCM ndicho chama tawala na hivyo kikipata mgombea mbovu taifa litaathirika.

Mwandishi huyo hakupima hata utetezi wake butu kwa sababu wakati huo kulikuwa na vyama vingine vipatavyo kumi na tano ambavyo vyote vilikuwa na nafasi ya kusimamisha wagombea urais.

Hivyo kama Watanzania wangeona CCM wamesimamisha mgombea mbovu, bila kujali sababu za kufanya hivyo, wangechagua mgombea wa chama kingine. Na hili ndilo lengo hasa la demokrasia ya vyama vingi.

Sasa mwandishi alijuaje kwamba lazima CCM ndiyo ishinde na nani alimwambia kwamba wajumbe wa vikao husika vya uteuzi ndani ya chama hicho hawana uwezo wa kumtambua na kumpitisha mgombea bora kati ya hao kumi na moja mpaka yeye awape wasifu wa kila mgombea?

Waandishi wa namna hii hawakuwa mmoja wala wawili, walikuwa ni wengi, tena ambao hatukuwatarajia. Jitihada zao zilizaa matunda pale ambapo mgombea wao ndiye hatimaye alipitishwa.

Siku ile alipopitishwa, hakuna atakayenibishia nikisema kwamba nchi ililipuka kwa kelele za shangwe na vifijo, maana shangwe haikuwa ndani ya Ukumbi wa Chimwaga pekee, bali kila kona nchi ilizizima, watu wakikokodolea macho kwenye TV.

Wakati Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Spika Msekwa akisimama kusoma matokeo, nilikatiza mtaa mmoja hapa Arusha na kuona watu wamerundikana kwenye pharmacy moja.

Niliposogea, ndipo nikaelewa kilichokuwa kinaendelea. Tukio hilo liliniachia mshangao na maswali mengi, hasa nikijiuliza Jakaya Kikwete alikuwa na umaarufu gani kiasi cha kushangiliwa vile kwa kuteuliwa kwake kugombea urais.

Ni kweli kwamba hakuwa hata na robo tatu ya umaarufu wa Augustine Mrema mwaka 1995. Hakukaribia hata umaarufu wa Pombe Magufuli, mjenga barabara ambaye alihifadhi kichwani mtandao wote wa barabara zilizo chini ya TANROADS nchi nzima ikiwa ni pamoja na makandarasi wanao/walio – zijenga, wafadhili wanao/walio – toa pesa na hatua zilizofikia.

Huwezi kulinganisha umaarufu wake na ule wa Dk. Salim Ahmed Salim, aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na aliyeukosa Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa tundu la sindano.

Kampeni zilipoanza ndipo nikaelewa kilichofanyika, ambacho sasa ni dhahiri kwa wananchi wote. Kwamba kulikuwa na mtandao uliojumuisha wafanyabiashara, waandishi wa habari, wasanii na watendaji wakuu wa chama na serikali, ulioanza kutengenezwa tangu mwaka 1995 kwa lengo la “kumkuza” na “kumtangaza” mteule wao, hata aonekane maarufu kuliko marais wengine waliopita, isipokuwa tu Mwalimu Nyerere, ambaye ndiye aliyekuwa analinganishwa naye. Kazi hiyo ilifanywa kwa ustadi hadi akaonekana ni “chaguo la Mungu” na wengi wakaaminishwa hivyo.

Utawala wa huyu mteule ulipoanza kwa ari, kasi na nguvu ya soda, kila mtu alikubali kwamba huyu ndiye rais. Hata wanasiasa wa kambi ya upinzani walionyesha kumkubali, hata baadhi yao kufikia kusema “anafanya kazi ya upinzani”.

Watu wakamkubali kwa maneno yake na kwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa mwanzoni mwa utawala wake. Kila kukicha kukawa na kauli mbalimbali kwenye magazeti kama; “Awamu ya nne spidi 120”, “Kasi ya Kikwete yamkumba kigogo”, “Sumaye aonja shubiri ya ari na kasi mpya”, “Lowassa hatari, asafiri Arusha – Dar – Arusha kwa siku moja, asimamisha mhandisi wa wilaya”, n.k.

Muda si muda, wananchi wakang’amua kwamba matendo hayo yote yalikuwa nguvu ya soda, walikuwa “wameuziwa mbuzi kwenye gunia”. Kumbe waliotabiri kwamba Kikwete alikuwa ni chaguo la Mungu na wale waliosema ni tumaini lililorejea, walikuwa ni manabii wa uongo. Ukweli ni kwamba alikuwa ni chaguo la wanamtandao na si tumaini lililorejea, bali ni kukata tamaa kulikorejea.

