Thursday, November 18, 2010

CHADEMA yamwadhiri Ndugai

Yamtuhumu kumbeba Sophia Simba

na Salehe Mohamed, Dodoma

NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai, juzi alianza kuonja machungu ya kiti chake baada ya kukaliwa kooni na wabunge wa CHADEMA kwa madai anakipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na John Mnyika wa Ubungo, walipinga kitendo cha mbunge wa viti maalum kupitishwa bila kupingwa kuwakilisha Tanzania katika Bunge la nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).

Mnyika aliomba mwongozo wa Naibu Spika kuhoji ni kanuni ipi iliyotumika kumpitisha Simba ilhali wenzake walijieleza kwa lugha ya Kiingereza na baadaye kupigiwa kura.

Alisema kanuni za uchaguzi wa wabunge wanaokwenda kwenye vyombo vingine vya uwakilishi kifungu cha 5(2)c kinasema mgombea mmoja wa nafasi inayohusika wabunge watampigia kura za ndiyo au hapana.

“Mimi napinga Sophia Simba, kutoitwa kujieleza, kuulizwa maswali na kupigiwa kura, kinyume na kanuni ametangazwa na amepita bila kupigwa,” alisema Mnyika.

Akitoa mwangozo, juu ya jambo hilo Naibu Spika Ndugai, alisema Mnyika yuko sahihi, lakini alichelewa kutoa hoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda ndiye aliyeanza mchakato wa uchaguzi kabla ya kumuachia kiti hicho.

Jibu hilo lilimfanya Zitto na Mnyika kupinga hoja hiyo na kuzua mjadala ambao ulimfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Federick Werema kuingilia kati.

Werema, alisema hoja iliyotolewa na Mnyika ni sahihi lakini haitoweza kujadiliwa au kubadili utaratibu uliofanyika kwa sababu ilichelewa kutolewa.

Alisema kuwa makundi mengine yalishafanya uchaguzi huo hivyo haitokuwa rahisi kwa Sophia Simba kuitwa kujieleza, kuulizwa maswali na hatimaye kupigiwa kura.

Maelezo hayo, yalipingwa na Zitto kwa madai kuwa kanuni zimekiukwa na Bunge haliwezi kuendeshwa kwa ukiukaji kanuni au upendeleo kwa chama fulani.

Mjadala wa kupinga jambo hilo ulizidi kushika kasi na kumfanya Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), kusimama kutoa taarifa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) inayohusu mamlaka ya Spika.

Alisema kanuni hiyo, inamtaka mbunge ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika kuwasilisha sababu za kutoridhika kwake kwa katibu wa Bunge, ambaye atawasilisha malalamiko hayo kwa Spika.

Chenge alibainisha kuwa vifungu vidogo vya (5) na (6) vinaeleza Spika atawajibika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa na kamati.

Aliongeza kuwa Spika au Naibu wake hawatakuwa wenyeviti wa kikao hicho, ili kutoa nafasi na haki kwa shauri husika kusikilizwa.

Aliongeza kuwa majibizano kati ya kiti (Spika au Naibu Spika) na baadhi ya wabunge kutokana na uamuzi wa Spika hayana nguvu.

Zitto aliinuka na kumjibu Chenge kuwa Kamati ya Kanuni za Bunge bado haijaundwa, hivyo hawawezi kuwasilisha taarifa ya kutoridhishwa kwake.

Akizungumzia kuhusu uadilifu kwa kiongozi wa Bunge (Spika, Naibu wake au wenyeviti wa Bunge), kwa kutumia kanuni ya nane, inayozuia upendeleo, Zitto alitaka Sophia ajieleze na apigiwe kura.

Mjadala huo ulihitishwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ambaye aliwaonya wabunge wanaotaka kucheza na mamlaka ya Spika au Naibu Spika kujirekebisha mara moja, ili kuepuka adhabu.

Mjadala huo, ulisababishwa na uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la SADC.

Aliongeza kuwa mabishano hayo yanapaswa yachukuliwe na wabunge wapya kwa umakini mkubwa hasa kwa kusoma sheria na kanuni za kudumu za Bunge.

Pamoja na Sophia, wajumbe wengine wa Bunge la SADC-PF ni Mohammed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF), ambaye baada ya kutangazwa mshindi kwa kura 275 dhidi ya kura 47 za mgombea wa CHADEMA, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Mwingine ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye (CCM) aliyepata kura 180. Waliopiga kura walikuwa wabunge 324.

0 comments:

Post a Comment