Monday, November 15, 2010

Mpendazoe: Taifa linaelekea utumwani

na Ratifa BaranyikwaALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Fred Mpendazoe, amesema nchi inaelekea utumwani kwa sababu ya kundi la watu wachache wenye nguvu ya fedha kuamua juu ya nani awe kiongozi.

Mpendazoe aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Segerea, kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa kampeni mpaka Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Katika mkutano huo, uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Liwiti, eneo la Tabata Segerea, Mpendazoe alisema kutokana na matukio mbalimbali ya kisiasa yaliyojiri wakati wa uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo, ana kila sababu ya kubashiri kuwa nchi inaelekea kwenye utumwa.

“Ninasema hivyo, kwa sababu hivi sasa watu wachache wenye nguvu ya fedha wanaamua mustakabali wa viongozi kwa maslahi yao binafsi,” alisema.

Mpendazoe alisema ikiwa Watanzania hawatakataa kuamuliwa nani awe diwani, mbunge, rais au spika, ina maana hakuna tofauti ya kuwa watumwa, kwa sababu hawawezi kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Alisema rais aliyechaguliwa kwa uovu, kamwe hawezi kutenda haki na badala yake atacheza muziki mmoja na mafisadi.

Akizungumzia uchaguzi wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo uliompatia ushindi Makongoro Mahanga (CCM), Mpendazoe aliwaambia wananchi hao kuwa hakuna ambaye atabisha kama CHADEMA walishinda Segerea, lakini kwa sababu ya udhalimu, matokeo yaliyotangazwa na tume yalikuwa kinyume.

Aliwaambia kuwa amefungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kupigania haki ambayo ni ya wananchi.

Alisema leo watakwenda kwa Msajili wa Mahakama, kufuatilia gharama za kuendesha kesi, na kwamba tayari wananchi waliojitokeza awali wamekwisha wachangia kiasi cha sh mil. tano.

TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment