Thursday, November 25, 2010

Dk Slaa anena: Sitta akikubali, nitamshangaa

Fidelis Butahe
VIONGOZI wa vyama vya upinzani wameponda uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa Baraza la Mawaziri, huku katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa akisema atashangaa kama Samuel Sitta ataridhia uteuzi wake wa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao amesema utamshushia hadhi.

Sitta alikuwa amechukua fomu za kutaka achaguliwe tena kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano lakini CCM ikamuengua kwa kile ilichoeleza kuwa ni kutaka wanawake waongoze moja ya mihimili ya nchi.
Kuenguliwa kwake kulifanya wengi wabashiri kuwa Rais Kikwete angempa wizara nyeti kama ya Katiba na Sheria ili aongoze mabadiliko ya katiba baada ya Zanzibar, lakini jana alitangazwa kushika wizara hiyo ya ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dk Slaa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema, alisema kuwa uteuzi wa Sitta umelenga kuendeleza ufisadi na kwamba iwapo spika huyo wa zamani ataikubali kushika nafasi hiyo, atakuwa amejishushia hadhi.
Dk Slaa, ambaye aligomea matokeo ya kura za uchaguzi wa rais na baadaye chama chake kutangaza kutotambua matokeo hayo, alisema: “Nilitegemea kusikia Baraza la Mawaziri 20 hadi 25. Sasa hawa mawaziri wote wanakwenda wapi, watapewa nyumba na magari ya Sh200 milioni, hivyo fedha nyingi zitatumika kwa matumizi yasiyo na ulazima.”
“Hili baraza limeundwa kujenga utawala wa kifisadi, kazi ya Baraza la Mawaziri si kumlinda rais ni kuwahudumia Watanzania; hizi si sura sahihi.”

Dk Slaa alisema kwa kiongozi makini kama Sitta kupelekwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni mwendelezo wa ufisadi na kusisitiza kuwa atamshangaa kama atakubaliana na uteuzi huo.
“Naelewa kilichomkumba Sitta... kila siku nasema hii kauli na sitachoka kuisema kwa kuwa naipenda nchi yangu. Inakuwaje unatoa nafasi za uwaziri kwa ajili ya kulipa fadhira? Hii si sahihi hata kidogo,” alisema Dk Slaa.
“Uteuzi wa Sitta kwenye wizara hiyo ndio utatudhihirishia kama kweli yeye ni mpambanaji wa ufisadi au la.”
Dk Slaa pia aliponda uteuzi wa William Ngeleja kuwa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Makongoro Mahanga kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi na Ajira kuwa hauna mantiki.

Hata hivyo hakufafanua zaidi sababu za kauli yake hiyo kuponda mawaziri hao.
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema kuwa baraza hilo halina jipya na akamshangaa Rais Kikwete kutumia siku nyingi kabla ya kutangaza baraza wakati hakuna jipya alilolifanya katika uteuzi wake.
“Watanzania wategemee maisha yaleyale tu, hakuna mabadiliko yoyote... labda kikubwa ni uteuzi wa (Waziri mpya wa Ujenzi, John) Magufuli na waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Anna) Tibaijuka. Lakini, Tibaijuka naye hatakuwa na kazi rahisi kwa kuwa ndio mara yake ya kwanza anakuwa waziri na alikuwa ameshazoea kazi za kimataifa ambazo ni tofauti na za wizara,” alisema Mziray.

Alisema kwamba kuona baraza dogo lenye mawaziri wasiozidi 30 na kusisitiza kuwa uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete unaendeleza mfumo wa CCM wa kupeana ulaji.
“Ili Watanzania waondokane na karaha hii, suluhisho ni kuwachagua wapinzani. Siku wapinzani wakiingia madarakani haya yote yatakwisha,” alisema Mziray.
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema kuwa uteuzi huo umewapa watu ambao ni wagumu wa kufikiri matatizo na shida za Watanzania akipinga uteuzi wa Wazanzibar katika baraza hilo.
“Haiwezekani; Zanzibar wamevunja Muungano inakuwaje nao wanaingizwa katika baraza la mawaziri. Huku ni kujipendekeza kwa namna ya kipekee,” alisema Mtikila.

Mchungaji Mtikila ambaye alienguliwa katika kinyang’anyiro cha urais kwa madai ya kutokuwa na wadhamini katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, alidai kuwa alichokifanya Rais Kikwete ni kuwafurahisha watu fulani ambao hakuwataja watu hao.

“Uteuzi huu si kwa ajili ya maslahi ya Watanzania; baraza hili la mawaziri ni maafa makubwa. Nchi ya Ujerumani ina mawaziri 14, Marekani hawazidi 30, lakini sisi ndio tunaendeleza kufurahishana. Nakwambia baada ya miaka mitano nchi hii itakuwa imekwisha kabisa,” alisema Mchungaji Mtikila.
Naye mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema Kikwete anatakiwa kuwa mkali kwa baraza hilo ili mawaziri wake wasifanye mzaha.

“Yaani hawa mawaziri naona wangekuwa na barua za kujiuzuru mkononi ili watakapovurunda iwe ni kukabidhi barua hizo na kuachia ngazi. Ni kweli baraza ni kubwa, lakini kama kutakuwa na uwajibikaji, sidhani kama kutakuwa na tatizo, ila kama wakilala, hapo ndio mambo yatakapoanza kuwaharibikia,” alisema Mrema.
Mrema alimpongeza Rais Kikwete kwa kuwateua Magufuli na Anna Tibaijuka akisema kuwa ni watendaji wazuri.

SOURCE : MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment