Wednesday, November 17, 2010

Madonda ya uchaguzi yawe tiba 2015

Christopher Nyenyembe

BAADA ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika, Oktoba 31 mwaka huu huku kila sehemu matokeo yakitangazwa kwa muda na nyakati tofauti, kuliamsha furaha kwa wale walioshinda na kilio kwa walioshindwa.

Jambo la msingi ambalo linaweza kuwa fundisho kubwa sio kujua nani kashinda na nani kashindwa na kushinda au kushindwa hakumaanishi sana kuwepo kwa uzito wa kura haramu na halali isipokuwa matokeo yote yaliyopatikana yanahitaji utayari wa kujuuliza ni wapi kila mmoja alipokosea.

Kwa maana ya kuwa na ushindani wa nguvu kati ya chama tawala CCM na vyama vingine vya siasa kutoka kambi ya upinzani kulipimwa zaidi kwa uwezo wa wagombea kuliko picha waliyokuwa nayo wagombea wengi kuwa pesa zinaweza kuteka maamuzi ya watu.

Watu wamejionea jinsi ambavyo wagombea wenye pesa na mamlaka walivyoweza kuangushwa na pesa zao,wapiga kura wametumia haki yao ya kuchagua mtu waliyemtaka bila kujali pesa, umri, utajiri au umaarufu wa yule aliyedhani atapita kutokana na vigezo hivyo.

Kimsingi uchaguzi huu umeweza kutoa fundisho kubwa na la aina yake kwa wanasiasa, wapiga kura na watazamaji wa kimataifa kuwa nguvu za umma ni imara zaidi kuliko pesa, wapo waliotumia pesa nyingi wamejikuta wakimwagwa na wapo waliotumia pesa nyingi zikaliwa na watu wasiowajua.

Hayo naweza kuyaita kuwa ni madonda ya uchaguzi mkuu na ipo haja ya kutambua kuwa kitendo cha kutoa rushwa kwa wapiga kura ili wakupe kura na huo unakuwa ndio mwanzo wa kilio na kusaga meno kwa watu waliotumia pesa kwa ajili ya kupata madaraka.

Madonda ya uchaguzi mkuu hayatapona kama kila mtu aliyetumia pesa ili kuupatq, udiwani,ubunge au urais atakuwa amekosa nafasi hiyo kwa kigezo cha pesa au yule aliyeshinda naye ameshinda kwa ajili ya kutumia pesa, basi kwa njia hiyo wanapaswa kujua kuwa madonda hayo hayatapona hadi mwaka 2015.

Kutokupona kwa vidonda hivyo kwa namna yoyote ile pia kutasababishwa na namna kila mmoja alikoweza kuzipata fedha hizo, nikimaanisha kuwa wapo walioamua kwenda kukopa kwenye mabenki ili kupata fedha za kuwahonga wapiga kura.

Wapo wale walioamua kwenda kuazima kwa ndugu zao, kukopa kwa riba mitaani na wengine kudiriki hata kutumia fedha walizopewa na wahisani kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, zimetumika kwenye uchaguzi kwa ahadi ya kuzirudisha baada ya ushindi kupatikana.

Wale walioshinda wanajua watapata wapi fedha za kulipia madeni hayo na wale walioshindwa unakuwa ndio mwanzo wa kuwakimbia wadai wao, kuziacha familia zao na kujikuta hakuna mahali pa kukalika, kila sehemu moto, nyumbani moto, mitaani nako moto unawaka.

Lakini kuna jambo muhimu la kujiuliza kuwa ni ujasiri gani wanaoupata watu wanaotaka uongozi wa kufikiria kuwa fedha wanazozitoa zinaweza kuwafikia wapiga kura wote kwenye, kata, jambo au nchi, nadhani hayo tunaweza kuyaita kuwa ni mawazo ya kitoto.

Mtindo huo umeweza kuibua kundi mbaya na la hatari katika uwanja mzima wa demokrasia, hawa madalali wa siasa, wapiga debe au tunaweza kuwaita kuwa wapambe wa wagombea wanajinufaisha kwa kupewa fedha nyingi ili ziweze kuwafikia wapiga kura.

Ukweli ni kwamba fedha hizo haziwafikii walengwa na kama zinafika huko ni tofauti kabisa na matarajio ya mtu aliyewapa fedha hizo kwa ajili ya kuwahoga wapiga kura ambao kadri elimu ya uraia inavyozidi kukua watu wengi sasa hawahongeki.

Madhara ya kufanya biashara bila utafiti ndio hayo na kwa ujumla wake watu wamejionea namna wapendwa wao walivyoweza kubwagwa vibaya pamoja na ujasiri wao wa kutumia pesa bila kukamatwa na TAKUKURU, wamehukumiwa na wananchi.