Safari za rais nje ya nchi zikatumbua zaidi ya sh bilioni 24 ndani ya mwaka mmoja wa fedha wakati nchi ikiwa gizani bila umeme, thamani ya shilingi yetu haikushuka bali iliporomoka, mfumuko wa bei ukaongezeka, akiba ya fedha za kigeni aliyoacha mzee Ben ikanywea, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikakatwa kwa asilimia 40 kinyume cha sheria iliyoanzisha mikopo hiyo, rushwa na ufisadi vikaongezeka, mikataba mibovu ikazidi kusainiwa huku watuhumiwa wakifichwa na kulindwa, kodi za mafuta zikapanda na kuongeza ugumu wa maisha huku mishahara ikiongezeka kiduchu.

Lakini katikati ya shida hizo za wananchi, ofisi ya waziri mkuu ikinunua gari mbili tu kwa shilingi milioni 400, posho za wabunge zikipanda hadi sh 100,000 kwa kikao kimoja tu cha siku moja, matumizi ya serikali yenye mawaziri na manaibu wao wapatao 60 zikazidi kuliliza taifa huku kazi wanayoifanya haionekani.

Ndipo kuelekea mwishoni mwa utawala huu, wananchi watapiga kelele. Baadhi ya vyombo vya habari vilivyoupigia debe utawala huu vitajiona viliwasaliti Watanzania. Vitaungana na vyombo vya habari makini kupiga kelele itakayosikika kila kona ya nchi kwamba uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli bado yanahitajika.

Wanafunzi wa vyuo na sekondari watapaza sauti, watumishi wa umma na binafsi watapiga kelele kila kona wakiambiana “hakuna njia ya kuleta mabadiliko nchi hii bila kuipiga chini CCM”.

Baada ya “chaguo la Mungu” kushindwa kuleta mabadiliko, sasa itakuwa ni dhahiri kwamba hata malaika ndiye awe rais wa Tanzania kupitia CCM kwa mfumo uliopo, hakuna mabadiliko yoyote.

Kule vijijini, walimu wa shule za msingi na sekondari watageuka na kuwa walimu wa wananchi wa vijijini wasio na uelewa mpana na mwamko wa mambo ya kisiasa. Watawaelewesha kuwa mabalozi wa nyumba kumi ni viongozi wa CCM tu, na hawana haki wala uwezo wa kuwatisha wananchi hata waichague CCM bila ridhaa yao.

Watawaelimisha kwamba Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani tena amani ya kweli (si ya uongo) bila CCM. Wala anguko la CCM halitaifanya nchi iwe na vita kama Rwanda na Burundi.

Watawaelimisha wananchi nao watayapuuza madai hayo ya kutungwa na CCM, wasiwe na wasiwasi maana chama cha upinzani kikishinda majeshi yote yataitii serikali mpya na kama CCM wana mpango wa kushika silaha na kuingia msituni watakamatwa hata kabla hawajafika ukumbi wa Chimwaga kupanga mipango hiyo.

Ni katika wakati huo ambako walimu hawa watawaonyesha wananchi kodi zote wanazolipa wanaponunua viberiti, chumvi, sukari, sabuni, n.k kutokana na vipesa wapatavyo kwa kutembea kilometa 30 kwa miguu isiyo hata na kandambili kwenda kuuza vitu kama kuni, ndizi, viazi, mbogamboga, n.k. watagundua kwamba kumbe kodi si tu ile waliyokuwa wanalipa ikiitwa ya maendeleo iliyofutwa.

Watatambua kuwa kumbe kuna kodi za moja kwa moja (Direct – taxes) na za mlango wa nyuma (Indirect taxes), ambazo ndizo zinaathiri sana maisha yao ya kila siku.

Watagundua kwamba kumbe wao ni watu wakubwa sana na wanaopaswa kuheshimiwa ndani ya nchi hii. Maana wao ndio waajiri wa serikali.

Ndio wanaowaajiri wabunge, rais na mawaziri wake. Watatambua kuwa wao walio vijijini ndio wanapaswa kuheshimiwa zaidi maana kwa wingi wao ndio wanashikilia cheo cha juu zaidi katika ofisi ya ajira ya wabunge na rais. Wao ndio hutia saini ya mwisho ya ajira ya vigogo baada ya kupata mapendekezo toka kwa wasaidizi wao (wananchi wa mijini).

Watasema sasa tunaitumia vema sahihi yetu, kwa kuheshimu mapendekezo ya wasaidizi wetu walio mijini, na ambao ndio huwafanyia usahili viongozi kwa kupima vitendo vyao, maisha yao ya ukwasi na umaskini wa Watanzania. Wataazimia kuinyima CCM kura.

