Thursday, November 25, 2010

Shitambala ajibu agizo la Dk. Slaa

WAKATI uongozi wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ukikataa ombi la kujiuzulu kwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Sambwee Shitambala, kwa kutokidhi vigezo vya katiba ya chama, mwenyekiti huyo amesisitiza hatakuwa tayari kurudi katika nafasi hiyo kwa sasa hadi hapo chama hicho kitakapomaliza kabisa uchunguzi wake.

Shitambala ambaye ni wakili wa kujitegemea alisema ataendelea kukaa nje ya cheo hicho ili kupisha uchunguzi huru dhidi ya tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwake lakini pia kulinda hadhi ya kazi yake ya kutetea haki za raia kupitia kada ya sheria.

Msimamo huo aliutoa jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kujibu maagizo ya chama chake, ikiwa ni siku moja tu baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, Dk. Willibrod Slaa, kulikataa ombi lake na kumsihi aendelee na uenyekiti.

Kwa mujibu wa barua ya Shitambala aliyokiandikia chama hicho na Tanzania Daima kupata nakala yake, sababu kuu nne ndizo zilizomfikisha kwenye uamuzi wa kujiuzulu wadhifa huo.

Miongoni mwa sababu hizo ni yeye kutupiwa lawama za kupokea rushwa kwenye uchaguzi wa ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini pamoja na mkoa kukosa mgawo wa wabunge wa viti maalumu.

Alisema mbali na ukweli ulivyo juu ya mfumo uliotumika kupata nafasi za wabunge wa viti maalumu, wanachama na baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoa wamekuwa wakitaka majibu, hali ambayo imekuwa ikimuweka katika wakati mgumu kwani hakuhusika katika mchakato huo.

Alisema katika hali ya kushangaza uongozi huo wa juu wa chama badala ya kufikiria kwa kina hoja hizo nzito na kuzitafutia majibu yanayoweza kuwatuliza wanachama wenye hasira wao wameendelea kutoa majibu mepesi.

“Hoja iliyopo mbele ni nzito, haiingii akilini Mkoa wa Mbeya kukosa nafasi ya viti maalumu wakati tumefanya kazi kubwa ya kukiinua chama tena kwa muda mfupi, walipaswa kutoa tiba kwanza kwa hili ndipo waamuru mimi nirudi kwenye nafasi yangu,” alifafanua Shitambala.

Aliongeza kuwa baada ya kupata nafasi ya kuwa mwenyekiti maisha yake yalitengenezwa katika sura mbili hivyo kitendo chake cha kuamua kujiuzulu kutokana na tuhuma za rushwa zinazotokana na mambo ya siasa kina lengo la kuokoa hadhi ya maisha ya upande wa pili wa taaluma yake ya sheria.

“Si rahisi mimi kuona maisha ya siasa yanaharibu maisha yangu ya kawaida na wala maisha yangu ya kawaida yakiharibu maisha ya siasa, ni vizuri nikaeleweka hivyo. Mimi bado ni mwanachama mwaminifu na punde yote haya yakishughulikiwa na mimi kuonekana sikuhusika basi nitarudi kuwatumikia wananchi,” alisisitiza Shitambala.

source : tanzania daima

0 comments:

Post a Comment