Saturday, November 20, 2010

Chadema 'yaitikisa' nchi :NI KUTOKANA NA WABUNGE WAKE KUSUSIA HOTUBA YA JK

source : mwananchi

Na Waandishi Wetu

HATUA ya wabunge wa Chadema kutoka nje ya ukumbi wa bunge mjini Dodoma wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia, imetikisa nchi kutokana na wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi kuibuka na maoni tofauti.

Chadema wametangaza kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wakidai kuwa kulikuwa na kasoro nyingi kwenye zoezi zima la uchaguzi na kwamba Tume ya Uchaguzi (Nec) ilikuwa imelenga kumbeba mgombea urais kutoka chama tawala.

Chadema, ambayo safari hii imeingiza watu wengi bungeni, imeamua kutumia njia hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais kushinikiza kuundwa kwa katiba mpya kutokana na katiba ya sasa kutotoa haki ya kupinga matokeo ya urais na inataka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Katika mahojiano ambayo Mwananchi iliyafanya jana katika mikoa tofauti nchini lilibaini kuwa wapo wanaoona kitendo hicho kilikuwa halali wakieleza uamuzi huo unaweka bayana msimamo wao wa kutokubaliana na mfumo uliomweka madarakani Rais Jakaya Kikwete , huku wengine wakikosoa kwa kusema kwamba hawakustahili kufanya hivyo mbele ya rais, wakitafsiri kuwa huenda hizo ni chokochoko za kuvuruga amani na utulivu nchini.

Wasomi, wanazuoni wanaounga mkono
Mhadhri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abdallah Safari alisema kitendo hicho nio cha ni aibu kwa serikali ya Kikwete na Nec na kutaka kitafsiriwe kuwa ni kiashirio cha udhaifu katika uchaguzi na mahitaji ya tume hiyo.

“Ni silaha ya haki kwa kila mwanasiasa, ndio maana hata katika historia wabunge waliokuwa kwenye mabunge aliyokuwa akihutubia Fidel Kastro walikuwa wakitoka nje. La kujitakia halina majuto,” alisema Profesa Safari.

Mhadhiri mwingine katika Chuo hicho, Dk Azaveli Lwaitama alisema kitendo cha Chadema cha kawaida kwa kuwa siasa huambatana na suala la kisheria na hisia.

“Wao wamesema kuwa hawamtambua, lakini tayari rais wetu ameshaapishwa, hivyo kinachowafanya waseme hivyo ni hisia tu. Wanataka kuwaonyesha Watanzania kuwa hawakubaliani na matokeo ya urais, lakini kisheria hawawezi kufanya lolote kwa kuwa sheria inawabana,” alisema Dk Lwaitama.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Kilimanjaro ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema hakuna kosa lolote kwa wabunge kutumia njia hiyo kuonyesha dhamira yao ya kutokubaliana na matokeo ya Urais kwa kuwa hawana njia nyingine.

“Ibara ya 41 Ibara ndogo ya 7 ya katiba yetu inakataza matokeo ya urais kuchunguzwa baada ya kutangazwa na Nec… sasa kama umemfunga mshindani wako mikono, afanyeje kukuonyesha hakubaliani nawe,” alihoji.

"Katika hali ya kawaida ni jambo lisilowezekana kukubali goli ambalo unaamini limefungwa kwa mkono na kwamba hakuna mfumo unaomlazimisha mtu kumsikiliza Rais.”

Alisema haiwezekani Tanzania kujisifu kwa maendeleo ya kidemokrasia wakati katiba inazuia watu kuhoji uhalali wa matokeo ya urais, lakini katiba hiyo inaruhusu watu kuhoji uhalali wa matokeo ya wabunge na madiwani.

“Senegal kuna mahakama ya katiba ambayo inataka baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais kutangazwa, ni lazima yathibitishwe na Mahakama ya Kikatiba… kunakuwepo kipindi maalumu cha kushughulikia malalamiko kabla ya Rais kuapishwa,” alisema.

Harod Tairo, mhadhiri wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kitendo cha Chadema hakikumfurahisha kwa sababu kilijenga taswira ya mgawanyiko na machafuko bungeni.

“Mimi nashauri CCM wakae chini na Chadema wazungumze tatizo lilikuwa wapi ili kuziba mianya itakayoweza kuleta machafuko kama yaliyotokea Zanzibar,” alisema Tairo na kuongeza kuwa kama serikali inataka kukuza demokrasia, ni lazima ikubali msimamo na kitendo kilichofanywa na Chadema.

Naye mhitimu wa shahada ya sheria wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa, Clement Kihoko alisema kitendo hicho ni kabisa japokuwa wanaweza kueleweka tofauti.

“Ni utaalamu wa kifalsafa na ni mambo ya kuangalia kwa umakini zaidi kwa sababu kama walivyosema awali kwamba hawamtambui Kikwete kama rais ,wangebaki kumsikiliza bungeni wangeonyesha kumuunga mkono na kumkubali,” alisema Kihoko.

Kihoko alibainisha kuwa katika tafsiri ya kifalsafa na hata falsafa ya sheria, kitendo walichokifanya chadema ni sahihi kabisa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), Ali Nassor alisema kitendo cha Chadema ni kuwaonyesha wananchi kwamba wako makini na wanatambua jukumu walilokabidhiwa na wananchi bungeni.
“Kwa kitendo hiki Chadema wanajiweka hadharani ili kupata wanachama wengi,” alisema Nassor.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Dk Fairles Ilomo alielezea Chadema kuwa ni wapigania makabadiliko wachache waliojitoa kuwambwa msalabani kwa manufaa ya wananchi wengi.

Hata hivyo Dk Ilomo hakuunga mkono njia waliyotumia kupigania mabadiliko kwa kusema kuwa hawakupaswa kususia hotuba ya rais bali walipaswa kuwa wavumilivu na kutumia Bunge kufanya mabadiliko.

“Ni kitendo kilichoonyesha ujasiri kwa sababu kukiwa na viongozi ambao ni waoga watupu itachukua muda mrefu kufanya mabadiliko,” alisema Dk ILomo.

“Hayati Baba wa taifa Julias Nyerere alipoanza kupigania uhuru wakoloni walisema ni mvurugaji wa amani na kumweka rumande kwa saa kadhaa, lakini sasa tunafaidi matunda ya uhuru aliopigania. Vivyo hivyo wananchi watakuja kufaidi matunda ya mgomo Chadema."

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walisema kitendo cha wabunge wa Chadema kinastahili kupongezwa kwa kuwa wameonyesha kwa vitendo kuwa uchaguzi ulikuwa na dosari.

Wanafunzi hao ambao wapo Jijini Tanga kwa ajili ya mazoezi walisema wabunge hao hawakutaka kuwa wanafiki mbele ya Rais Kikwete na badala yake wakaonyesha kilichokuwa mioyoni mwao.

“Walichofanya ni kupaza sauti ili dunia ielewe kwamba kulikuwa na dosari kubwa katika zoezi zima la kutangaza matokeo na hilo linaegemea kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema Saida Hamis mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho.

Mawakili na Wanasheria
Mwanasheria wa Ngorongoro mkoani Arusha, Imanuel Saringe alisema: "Kisheria jambo hili halina tatizo na binafsi ninaaamini ujumbe wao umefika kwa walengwa bila vurugu au damu kumwagika."

Hata hivyo, alisema hutuba ya Rais Kikwete imekuwa ya ujumla sana na hivyo ni vigumu kuitathimini katika utekelezaji wa aliyosema.

Naye wakili mashuhuri mjini Moshi (jina limehifadhiwa) alisema kwa mtu mwenye mawazo finyu anaweza kusema kitendo cha Wabunge hao ni usanii fulani, lakini mtu upeo mpana atagundua Tanzania ina mgogoro wa kikatiba.

“Tuna tatizo la ubovu wa sheria nzima ya uchaguzi na kwa bahati nzuri sana wabunge hawa wameishia tu kutoka nje lakini tukiendelea na mfumo huu wa katiba unaokataza kuhoji matokeo ya rais, iko siku tutamwaga damu.”

Alisema: ”Tukiendelea na katiba hii tutajikuta tunakuwa na kiongozi aliyetangazwa kuwa ni rais, lakini si kiongozi aliyeshinda urais... kisheria anakuwa Ikulu, lakini kiuhalali hastahili na hapa ndipo mgogoro unapoanzia.”

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
Mkurugenzi mtendaji wa wanaharakati wa Agenda 2000, Moses Malaba alisema kitendo kilichofanywa na Chadema, kimefikisha ujumbe uliokusudiwa.

“Kisiasa walichofanya Chadema ni sawa; wamefanikiwa kufikisha ujumbe wa kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi kama walivyokusudia,” alisema Malaba lakini akaonyesha wasiwasi kama wananchi wataelewa lengo la chama hicho.

“Lakini wameenda mbali sana... wanachotaka wananchi waliowachangua ni kupata uwakilishi bungeni. Kwa sasa wanataka kujivunia kuwa na wabunge wengi.”

Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama alisema haoni kosa lolote kwa wabunge hao kufanya kitendo hicho.

“Kwa maoni yangu walichokifanya ni sahihi kwa sababu usipokubaliana na mtu huwezi kumsikiliza... ni vizuri hisia zako usizifanye ni siri ni vizuri ukazionyesha badala ya unafiki; mimi sioni tatizo hapa,” alisema.

Vyama vya siasa
Aliyekuwa mgombea urais wa TLP, Mutamwega Mugahwa alisema kitendo cha Chadema kinampasa Rais Kikwete kukaa chini na kutafakari tatizo lililopo na kulipatia ufumbuzi.

“Ningekuwa mimi ndio nimesusiwa Bunge, kiukweli nisingeweza kuchukulia kirahisi; lazima ningekaa na wahusika na kujua tatizo lililopo na kutafuta njia ya kulitatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Mugahwa.
Alisema kwa mujibu wa katiba mtu ana uhuru wa kusikiliza na kutosikiliza ili mradi tu katika maamuzi yake asiingilie uhuru wa mtu mwingine.

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alisema kitendo hicho binafsi kimempa faraja na kwamba huo ni mwendelezo wa kupinga katiba na kutaka ibadilishwe.

Mtei ambaye pia aliwahi kuwa gavana wa Benki Kuu nchini pia alimuunga mkono mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Amir Manento kuwa sasa ni muda wa kulilia katiba mpya.

Wananchi na makundi mengine
Mkoa wa Iringa
Baadhi ya wananchi wamewapongeza wabunge wa Chadema kwa hatua yao wakieleza kuwa msimamo huo unaweza kumfanya rais ajue kwamba wapo Watanzania wengi ambao hawana imani na utendaji kazi wa Nec.

Walisema Chadema wangeweza kuitisha maandamano na kufanya fujo kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya, lakini kwa busara wametumia njia ya kususia hotuba kuonyesha kuwa hawamtambui rais kama alivyotamka katibu mkuu wa Chadema, Dr Willibrod Slaa.

Enock Mwasondole ambaye ni mkazi wa Mtwivila alisema umefika wakati ambao Nec inapaswa kuwa huru ili malalamiko yatokanayo na uchaguzi yapungue.

“Ni bora kususia kuliko wangeitisha mgomo na maandamano makubwa kama yaliyotokea Kenya. Rais asipuuzie hali ile badala yake anapaswa kuhakikisha Tume ya Uchaguzi inakuwa huru na kutenda haki,” alisema Mwasondole.

Mkazi mwingine wa Gangiolonga, Anania Mlelwa alisema huu ni wakati wa Tanzania kubadilisha katiba ambayo Iliandaliwa wakati wa chama kimoja na hivyo kusababisha tume hiyo kuwa mikononi mwa rais ambaye ni mwanachama wa chama kimoja.

“Katiba ndiyo tatizo kubwa; kama katiba ingelingana na wakati wa vyama vingi, tume isingekuwa ikilalamikiwa kwa kuwa isingekuwa chini ya rais,” alisema.

Naye rais wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari, Keneth Simbaya alisema suala hilo ni la kiitikadi zaidi la kwamba wabunge hao wanapaswa kusikilizwa kwa kuwa yawezekana wana madai sahihi,

"Mara nyingi tuhuma za wanasiasa zinatakiwa kuangaliwa pande mbili kwa kuwa upande mmoja inaweza kuwa ni kweli na kwa upande wa pili inaweza kuwa si kweli, hivyo wabunge hao wasikilizwe ili kubaini wanachokilalamikia," alisema mwanahabari huyo.

Mkoa wa Mwanza
Uamuzi wa Chadema pia uliungwa mkono mkoani Mwanza ambako walisema unalenga kurejesha thamani ya kura.
Yohana Kagenzi, mkazi wa jijini Mwanza, alisema Chadema wameanzisha njia ya amani na ya kiungwana ya kudai katiba na tume huru ya uchaguzi ambayo haiwezi kusababisha umwagaji wa damu na kuzusha vurugu.

“Walisema kuwa hawayatambui matokeo, lakini serikali iliona ni jambo la kawaida nadhani njia hii sasa itamkera rais na kuamua kuwasikiliza. Kama hakuchakachua kura kwa nini asisikilize malalamiko yao,” alihoji Kagenzi.

Mkazi mwingine, Saida Mbwana alisema kitendo hicho kisipuuzwe kwa kuwa kinaweza kuwa na athari kubwa.
"Kama hawamtambua Rais Kikwete, basi hata serikali atakayoiunda hawataitambua, jambo ambalo litawakosesha maendeleo katika majimbo," alisema.

Mkoa wa Arusha
Arnold Kamde, Gervas Mgonja pamoja na Prosper Mfinanga ambao ni wakazi wa Arusha walidai ya kuwa kitendo hicho si tu kwamba kimeonyesha dalili za kukua kwa demokrasia nchini, bali pia kinatoa ujumbe kwa serikali ya Rais Kikwete kuwa Chadema hawakubaliani na matokeo ya urais kwa kuwa yalichakachuliwa.

"Sheria ya nchi inasema kuwa mara matokeo ya urais yakishatangazwa, hakuna mtu wa kuyapinga mahakamani. Sasa hiki kitendo si tu kwamba kinaonyesha kukua kwa hali ya demokrasia nchini bali pia ni ujumbe tosha kwa serikali ya Kikwete," alisema Mgonja.

Mfanyabiashara John Lyimo wa soko kuu la Arusha alipongeza wapinzani kwa kuonyesha hasira zao za kupinga matokeo na pia alimpongeza Rais Kikwete kwa kutoa hutuba nzuri.

"Mimi sina chama ila naona Chadema wamefanya vizuri tu na wamefanikiwa kufikisha ujumbe... rais aliongea vizuri na ameonyesha ameupata ujumbe," alisema Lyimo.

Mkoa wa Mbeya
Watu wengi walioongea na Mwananchi mkoani Mbeya waliunga mkono kitendo cha Chadema wakisema ujumbe waliotaka kumfikishia rais ulifika.

“Chadema wana ujumbe ambao wamewasilisha kwa serikali ya Rais Kikwete na ni haki yao kufanya hivyo,” alisema Jeremiah Osward ambaye ni mkazi wa Vwawa wilayani Mbozi.

"Kutokana na tamko lao la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, isingekuwa ni rahisi kwao kumsikiliza."

Mkazi wa Mwanjelwa, Zawadi Pangani alisema wabunge hao walikuwa sahihi kwa kuwa wanajua wanachokifanya ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi na kwamba bila kufanya hivyo, haki haitaweza kupatikana.

Alisema inawezekana Chadema wana uhakika kuwa mgombea wao wa urais, Dk Slaa alishinda, lakini matokeo yakatangazwa kuwa ameshindwa, hivyo wana haki ya haki yao kufanya hivyo.