Mtindo huo wa kuupata uongozi kwa kutegemea pesa unaweza kuwa ukoma wa kisiasa unaowatafuna watu bila kujua faida ya baadaye kuwa kigezo cha kuwa na kiongozi bora sio pesa isipokuwa ni sifa za mtu.

Hata kama kiongozi fulani atafanikiwa kuingia madarakani kwa ajili ya pesa hawezi kupona madonda na huyo anaweza kuwa na maumivu zaidi kwa sababu hana mashiko ya uongozi kutoka moyoni.

Kiongozi wa aina hiyo ni yule mwenye kinyongo, kisasi, hasira na mnyanyasaji akiamini kuwa uongozi alioupata haukuja kwa nguvu za wananchi isipokuwa umetokana na fedha zake nyingi alizozimwaga kila sehemu.

Najua fika kuwa baada ya watu kushinda na wengine kushindwa huu sasa unapaswa kuwa mwanzo wa kutibu vidonda vya ufisadi, kujitakasa na kuamini kuwa pesa ni sehemu ndogo sana ya mafanikio ya mtu katika uongozi wake.

Kujua kuwa fedha zikitumiwa kama silaha ya kuupata uongozi haziwezi kuleta tija kwa wananchi kwa kuwa hata wao hukosa mashiko na upendo kwa kiongozi wa aina hiyo wakijua wazi kuwa hawakumchagua, isipokuwa alijichagua kwa fedha zake.

Kiongozi aliyejiweka madarakani kwa fedha zake, akaweza kuwanunua wapiga kura masikini au akafanya kila njama na hila ya kuwa mgombea aliyepita bila kupingwa huo ndio mwanzo wa kuua demokrasia.

Naamini kabisa kuwa kiongozi anaweza kupita bila kupingwa kwa kukosa mshindani wake lakini hana sifa za kupita bila kupingwa kwa wapiga kura 100,000 waliopo kwenye jimbo lake, ipo haja kiongozi akapimwa na wananchi wenyewe na sio wagombea wenzake.

Hayo yote yanaweza kuwa madonda ambayo tiba yake lazima ipatiwe ufumbuzi kabla ya mwaka 2015 nikiamini kila mmoja atakuwa amejifunza na kushuhudia namna uchaguzi ulivyofanyika mwaka huu.

Kuteteleka kwa nguvu za CCM katika uchaguzi huu na kuruhusu kupoteza majimbo mengi kisiwe kigezo cha upinzani kubweteka, kazi ndio imeanza na ni wazi kuwa CCM nao watajipanga upya kutibu madonda waliyoyapata.

Ili madonda hayo yaweze kutibiwa jibu ni moja tu sasa wananchi wanataka kuona ahadi zilizoahidiwa zinaanza kutekelezwa mara moja bila visingizio wala sababu za kupanda au kushuka kwa thamani ya shilingi.

Wananchi wanataka kuona meli mpya ikielea Ziwa Nyasa, wanataka kuona mv Bukoba mpya ikizaliwa, wanataka kuona mv Liemba mpya ikipiga nanga katika Ziwa Tanganyika na kuwa na babaraba ya juu inayovuka kwenda Kigamboni.

Wanataka kuona viwanja vya ndege vya kisasa vikijengwa kwenye nchi isiyokuwa na shirika makini la ndege, kuwa na barabara zisizokwenda kwenye maeneo ya uzalishaji na wanataka kuona hospitali zikipandishwa hadhi bila ya kuwepo kwa madaktari na wauguzi wa kutosha.

Lengo la wananchi sasa ni kuziona ahadi hizo zinatekelezwa, zitekelezwe bila kujali kuwa maeneo hayo walioshinda ni wapinzani kwa kuwa Rais aliyeshinda alipita kila sehemu akiahidi bila kujua kama chama chake kuna maeneo kitaangushwa.

Kwa kuwa ahadi nyingi zimeahidiwa na rais aliyeshinda, akumbuke kuwa sio rais wa CCM isipokuwa Watanzania wanaye rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeapa kulitumikia taifa hili na kiapo chake ndio ndoa aliyoifunga na Watanzania wote bila kujali itikadi zao kwa miaka mitano.

Najua madonda ya uchaguzi yamemgusa kila mtu na huo uwe mwanzo wa kujipima, kujirekebisha na kuamua sasa kuwatumikia wananchi bila kinyongo, vinginevyo madonda hayo hayatatibika na tiba yake sio rushwa ni nguvu ya umma.

0 comments:

Post a Comment