Wakati huu ndipo vyama vya upinzani vitajiona vina deni. Wananchi watavilazimisha viunganishe nguvu zao na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais hata kama CCM haitakuwa imebadilisha sheria ya vyama vya siasa ili kuruhusu vyama kuungana.

CHADEMA, TLP, CUF, NCCR – Mageuzi, UDP na vyama vingine makini vitakaa pamoja na kumpitisha mgombea mmoja na mgombea mwenza wake wa urais. Kila jimbo la uchaguzi atakuwapo mgombea mmoja tu anayekubalika wa upinzani anayewakilisha vyama vitakavyokuwa vimesaini mkataba wa ushirikiano.

Kauli za hamasa kama “hakuna kulala mpaka kieleweke”, “haki sawa kwa wote”, “wananchi tujazwe mapesa”, “nguvu ya umma” nk, zitasikika kila mahali, wakati wa kampeni.

Viongozi wa upinzani watajigawa kila pembe ya nchi na kusambaa, huku wote wakimpigia debe mgombea mmoja tu wa urais na mgombea mmoja wa ubunge katika kila jimbo.

Tukumbuke kuwa kabla ya kampeni, vyama vilivyoamua kushirikiana vitakuwa vimekaa chini na kukubaliana juu ya sera murua za kuiongoza nchi yetu, zitakazotokana na muunganiko wa sera za vyama mbalimbali vya upinzani.

Kubwa likiwa ni kuunda katiba mpya baada ya uchaguzi na kubadili mfumo wa utawala wa nchi hii kubwa ili kuanzisha serikali za majimbo na kufuta kabisa cheo cha waziri mkuu, mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.

Naam, wakati wa kura utawadia. Kura zitapigwa na ingawa CCM itajitahidi kuiba kura kama kawaida yake, lakini bado zitakazobaki zitatosha kuupa upinzani ushindi mzito na kuuwezesha kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Mara tu baada ya rais kuapishwa atalihutubia Bunge na kutangaza mchakato wa kukusanya maoni ya kuunda katiba mpya kwa kutumia tume maalum itakayoongozwa na jaji maarufu kama Robert Kissanga.

Wakati mchakato huo ukiendelea, mali zilizohodhiwa na CCM wakati zikiwa ni za wananchi wote, kama viwanja vya mpira, zitarejeshwa serikalini. Wakati huo huo nyumba zote za serikali walizojiuzia vigogo zitarudishwa serikalini.

Mikataba mibovu ya madini, IPTL, Richmond, ATCLM, TTCL n.k itapitiwa upya sambamba na kuwafikisha mawaziri wote wa zamani kama kina Nazir Karamagi na watendaji wakuu mbele ya jopo maalum la majaji ili kujieleza kwa nini walisaini mikataba isiyo na masilahi kwa taifa.

Watumishi wote wa umma watalishwa yamini kuhakikisha hakuna hata shilingi moja ya serikali inayopotea kwa njia yoyote ile bila kunufaisha Watanzania wote.

Hata hivyo kima cha chini cha mshahara kitapanda hadi sh 275,000 bila kugusa kodi za vitu ‘sensitive’ kama mafuta, ili kuepuka mfumuko wa bei na hivyo ongezeko la mshahara kumnufaisha mfanyakazi wa kawaida. Hii itakuwa motisha kwa watumishi wa umma kuachana na rushwa na ubadhirifu.

Muda si muda serikali itakuwa na pesa nyingi, kwani TRA watakusanya si chini ya sh bilioni 300 kwa mwezi, utalii na maliasili zingine zitamwaga trilioni za shilingi ndani ya hazina kufuatia udhibiti wa maliasili zetu na kurekebisha mikataba mibovu ambayo hata hivyo itasitishwa kila inapofikia mwisho wa kipindi cha mkataba.

Pesa hizi zitatumika kutoa elimu bure hadi chuo kikuu, matibabu bure, kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo na ujenzi wa miundombinu kama barabara za lami, viwanja vya ndege vya kisasa, umeme wa uhakika na mawasiliano.

Katiba itakapokamilika na kuruhusu uanzishwaji wa serikali za majimbo, italeta ushindani baina ya majimbo huku kila jimbo kikiongozwa na viongozi wazawa ndani ya jimbo husika, wenye uchungu na maliasili zao na nia ya kuleta maendeleo majimboni mwao kwa msaada wa karibu wa serikali kuu.

Hii itaongeza kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi na hapo ndipo Tanzania itakuwa tayari KUPAA!!!

0 comments:

Post a Comment