Mkoa wa Morogoro
Mmoja wa wakazi wa Morogoro, Anthony Chalamila alisema tukio hilo lilitarajiwa kwa sababu mgombea wao alitamka wazi kuwa hakubaliani na matokeo yaliyomtangaza Kikwete kuwa rais kwa madai yana walakin.

“Ni lazmima wasimamie na kuyatetea maamuzi yao, hivyo haingewezekani mtu ambaye walisema hawamtambui, wakae kumsikiliza,” alisema.

"Kama wangekubali kukaa na kumsikiliza rais akihutubia, ingeonyesha wazi kuwa hawana msimamo."
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Naye Simon alisema ni haki yao kufanya hivyo kwa kuwa walishatoa sababu za msingi za kutomtambua rais.

Wanaopinga kitendo cha Chadema
Wasomi na wanazuoni
Mbali na wengi kuunga mkono kitendo hicho, wapo ambao wanakipinga wakiongozwa na kiongozi wa zamani wa waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Profesa Ernest Wamba dia Wamba ambaye alisema si cha kiungwana.

Akizungumza katika mkutano wa wanafalsafa ulioandaliwa na Chama wa Falsafa Tanzania (Phata) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Wamba alisema ni vizuri kama chama hicho kingekubaliana na matokeo hayo.

“Kawaida katika siasa changamoto ni jambo la kawaida, lakini kwa jinsi ulivyoniuliza kuhusu uchaguzi wa hapa Tanzania ni kweli umefanyika na mshindi kapatikana, lakini ingekuwa vizuri kama walioshindwa wangekubali tu matokeo,” alisema Profesa Wamba.

“Wabunge wameshakula kiapo, lakini wanasema hawatambui ushindi wa rais. Wana haki ya kuzungumza kwa kuwa hiyo ndio maana ya falsafa, lakini kwa hili la kiapo litawabana. Wangekubaliana na matokeo.”

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali......

Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) limeelezea kutofurahshwa na kitendo kilichofanywa na Chadema na kukitaka kutafuta njia mbadala ya kutoa dukuduku lao.

Katibu wa TEC, Padri Antony Mkunde alisema vyama vya siasa na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kutambua kuwa amani iliyopo haikushuka kutoka mahali popote bali ni mshikamano na busara katika uongozi.

"Mahali penye vurugu hata viongozi wa dini hawawezi kuhubiri; kinachotakiwa ni busara za viongozi wa nchi katika kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo," alisema Makunde.

Kwa upande wake Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISATAN) imekielezea kitendo cha Chadema kuwa ni utovu wa nidhamu.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Rose Haji alisema viongozi wa Chadema ni kati ya viongozi waliokula kiapo walipoapishwa hivyo wasingepaswa kususia hotuba ya rais.

"Chadema wanatakiwa kumheshimu rais kama baba mzazi kwa sababu baba anapokosea huwezi kumdhalilisha mbele ya kadamnasi hivyo heshima inatakiwa pia katika suala la uongozi," alisema Haji.

Naye mwenyekiti wa taasisi ya kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khaliha Khamis alisema uamuzi wa Chadema utasababisha chuki dhidi ya chama hicho na wananchi waliowachagua.

Alisema kitendo hicho kinaonyesha dhahiri kuwa chama hicho hakiko tayari kukubali misingi ya demokrasia nchini na kuwatumikia wananchi.

Vyama vya siasa....

CCM imewataka wabunge wote waliokiri kutomtambua rais kujitoa haraka bungeni vinginevyo wataondolewa na azimio la bunge hadi watakapotambua uwepo wa rais.

Katibu wa kamati kuu ya CCM, John Chiligati alisema kuwa kila mbunge amekula kiapo cha kutii na kulinda katiba na kitendo cha kutomtambua rais ni uvunjaji wa katiba na hivyo wabunge hao wanatakiwa kujiondoa bungeni.

Chiligati alisema kitendo cha Chadema kuruhusu wabunge na madiwani wake kuendelea na kazi wakati hawamtambui rais na serikali ni unafiki wa hali ya juu.

Chiligati aliwataka wananchi kukataa tabia za viongozi wanaokataa matokeo kwa kuwa ni tabia inayoweza kusababisha matatizo na kuchochea vurugu nchini.

Katibu mwenezi wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila alisema kitendo hicho hakikuwa cha kiungwana huku akikielezea kuwa ni sanaa ya maigizo.

Wananchi na makundi mengine
Mkoa wa Kagera
Aliyewahi kuwa waziri kwa nyakati tofauti katika awamu ya kwanza na pili Balozi Joseph Rwegasira amewaponda wabunge wa Chadema kwa kususia hotuba hiyo.

Mwanasiasa huyo alisema kitendo hicho kilikosa hekima kwa madai kuwa hawakujua sheria na taratibu.

Balozi Rwegasira, ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Nkenge, alisema rais hawezi kususiwa na wabunge kwa kuwa kwa mujibu wa taratibu hata yeye ni sehemu ya Bunge na kuhoji iweje wasisusie Bunge zima.

Mkoa wa Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashar Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema kilichofanywa na wabunge hao wa Chadema hakikuwa cha uungwana na si mfano mzuri wa kuigwa.

“Kama hawataki kutambua matokeo yaliyompa Kikwete urais ina maana kwa miaka yote mitano hakuna siku watashiriki kutunga sheria Bungeni kwa sababu ni lazima mwisho wa siku iidhinishwe na Rais wanayemkataa,” alisema.

Alisema anachokiona ni ubinafsi wa Chadema kwamba kionekane ndicho chama kikuu cha upinzani nchini kama ilivyo CUF kwa Zanzibar ili siku za usoni wapate nafasi ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Bendera Isinika, ambaye mkazi wa Kaloleni anayefanya kazi ya uchoraji, alipinga kitendo cha wabunge wa Chadema kususia hotoba ya Rais Kikwete kwa madai kuwa hawakuwatendea haki wananchi waliowachagua kwa kuwa walipaswa kuwashirikisha kwanza kabla ya kufanya tukio hilo.

"Kama kuna tatizo la uchakachuaji wa kura wao walipaswa kutumia njia bora na sio kususia hotuba ya Rais Kikwete kwa kuwa wao tumewachagua sisi hivyo wangetuambia kwanza kama wanataka kutoka nje ya Bunge na si kuchukua maamuzi yao," alisema Isinika.

Mkoa wa Mbeya
Mkazi wa wilayani Mbozi, Imelda Ngarawa alisema kuwa hayo ndiyo matokeo ya upinzani kwa kuwa wanafikiri bungeni ni mahali pa kufanya sanaa, hivyo wameenda huko si kwa ajili ya kuwatetea wananchi bali kufanya sanaa.

Naye mkazi wa Tukuyu wilayani Rungwe, Fadhili Sikumoja alisema kuwa wabunge hao hawajafanya vizuri kwani rais Kikwetye bado ni rais wao kwani yupo madarakani na kwamba ilikuwa vizuri wangemsikiliza hotuba yake na kama wanahopja za msingi wangewasilisha wakati wa bunge lijalo.

Mkoa wa Morogoro
Mkazi wa Morogoro Leonard Mtete alisema kuwa hatua iliyoonyeshwa na wabunge wa chama cha Chadema haikuwa nzuri kwa vile inaweza kuwashushia umaarufu ulioanza kujijenga katika chama hicho.

Alisema kuwa hali hiyo pia inaweza kuionyesha jamii kuwa chama hicho ni chama cha washari na wagomvi tofauti na jinsi ambavyo watu walinavyokichukulia kuwa mapambano yake ni kidemokrasia na ya amani.

“Mimi nafikiri wabunge wa chadema wangetumia fursa waliyonayo bungeni kupambana kwa hoja na siyo kutoka kama walivyofanya wao” alisema mkazi huyo wa Morogoro.

Mkoa wa Iringa
Mkazi wa Iringa, Fanuel Kagambo alisema haoni kama msimamo huo unaweza kuwa na manufaa zaidi ya kuwaumiza Chadema na akawashauri kuanzisha njia nyingine ya kudai madai yao kwa vile kumkataa rais na kushiriki kupiga kura za kumthibitisha waziri mkuu aliyeteuliwa naye kuonaonyesha kumtambua.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe anasemaje...
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mbowe alisema wanaowapinga au kuwa na mawazo tofauti na uamuzi huo, wasilitazame suala hilo juu juu na badala yake waangalia hoja wanazozitoa.

Alisema Chadema haikuamka tu na kutangaza kutomtambua rais, bali inazo sababu za msingi ambazo imeziweka bayana na imekuwa ikizieleza kila kukicha na kulaumu vyombo vya habari vinavyoshindwa kuainisha malalamiko au hoja zao kwa wananchi.

Mbowe alisema, msingi wa madai na malalamiko ya Chadema ni kutaka mazingira mazuri katika chaguzi zijazo wananchi wapate viongozi waliowachagua.

“Harakati ni kitu endelevu, michakato huzaa tunda la haki, miaka 19 sasa tangu siasa za vyama vingi ziruhusiwe, kumekuwa na vilio vingi toka kambi ya upinzani na kwa wananchi, lakini wenzetu walioko madarakani hawaonekani kusikia, tunatafuta lugha mbadala baada ya lugha ya upole kusikia” alisema.

Alisema, jambo wanalopigia kelele sio kilio cha Chadema pekee, bali ni kilio cha watanzania wote na akasema wanachofanya ni kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi wa mwaka 2015.

“Yapo matatizo ya msingi na ni lazima yafanyike mabadiliko ya haraka na ya msingi, kwanza ni suala la katiba, tutahitaji kuangalia katiba kama chombo muhimu kinachoweza kumkomboa mtanzania na kupunguza vilio vya watu wengi” anasema.

Akizungumza kwanini wanayakubali matokeo ya wabunge na kuyakataa yale ya rais, Mbowe anasema, “Hili ni muhimu likawa wazi, sheria iko wazi kabisa, kwamba Rais akishatangazwa na Tume ya Uchaguzi hakuna anayeweza kubadilisha wala kwenda mahakamani, lakini ukiwa huridhiki na ushindi kwa wabunge au madiwani, sheria inaruhusu kwenda mahakamani kupinga” anasema.

Anasema, kutokana na sheria hizo ambazo anasema ni miongoni mwa mambo wanayoyapigia kelele wameamua kutumia njia hiyo ya kutomtambua rais ikiwa ni katika hatarakati za kutaka marekebisho katika sheria kandamizi kama hiyo ya kutokuwa na haki ya kupinga endapo wagombea wengine watakuwa hawajaridhishwa na ushindi wa mgombea mwingine.

Hata hivyo Mbowe alisema, Chadema inatambua kuwa kwa kufanya hivyo hakuwezi kubadilisha matokeo na hakuwezi kuzuia Kikwete kuwa rais au kuongoza serikali isipokuwa kwa kufanya hivyo kutafikisha ujumbe wao kwake Kikwete na serikali yake pamoja na dunia nzima.

Habari hii imeandaliwa na Joyce Mmasi, Nora Damian, Tumsifu Sanga, Fidelis Butahe, Hussein Kauli, Minael Msuya, Fredy Azzah, Michael Matemanga, Petro Tumaini, Hussein Issa, Aziza Masoud, Hidaya omary, Burhani Yakub,Tanga, Daniel Mjema, Moshi, Moses Mashalla na Mussa Juma,Arusha, Brandy Nelson, Mbeya, Tumaini Msowoya na Habel Chidawali,Iringa,Venance George, Morogoro, Phinias Bashaya,Bukoba, Geroda Mabumo na Masoud Masasi Dodoma na Frederick Katulanda, Mwanza.

0 comments:

Post a Comment